Jee, unaanza kuona kuwa yafuatayo yanakusumbua?
1. Kukosa kumbukumbu kama vile kusahau tarehe muhimu au matukio muhimu
2. Kupata shida katika kufanya mambo ya kawaida, kama kukumbuka sheria za mchezo unaoupenda au kuendesha gari kuelekea sehemu unayoifahamu vizuri
3. Kupata shida katika mazungumzo na wenzako au katika kuandika, kwa mfano kupata shida katika kukumbuka maneno sahihi au majina ya watu na sehemu mbalimbali
4. Kupoteza mwelekeo wa muda na mahali, kama kusahau sehemu ulipo, kutojua msimu wa mwaka, tarehe, na muda uliotumia katika shughuli
5. Kupungua uwezo wa kutoa maamuzi kama kukosa usafi, kushindwa kutoa maamuzi ya pesa n.k.
6. Matatizo katika kuona kama matatizo katika kusoma au kukadiria umbali
7. Kupungua kwa uwezo wa kutatua matatizo na kuweka mikakati kama ufuatiliaji wa bili mbalimbali au kukumbuka mapishi
8. Kupoteza vitu kila wakati au kusahau villipowekwa
9. Mabadiliko katika tabia
10. Kukosa ubunifu au kujitoa kwenye shughuli za jamii.
Ni jambo la kawaida kuanza kupoteza uwezo wa kukumbuka vitu kama orodha ndefu ya maneno umri unapokuwa mkubwa. Ukweli ni kuwa mtu wa miaka 50 ana uwezo wa kukumbuka asilimia 60 ya vitu kwenye orodha akipewa mtihani wa kumbukumbu ukilinganisha na kijana wa maiaka 20. Lakini kila mtu anasahau, na vijana wote wa miaka 20 wamepata kuona kuwa wameshindwa kukumbuka jibu la swali kwenye mtihani ambalo awali walilijua vizuri.
Ukiona baadhi ya mambo yaliyoorodheshwa hapo juu yanakuhusu, ujue una dalili za ugonjwa wa Alzheimer’s.
Ugonjwa wa alzheimer’s ni dosari inayoendelea kuongezeka taratibu ambapo husababisha seli za ubongo kuharibika na kufa. Ugonjwa wa alzheimer’s ndiyo chanzo kikubwa cha tatizo liitwalo dimentia – kuendelea kupoteza uwezo wa kufikiri, tabia katika jamii na linalomfanya mtu ashindwe kumudu shughuli zake yeye peke yake.
Dalili za mwanzo kabisa za tatizo hili ni kusahau matukio au mazungumzo ya hapa karibuni. Kadiri ugonjwa unavyoongezeka, mtu atapata matatizo makubwa zaidi ya kumbukumbu na kumfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Dawa za sasa hivi kwa ajili ya ugonjwa huu zinaweza kumpa mtu nafuu ya muda mfupi au kusadia kuzuia kuongezeka kwa hali hiyo mbaya kwa kasi zaidi. Tiba hizi zinaweza kumfanya mtu afikie kiwango chake za uzalishaji na kujitegemea kwa muda fulani.
Dalili Za Ugonjwa Wa Alzheimer’s
Kumbukumbu
Kukosa kumbukumbu kwa wakati fulani ni kitu kinachompata kila mmoja wetu. Ni kitu cha kawaida kusahau ulipoziweka funguo zako au kulisahau jina la mtu wako wa karibu. Kukosa kumbukumbu kunakoambatana na ugonjwa huu huwa ni endelevu na hali huwa mbaya zaidi na zaidi kila siku, na kufikia kumsababishia mtu ashindwe kuendelea kuzifanya kazi zake za kawaida.
Mtu mwenye alzheimer’s anaweza:
. Kurudiarudia maswali au maneno
. Kusahau mazungumzo, ahadi au matukio, na asikumbuke tena baadaye
. Kila wakati kupoteza vitu vyake, mara nyingi akiwa anaviweka sehemu ambazo hazitegemewi
. Kuanza kupotea maeneo aliyoyazoea
. Hatimaye kusahau majina ya watu wa familia yake na vitu vya kila siku
. Shida katika kupata maneno sahihi kutambulisha vitu, kuelezea mawazo yake au kushiriki kwenye mazungumzo
Kufikiri Na Kuchambua
Ugonjwa wa alzheimer’s humfanya mtu ashindwe kutuliza mawazo kwenye kitu kimoja na kufikiri, hasa kuhusu vitu vya kinadharia kama namba.
Kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja huwa ngumu, na huwa vigumu kutumia pesa vizuri, kuweka kumbukumbu kwenye vitabu na kulipa bili kwa wakati. Hali hii huweza kuendelea hadi kufikia kushindwa kutambua namba na kufanya hesabu.
Kufanya Maamuzi
Uwezo wa kutoa maamuzi yanayofaa kwenye mazingira ya kila siku utapungua. Kwa mfano, mtu anaweza kutoa maamuzi mabovu kwenye mahusiano ya kila siku au akavaa nguo ambazo haziendani na hali ya hewa. Atashindwa kukabiliana na matatizo ya kila siku, kama moto wa ghafla jikoni au maamuzi ya kushtukiza wakati akiendesha gari.
Kuweka Na Kutekeleza Mipango Ya Kila Siku
Shughuli za kufanya mara moja zenye hatua kadhaa za kuzikamilisha, kama kufikiria na kuandaa chakula fulani au kucheza mchezo unaoupenda, vinaanza kuwa vigumu kadiri ugonjwa unavyozidi. Hatimaye, mtu akifikia kiwango cha juu cha ugonjwa anaweza kusahau namna ya kukamilisha shughuli za msingi kama kuvaa nguo au kuoga.
Mabadiliko Ya Kimwonekano Na Ya Kitabia
Mabadiliko katika ubongo wa mgonjwa wa alzheimer’s huweza kubadili hisia na tabia za mtu. Matatizo yanaweza kuhusisha yafuatayo:
. Mfadhaiko
. Kutopenda vitu/ kutokuwa na hisia
. Kujitoa kwenye mambo ya kijamii
. Kubadilikabadilika kwa hisia kwa ghafla
. Kutopenda wenzake
. Hasira
. Kubadili ratiba ya kupata usingizi
. Kuzurura
. Kushindwa kujizuia vishawishi
. Kuwa na imani za uwongo, kama kuamini kuwa ameibiwa
Ujuzi Wa Siku Nyingi
Stadi muhimu alizo nazo hutunzwa kwa muda mrefu zaidi hata kama hali yake mgonjwa itazidi kuwa mbaya. Stadi hizo ni pamoja na kusoma, kusimulia hadithi, kuimba, kusikiliza muziki, kucheza muziki, kuchora, au kazi za mikono.
Stadi hizi zinaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi kwa sababu hutunzwa kwenye eneo la ubongo ambalo huathirika baadaye zaidi wakati ugonjwa ukiendelea kukua.
Chanzo Cha Ugonjwa Wa Kukosa Kumbukumbu
Wanasayansi wanaamini kuwa kwa watu wengi ugonjwa wa alzheimer’s unatokana na mchanganyiko wa urithi, mtindo wa maisha na mazingira, vitu ambavyo vinauathiri ubongo kwa muda mrefu.
Chanzo kamili cha ugonjwa huu bado hakijaeleweka, lakini unapofika kilele chake huwa ni matatizo katika protini za ubongo ambazo zinashindwa kufanya kazi vizuri, kuvuruga utendaji wa seli za ubongo (neurons) na kutoa sumu za aina mbalimbali. Neurons huharibiwa, hupoteza mawasiliano na kisha kufa.
Uharibifu mara nyingi huanza kwenye sehemu ya ubongo inayohusiana na kumbukumbu. Ukosefu huu wa neurons kisha husambaa kwenye maeneo mengine ya ubongo. Ugonjwa unapokuwa mkubwa, ubongo huwa umesinyaa kwa kiasi kikubwa.
Utafiti umeelekeza uchunguzi kwenye aina mbili za protini:
. Plaque. Beta-amyloid ni kipande ambacho ni mabaki ya protini kubwa. Vipande hivi vikiungana, vinaonekana kuwa ni sumu kwa neurons na vinavuruga mawasiliano baina ya seli. Vikundi hivi hujenga matabaka makubwa yanayoitwa amyloid plaques, ambayo yanachangayikana na mabaki ya aina nyingine za seli.
. Tangles. Tau proteins ni protini zinazoziwezesha neurons kusaidiana na kusafirisha virutubishi na vitu vingine vya muhimu. Ugonjwa wa alzheimer’s hubadili maumbo ya protini hizi na huzifanya zitengeneze maumbo yaitwayo neurofibrillary tangles. Maumbo haya huvuruga mfumo wa usafirishaji na ni sumu kwa seli.
Vihatarishi Vya Alzheimer’s
Umri
Kihatarishi kikubwa zaidi kuliko vyote cha ugonjwa wa alzheimer’s ni umri mkubwa. Kadiri kundi la jamii linavyozidi kuwa na umri mkubwa, ndivyo watu wenye tatizo hili wanavyozidi kuongezeka. Asilimia 15 ya watu wanaozidi miaka 65 na asilimia 50 ya wale wanaozidi miaka 85, wana tatizo la alzheimer’s.
Historia Ya Familia
Uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huu unachangiwa pia na vinasaba. Watu wengi huupata ugonjwa huu umri wao unapofikia miaka 70. Lakini, pungufu kidogo ya asilimia 10 ya watu hupata ugonjwa huu wakiwa na umri wa maika kati ya 40-50. Yapata nusu ya watu hawa hupata ugonjwa huu kwa sababu za kiurithi.
Jinsia
Tafiti zimeonyesha kuwa wanawake wanaupata ugonjwa huu zaidi ya wanaume. Ni ukweli kuwa wanawake wanaishi maisha marefu zaidi ya wanaume, lakini pekee haitoshi kuelezea sababu ya kuzidi kwa ugonjwa huu kwa wanawake. Tafiti zimeonyesha kuwa haifai kuwapa estrogen wanawake waliokwisha koma hedhi kwa madhumuni ya kupunguza wagonjwa baina yao.
Kuumia
Watu waliopata maumivu makali ya kichwani (emotional or physical damage) wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuupata ugonjwa huu.
Kujisomea Muda Wote Katika Maisha Na Kushiriki Shughuli Za Jamii
Utafiti umeonyesha kuwa kuna uhusiano kati ya ushiriki katika mambo ya kutumia akili na ya kijamii na kupungua kwa uwezekano wa kupata ugonjwa wa alzheimer’s. Kuwa na kiwango kidogo cha elimu – pungufu ya elimu ya sekondari – kumeonekana kuchangia upatikanaji wa ugonjwa huu wa alzheimer’s.
Msaada Kwa Mgonjwa Wa Alzeimer’s
Watu wenye tatizo hili la kukosa kumbukumbu hupatwa na mchanganyiko wa hisia – kuchanganyikiwa, kukata tamaa, hasira, woga, uchungu na mfadhaiko.
Kama unamhudumia mtu wa namna hii unaweza kumsaidia zaidi kwa kuwa msikivu kwa shida zake, kwa kumhakikishia kuwa bado anaweza kuishi maisha ya kawaida, kumpa misaada na kufanya uwezavyo kumrudishia hali ya kujiamini na kuheshimiwa.
Mazingira tulivu yanaweza kumsaidia matatizo yake ya kitabia. Mazingira mapya, kelele, mikusanyiko ya watu, kumharakisha kukumbuka vitu, au kumtaka afanye shughuli zinazohitaji fikra vinaweza kumfanya apate wasiwasi. Na mtu wa tatizo hili akipatwa na wasiwasi, uwezo wake wa kufikiri hupungua zaidi.
Tiba Ya Alzheimer’s
Dawa zilizopo sasa hivi zina uwezo wa kumsaidia mgonjwa kwa muda kwenye tatizo la kumbukumbu na mabadiliko mengine ya ufahamu. Dawa za aina mbili ndizo zinazotumika sana.
. Cholinesterase inhibitors zinasaidia kuboresha mawasiliano baina ya seli. Huleta matokeo mazuri kiasi. Dawa hizi zinaweza pia kusaidia matatizo ya mfadhaiko. Dawa hizi ni pamoja na donepezil (Aricept), galantamine (Razadyne) na rivastigmine (Exelon).
. Memantine (Namenda). Dawa hii humsaidia mtu mwenye tatizo la kadiri asiingie kwenye tatizo kubwa. Mara nyingine hutumika pamoja na Cholinesterase inhibitors.
Mwaka 2014, FDA (Food and Drug Administration) ilipasisha dawa nyingine, Namzaric, kama dozi inayojitegemea. Dawa hii hutibu alzheimer’s ya kadiri hadi ile iliyokomaa.
Tiba mbadala
Baadhi ya mimea, vitamini na virutubishi vinatumika sana kusaidia kuzuia au kupunguza kasi ya ugonjwa wa alzheimer’s. Baadhi ya tiba hizo mbadala ni:
. Omega-3 fatty acids. Omega-3 fatty acids kutokana na kula samaki au kutokana na virutubishi vinaweza kuondoa uwezekano wa kupata ugonjwa wa alzheimer’s, lakini haijathibika kutibu dalili za alzheimer’s.
. Curcumin. Mmea huu hutokana na tumeric na una tabia ya kuondoa uvimbe na za antioxidants ambazo zinaweza kuleta mabadiliko ya kikemikali ndani ya ubongo. Hadi sasa majaribio katika kliniki hayajaonyesha kutibu alzheimer’s.
. Ginkgo. Mmea wa ginkgo una tabia nyingi za tiba. Watu wengi huliita ginkgo jani la ubongo “brain herb”, ambalo limeonyesha kuboresha utendaji kazi wa ubongo. Ubongo hutumia asilimia 20 ya oksijeni ya mwili. Kwa sababu ginkgo husaidia mzunguko wa damu katika ubongo, kwa kupeleka oksijeni kwa haraka zaidi na kiufanisi. Faida ni nyingi, kama kutoa tiba ya mfadhaiko (depression) na kuongeza kumbukumbu, matendo hisia (Reflexes), na ufanyaji kazi wa ubongo kwa ujumla. Utafiti wa karibuni umeonyesha kuwa inaweza kupunguza madhara ya dementia kwa wagonjwa wenye Alzheimer’s, na kufungua njia ya tiba ya aina mpya ya ugonjwa huu ulioenea na usioeleweka vizuri.
. Vitamin E. Vitamin E inaweza kuzuia ukuaji wa ugonjwa wa alzheimer’s.
Katika kurasa nyingine tutaona matatizo ya Kifafa, msongo wa mawazo na mfadhaiko. Usisite kutoa maoni uliyo nayo kuhusu uandishi wa mada hii yetu ya leo.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya muda wa kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.