Acid Reflux au Kucheua Tindikali Ni Nini?

 

 

 

Kuna hali inaweza kukutokea ambapo utasikia kiungulia, uchungu mdomoni, kupata shida katika kumeza au kusikia kama chakula kinakwama kwenye koo au pengine matatizo mengine. Ni tatizo ambalo linaweza kukutokea muda wo wote lakini mara mara nyingi litakusumbua zaidi baada ya kula na kuwa zito zaidi pale unapoingia kitandani kulala hadi pengine kusababisha ukakosa kupata usingizi mzuri. Katika ukurasa huu tutalizungumzia tatizo hili ambalo kitaalamu huitwa chronic acid reflux au gastroesophageal reflux disease. Kwa lugha yetu tunaweza kuliita tatizo la kucheua tindikali.

Kucheua Tindikali Maana Yake Nini?

 

Kucheua tindikali (gastroesophageal reflux disease, au chronic acid reflux) ni hali ambapo mchanganyiko wa chakula wenye tindikali uliopo tumboni kila wakati hupanda juu kupitia umio (esophagus). Hali hii hutokea kwa sababu vali iliyopo unapoishia umio, lower esophageal sphincter, haifungi vizuri chakula kinapokuwa kimeingia tumboni. Tindikali, kwa hiyo, hupanda kupitia umio kuingia kooni na kisha mdomoni, na kukufanya usikie ladha ya uchungu.

 

 

Kila mtu wakati fulani katika maisha yake amepatwa na tatizo hili la acid reflux. Kucheua tindikali na kupata kiungulia, kwa wakati fulani, ni kitu cha kawaida. Lakini unapopatwa na tatizo hili zaidi ya mara mbili kwa wiki kwa kipindi cha wiki kadhaa mfululizo, na unatumia dawa za kiungulia na antacids na dalili zinakurudiarudia, unaweza kuwa na gastroesophageal reflux disease (GERD). Ukishakuwa na GERD unahitaji tiba ya mtaalamu, kwa sababu GERD huweza kuleta matatizo makubwa zaidi ya kiafya.

Dalili Za Acid Reflux

Dalili kuu za acid reflux ni kiungulia na kucheua tindikali. Watu wengine wana acid reflux bila kiungulia. Badala yake, wanasikia maumivu kwenye kifua, sauti kukwaruza asubuhi au matatizo ya kumeza. Unaweza kuhisi kuwa chakula kimekwama kwenye koo, au kama unakosa pumzi au koo limekabwa. GERD inaweza pia kusababisha kikohozi kikavu au kutoa harufu mbaya kinywani.

Ukiona kiungulia na kucheua tindikali vinakusumbua kila baada ya muda mfupi -utando laini juu ya umio unaunguzwa kila wakati na tindikali kutoka tumboni. Hatimaye utando huu huharibika. Tatizo hili likiwa sugu, tabia zako za ulaji na kulala vitabadilika.

Watu tofauti huathirika kwa namna tofauti na acid reflux. Dalili ambazo huwatokea wengi ni:

. Kiungulia
. Kucheua chakula
. Hisia kwamba chakula kinakwama kooni
. Kukohoa
. Maumivu ya kifuani
. Shida wakati wa kumeza
. Kutapika
. Kukauka koo na sauti kukwaruza.

Watoto wadogo wanaweza kupata dalili hizo hizo, kama:

. Vipindi vifupi vya kutapika vya mara kwa mara
. Kulia kupita kiasi, kukataa kula (watoto na vichanga)
. Matatizo mengine ya upumuaji
. Ladha ya tindikali ya mara kwa mara, hasa ukiwa umelala
. Koo linalokwaruza
. Kusikia kukabwa ambako kunaweza kumwamsha mtoto
. Harufu mbaya akipumua
. Shida kulala baada ya kula, hasa kwa watoto.

Acid reflux husababishwa Na Nini?

 

Acid reflux husababishwa na udhaifu au kulegea kwa vali ya chini ya umio (lower esophageal sphincter). Kwa kawaida vali hii hufunga kikamilifu mara baada ya chakula kuingia tumboni. Ikijilegeza wakati ambapo haitakiwi, mchanganyiko wa chakula wa tumboni hupanda kwenye umio, na kusababisha acid reflux.

Vipengele ambavyo vinavyosababisha hali hii kutokea ni pamoja na:

. Msukumo mkubwa mno kwenye tumbo. Baadhi ya wanawake wenye ujauzito hupata kiungulia karibu kila siku kwa sababu ya mwongezeko wa msukumo
. Aina fulani za chakula (kama bidhaa za maziwa, chakula kilichojaa viungo au kilichokaangwa) na tabia za kula
. Dawa zikiwa ni pamoja na dawa za asthma, high blood pressure na mzio, pia dawa za kuzuia maumivu, sedatives na anti-depressants.
. Hiatal hernia.

 

Unaweza Kufanya Nini Kuzuia Acid Reflux?

 

1. Uweke mwili wako kwenye uzito unaofaa
2. Kula chakula kidogo, mara nyingi badala ya milo michache mikubwa
3. Jaribu kupunguza mafuta kwa kupunguza siagi, mafuta na bidhaa za maziwa
4. Kaa wima wakati wa kula na dumisha mkao au simama wima kwa dakika 45 hadi 60 baadaye
5. Acha kulala mara baada ya kula. Kaa angalau saa 3 baada ya kula ndipo ulale
6. Acha kuvaa nguo zinazobana maeneo ya tumbo. Zinaweza kulibana tumbo na kukamua tindikali ya tumboni ipande kwenye umio
7. Ulalapo nyanyua kichwa cha kitanda chako nchi 6 hadi 8, kwa kutumia vipande vya mbao. Mito haifai.
8. Acha uvutaji wa sigara
9. Unaweza kushauriwa kutumia antacids. Fuata maelekezo ya daktari.
10. Acha kula chakula kinachosababisha acid reflux.

 

dawa za kiungulia

Chakula Gani Ukiache Kama Una Tatizo La GERD?

 

Kuchagua chakula na tabia za ulaji zina mchango mkubwa sana katika kudhibiti tatizo la GERD. Jaribu kuacha kula chakula ambacho hukusababishia kiungulia kila wakati. Watu wengi hupata shida wakila aina za chakula zifuatazo:

. Chakula chenye viungo vingi
. Chakula kilichokaangwa
. Chakula chenye mafuta mengi
. Chocolate
. Tomato sauce
. Garlic na vitunguu
. Pombe, kahawa na vinywaji vyenye kaboni
. Matunda ya aina ya machungwa.

Tunza kumbukumbu ya chakula kinachokupa shida.  Mwone tabibu kwa ushauri.

Mada yetu nyingine itachambua tatizo la kiungulia. Usisite kuuliza maswali kuhusu mada yetu ya leo.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya saa za kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.