Vitiligo Ni Ugonjwa Gani?

 

vitiligo mikononi

Vitiligo ni ugonjwa unaomfanya mtu apoteze rangi ya ngozi na kusababisha awe na mabaka mwilini mwake. Sehemu zinazopoteza ngozi huongezeka kadiri siku zinavyoongezeka. Hali hii huweza kutokea sehemu yo yote katika mwili. Inaweza kutokea kwenye nywele na hata ndani ya mdomo.

Kwa kawaida, rangi ya nywele na ngozi ya mtu hutegemea melanin. Vitiligo hutokea pale seli za kutengeneza melanin zinapokufa au zinapoacha kufanya kazi. Vitiligo huwapata watu wa rangi zote, lakini huweza kuonekana zaidi kwa watu wenye rangi nyeusi. Hii si hali inayohatarisha maisha wala kuambukiza. Inaweza kuwa ni hali inayochukiza au mtu akajisikia vibaya.

Tiba ya vitiligo inaweza kurudisha rangi ya ngozi iliyoharibiwa. Lakini, haiwezi kuzuia uharibifu wa rangi ya ngozi.

Chanzo Cha Vitiligo

vitiligo chanzo chake

Vitiligo hutokea wakati seli za kutengeneza rangi (melanocytes) zinapokufa au zinapoacha kufanya kazi ya kuzalisha melanin – pigmenti inayoipa ngozi yako, nywele na macho rangi. Sehemu zilizoathirika huwa angavu au nyeupe. Haijajulikana kiuhakika ni nini kinaachosababisha seli za pigmenti kufa au kuacha kufanya kazi. Yaweza kuwa inahusiana na:

. Matatizo ya ufanyaji kazi wa mfumo wa kinga za mwili (autoimmune condition)
. Historia ya familia (heredity)
. Tukio la kuanzisha, kama msongo wa mawazo, jua kali au kuumia kwa ngozi, kama kugusa kemikali.

Madhara Yatokanayo Na Vitiligo

Watu wenye vitiligo wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata:

. Msongo wa kijamii au wa kisaikolojia
. Kubabuka kwa jua
. Matatizo ya macho
. Matatizo ya kusikia.

Dalili Za Vitiligo

Dalili za vitiligo ni pamoja na:

. Mabaka ya ngozi iliyopoteza rangi, ambayo mara nyingi huanzia mikononi, usoni, na kuzunguka maeneo ya mwili yenye matundu na sehemu za siri.
. Kuota mvi kabla ya muda maeneo ya kichwani, kwenye kope, kwenye nyusi au ndevu
. Kupoteza rangi kwenye tishu zinazofunika eneo la ndani ya mdomo na pua (mucous membranes).

Vitiligo huweza kuanza kwenye umri wo wote, lakini mara nyingi huanza mtu akiwa na miaka chini ya 30.

vitiligo mdomoni

Kulingana na aina yake, vitiligo huweza kuathiri:

. Karibu maeneo yote ya ngozi. Aina hii, inayoitwa universal vitiligo, mabaka huenea karibu kwenye maeneo yote ya ngozi.

. Sehemu nyingi za ngozi. Kwenye aina hii ambayo ndiyo inayoonekana zaidi, na iitwayo generalized vitiligo, mabaka ya rangi huenea kwa kulingana kwenye maeneo ya mwili yanayohusiana (symmetrically).

. Upande mmoja au sehemu ya mwili. Aina hii, inayoitwa segmental vitiligo, ambayo hupenda kuonekana hasa kwenye umri mdogo, huongezeka kwa mwaka au miwili, kisha husimama.

. Sehemu moja au sehemu chache za mwili. Hii huitwa localized (focal) vitiligo.

. Uso na mikono. Kwenye aina hii, inayoitwa acrofacial vitiligo, ngozi inayoathiriwa ni ya kwenye uso na mikono, na kuzunguka matundu ya mwilini,  kama macho, pua na masikio.

Tiba Ya Vitiligo

Uchaguzi wa njia ya uponyaji hutegemea umri wako, kiasi cha ngozi kinachohusika na ni wapi, kasi ya kuenea ya ugonjwa wako, na jinsi unavyoathiri maisha yako.

vitiligo usoni

Kuna dawa na tiba nyepesi za kusaidia kurudisha rangi ya ngozi, ingawa matokeo hutofautiana na hayatabiriki. Baadhi ya tiba zina athari kubwa. Kwa hiyo daktari anaweza kukushauri ujaribu kwanza kubadilisha mwonekano wa ngozi yako kwa kutumia bidhaa ya kubadilisha rangi au makeup.

Kama daktari wako ataamua kukutibu kwa dawa au upasuaji, miezi kadhaa inaweza kupita kabla ya kuona matokeo. Pengine utahitaji kujaribu zaidi ya njia moja au mchanganyiko wa njia kabla ya kubaini tiba inayofanya vizuri kwako.

Hata kama njia moja itafanya kazi, matokeo si lazima yawe ya kudumu au mabaka mengine yanaweza kujitokeza. Daktari anaweza kushauri matumizi ya dawa ya kupaka juu ya ngozi ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa.

Dawa

Hakuna dawa ya kuzuia kuenea kwa vitiligo – kuharibika kwa seli za pigmenti (melanocytes). Lakini, baadhi ya dawa, zikitumika zenyewe, au zikiambatana na tiba nyepesi, zinaweza kurudishia kiasi cha rangi ya ngozi.

. Dawa za kuzuia madhara. Kutumia cream za corticosteroids kunaweza kurudisha rangi. Hizi zinafanya kazi vizuri kwenye hatua za mwanzo za vitiligo.
. Dawa zinazoathiri kinga za mwili. Hili ni kundi la dawa la Calcineurin inhibitor, kama tacrolimus au pimecrolimus.

Upasuaji

Mbinu kadhaa hutumika kufanya rangi ilingane

– Skin grafting
– Blister grafting
– Cellular suspension transplant

Tiba Mbadala

Utafiti mdogo umeoonyesha kuwa mmea wa Ginkgo biloba unaweza kurudisha rangi kwa mtu mwenye vitiligo. Utafiti mwingine umeonyesha kuwa alpha-lipoic acid (inayopatikana ndani ya yeast, maini, figo, spinachi, broccoli na viazi), folic acid, vitamin C na vitamin B-12 pamoja na phototherapy vinaweza kurudisha rangi ya mtu mwenye vitiligo.

Katika mada yetu nyingine, tutazungumzia chanzo cha ukurutu juu ya ngozi. Usisite kuuliza maswali uliyo nayo kuhusu uandishi wa mada hii yetu ya leo.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya saa za kazi   kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.