Vipindi Katika Mzunguko Wa Hedhi Ya Mwanamke

 

period

Mzunguko wa hedhi unaufanya mwili upitie hatua nyingi tofauti, zote zikiwa na lengo kuu moja. Mzunguko wa hedhi una kazi ya kuuandaa mwili kwa ujauzito unaoweza kutokea. Ni jambo la busara kujifunza kuhusu mzunguko wako wa hedhi ili uweze kuepukana na mimba zisizotarajiwa au kufanikisha upatikanaji wa mimba. Elimu hii itakusaidia kujibu maswali ambayo wengi hujiuliza, maswali kama; “Ni siku gani nzuri ya kupata mimba?” au “Siku za hatari za kupata mimba ni zipi?”

Kabla ya kuanza kujadili kuhusu mzunguko wa hedhi, tutazungumzia balehe, mimba na kisha tutalijadili kwa undani kidogo umbile la mfumo wa uzazi wa mwanamke.

Kubalehe

Kubalehe ni kufikia umri wa kuweza kuzaa. Msichana hubalehe anapofikia umri wa miaka 11, wengine huwahi au kuchelewa kidogo. Ni jambo la kawaida msichana kuanza kubalehe kati ya miaka 8 hadi 14. Balehe ni mlolongo wa mabadiliko unaochukua hadi miaka 4.

Dalili ya mwanzo ya balehe ni kuanza kuota matiti. Ni kawaida kabisa titi moja kuanza kuota miezi kadhaa kabla ya titi la pili. Mavuzi huanza kuota, na kwa baadhi ya wasichana, kunatokea mwongezeko wa nywele (malaika) kwenye mikono na miguu.

Mwaka mmoja au zaidi kidogo baada ya dalili za mwanzo za balehe na kwa kipindi cha kama miaka minne:

. matiti ya msichana huendelea kukua na kufikia kuwa makubwa kabisa
. kama miaka 2 baada ya kuanza balehe, msichana huanza kuona siku kwa mara ya kwanza
. mavuzi huwa magumu zaidi na ya mawimbimawimbi
. msichana hutoa jasho jingi zaidi
. wasichana wengi hupata chunusi
. wasichana hutokwa uchafu mweupe ukeni
. msichan hurefuka ghafla – msichana hurefuka kwa nchi 2 hadi 3 kwa mwaka katika mwaka mmoja au miwili toka alipoanza hedhi na kufikia ukomo wa kukua
. wasichana wengi hunenepa na kubadilika kimaumbile – hujenga nyama zaidi kwenye mikono, mapaja na maeneo ya shingo, maeneo ya nyonga huwa ya mviringo zaidi na viuno huwa vyembamba zaidi.

Baada ya miaka kama 4 ya kuanza balehe

. matiti huwa kama mtu mzima
. mavuzi huenea hadi kwenye maeneno ya ndani ya mapaja
. viungo vya uzazi huwa vimekua kabisa
. huacha kurefuka zaidi

Mimba

Hiki ni kipindi ambacho mtoto hukua ndani ya tumbo la mwanamke. Mwisho wa mimba waweza kuwa mtoto, abortion au mimba kuharibika. Mwisho wa mimba ni kama wiki 40 kuanzia hedhi ya mwisho. Kipindi hiki ni zaidi kidogo ya miezi 9 ya siku 31. Ukihesabu kuanzia kurutubishwa kwa yai, ni wiki 38. Dalili za awali za mimba ni pamoja na kukosa hedhi, maumivu kwenye matiti, kichefuchefu na kutapika, njaa, na haja ndogo ya mara kwa mara.

Tumbo La Uzazi 

Tumbo la uzazi (uterus) ni kiungo cha mfumo wa uzazi wa mwanamke kilichopo kati ya kibofu cha mkojo na rektamu. Kazi yake ni kutunza yai lililorutubishwa hadi hapo mtoto atakapokuwa tayari kuzalishwa.

uterus

Tumbo la uzazi lina sehemu kuu nne: fundus ni sehemu ya juu iliyojipinda ambapo mirija ya uzazi (fallopian tubes) inaungana na uterus; body, eneo la juu la uterus, linaanzia mara baada ya usawa wa mirija ya uzazi na kuendelea chini kwenye kuta za uterus na kisha mapana kuanza kupungua; isthmus, ni sehemu ya chini, yenye mapana madogo zaidi; na sehemu ya chini kabisa, cervix, ambayo inaungana na isthmus na kuelekea chini hadi kwenye tundu la uke. Uterus ina urefu wa sentimeta 6 hadi 8 (inchi 2.4 hadi 3.1) na unene wa sentimeta 2 hadi 3 (inchi 0.8 hadi 1.2). Upana wa uterus unatofautiana, huwa yapata sentimeta 6 kwenye fundus na kama nusu yake kwenye isthmus.Mfuko huu wa nyumba ya uzazi huishia kwenye tundu la uke na hivi viwili hufanya mkondo wa uzazi.

Juu ya mvungu wa tumbo la uzazi ni utando telezi (mucous membrane) unaoitwa endometrium ambao unene wake hubadilika wakati wa mzunguko wa hedhi, ukiwa mnene zaidi wakati yai linaachiwa na ovari . Yai lililorutubishwa hunata juu ya utando huu mnene wa uterus na kuanza kukua. Yai lisiporutubishwa, utando huu hubandua tabaka lake la juu, yai pamoja na tishu nyingine za ziada hutolewa nje wakati wa hedhi. Utando huu laini wa endometrium hutoa majimaji yenye kemikali ambayo husaidia kuliweka hai yai na mbegu za mwanamme. Majimaji haya huwa na maji, madini ya chuma, potassium, sodium, glucose na protini. Protini hulisaidia yai lililorutubishwa kunata juu ya uterus.

Mirija Ya Uzazi (Fallopian Tubes)

Mirija ya uzazi (fallopian tubes au uterine tubes) husafirisha mayai yaliyopevushwa (ova) kutoka kwenye ovari hadi kwenye nyumba ya uzazi. Kila mmoja wa mirija hii miwili una sehemu kuu tatu: Eneo la mwisho lenye umbo la faneli, au infundibulum; eneo la kati, ampulla; na eneo lililo kama kamba linaloishia kwenye nyumba ya uzazi, isthmus. Eneo la infundibulum lina maumbo yaliyochongoka yasiyo ya kawaida yaitwayo fimbriae. Fimbria moja ambayo ni kubwa kuliko nyingine huungana na ovari. Yai kwa kawaida hurutubishwa ndani ya ampulla. Kwa kawaida yai hili husafirishwa kuelekea kwenye nyumba ya uzazi, ingawa mara chache huweza ikatokea kuwa yai lililorutubishwa likanata kwenye ukuta wa eneo hili na kuanza kukua. Ujauzito wa namna hii huitwa ectopic pregnancy, au tubal pregnancy. Eneo hili haliweza kusaidia ukuaji wa mimba, hivyo madhara yatatokea,  mojawapo linaweza kuwa la kupasuka kwa mirija na kusababisha uvujaji wa damu.

Eneo kubwa la mirija ya uzazi hufunikwa na peritoneum. Ngozi yake ya ndani ina mikunjo kadhaa na hufunikwa na seli zenye vinywelea zinazotoa majimaji. Kujikamua kwa misuli, kucheza kwa vijinywelea (hairlike cilia) na kupita kwa ute huenda ndivyo vinavyosaidia mbegu kusafiri hadi kwenye ampulla na yai lililorutubishwa kusafiri kuelekea kwenye nyumba ya uzazi.

Ovari

Ovari mbili zinafanana na korodani katika mwili wa mwanamme na ni viungo vya kuzalisha seli za uzazi. Kila ovari ina urefu wa zaidi kidogo ya sentimeta 2.5 (inchi 1), mapana ya sentimeta 1.25 (1/2 inchi), lakini ukubwa habadilika na umri.

Eneo la ovari inapoingilia mishipa ya damu linaitwa hilum. Maeneo mengine muhimu ya ovari ni cortex na medulla. Cortex ni eneo mara baada ya ngozi inayofunika ovari, ambayo ndani yake kuna tunica albuginea, follicles na corpora lutea. Ovarian follicles ambazo mara nyingine huitwa graafian follicles, ni viungo vya mviringo ambavyo ndani yake mayai hukua. Msichana anaweza kuwa na follicles yapata 700,000 ndani ya ovari zake mbili.

Baada ya kuuelewa mfumo wa uzazi wa mwanamke, turejee kwenye mada yetu ya mzunguko wa hedhi. Yafaa kwanza tuyajue yafuatayo:

. Mzunguko wa hedi huanza siku ya kwanza damu inapoanza kutoka na unaisha siku hedhi inapoanza tena

. Ishara za homoni hupelekwa na kurudi kutoka kwenye ubongo na ovari, na kusababisha mabadiliko kwenye vifuko vya kwenye ovari vyenye mayai (follicles na kwenye nyumba ya uzazi (uterus)

. Sehemu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi huandaa yai liachiwe kutoka kwenye ovari na kujenga ukuta (utando laini) wa nyumba ya uzazi

. Sehemu ya pili ya mzunguko wa hedhi huandaa nyumba ya uzazi na mwili kulikubali yai lililorutubishwa, au kuuanza mzunguko mwingine endapo mimba haikutungwa.

Mzunguko wa hedhi huundwa na sehemu kuu mbili zinazoingiliana – moja ikitokea kwenye ovari na nyingine ndani ya nyumba ya uzazi. Ubongo, ovari, na nyumba ya uzazi hufanya kazi pamoja na kuwasiliana kupitia homoni (ishara za kemikali zinazopitishwa kupitia ndani ya damu kutoka sehemu moja ya mwili hadi nyingine) na kukamilisha mzunguko wa hedhi.

Mzunguko wa hedhi huchukua siku kati ya 24 na 38, mzunguko mmoja ukiweza kuwa na siku tofauti na mwingine, na unaweza kubadilika miaka ikisogea mbele. Urefu hubadilika kutoka mzunguko wa kwanza baada ya kuvunja ungo (menarche) na kukoma hedhi (menopause).

Kuwa na elimu ya mzunguko wa hedhi ni muhimu kwani hedhi huweza kuathiri mwili kuanzia kichwani hadi kwenye dole gumba la mguu. Watu wengine huona mabadiliko kwenye nywele, ngozi, dalili za magonjwa sugu, afya ya ubongo, kuumwa kichwa, namna ya kujisikia wakati wa tendo la ndoa nyakati tofauti wakati wa mzunguko.

Vipindi Katika Mzunguko Wa Hedhi

. Menstruation: Hedhi – utando laini juu ya nyyumba ya uzazi kubanduka na kutoka nje. Viwango vya estrogen na progesterone kuwa chini

. The follicular phase: Kipindi kati ya siku ya kwanza ya kuanza kutoka damu na yai kuachiwa (ovulation). Estrogen kupanda juu na yai kujiandaa kuachiwa

. The proliferative phase: Baada ya hedhi, utando laini juu ya uterus kuanza kujijenga upya

. Ovulation: Yai kuachiwa kutoka kwenye ovari, katikati ya mzunguko. Estrogen hufika kiwango chake cha juu kabisa na kushuka ghafla baada ya yai kuachiwa.

. The luteal phase: Kipindi kati ya kuachiwa kwa yai na kabla ya kuanza kwa mzunguko mpya, wakati mwili unajiandaa kwa mimba inayoweza kutungwa. Progesterone hutolewa, hufika kilele na kushuka.

. The secretory phase: Utando laini juu ya uterus hutoa kemikali ambazo au zitasaidia ukuaji wa mimba au zitaandaa kujibandua kwa utando huu na kutoka nje endapo mimba haikutungwa.

Sehemu Ya Kwanza Ya Mzunguko

Nyumba ya uzazi: Hedhi

Hii huanza siku ya kwanza damu inapoanza kutoka hadi inapoacha. Tishu za zamani za kwenye nyumba ya uzazi zinatoka nje kupitia uke.

Mzunguko wo wote wa hedhi huanza na kutoka damu. Hedhi ni kutoka kwa damu na utando laini wa juu ya nyumba ya uzazi (endometrium) nje kupitia cervix na uke. Muda wa kawaida ni hadi siku 8 lakini kwa wastani ni siku 5 hadi 6.

Ovari: Follicular phase:

Hiki ni kipindi kati ya mwanzo wa hedhi hadi kuachiwa kwa yai (ovulation.) Ishara kutoka kwenye ubongo huagiza ovari kuandaa yai litakaloachiwa.

Ndani ya kipindi hiki, tezi ya pitutary (eneo dogo chini ya ubongo linalotengeneza homoni) hutoa homoni iitwayo follicle stimulating hormone (FSH). FSH huziagiza ovari kuandaa yai kwa ajili ya kuachiwa. Inapofika nusu ya kipindi hiki, follicle (kifuko cha majimaji chenye yai) moja kutoka moja ya ovari huwa ni kubwa kuliko follicle nyingine zote (kama sentimeta 1). Follicle hii huwa ndiyo inayoandaliwa kutolewa wakati wa ovulation. Follicle hii hutoa homoni ya estrogen wakati ikikua, na hufikia kilele mara tu kabla ya yai kutolewa (ovulation). Kwa wanawake wengi kipindi cha follicular hudumu siku 10-22, lakini muda huweza kubadilika kutoka mzunguko mmoja hadi mwingine.

Uterus: Proliferative phase

Hiki ni kipindi cha kati ya kumaliza hedhi na kuachiwa yai (ovulation). Wakati huu tumbo la uzazi (uterus) hujenga utando mnene juu yake.

Wakati ovari zinafanya kazi ya kukuza vijifuko vyenye mayai (follicles), uterus inafuata ishara za estrogen inayotengenezwa kwenye follicles, na kujenga upya utando ulioondolewa kwenye hedhi iliyopita. Hiki kipindi kinaitwa proliferative phase kwa sababu utandao (endometrium) huwa nene zaidi. Endometrium huwa nyembamba zaidi wakati wa hedhi, na kukua zaidi na zaidi ndani ya kipindi hiki hadi yai linapoachiwa. Uterus hufanya kazi hii ili kuweka nafasi ambapo yai likalorutubishwa litaweza kunata na kukua.

Pumziko: Ovulation – Yai Kuachiwa

Karibu katikati ya mzunguko wa hedhi. Kuachiwa kwa yai hugawa sehemu mbili za mzunguko wa ovari, follicular phase na luteal phase.

Yai linaachiwa na ovari na kuingia ndani ya fallopian tube (mrija wa uzazi).

Ile follicle kubwa kuliko zote inazalisha estrogen zaidi na zaidi kadiri inavyokua. Follicle hii hufikia ukubwa wa karibu sentimeta 2 – lakini yaweza kufika sentimeta 3 – ikifikifia ukomo kabla ya kuachia yai. Viwango vya estrogen vikifikia viwango vya juu vya kutosha, vinatoa ishara kwenye ubongo na kusababisha mwongezeko wa juu na wa kasi wa luteinizing hormone (LH.) Mfumuko huu wa LH ndiyo unaosababisha yai kuachiwa. Kwa kawaida yai huachiwa siku 13 hadi 15 kabla ya hedhi inayofuata.

Sehemu Ya Pili Ya mzunguko

Ovari: Luteal phase

Kuanzia siku yai linapoachiwa hadi mwanzo wa hedhi ya pili. Mfuko uliokuwa na yai unazalisha estrogen na progesterone.

Baada ya yai kuachiwa, follicle iliyokuwa na yai hugeuka kuwa corpus luteum na huanza kuzalisha progesterone pamoja na estrogen. Progesterone hufikia kiwango cha juu katikati ya kipindi hiki. Mabadiliko ya homoni katika kipindi hiki ndiyo yanayosababisha dalili mbambali ambazo wanawake huzipata kabla ya hedhi; kama, mabadiliko ya kitabia, kuumwa kichwa, chunusi, na maumivu kwenye matiti.

Kama yai litapevushwa, progesterone kutoka kwenye corpus luteum itasaidia kwenye hatua za mwanzo za ujauzito. Kama yai halitarutubishwa, corpus luteum itaanza kujivunjavunja siku 9 hadi 11 baada ya yai kuachiwa. Hii itasababisha viwango vya estrogen na progesterone kushuka, na kusabibisha hedhi.

Wakati homoni ya estrogen ni muhimu, progesterone ni ya muhimu zaidi katika kipindi hiki. Progesterone ina shughuli nyingi, ikiwa ni pamoja na:

. Kuzuia utendaji kazi wa GnRH, FSH, na LH: homoni ambazo huamsha ovari na kusababisha yai kutolewa, vinginevyo mwanamke anaweza kupata ujauzito tena wakati tayari ni mjamzito.

. Kuiandaa endometrium: progesterone huiamuru endometrium kutoa aina fulani ya protini, ambazo hulisha embryo.

. Kuzuia hedhi: progesterone huzuia ngozi laini inayotanda juu ya endometrium isibanduke, tendo ambalo lingeweza kusababisha kutoka kwa mimba (miscarriage) kama mwanamke ana ujauzito

Progesterone husababisha joto la mwili kupanda. Joto la mwili wa mwanamke hupanda mara baada ya ovulation. Mwanamke akipata ujauzito, joto la mwili litabaki juu kipindi chote cha luteal na kuendelea baada ya hapo. Kama hakuna ujauzito, joto la mwili litaanza kushuka kabla ya kuanza hedhi. Kushuka kwa progesterone kutashusha joto na kuruhusu hedhi.

Luteal Phase Huwa Ina Urefu Gani ?

Kwa wastani, luteal phase hudumu siku 12 hadi 14. Lakini yaweza kuwa fupi ya siku 8 au ndefu ya kufikia siku 16. Urefu wo wote ulio wa kawaida kwa mwili wako, huwa ni wa kujirudiarudia katika mzunguko wako wa hedhi.

Mathalani, mwanamke mwenye urefu wa kawaida wa siku 12, huchukua siku 11 hadi 13. Endapo urefu utazidi siku 13, basi mojamoja huwa ni dalili ya ujauzito.

Urefu wa siku pungufu ya 8 (au 10), huashiria matatizo ya uzazi, ingawa si lazima. Wakati wanawake wengi wanaohangaika kupata ujauzito au wenye matatizo ya mimba kuharibika huwa na luteal phase fupi ingawa si ajabu pia kuona mwanamke mwenye afya nzuri akawa na luteal phase fupi.

Uterus: Secretory Phase

Kuanzia yai linapoachiwa hadi mwanzo wa hedhi nyingine. Utando juu ya uterus unaachia kemikali ambazo au zitasaidia ujauzito kama yai limerutubishwa au kusaidia utando kuvunjika na kutoka nje kama yai halikurutubishwa.

Wakati wa kipindi hiki, endometrium inajiandaa au kusaidia ujauzito au kuvunjika na kutoka nje. Kuongezeka kwa kiwango cha progesterone kunasimamisha unenepaji wa endometrium na kuanza kujiandaa kwa kunata kwa yai ambalo litakuwa limerutubishwa. Jina la secretory phase linatokana na endometrium kutoa (secrete) aina mbalimbali za wajumbe wa kikemikali. Wajumbe wanaofahamika zaidi ni prostaglandins, ambao hutolewa na seli za endometrium na kuleta mabadiliko kwenye seli za karibu.

Prostaglandins mbili za muhimu zinazoitwa PGF2a Na PGE2, husababisha misuli ya uterus kujikamua. Viwango vya prostaglandins hizi mbili huongezeka baada ya yai kuangushwa na kufikia kilele wakati wa hedhi. Kujikamua kunakotokana na prostaglandins hizi husaidia kuanzisha hedhi.

Katika mada yetu nyingine tutazijadili sababu za mwanamke kukosa mtoto au ugumba kwa mwanamke. 

Usisite kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo au kuuliza maswali uliyo nayo. Furaha yetu ni kuona kuwa umeielewa vizuri mada yetu.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.