Kuziba Kwa Mirija Ya Uzazi; Ufahamu Ugonjwa wa Salpingitis

 

salpingitis bango

 

 

Mirija ya uzazi (fallopian tubes) huanzia kwenye nyumba ya uzazi (uterus) na kwenda pande zote mbili hadi kwenye ovari. Yai lililoachiwa huingia kwenye mirija ya uzazi na kusukumwa na vijinywele vidogo kuelekea kwenye nyumba ya uzazi.

Salpingitis ni mashambulizi ya mirija ya uzazi. Mashambulizi haya mara nyingi ni ya bakteria, yakijumuisha yale yanayotokana na ngono kama gonorrhoea na chlamydia. Mashambulizi haya husababisha majimaji ya ziada au hata usaha kujazana ndani ya mirija ya uzazi. Mashambulizi ya upande mmoja huweza kuhamia hupande wa pili.

 

 

fallopian tube

 

Salpingitis ni ugonjwa unaochangia kwa kiwango kikubwa kwenye tatizo la ugumba kwa wanawake. Tatizo lisipotibiwa kwa wakati, mirija ya uzazi huweza kuharibiwa kabisa na kusababisha mayai yanayoachiwa wakati wa mzunguko wa hedhi kushindwa kukutana na mbegu za kiume. Makovu na kuziba kwa mirija ya uzazi ni moja ya matokeo ya kudumu ya mashambulizi ya maeneo ya pelvis, hali ambayo huitwa Pelvic Inflammatory Disease (PID). PID ni neno la jumla la kuelezea mashambilizi ya viungo vya uzazi vya mwanamke, likihusisha mashambulizi ya uterus na ovari.

 

Dalili Za Salpingitis

 

Katika hatua za mwanzo, salpingitis inaweza isionyeshe dalili zo zote. Hii ina maana kuwa mirija ya uzazi inaweza kuendelea kuharibika bila mwanamke kujua kuwa ana maambukizo. Dalili za salpingitis zinaweza kuwa:

. Uchafu ukeni usio wa kawaida, kama harufu au rangi isiyo ya kawaida
. Maummivu wakati wa hedhi
. Maumivu wakati mayai yakiachiwa
. Maumivu wakati wa tendo la ndoa
. Homa
. Maumivu ya tumbo, pande zote mbili
. Maumivu ya mgongo, sehemu ya chini
. Haja ndogo mara kwa mara
. Kichefuchefu na kutapika
. Dalili kutokea baada ya hedhi

Salpingitis huwekwa kwenye makundi mawili, acute na chronic. Salpingitis ikiwa ni acute, mirija ya uzazi huwa myekundu, iliyovimba na hutoa majimaji hivi kwamba kuta za ndani hukamatana. Mirija inaweza pia kukamatana na viungo vingine kama utumbo. Wakati mwingine mirija hujaa usaha. Mara chache, mirija huweza kupasuka na kusababisha maambukizo mabaya kwenye uvungu wa tumbo (peritonitis). Chronic salpingitis hufuatia acute salpingitis. Maambukizo huwa siyo makali sana, huchukua muda mrefu na pengine kusiwe na dalili zo zote.

 

Chanzo Cha Salpingitis

 

Kati ya watu 10 wenye salpingitis, 9 huwa wameathiriwa na bakteria. Bakteria wanaohusika zaidi na salpingitis ni:

. chlamydia
. gonococcus
. mycoplasma
. staphylococcus
. streptococcus

Bakteria hawa ni lazima wawe wameingia kwenye viungo vya uzazi vya mwanamke na njia zifuatazo zaweza kuhusika:

. kujamiiana
. kupenyeza kifaa cha IUD (intra-uterine device)
. mimba kuharibika
. kutoa mimba
. uzazi
. appendicitis

 

Madhara Yatokanayo Na Salpingitis

 

Bila tiba, kuna madhara mengi yanayoweza kutokea, ikiwa ni pamoja na:

 

 

. Maambukizi ya ziada – maambukizi yanaweza kusambaa hadi kwenye ovari, uterus, n.k.
. Kuwaambukiza wenza -wenza wa mwanamke wanaweza nao kuambukizwa
. Tubo-ovarian abscess – asilimia 15 ya wanawake wenye salpingitis hujenga uvimbe wenye usaha
. Ectopic pregnancy – Mrija wa uzazi ulioziba huzuia yai lililorutubishwa kuingia kwenye nyumba ya uzazi (uterus). Yai linalokua (embryo) huendelea kukua kwenye nafasi finyu ndani ya mirija ya uzazi. Uwezekano wa mwanamke mwenye salpingitis au tatizo jingine la PID kupata ujauzito wa namna hii ni hadi asilimia 20.
. Ugumba -Mrija wa uzazi huweza kupoteza umbo lake au ukawa na makovu kiasi kwamba yai la mwanamke na mbegu za mwanamme vikashindwa kukutana. Kuugua mara moja salpingitis kunaongeza ugumba kwa mwanamke kwa asilimia 15. Asilimia hupanda hadi 50 mwanamke akiuugua salpingitis mara 3.

 

Tiba Ya Salpingitis

 

Tiba ya salpingitis hutegemea ukubwa wa tatizo, lakini inaweza kuwa:

. Antibiotics – ili kuwaua wadudu, ambayo hufaaa kwa asilimia 85. Yafaa pia washiriki wa kimapenzi wa mwanamke kupata tiba.
. Kulazwa – ili kupewa dawa kupitia mishipa ya damu
. Upasuaji – Kama salpingitis imetunga usaha, daktari anaweza kufanya upasuaji wa laparoscopy ili kuuondoa. Na kama salpingitis imeweka makovu au kujaza maji kwenye mirija ya uzazi, daktari anaweza kufanya upasuaji kuondoa eneo lililoathirika, hasa kama mwanamke bado anahitaji kupata watoto.

Katika mada yetu nyingine tutalizungumzia tatizo la high blood pressure. Usisite kuuliza maswali uliyo nayo au kutoa ushauri kuhusu mada yetu ya leo.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.