Ni Nini Chanzo Cha Kipandauso (Migraine)?

 

 

 

Kipandauso (migraine) huweza kusababisha kichwa kugonga kikiambatana na maumivu makali. Mara nyingi ikiwa ni upande mmoja wa kichwa. Mara nyingi kipandauso huambatana na kichefuchefu, kutapika, ganzi, na hali ya juu ya kutopenda mwanga au sauti. Kipandauso hudumu kwa saa kadhaa au siku kadhaa, na maumivu huweza kuwa makali hivi kwamba ukashindwa kuendelea na shughuli zako za kila siku. Kipandauso kwa kawaida hushambulia baadhi ya koo (tatizo la kurithi) na huwapata watu wa rika zote. Kipandauso huweza kuanza utotoni au kikatokea miaka ya balehe. Wanawake husumbuliwa na kipandauso zaidi ya wanaume.

Baadhi ya watu hupata kiashiria (aura) kama baridi ya ghafla na ya muda mfupi au mwanga mkali wa ghafla kabla au vikiambatana na maumivu ya kichwa. Kiashiria kinaweza kuambatana na matatizo katika kuona, kama miale ya mwanga au madoa meusi, au mara nyingine usumbufu wa aina nyingine, kama vitu kutembea upande mmoja wa uso au kwenye mkono au mguu na matatizo katika kuzungumza.

Dawa zina uwezo wa kuzuia baadhi ya aina za kipandauso na kupunguza maumivu. Dawa sahihi, zikiambatana na hatua za kujisaidia binafsi pamoja na utaratibu mzuri wa kuishi, vinaweza kusaidia zaidi.

Dalili Za Kipandauso

Dalili za kipandauso huanza kuonekana siku moja au mbili kabla ya maumivu ya kichwa kutokea. Kipindi hiki kitalaamu huitwa prodrome stage. Dalili katika kipindi hiki ni pamoja na:

 

. Kupenda kulakula
. Mfadhaiko
. Uchofu au nguvu za mwili kupungua
. Chafya mara kwa mara
. Uchangamfu wa kuzidi
. Kukasirika haraka
. Shingo kukaza

 

Ikiwa kipandauso ni chenye kiashiria (aura),  kiashiria cha kipandauso hutokea baada ya kipindi cha prodrome. Wakati wa kiashiria, unaweza kupata matatizo ya kuona, usikivu, miondoko, na usemaji. Mifano ya matatizo hayo ni kama:

. shida kuzungumza vizuri
. vitu kutembea usoni, mikononi, au miguuni
. kuona maumbo, miale ya mwanga, au madoa meusi
. vipindi vifupi vya kupoteza uonaji

Hatua ya pili huitwa attack phase. Hii ndiyo hatua mbaya ya zote kwani hapa maumivu halisi ya kipandauso hutokea. Kwa baadhi ya watu, vipindi hivi huweza kuingiliana. Kipindi cha maumivu huweza kudumu saa kadhaa au siku kadhaa. Dalili za kipandauso hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Nazo zaweza kuwa:

. Kuongezeka kwa hali ya kutopenda mwanga mkali au sauti
. Kichefuchefu
. Kizunguzungu au kujisikia kuzirai
. Maumivu ya upande mmoja wa uso, kushoto au kulia, mbela au nyuma ya kichwa, upande wa kulia au wa kushoto wa paji la uso
. Kugonga kichwa
. Kutapika

Baada ya hatua hii ya maumivu makali, mara nyingi mtu huingia kwenye hatua iitwayo postdrome phase. Katika hatua hii mtu huona mabadiliko kwenye hisia zake na jinsi anavyojisikia. Mtu huweza kujisikia mwenye uwingi wa furaha, au kujisikia mchovu sana na asiyependa cho chote. Kuumwa kichwa kwa mbali kunaweza kuendelea.

Urefu na ukali wa kila hatua hutofautiana baina ya mtu na mtu. Wakati mwingine hatua moja inaweza kurukwa na vile vile inaweza kikatokea kipandauso bila maumivu.

Kipandauso Husababishwa Na Nini?

Watafiti bado hawajaweza kutambua chanzo halisi cha kipandauso. Lakini wameweza kubaini baadhi ya vitu vinavyoweza kuchangia kuileta hali hiyo. Hivyo ni pamoja na mabadiliko ya kemikali ndani ya ubongo, kama kupungua kwa kiwango cha kemikali ya ubongo iitwayo serotinin.

Baadhi ya sababu nyingine zikiwa ni:

. mwanga mkali
. joto kali, au hali mbaya ya hewadalili za kipandauso
. upungufu wa maji mwilini
. mabadiliko ya mgandamizo wa hali ya hewa
. mabadiliko ya homoni kwa wanawake, kama kushuka na kupanda kwa estogen na progesterone wakati wa hedhi, ujauzito, au kukoma hedhi
. msongo mkali wa mawazo
. sauti za juu
. kufanya kazi ya nguvu
. kuruka milo
. kubadili ratiba ya kulala
. matumizi ya baadhi ya kemikali, kama dawa za kuzuia mimba
. harufu zisizo za kawaida
. baadhi ya chakula
. uvutaji wa sigara
. unywaji wa pombe.

Chakula Kiletacho Kipandauso

Baadhi ya chakula au viungo vya chakula vinaweza kuchochea kipandauso kuliko vingine. Vyakula hivyo ni pamoja na:

. Chakula chenye kilevi au kahawa
. Viungo vya chakula, kama nitrates (zitumikazo kuhifadhi nyama isioze), aspirtame (namna ya sukari), au monosodium glutamate (MSG)
. tyramine

Tyramine ni kitu kipatikanacho ndani ya baadhi ya chakula. Tyramine huongezeka ndani ya chakula kilichochachushwa au cha zamani, kama jibini ya zamani, sauerktraut na soya.

Aina Za Kipandauso

Kuna aina nyingi za kipandauso. Aina kuu mbili ambazo zinaonekana zaidi ni kipandauso bila kiasharia (migraine without aura) na kipandauso chenye kiashiria (migraine with aura). Baadhi ya watu wana aina zote hizi mbili.

Watu wengi wenye tatizo la kipandauso wana aina zaidi ya moja ya kipandauso.

Kipandauso Bila Kiashiria (Migraine Without Aura)

Kipandauso cha aina hii zamani kiliitwa common migraine. Watu wengi wenye kipandauso hawakuona kiashiria.

Watu wenye kipandauso kisicho na kiashiria huwa wamepatwa na angalau mashambulio matano yenye tabia zifuatazo:

. Maumivu y a kichwa yaliyodumu saa 4 hadi saa 72 kama tiba haikutolewa au kama tiba haikufanya kazi
. Maumivu ya kichwa yenye angalau tabia mbili kati ya hizi:

> maumivu yaliyopo upande mmoja tu wa kichwa
> maumivu ya kugonga
> maumivu ya kadiri au makali
> maumivu yanayozidi ukitembea, au ukipanda ngazi

. Maumivu ya kichwa yenye angalau tabia moja ya hizi:

> maumivu yanayokufanya uwe na hisia za juu za mwanga (photophobia)
> maumivu yanayokufanya uwe na hisia za juu za sauti (phonophobia)
> kama unajisikia kichefuchefu kikiambatana na kutapika au bila kutapika au kinachoambatana na kuharisha

Kipandauso Chenye Kiashiria (Migraine With Aura)

Aina hii ya kipandauso pia iliitwa classic migraine, complicated migraine, na hemiplegic migraine. Aina hii huwapata asilimia 25 ya watu wenye kipandauso.

Kipandauso cha aina hii ni kile ambacho kina tabia tabia zifuatazo katika angalau mashambulio yake mawili:

. Kiashiria kinachokuja na kupita, ambacho kinaweza kujirudia, na kina angalau dalili moja katika zifuatazo:

> matatizo ya kuona (kiashiria kinachojitokeza zaidi)
> matatizo ya usikivu katika mwili, uso, au ulimi, kama ganzi, vitu kucheza au kizunguzungu
> matatizo ya kuzungumza au lugha
> Matatizo ya kutembea au udhaifu, ambayo yanaweza kudumu hadi saa 72
> dalili zinazoanzia kwenye ubongo, kama:

> shida katika kuzungumza au mazungumzo yasiyoeleweka vizuri (dysarthria)
> vertigo (kuona vitu vikizunguka)
> sauti masikioni (tinnitus)
> shida kusikia (hypacusis)
> kuona vitu viwiliviwili (double vision)
> shida kudhibiti miondoko ya mwili (ataxia)
> upungufu wa ufahamu (decreased consciousness)

>  Matatizo ya macho katika jicho moja, pamoja na miale ya mwanga, madoa meusi, au kutoona kwa vipindi vifupi (retinal migraines)

Kipandauso Na Ujauzito

Kwa wanawake walio wengi, kipandauso hupungua pale wanapokuwa na ujauzito. Lakini, hali huweza kubadilika pindi wanapokuwa wamejifungua kwa sababu ya mabadiliko ya ghafla ya homoni.

Utafiti mdogo umeonyesha kuwa wanawake wenye tatizo la kipandauso wakiwa wajawazito wanakuwa na hatari kubwa ya:

. kuzaa kabla ya wakati
. kuzaa watoto wenye uzito mdogo
. kupatwa na pressure na matatizo ya figo.

Tiba Ya Kipandauso

Kipandauso hakina dawa ya kukiondoa, lakini tabibu anaweza kukushauri namna ya kukizuia au kutibu dalili zilizotokea. Tiba inaweza pia kupunguza makali ya kipandauso kinachokupata.

Kama unapatwa na kipandauso mara kwa mara, unaweza kutumia dawa za kuondoa maumivu. Hakuna dawa moja ambayo imeonekana kuwa bora kuliko nyingine. Fanya utafiti wako mwenyewe na kuona dawa ipi inakufaa zaidi.

Kuna baadhi ya virutubishi ambavyo vimethibitishwa kuwasaidia watu wenye kipandauso. Navyo ni:

. Mmea wa feverfew
. Magnesium
. Coenzyme Q10
. Vitamini B: B2 (riboflavin), B6 (pyridoxine), na B12 (cobalamin), B9 (folic acid)
. Vitamini E.

Yafaa kuwa mwangalifu usitumie virutubishi vingi kupita kiasi. Vitamini B6 yaweza kuwa sumu ikitumiwa kwa wingi mno.

Ufanye Nini Ukipatwa na kipandauso?

kipandauso kitambaa baridi

Jaribu haya endapo umepatwa na kipandauso:

. Lala chini ndani ya chumba kisicho na kelele, chenye giza
. Kanda ngozi ya kichwa au maeneo ya pembeni mwa paji la uso
. Weka kitambaa baridi juu ya paji la uso au nyuma ya shingo yako.

 

Katika mada yetu nyingine tutazungumizia tatizo la kifafa. Usisite kutoa maoni yako au kutuuliza swali lo lote kuhusu mada hii yetu ya leo.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.