Ni Nini Maana Ya Panic Attack? Utakabiliana Vipi Na Panic Attack?

 

panic attack ushauri

 

“Ghafla nilisikia wimbi la hofu likitambaa mwilini bila sababu yo yote ile. Moyo wangu ulienda kasi sana, kifua kiliuma na ikawa inazidi kuwa ngumu zaidi kupumua. Nilifikiri kuwa muda wangu wa kufa ulikuwa umewadia.”

Hii ni mfano wa sentensi inayotoka kinywani mwa mtu mwenye tatizo la panic attack. Panic attack inaweza kuelezewa kuwa ni kipindi kifupi cha mtu kukamatwa na hofu kubwa na wasiwasi vinavyokuja ghafla. Moyo ghafla unakwenda mbio na unashindwa kupumua. Unaweza pia kufikiria unakufa au unapata wazimu.

Panic attacks huja bila sababu na huja bila kutoa ishara. Panic attacks huweza kutokea wakati umejipumzisha au hata wakati umelala.

Panic attack ni kitu kinachoweza kukutokea mara moja tu katika maisha, lakini watu wengi hurudiwa na vipindi vya mishtuko ya hofu na wasiwasi. Panic attacks zinazojirudia mara nyingi husababishwa na mazingira fulani, kama kuvuka daraja au kuzungumza mbele ya kadamnasi – na hasa kama mazingira hayo yalikwisha sababisha panic attack siku za nyuma. Kwa kawaida mazingira yanayosababisha panic attack ni yale yanayokufanya ujisikie kuwa upo hatarini na huna jinsi ya kujinasua.

 

 

panic attack visababishi

 

 

 

Tatizo la kupata vipindi vya kukamatwa na panic attack linawagusa watu wengi katika vipindi fulani vya maisha yao, idadi ya wanawake ikiwa mara mbili ya ile ya wanaume. Umri ambapo watu wengi hupatwa na panic attack kwa mara ya kwanza ni ule wa kati ya miaka 15 na 19. Panic attacks huja ghafla na mara nyingi haziwezi kutegemewa, huja bila kisababishi na humfanya mtu ashindwe kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Uchunguzi unaoyesha kuwa asilimia 0.7 ya watoto wadogo hushikwa na tatizo la panic attack, ikiwa kama nusu ya utokeaji wa tatizo hilo kwa  vijana wa umri wa balehe. Pamoja na kwamba kwa watu watu wazima tatizo huwa kubwa zaidi kwa wanawake, mara mbili ya lile la wanaume, wasichana na wavulana wanaonekana kupatwa na shida hii kwa viwango vinavyolingana.

Mtu akishakuwa alishikwa na panic attack mara moja, kwa mfano, akiwa anaendesha gari, ananunua bidhaa ndani ya duka kubwa lenye watu wengi, au akiwa ndani ya lifti, anaweza kujenga woga wa kutopenda kitu fulani (phobia), na akaanza kukwepa mazingira ya vitu hivyo vinavyomwogofya. Hatimaye, ukwepaji huu na kiwango cha wasiwasi anachokipata kuhusu kutokewa tena na kipindi cha kukamatwa na hofu vinaweza kufikia kiwango ambapo lile wazo tu la kuyarudia mazingira yaliyomsababishia tatizo kwa mara ya kwanza, likaweza kumsababishia panick attack. Hali itafikiwa ambapo sasa mtu huyu mwenye tatizo hili hatoweza kuendesha tena gari au kutoka nje ya nyumba yake. Hii huitwa agoraphobia. Kwa hiyo kuna aina mbili za matatizo ya hofu za ghafla. Hofu za ghafla zenye agoraphobia na hofu zisizo na agoraphobia. Kama ilivyo kwa matatizo mengine yanayohusu akili ya binadamu, hofu za ghafla zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa maisha ya kawaida ya mgonjwa kama hatopata tiba ifaayo.

Panic attacks kwa watoto huchangia kushuka kwa uwezo wa mtoto darasani, kukataa kwenda shule na kujitenga na wazazi wake, na hata kujisikia upweke, kupata mfadhaiko, mawazo na plani za kujiua.

Panic attacks ni hali halisi zinazoweza kutokea na zina uwezo mkubwa wa kuvuruga hisia za mtu. Bahati nzuri kuna tiba mahsusi za kuweza kumsaidia mwathirika. Kwa sababu ya dalili zinazousumbua mwili, panic attacks mara nyingi huchanganywa na tatizo la mshituko wa moyo au magonjwa mengine hatarishi kwa maisha. Inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya watu wanaomwona daktari kwa maumivu ya vifua, huwa wana matatizo ya panic attacks. Hii husababisha mara nyingi mtu kupitia vipimo vikubwa sana ili kujiridhisha juu ya matatizo mengine kwanza. Kibaya zaidi, asilimia 90 ya watu hawa hawapati majibu sahihi kuwa tatizo lao ni panic attacks.

Pamoja na kuwa panic attacks zinaweza kuwa mbaya sana, hazileti uharibifu wa viungo vya mwili. Kwa hiyo moja ya njia ya kuitumia katika kumsaidia mwathirika ni kumhakikishikia kuwa kinachotokea hakina madhara kwa maisha yake na kuwa kinaweza kupata tiba kamilifu.

 

Chanzo Cha Panic Attacks Ni Nini, Na Vitu Gani Vinavyochangia?

 

Pamoja na kuwa hakuna sababu maalumu ya panic attacks kwa watu wazima, vijana na watoto, kama ilivyo kwa matatizo mengine ya kihisia, inasadikika kuwa panic attacks ni matokeo ya mchanganyiko wa vihatarishi vya kibayolojia, namna ya kufikiri, na vitu vingine vya kwenye mazingira kama matatizo ya kijamii.

Panic attacks zinaokekana pia kuwa ni tatizo la kurithi. Kuna uhusiano pia wa panic attacks na mapito muhimu katika maisha kama kumaliza chuo na kuingia kwenye ajira, kuoa au kuolewa na kupata mtoto. Misongo ya mawazo mikubwa, kama kufiwa na mtu wa karibu sana, kuvunjika kwa ndoa, kuachishwa kazini vinaweza pia kusababisha panic attacks. Panic attacks zinaweza kusababishwa na matatizo ya kiafya.

 

Dalili Za Panic Attacks Kwa Watu Wazima, Vijana Na Watoto Ni Zipi?

 

Viashiria na dalili za panic attack hutokea ghafla na hufika kileleni katika dakika 10. Panic attacks nyingi huisha katika dakika 20 hadi 30, mara chache huchukua zaidi ya saa moja.

Dalili na viashiria vya panic attack

. Kushindwa kupumua vizuri au kupumua kwa haraka
. Moyo kwenda kasi
. Maumivu ya kifua
. Kutetemeka
. Kubanwa pumzi
. Kujisika upo kwenye ulimwengu mwingine
. Kuvuja jasho
. Kichefuchefu au tumbo kuchafuka
. Kizunguzungu au kuzimia
. Kufa ganzi
. Kusikia joto kali
. Wasiwasi wa kufa au kupata wazimu

 

Panic Disorder

 

Kama tulivyosema awali, watu wengine hupatwa na panic attack mara moja, bila kujirudia baadaye wala kupata madhara. Huna haja ya kuwa na wasiwasi kama umepata panic attack mara moja au mara mbili. Lakini watu wengine waliopata panic attacks huendelea na kujenga panic disorder. Panic disorder hutambuliwa kwa panic attacks endelevu, zikiambatana na mabadiliko katika tabia ya mtu, au wasiwasi usioisha kuhusu kupatwa na panic attacks nyingine.

Utamtambuaje Mtu Mwenye Panic Disorder?

Unaweza kuwa unasumbuliwa na panic disorder endapo utaona yafuatayo:

> Unapatwa na mishtuko ya hofu na wasiwasi ya mara kwa mara ambayo haihuishwi na mazingira yo yote yale.

> Unakuwa na wasiwasi wa kupatwa na mishtuko mingine ya hofu na wasiwasi.

>Umekuwa na tabia ya kitofauti kutokana na panic attacks, kama kukwepa mazingira ambayo yalikusababishia kupata mshituko wa hofu na wasiwasi.

 

 

panic attack

 

 

Pamoja na kuwa mshituko mmoja wa hofu na wasiwasi unachukua dakika chache, matokeo ya mwonjo huo yanaacha kumbukumbu ya kudumu. Kama una panic disorder, panic attacks zinazojirudiarudia huathiri hisia zako. Kumbukumbu kuhusu woga mkubwa na hatari unazohisi unapokumbwa na mshtuko wa hofu vinaweza kuathiri namna yako ya kujiamini na kuharibu kabisa mwenendo wako wa maisha. Mwishowe, hali hii huleta dalili zifuatazo za panic disorder:

– Badala ya kutulia na kujipenda muda wa katikati ya mishtuko, unakuwa mtu mwenye wasiwasi na mawazo. Wasiwasi hutokana na woga wa kupatwa na panic attacks. ” Woga huu wa woga” unakuwa nao muda wote na huweza kukuvurugia kabisa shughuli zako. Kiutaalamu hali huitwa “Anticipatory anxiety”.

– Unaanza kukwepa baadhi ya vitu au mazingira. Ukwepaji huu unaanzia kwenye imani kuwa mazingira unayoyakwepa ndiyo yaliyokusababishia panic attacks za mwanzo. Au, unaanza kukwepa maeneo ambayo unafikiri kujinasua itakuwa ngumu au utakosa msaada kama utapatwa na panic attack. Kila siku utakwepa vitu zaidi. Kwa mfano, utaanza kukwepa maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama shopping malls au viwanja vya michezo. Utakwepa pia magari, ndege, vituo vya treni, na njia nyingine za usafiri. Mwishowe utaona kuwa unakuwa salama pale tu unapokuwa nyumbani kwako. Kiutaalamu, hii huitwa “Phobic avoidance”. Hali hii ikizidi huishia kuwa agoraphobia.

 

Vitu Binafsi Unavyoweza Kuvifanya Ukiwa Na Tatizo La Panic Attacks

 

Hapa chini ni baadhi njia za kuzitumia ikiwa tayari umeshikwa na panic attack au ukihisi unanyemelwa:

1. Kuvuta Pumzi

Kuhema kwa haraka ni moja ya dalili za panic attacks inayoweza kuongeza hofu, kuvuta pumzi kwa nguvu kunaweza kupunguza hofu wakati umeshikwa na panic attack. Kama unaweza kudhibiti upumuaji wako, unaweza kupunguza mihemuko ambayo huleta dalili nyingine – pamoja na panic attack yenyewe.

Zingatia kuvuta hewa ndani kwa nguvu na kutoa nje kupitia kinywa chako, ukisikilizia hewa inavyojaza kifua na tumbo lako taratibu halafu taratibi itoe nje. Vuta pumzi ndani kwa nguvu ukihesabu hadi nne, ibane kwa sekunde moja, halafu itoe nje taratibu ukiwa unahesabu tena hadi nne.

2. Tambua Kuwa Una Panic Attack

Ukitambua kuwa una panic attack na si mshituko wa moyo, unaweza kujikumbusha kuwa hicho ni kitu cha muda mfupi, kinachopita, na hakiwezi kukuletea madhara ya mwili. Ondoa woga kuwa utakufa au kuwa kuna jambo kubwa linakuja. Hii itakusaidia kuendelea na njia nyingine za kuikabili panic attack na kupunguza makali yake.

3. Funga Macho Yako

Panic attacks nyingine huamshwa na vitu ambavyo vinauzidi uwezo wako. Kama upo kwenye mazingira yaliyojaa viamshi, panic attack hupata nguvu. Kupunguza viamshi, funga macho yako wakati umeshikwa na panic attack. Hii itaziba viamshi vya ziada na kukuacha uweze kutuliza mawazo kwenye upumuaji wako.

 

panic attack msongo

 

4. Jenga Tabia Ya Uzingatifu

Uzingatifu ni kuwa makini na mazingira uliyopo, kuona kwa ukaribu vitu vilivyopo kwenye mazingira yako. Uzingatifu utakusaidia kuwa kwenye mazingira uliyomo. Kwa vile panic attacks huleta hisia za kuwa kwenye mazingira tofauti au kukutoa kwenye uhalisia wa vitu, hii itakusaidia kupambana na panic attacks wakati inakuyemelea au hata kama tayari ilikwisha kukupata.

Weka akili kwenye maono na hisia unazozifahamu, kama kugonga mguu ardhini, au kusikilizia msokotano wa suruali yako ya jeans kwa mikono yako. Hisia halisi kama hizi hukurudisha kwenye uhalisia na hukupa kitu cha kutulizia fikra.

 

5. Tafuta Kitu Na Kuhamishia Fikra

Watu wengine wanaona inawasaidia kutafutua kitu kimoja na kuhamishia fikra zao zote kwenye kitu hicho wakati wamekamatwa na panic attack. Chagua kitu kimoja kinachoonekana kisha elekeza ufahamu wako wote kwenye kitu hicho na kutambua kila unachoweza kuhusu kitu hicho. Elezea muundo, rangi, umbile na ukubwa wa kitu hicho. Weka nguvu zako zote kwenye kitu hicho, na mshituko wako wa hofu unaweza kutoweka.

 

panic attack viashiria

 

6. Hamishia Mawazo Kwenye Eneo La Furaha

Ni eneo gani katika dunia hii unafikiri litakustarehesha au kukupumzisha? Beach yenye jua na mawimbi mepesi ya bahari? Kibanda juu ya mlima? Jifikirie upo kwenye eneo hilo, na jaribu kuyaelezea mazingira ya eneo hilo kwa kadiri ya uwezo wako. Fikiria kuwa unatumbukiza vidole vyako vya miguu kwenye mchanga wa joto kwenye beach hiyo, au ukinusa harufu nzuri ya miti ya misonobari. Eneoo hili linapaswa kuwa na ukimya, tulivu na la kupumzisha akili.

 

7. Rudia Mantra Kimoyomoyo

Mantra ni maneno yo yote yanayorudiwarudiwa, kwa mfano “Hakuna Hatari hapa, Ni kitu cha mpito.” Kurudiarudia mantra kutakupa faraja na kukupa ushujaa. Mantra itakupa kitu cha kushikilia wakati wa panic attack. Endelea kuimba mantra yako hadi utakapoona kuwa panic attack inakwisha.

 

Ni Zipi Tiba Kwa Mtu Mwenye Panic Attacks Na Panic Disorder

 

Panic attacks na panic disorder ni matatizo ambayo yanatibika. Ni matatizo yanayotibika vizuri kwa kuchukua hatua za kujisaidia mwenyewe au kupata ushauri kwenye vituo maalumu.

 

 

panic attack

 

 

Cognitive behavioral therapy ni namna ya tiba inayoonekana kufanya vizuri zaidi kwa watu wenye matatizo ya panic attack, panic disorder na agoraphobia. Tiba hii huweka mkazo juu ya fikra na matendo yako yanayokusababishia hofu na wasiwasi wa ghafla. Inakufanya ufikiri juu ya hofu zako kwa ukaribu na usahihi zaidi.

Kwa mfano, kama ulikamatwa ghafla na hofu kubwa wakati unaendesha gari, ni kitu gani kibaya zaidi ambacho kingeweza kutokea? Pengine ungewajibika kuegesha gari yako kando kando mwa barabara, bila kufanya ajali wala kupata mshituko wa moyo. Ukishajua kuwa hakuna kitu kibaya ambacho kinaweza kutokea, kujitokeza kwa hofu hakutakuwa tishio kubwa kwako.

Exposure therapy kwa tiba ya panic disorder hufanywa kwa kukusababishia hofu kubwa kwa maksudi kwenye mazingira yaliyodhibitiwa, ili kukufanya ujifunze njia salama za namna ya kushindana au kuizoea hali hiyo. Unaweza kuamriwa kupumua kwa haraka sana, kutikisa kichwa toka upande hadi mwingine, au kubana pumzi. Mazoezi haya tofauti humfanya mtu apate hisia zinazolingana na zile za mtu aliyeshikwa na panic attack. Kila apatapo zoezi hili, hofu hupungua na kujisikia kupata uwezo zaidi wa kudhibiti panic attacks.

Kama mtu ana agoraphobia, ataingizwa kwenye mazingira yale anayoyaogopa. Kama ilivyo hapo juu, unaingizwa kwenye mazingira yanayokuogofya hadi hofu itakapoanza kupungua na kutoweka. Mazoezi haya yanakufanya ujifunze kuwa hakuna hatari na unaanza kujenga uwezo wa kudhibiti hisia zako.

 

Nini Kitatokea Kama Mtu Mwenye Panic Attacks Hakutibiwa?

Bila kupata tiba, panic attacks zitatokea mara kwa mara kwa miezi au miaka. Pamoja na kuwa panic attacks huanza kutokea mara nyingi kwenye miaka ya mwanzo ya utu uzima, kwa wengine hutokea mapema zaidi au baadaye. Madhara ya kudumu yaweza kuwa ni kuwa ni, hofu (specific irrational fears-phobias), hasa ya kuwa mbali na mazingira ya nyumbani (agoraphobia) na kutopenda kuwa kwenye mazingira ya watu wengi. Madhara mengine yaweza kuwa ni mfadhaiko, matatizo ya kazini au shuleni, mawazo ya kujiua, matatizo ya kifedha na ulevi wa pombe au vitu vingine. Panic disorder huwafanya watu wengi wengine kupata maradhi ya moyo na kufa mapema.

Kwa ujumla, watu wengi wamepata matatizo ya mahusiano ya kifamilia na marafiki, wameshindwa katika masomo, na wamepoteza kazi zao wakiwa wanahangaika kuondokana na tatizo hili. Kunaweza kukatokea vipindi vya kupata nafuu, lakini tatizo la panic attacks huwa haliondoki lenyewe hadi mhusika apewe tiba stahiki.

 

Katika ukurasa wetu mwingine tutazungumza kuhusu dalili na tiba ya mfadhaiko. Usisite kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo. Itakuwa faraji kwetu kukujibu.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.