Leukemia Ni Ugonjwa Gani?

 

leukemia

Mara nyingi watu hufikiri kuwa leukemia ni hali inayowatokea watoto wadogo tu, lakini ukweli ni kwamba huwaathiri zaidi watu wazima kuliko watoto. Na huwaathiri zaidi wanaume kuliko wanawake na watu weupe huathirika zaidi ya weusi.

Hakuna la kufanya kuizuia leukemia. Ni saratani ya tishu zinazotengeneza damu, ambazo ni uboho na tishu za limfu, inayosababisha kuongezeka kwa idadi ya chembechembe nyeupe za damu katika mwili. Chembechembe hizi huzizidi kabisa chembechembe nyekundu za damu na platelets zinazohitajika ili mwili kuwa na afya. Chembechembe hizo nyeupe za damu zilizozidi hazifanyi kazi ipaswavyo na hali hiyo huleta matatizo.

Hali Hiyo Hutokea Vipi?

Damu ina aina tatu za seli: seli nyeupe zinazozuia maambukizo, seli nyekundu zinazosafirisha oksijeni, na platelets inazosaidia damu kuganda.

leukemia chembechembe za damu

Kila siku mabilioni ya seli za damu mpya hutengenezwa ndani ya uboho – nyingi ya hizo zikiwa ni seli nyekundu. Pale unapokuwa na leukemia, mwili wako hutengeneza seli nyeupe zaidi ya kiwango kinachohitajika.

Kuna aina mbili za seli nyeupe katika mwili wako: lymphoid cells na myeloid cells. Leukemia inaweza kutoka kwenye aina ye yote katika hizo mbili.

leukemia seli nyeupe za damu

Seli za leukemia hazina uwezo wa kupambana na maambukizo kama zinavyofanya seli nyeupe za kawaida. Na kwa vile ni nyingi sana, zitaanza kuathiri utendaji kazi wa viungo vingine vya mwili. Mwishowe, kutatokea uhaba wa seli nyekundu za kusafirisha oksijeni, platelets za kuwezesha damu kuganda, au seli nyeupe za kutosha kupambana na maambukizo.

Pamoja na hayo juu, kunaweza kutokea matatizo ya upungufu wa damu (anemia), michubuko, na kuchirizika kwa damu nje ya mwili (bleeding.)

Aina Za Leukemia

Madaktari huigawanya leukemia kwenye makundi mawili kulingana na:

1. Kasi ya kukua na kuwa mbaya zaidi
2. Aina ya seli nyeupe zilizohusika (kwa kawaida myeloid au lymphoid)

Kwenye kundi la kwanza, leukemia hugawanywa katika:

. Acute leukemia. Acute leukemia maana yake seli zisizo za kawaida za damu si komavu (blasts). Hazina uwezo wa kufanya kazi kikamilifu, na zinajiongeza kwa haraka, na tatizo kukua kwa haraka. Hii inahitaji tiba nzito na kwa wakati.

. Chronic leukemia. Kuna aina nyingi za chronic leukemia. Nyingine huzalisha seli nyingi kupita kiasi na nyingine husababisha uzalishaji mdogo wa seli. Chronic leukemia inahusika na seli za damu zilizo komavu zaidi. Seli nyingine za damu hujiongeza taratibu zaidi na kufanya kazi ipaswavyo kwa kipindi fulani.

Mgawanyo wa pili huhusisha aina ya seli nyeupe za damu zinazohusika:

. Lymphocytic leukemia. Aina hii inahusu seli za lymphoid (lymphocytes), ambazo hujenga tishu za limfu (lymphatic tissue). Tishu hizi hujenga mfumo wa kinga za mwili.

. Myelogenous leukemia. Hii inahusu seli za myeloid. Seli za myeloid huzalisha chemechembe nyekundu za damu, chembechembe nyeupe za damu na seli zinazozalisha platelets.

Chanzo Cha Leukemia

Hakuna mtu ajuae kiuhakika chanzo cha leukemia. Watu wenye leukemia wana chromosomes ambazo si za kawaida, lakini chromosomes hazisababishi leukemia.
Inaonekana kuanzia kwenye mchanganyiko wa urithi na mazingira.

Leukemia hutokea pale DNA za seli za damu, hasa seli nyeupe, ambazo hazijakomaa zinapoharibiwa kwa namna fulani. Hiyo husababisha seli za damu kukua na kujigawa bila kusimama na kuzifanya kuwa nyingi kupita kiasi.

Seli za damu zenye afya hufa baada ya muda fulani na nafasi zao kuchukuliwa na seli mpya zinazotengenezwa na uboho.

Seli ambazo si za kawaida hazifi wakati ukikifika. Zinajazana na kuchukua nafasi zaidi. Seli hizi za kansa zikizidi kuongezeka, zinazizuia seli zenye afya kukua na kufanya kazi inavyotakiwa kwa kuziba nafasi ndani ya damu.

Huwezi kuzuia leukemia, lakini kuna vitu katika mazingira vinavyoonekana kuanziasha ukuaji wa leukemia. Kama unavuta sigara unakuwa katika hatari ya kupata aina fulani za leukemia. Leukemia vile vile inaambatana na mionzi mikali na baadhi ya kemikali.

Tiba za aina fulani za chemotherapy na mionzi zinazotumika kutibu saratani nyingine zinaweza kusababisha leukemia.

Dalili Za Leukemia

Dalili za leukemia ni tofauti kulingana na aina ya leukemia. Dalili za kawaida ni:

. Homa au kusikia baridi
. Uchovu sugu, udhaifu wa mwili
. Maambukizo mazito ya mara kwa mara
. Kukonda
. Kuvimba kwa tezi za limfu, kuvimba maini na bandama
. Kuvuja damu kirahisi au michubuko ya kiurahisi
. Kutoka damu puani mara kwa mara
. Vijidoa vidogo vyekundu juu ya ngozi (petechiae)
. Kuvuja jasho jingi, na hasa usiku
. Maumivu ya mifupa au mifupa laini.

Tiba Ya Leukemia

Tiba ya leukemia hutolewa baada ya kuangalia vigezo vingi. Daktari atatazama umri wako na afya yako kwa ujumla, aina ya leukemia uliyo nayo, na kama imesambaa kwenye maeneo mengine ya mwili ikiwa ni pamoja na central nervous system.

Tiba za kawida ni:

. Chemotherapy
. Biological therapy
. Targeted therapy
. Radiation therapy
. Stem cell transplant. 

Stem cells za damu hutengenezwa ndani ya uboho (bone marrow) ambazo baadaye huweza kuwa aina yo yote ya chambechembe za damu zitakazohitajika na mwili. Stem cells kila wakati hujigawanya, hukua na kuchukua nafasi ya aina mbalimbali za seli za damu, zikichukua nafasi ya seli zilizozeeka na kuchakaa. Stem cells hutengeneza mabilioni ya seli mpya za damu kila siku. Endapo stem cells zitashindwa kutengeneza seli mpya kwa kiwango kinachotakiwa, matatizo mengi ya kiafya yatatokea – matatizo ya kuvuja damu, upungufu wa damu na maambukizo. Saratani au tiba za saratani zinapoharibu stem cells, stem cell transplant (SCT) hulazimika kufanyika.

Stem cell transplant au bone marrow transplant ni utaratibu wa kumpa mgonjwa stem cell zenye afya kuchukua nafasi ya zile zilizoharibiwa.

. Upasuaji. Dakatari wako anaweza kuamua kuliondoa bandama lako kama limejaa seli za saratani na kusukuma viungo vya karibu yake. Hii huitwa splenectomy.

Katika mada nyingine tutatazama ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi. Usisite kutoa maoni yako au kutuuliza maswali uliyo nayo kuhusu mada yetu ya leo.

Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au kututumia barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.