Kansa Ya Matiti; Huu Ni Ugonjwa Gani?

 

saratani ya ziwwa upimaji

 

Kansa ya matiti ni uvimbe wenye madhara (mkusanyiko wa seli za kansa) unaotokana na seli za matiti. Pamoja na kuwa saratani ya matiti huwaathiri zaidi wanawake, huweza pia kuwapata wanaume. Kansa ya  matiti kwa wanaume hutokea kwa nadra, lakini pale itokeapo huleta madhara makubwa zaidi. Moja ya sababu ni kuchelewa kufanyiwa uchunguzi kwa sababu inapotokea wanafanyiwa uchunguzi kansa hii huwa imefikia hatua ya kusambaa. Dalili za saratani ya matiti kwa wanaume zinalingana na zile za wanawake, dalili kuu ikiwa ni uvimbe ndani ya  matiti au kubadilika kwa rangi kulizunguka titi au kutoa majimaji. Kansa ya matiti kwa wanaume huweza kutokea kwenye umri wo wote, lakini hujitokeza zaidi kwa wanaume wenye umri wa miaka 60 au zaidi. Katika mada yetu ya leo, tutazungumzia saratani ya  matiti kwa wanawake.

 

Muundo Wa Titi La Mwanamke

 

Ndani ya titi la mwanamke kuna sehemu kati ya 15 hadi 20 ziitwazo lobes. Kila moja ya sehemu hizi ina sehemu nyingi ndogo zaidi ziitwazo lobules. Lobules hizi zina vikundi vya tezi ndogo zenye uwezo wa kutengeneza maziwa. Mtoto akizaliwa, maziwa hutiririka kutoka kwenye lobules kupitia mirija myembamba iitwayo ducts hadi kwenye chuchu. Mafuta na tishu za nyuzinyuzi hujaza nafasi kati ya lobules na mirija hiyo midogo.

 

saratani ya ziwa umbo la ziwa

 

Matiti vile vile huwa na njia za limfu (lymph vessels). Njia hizi huelekea na kuungana na viungo vidogo vya mviringo viitwavyo lymph nodes. Vikundi vya lymph nodes vipo karibu na ziwa kwenye maeneo ya kwapa (axilla), juu ya mfupa wa mabega (collarbone), na kifuani nyuma ya breastbone.

 

Seli Za Kansa

 

Kansa huanza ndani ya seli, vitu vidogo vinavyojenga tishu. Tishu hujenga matiti na sehemu nyingine za mwili.

Seli za kawaida hukua na kujigawa na kufanya seli nyingine kadiri mwili utakavyozihitaji. Seli za kawaida zikizeeka au kuharibika, hufa, na seli mpya huchukua nafasi yao.

Wakati mwingine utaratibu huu huenda kombo. Seli mpya huzaliwa wakati mwili hauhizitaji, na seli zilizozeeka au kuharibika hazifi kama inavyotakiwa. Kujijenga kwa seli hizi mpya hujenga uvimbe. Uvimbe katika titi unaweza kuwa hauna madhara au ukawa na madhara (kansa).

Uvimbe usio na madhara (                                                 tumors) unaweza kuondolewa na usirudie tena, hauvamii tishu za jirani na hausambai kwenye sehemu nyingine za mwili. Uvimbe wenye madhara (malignant tumors) unaweza kuondolewa lakini mara nyingi huota tena, huweza kuvamia na kuharibu tishu na viugo vya karibu, huweza kusambaa kwenye sehemu nyingine za mwili.

 

saratani ya ziwa iliyokomaa

 

Seli za saratani ya matiti huweza kusambaa kwa kujitoa kutoka kwenye uvimbe wa awali. Seli hizi huingia ndani ya njia za mfumo wa damu au mfumo wa limfu ambazo husambaa kwenye tishu zote za mwili. Seli hizi huweza kuonekana kwenye tezi za limfu karibu na matiti. Seli hizi za kansa huweza kunasa kwenye tishu nyingine na kukua na kisha kujenga uvimbe utakaoharibu tishu hizo. Kusambaa huko kwa seli za kansa huitwa metastasis.

 

Ni Zipi Aina Za Kansa Ya Matiti?

 

Kuna aina nyingi za kansa ya matiti. Kansa nyingine huonekana zaidi ya nyingine na kuna aina za kansa ambazo hutokea kwa pamoja. Kansa ya matiti inaweza kuanzia kwenye sehemu yo yote ya titi – kwenye mirija ya maziwa (ducts,) kwenye lobules, au wakati mwingine kwenye tishu zilizopo katikati ya lobules. Aina za kansa ambazo hutokea mara nyingi ni:

Ductal carcinoma in situ (DCIS): Ductal carcinoma in situ ni kansa ambayo haivamii tishu za jirani. Kansa hii huanzia ndani ya mirija ya maziwa (ducts) na carcinoma ni kansa yo yote ambayo huanzia katika ngozi au tishu nyingine (pamoja na tishu za matiti) zinazofunika au kutanda juu ya viungo vya ndani. Kansa hii haijasambaa nje ya mirija ya maziwa. Si kansa hatarishi sana kwa maisha lakini huongeza uwezekano wa kupata kansa inayosambaa hapo baadaye.

 

picha ya ductal carcinoma in situ

 

Invasive ductal carcinoma: Invasive ductal carcinoma (IDC) ni aina ya kansa inayoonekana zaidi kuliko nyingine. Asilimia 80 ya kansa zote za matiti ni invasive ductal carcinomas. Kansa hii tayari imeshavamia na kusambaa kwenye tishu za jirani. Hii ni kansa ambayo imevunja kuta za mirija ya kutolea maziwa kutoka kwenye lobules hadi kwenye chuchu na kuanza kuharibu tishu nyingine za matiti. Baadaye kansa hii husambaa kwenye tezi za limfu na sehemu nyingine za mwili.

Tubular carcinoma:  Tubular carcinoma ni aina nyingine ya invasive ductal carcinoma. Tubular carcinomas huwa ni ndogo (sentimeta 1 au pungufu) huumbwa na vitu vilivyo kama vijibomba viitwavyo “tubules.”

Uvimbe huu huonekana kama wa kawaida, usio na madhara, na hukua taratibu sana.

Umri wa wastani wa kuonekana kwa kansa hii ni miaka ya mwanzo 50, ingawa huweza kuonekana kwenye umri tofauti. Ni kansa ambayo ni nadra sana kuonekana kwa wanaume.

Pamoja na kuwa tubular carcinoma husambaa kwenye tishu za jirani, haisumbui sana na inatibika kirahisi. Mara nyingi haisambai nje ya matiti.

Invasive lobular carcinoma: Invasive lobular carcinoma (ILC) ni kansa ya pili kwa kuonekana baina ya wanawake baada ya invasive ductal carcinoma. Hii ni kansa iliyosambaa kwenye tishu nyingine za matiti. Kansa hii inaanzia ndani ya lobules ambazo ndani yake hutengenezwa maziwa kabla hayajachukuliwa na ducts na kupelekwa kwenye chuchu. Kwa hiyo, hii ni kansa iliyovunja kuta za lobules na kavamia tishu za matiti. Baadaye kansa hii husambaa hadi kwenye tezi za limfu na sehemu nyingine za mwili. Kansa hii huweza kumpata mwanamke wa umri wo wote ingawa inaonekana zaidi kwa wanawake wa umri mkubwa.

Mucinous carcinoma:  Kansa hii pia huitwa colloid carcinoma na ni aina ya invasive ductal carcinoma (kansa inayoanzia ndani ya mirija ya maziwa na kusambaa hadi kwenye tishu za jirani). Katika aina hii ya kansa, uvimbe hujengwa na seli zisizo za kawaida ambazo huelea ndani ya vibwawa vya mucin, kiambato kikuu cha mucus.

Mucus ni ute unaotereza ambao hutanda juu ya kuta nyingi za ndani za miili yetu, kama mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, mapafu, maini na viungo vingine muhimu. Seli za kansa za aina nyingi – pamoja na seli za kansa ya matiti – hutengeneza mucus. Katika mucinous carcinoma,  mucin huwa ni sehemu ya uvimbe na huzizunguka seli za kansa za matiti.

Pamoja na kuwa mucinous carcinoma huonekana kwenye umri wo wote, hupenda kuwaathiri zaidi wanawake waliokoma hedhi.  Utafiti unaonyesha kuwa umri wa kuathirika ni miaka ya mwazo ya 60 na 70.

Mucinous carcinoma haisumbui sana na huweza kutibika. Kansa hii mara chache sana husambaa hadi kwenye tezi za limfu ukilinganisha na aina nyingine za kansa.

Medullary carcinoma:  Medullary carcinoma ni aina adimu ya invasive ductal carcinoma, ikiwa ni asilimia kama 5 ya kansa zote za matiti zinazoonekana. Inaitwa “medullary” carcinoma kwa sababu uvimbe ni laini, wa nyama unaofanana na sehemu ya ubongo iitwayo medulla.

Medullary carcinoma huweza kutokea kwenye umri wo wote, ingawa huathiri zaidi wanawake wa miaka ya mwisho ya 40 au ya mwanzo ya 50.

Medullary carcinoma hukua taratibu na ni nadra kusambaa nje ya matiti kuelekea kwenye tezi za limfu. Kwa sababu hiyo, huwa inatibika kirahisi zaidi kuliko kansa za aina nyingine.

Inflammatory breast cancer: Infalammatory breast cancer (IBC) ni aina ya kansa inayookana mara chache sana, ni kama asilimia 1 ya kansa zote za matiti zinazoonekana. Kansa hii inasumbua sana.

 

picha za inflammatory breast cancer

 

Kansa hii huanza kwa kuweka wekundu na kuvimba kwa matiti. Hukua na kusambaa haraka, dalili zikiongezeka kila siku au kila baada ya saa chache. Yafaa kuigundua mapema na kupata tiba.

Kansa hii huwapata zaidi wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 50. Kansa ya aina hii huweza pia kuwapata wanaume.

Triple-negative breast cancers:

Paget’s disease of the nipple:  Paget’s disease of the nipple ni aina ya kansa ya matiti ambapo seli za kansa hujikusanya ndani au kuzunguka chuchu. Seli za kansa hushambulia kwanza mirija ya maziwa ya kwenye chuchu, kisha kusambaa kwenye sehemu ya juu ya chuchu na areola (mduara mweusi wa ngozi kuzunguka chuchu.)

Kuzijua dalili ni muhimu sana, kwa vile asilimia 97 ya wanawake wenye paget’s disease wana kansa, yaweza kuwa DCIS au invasive cancer, pahala pengine ndani ya matiti. Mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye chuchu au areola ni ishara ya kwanza kwamba kuna saratani.

 

kansa ya paget's

 

Kansa hii huonekana zaidi kwa wanawake, ingawa huweza kuwashambilia wanaume. Ugonjwa huu huonekana zaidi kwa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 50.

Lobular carcinoma in situ:

Papillary carcinoma: Invasive papillary carcinoma ni kansa ambayo huonekana mara chache sana, chini ya asilimia 1 ya kansa zote zinazoshambulia tishu za jirani (invasive breast cancers). Kansa hii huonekana zaidi kwa wanawake ambao tayari wamekoma hedhi. Kansa hii huonekana kama vidole vidogo vilivyojitokeza. Mara nyingi kansa hii inapoonekana, kansa nyingine ya aina ya ductal carcinoma in situ huwepo.

Phyllodes tumor:  Huu ni uvimbe unaooneana mara chache sana, ni chini ya asilimia 1 ya uvimbe wote wa matiti unaoonekana. Jina “Phyllodes” linatokana na neno la kigiriki lenye maana ya “kama jani” kutokana na seli za uvimbe huu huota kwa mfano wa jani. Uvimbe huu, mara nyingine huitwa cystosarcoma. uvimbe huu hukua harak, lakini ni mara chache sana huweza kusambaa nje ya matiti.

Ingawa huu ni uvimbe usio na madhara, mara nyingine huweza kuwa na madhara (cancerous) na uvimbe mwingine huwa wa kati (kati ya ule usio na madhara na wenye madhara.) Uvimbe wa aina hii huhitaji uapasuaji.

Uvimbe wa Phyllodes unaweza kutokea katika umri wo wote, lakini hutokea zaidi mwanamke akiwa kwenye miaka ya 40.

Angiosarcoma:

 

Hali Hatarishi Kwa Saratani Ya Matiti Ni Zipi? Unapataje Kansa Ya Matiti?

 

Ukiambiwa kuwa una saratani ya matiti, kwanza utataka kujua ni nini hasa kilichosababisha saratani hiyo. Ukweli ni kwamba hakuna mtu anayejua saratani hii inasababishwa na nini. Madaktari pia hawajui kwa nini mawanamke mmoja anapata saratani ya matiti wakati mwingine hapati.

Lakini madaktari wanajua kuwa kuna mazingira au hali fulani vinavyochochea kutokea kwa kansa. Kuna hali zinazozuilika (kama unywaji wa pombe), na kuna hali ambazo haziwezi kuzuilika (kuzaliwa kwenye ukoo wenye historia ya saratani ya matiti).

Utafiti umeonyesha mazingira na hali hatarishi kwa kansa ya matiti  kuwa ni:

. Umri:
. Historia binafsi ya afya:
. Historia ya afya ya familia:
. Mabadiliko ya jeni:
. Tiba ya mionzi kifuani:
. Historia ya uzazi na mzunguko wa hedhi:
. Jamii:
. Ujazo wa ziwa:
. Unene baada ya kukoma hedhi:
. Kukosa mazoezi ya mwili:
. Utumiaji wa pombe:

.

Dalili Za Saratani Ya Matiti Ni Zipi?

 

Saratani ya matiti ya mwanzo kabisa kwa kawaida haitoi dalili zo zote. Kadiri uvimbe utakavyokua, unaweza kubadilisha mwonekano wa ziwa au utofauti ukilitomasa. Mabadiliko yanayoonekana mara nyingi ni:

 

saratani ya ziwa uchunguzi

 

. Uvimbe au ngozi ngumu ndani au karibu na titi au maeneo ya chini ya kwapa
. Mabadiliko ya umbo au ukubwa wa titi
. Mikunyanzi juu ya ngozi ya titi
. Chuchu ya titi kurudi ndani
. Kutokwa majimaji kwenye chuchu na hasa yenye damu
. Magamba, wekundu au kuvimba kwa ngozi ya titi, chuchu au areola (eneo jeusi kwenye ngozi, katikati ya titi). Ngozi yaweza kuwa na matuta.

Yafaa kumwona mhudumu wa afya endapo mabadiliko yaliyotajwa yatadumu kwa muda mrefu. Baadhi ya dalili hizi si za kansa, tatizo jingine la afya laweza kuwa ndiyo chanzo. Hivyo basi, yafaa kufika kituo cha afya kwa uchunguzi wa kina zaidi na kupata tiba ipaswayo.

 

Hatua Za Kansa Ya Matiti

 

Kama kipande cha tishu kimechukuliwa, kikapimwa na kuonekana kuwa na seli za kansa (biopsy), daktari wako atahitaji kujua hatua ya kansa iliyofikiwa ili ajue tiba unayostahili. Hatua ya kansa hutegemea ukubwa wa kansa, na kama kansa hiyo imeshashambulia tishu za jirani, na kama imeshasambaa kuelekea sehemu nyingine za mwili. Vipimo huchukuliwa kujua hatua iliyofikiwa na kansa hiyo.

Hatua za saratani ya matiti ni:

Stage 0 mara nyingine inaamisha uwepo wa seli zisizo za kawaida ambazo si shambulizi. Kwa mfano stage 0 huelezea ductal carcinoma in situ (DCIS). Mgonjwa huambiwa ana DCIS endapo seli zisizo za kawaida zitaonekana kutanda juu ya ngozi ya juu ya mirija ya matiti (breast duct), lakini seli hizo hazijashambulia tishu za jirani za titi au kusambaa nje ya mirija. Ingawa madaktari wengi husema DCIS si kansa, wakati mwingine huweza kugeuka kansa ya matiti kama tiba haikutolewa.

Stage I ni hatua ya awali ya mashambulizi ya kansa ya matiti. Seli za kansa zimeshambulia tishu zatiti nje ya eneo zilipoanzia, lakini seli hizo hazijatoka nje ya titi. Uvimbe haujazidi kipimo cha upana wa sentimeta 2.

Stage II ni moja kati ya hali zifuatazo:

. Uvimbe hauzidi upana wa sentimeta 2. Kansa imesambaa hadi kwenye tezi za limfu zilizopo chini ya kwapa.

. Uvimbe ni kati ya sentimeta 2 na 5. Saratani haijafika kwenye tezi za limfu za chini ya kwapa.

. Uvimbe ni kati ya sentimeta 2 na 5. Saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu za chini ya kwapa.

. Uvimbe ni zaidi ya sentimeta 5. Saratani haijafika kwenye tezi za limfu za chini ya kwapa.

 

Stage III ni kansa ya sehemu moja iliyofikia hatua ya juu. hatua hii hugawanywa tena katika hatua za IIIA, IIIB na IIIC.

Stage IIIA ni moja ya hatua zifuatazo:

. Uvimbe haujazidi upana wa sentimeta 5. Saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu za chini ya kwapa zilizoungana au zinazoungana na maungo mengine ya mwili. Au saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu zilizopo nyuma ya mfupa wa matiti (breastbone).

. Uvimbe una upana wa zaidi ya sentimeta 5. Saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu za chini ya kwapa zilizo pekee au zilizoungana au kuungana na maungo mengine. au saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu zilizopo nyuma ya mfupa wa titi.

Stage IIIB ni uvimbe wa ukubwa wo wote ule ulioota kwenye kuta za kifua au juu ya ngozi ya titi. Inaweza kuhusisha kuvimba kwa titi au uvimbe ndani ya ngozi ya titi.

. Uvimbe unaweza kuwa umesambaa hadi kwenye tezi za limfu za chini ya kwapa.

. Saratani inaweza kuwa imesambaa hadi kwenye tezi za limfu zilizopo chini ya kwapa zinazoungana au zinazoungana na maungo mengine. Au, saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu zilizo chini ya mfupa wa titi.

. Inflammatory breast cancer ni aina ya saratani inayoonekana mara chache sana. Titi  huwa jekundu, lililovimba kwa sababu seli za kansa huziba mirija ya limfu kwenye ngozi ya titi. Daktari agunduapo inflammatory breast cancer, huwa ni ya angalau hatua ya IIIB, lakini huweza kuwa ya hatua ya juu zaidi.

Stage IIIC ni uvimbe wa ukubwa wo wote ule. Uvimbe huu umeshasambaa kwa moja ya njia zifuatazo:

. Uvimbe umesambaa hadi kwenye tezi za limfu nyuma ya mfupa wa titi na za chini ya kwapa.

. Saratani imesambaa hadi kwenye tezi za limfu juu ya au chini ya mfupa wa bega.

 

satarani ya ziwa hatua ya juu

.

Stage IV ni kansa iliyosambaa maeneo ya mbali. Kansa imesambaa kuelekea sehemu nyingine za mwili, kama mifupa, mapafu, au ubongo.

 

Ni Nini Tiba Ya Saratani Ya Matiti?

 

Wanawake wenye saratani ya matiti wana njia nyingi za kupata tiba. Tiba iliyofanya vizuri kwa mmoja si lazima ifanye kazi vizuri kwa mwingine. Tiba zinazotolewa ni upasuaji, mionzi, hormone therapy, chemotherapy na targeted therapy. Mgonjwa anaweza kupewa tiba za aina tofauti zaidi ya moja katika hizi.

Upasuaji na tiba za mionzi ni aina za tiba zinazotolewa kwenye titi lenyewe. Zinaondoa au kuharibu seli za kansa kwenye titi.

 

saratani ya matiti komavu

 

Hormone therapy, chemotherapy na targeted therapy hutumia dawa zinazoingia kwenye mfumo wa damu na kuua au kudhibiti saratani mwili mzima.

Tiba ya kansa utakayopewa wewe mgonjwa itategemea vipimo vilivyochukuliwa, hatua ya kansa iliyofikiwa na afya yako kwa ujumla.

Tunaomba uupitie ukurasa wa saratani ya shingo ya kizazi kusoma kuhusu tiba za kansa kwa undani zaidi.

Katika ukurasa mwingine tumezungumzia saratani ya shingo ya kizazi. Usikose kutoa maoni yako au kuuliza maswali kuhusiana na mada yetu ya leo. Itakuwa faraja kubwa sana kwetu kukujibu.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.