Tatizo La Kuwa Na Wasiwasi – Nini Maana Ya Anxiety Disorder?

 

 

wasiwasi

 

 

Ni kitu cha kawaida kupata wasiwasi mtu anapokuwa na changamoto, kama kusailiwa kwa ajili ya ajira, kufanya mtihani mgumu shuleni, kukutana kwa mara ya kwanza na mpenzi au kuhofia hali yako ya kipesa baada ya matumizi makubwa. Lakini endapo wasiwasi na hofu vinakufanya ushindwe kumudu maisha yako ya kawaida kama unavyopenda, unaweza kuwa una tatizo la anxiety disorder. Kuna aina nyingi za anxiety disorders – na njia nyingi za kutibu au kumfanya mtu ajisaidie. Ukishakuwa umelijua tatizo lako la anxiety disorder, kuna hatua za kuchukua ili kupunguza dalili zake au kurudisha udhibiti wa maisha yako.

 

Wasiwasi Ni Nini?

 

Wasiwasi unaweza kuelezewa kuwa ni mwitiko wa mwili wako wa vitu hatarishi kwa maisha yako vinavyokuja au unavyofikiria vinaweza kuja. Wasiwasi unahusiana sana na hofu ambayo ni mwitiko wa mwili wako kwa hatari halisi (hatari iliyo mbele yako) au inayofahamika kuja siku za karibuni. Hofu na wasiwasi ni miitiko iliyojengeka kwa binadamu na wanyama , na njia za kupambana navyo zinahusiana na kushindana navyo au kutafuta njia ya kukwepa – fight-or-flight”. Mfumo wa ubongo hudhibiti mwitiko huu wa mwili wa kupambana na, au kuyakimbia mazingira hatarishi, na mara nyingi huambatana na kupanuka kwa mboni za macho, kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo, na kuongezeka kwa jasho/uhemaji.

 

 

wasiwasi tiba

 

Mwitiko kwa wasiwasi kunaweza kuambatana na uangalifu zaidi wa mazingira na kukaza kwa misuli tayari kuikabili hatari. Wasiwasi unaweza kuwa na manufaa, kama kuongeza ufaulu wa mtihani, kufanya vizuri zaidi kwenye michezo, au kuzungumza mbele ya kadamnasi. Pamoja na kuwa hii ni miitiko ya kawaida ya mwili na mara nyingi ni miitiko yenye manufaa wakati wa hatari, wasiwasi unaweza kuwa na athari endapo utazidi kiwango au ukiendelea kuwepo bila ya kuwepo kwa hatari. Wasiwasi wa kukithiri unaweza kukukosesha raha, na kuharibu utendaji wako wa kazi, na huu huitwa anxiety disorder.

Dalili Za Anxiety Disorder Ni Zipi?

 

Dalili za kawaida kwa mtu mwenye tatizo la anxiety disorder ni pamoja na:

. Kutotulia;
. Kuchoka kirahisi, uchovu;
. Shida kutuliza mawazo kwenye kitu ambayo inaweza kuonekana kuwa ni tatizo la kumbukumbu;
. Hisia kuwa ubongo unakuwa “mtupu”
. Hasira za haraka
. Kukakamaa kwa misuli
. Kuumwa kichwa
. Matatizo ya usingizi (kukosa usingizi, usingizi wenye usumbufu)

Wasiwasi unaohusiana na hofu ya kitu fulani (specific or simple phobia) au wasiwasi wa mambo ya kijamii (social phobia) unaweza kusababisha kuyakwepa mazingira fulani au kukuza dalili zinazoleta panic attack – hofu kubwa ya ghafla inayofikia kilele katika muda mfupi.

 

Aina Za Anxiety Disorder

 

Anxiety disorders hutofautishwa kufuatana na aina ya kitu au mazingira yanayosababisha woga na wasiwasi, pamoja na namna ya fikra anazokuwa nazo mtu akishikwa na hofu au wasiwasi. Kusudi mtu aitwe ana tatizo hili, hofu na wasiwasi lazima viwe vya muda mrefu, vilivyodumu miezi 6 au zaidi. Matatizo ya kuwa na wasiwasi kwa kawaida huanza utotoni lakini hudumu hadi ukubwani.

Aina ya tatizo la kuwa na wasiwasi lililo la kawaida zaidi ni specific phobias. Hii ni hali ya kuwa na hofu ya kukithiri ya kitu fulani au mazingira fulani, kama buibui, kuwa juu, kupanda ndege, au sehemu zilizofungwa. Katika mambo ya kijamii, kuna social phobia au performance anxiety, ambapo mtu anakuwa na wasiwasi na hofu kubwa ya kushirki shughuli za kijamii, au mazingira yanayomfanya watu wamwone au kumjadali.

 

wasiwasi kujinasua

 

Generalized anxiety disorder (GAD) ni aina ya tatizo linalojitambulisha kwa kuwa na wasiwasi na woga mkubwa unaodumu kwa kipindi kirefu unaotokana na maeneo tofauti ambayo ni vigumu kuyadhibiti. Woga unaoendana na GAD huathiri uwezo wa mtu wa kufikiri, kupata usingizi, au kufanya shughuli fulani. Dalili zake hujionyesha kwenye hisia na tabia na namna ya kufikiri ambavyo ni matokeo ya hali ya mwili kufikiria kuwa kuna hatari. Ukiwa na GAD, utapata wasiwasi kutokana na vitu vinavyowapa wasiwasi watu wote, lakini wewe utaupeleka wasiwasi huo kwenye ngazi nyingine, ya juu. Mfanya kazi mwenzako akitoa maoni yake kuhusu hali ya uchumi, kwako shida; rafiki yako asipotoa majibu kwa simu yako haraka, unaanza kufikiri kuwa mahusiano yenu si mazuri. Wakati mwingine hata wazo tu la kuwa utashinda kazini kwako ni mwanzo wa wasiwasi. Unaendesha shughuli zako ukiwa umejaa hofu isiyobainika, na hata kama hakuna kitu cha kuanzisha hofu hizo.

Waweza kuwa unatambua kuwa wasiwasi wako unazidi hali halisi, au unaamini kuwa wasiwasi wako unakulinda kwa namna fulani, mwisho wake ni ule ule. Huwezi kuyafuta mawazo yanayokuletea wasiwasi. Yanazidi kutembea kichwani mwako, yakijirudiarudia  bila mwisho.

 

 

Aina nyingine za wasiwasi ni separation anxiety disorder, selective mutism (kushindwa kuzungumza kwenye baadhi ya mazingira ya watu wengi kama shuleni), agoraphobia (woga wa kuwa mbali na nyumbani) na panic disorder.

 

Namna Ya Kujisaidia Ukiwa Na Tatizo La Kuwa Na Wasiwasi – Anxiety Disorder

 

Si kila mtu anayekuwa na wasiwasi sana ana tatizo la anxiety disorder. Unaweza kuwa na wasiwasi kwa sababu ya kuwa na ratiba kali ya kazi, kukosa usingizi au mazoezi, msongo ukiwa kazini au nyumbani, au kunywa kahawa kupita kiasi.

Kama maisha yako si ya furaha na ni ya msongo kila wakati, ni rahisi sana kuwa na wasiwasi. Kwa kufanya yafuatayo unaweza kupunguza wasiwasi na kudhibiti dalili za anxiety disorder:

Jichanganye na wengine. Upweke unaweza kukuletea au kukuongezea wasiwasi, kwa kuyazungumzia ana kwa ana matatizo yako ya kuwa na wasiwasi unaweza kuupunguza wasiwasi unaokuwa nao.

 

sherehe

 

Jitahidi kila wakati kukutana na marafiki zako, jiunge na kikundi cha kusaidiana, au mshirikishe mambo yanayokusumbua mtu umpendaye. Kama huna mtu wa namna hii, hujachelewa kuanza kujenga mahusiano mapya au kujiunga na kikundi cha kusaidiana.

Dhibiti msongo wa mawazo. Kama unasumbuliwa sana na msongo wa mawazo, ushauri wa kuondokana na msongo wa mawazo utakusaidia. Unaweza pia kuona ni majukumu yepi ya kuyaacha, kuyapunguza au kuwaachia wengine.

Jifunze njia za kuulegeza mwili. Vitu kama meditation, mazoezi ya kulegeza misuli, kuvuta pumzi kwa nguvu vinaweza kupunguza wasiwasi na kuongeza hisia za kuupumzisha mwili na hisia.

Jenga tabia ya kufanya mazoezi. Kufanya mazoezi ya mwili ni njia ya asili ya kupunguza msongo wa mawazo na kuondoa wasiwasi. Kupata matokeo bora kabisa, lenga kufanya mazoezi ya kuongeza mapigo ya moyo na kutoa jasho (aerobic exercises) kwa muda wa dakika 30 kila siku. Mazoezi au shughuli za kuifanya mikono na miguu kuwa katika mwendo kwa wakati mmoja (rhythmic activities) ni ya manufaa sana. Jaribu kutembea, kukimbia, kuogelea, kucheza muziki wa dansi n.k.

Pata usingizi wa kutosha. Kukosa usingizi wa kutosha kunaweza kukuza tatizo la kuwa na wasiwasi kwa hiyo jitahidi kupata saa 7 hadi 9 za usingizi mzuri.

 

usingizi mnono

 

Kuwa mwangalifu na matumizi ya kahawa, pombe na tumbaku. Kama unapambana na tatizo la kuwa na wasiwasi, jaribu kupunguza utumiaji wa kahawa, au kuiacha kabisa. Vile vile, utumiaji wa pombe unaweza kukuongezea tatizo lako la kuwa na wasiwasi. Pamoja na kuwa tumbaku huonyesha kuleta hali ya utulivu, nicotine
ni kichocheo chenye nguvu sana kinachoongeza wasiwasi kufika kiwango cha juu.

Amua kuacha tabia ya kuwa na wasiwasi. Kuwa na wasiwasi ni tabia ambayo unaweza kujifunza kuiacha. Mikakati kama ya kutengeneza vipindi vya kuwa na wasiwasi, kuyachambua mawazo yanayoleta hofu, inaweza kukupunguzia wasiwasi unaokuwa nao.

Katika kurasa nyingine tunazungumzia tatizo la panic attacks, namna ya kuondokana na mfadhaiko na jinsi usingizi unavyosaidia afya yako.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.