Usonji Ni Ugonjwa Gani?

 

 

Usonji (autism spectrum disorder -ASD) ni ugonjwa wa neva na wa kiukuaji unaoathiri namna mtu anavyoshirikiana na wenzake, anavyozungumza, anavyojifunza, na tabia yake. Ingawa usonji unaweza kugundulika katika umri wo wote, ugonjwa huu huelezewa kuwa ni ugonjwa wa matatizo ya ukuaji (developmental disorder) kwa sababu dalili huonekana katika miaka miwili ya mwanzo ya maisha.

Katika mada hii, tutazungumzia dalili za ugonjwa huu, kuelezea sababu za kupata ugonjwa huu na tiba na dawa zinazoweza kutumika kwa mtu mwenye tatizo hili.

Kulingana na Diagnostic and Statistical Manual of Mental Disorders (DSM-5), ambao ni mwongozo uliotengenezwa na American Psychiatric Association ambao wanataaluma ya afya huutumia kutambua matatizo ya afya ya akili, watu wenye usonji wana:

. Shida ya kufanya mawasiliano na kujichanganya na watu wengine
. Moyo wa kupenda kujifunza vitu vichache sana na tabia zinazojirudia
. Dalili zinazoathiri ufanisi wao wakiwa shuleni, kazini na maeneo mengine ya kimaisha.

Usonji huitwa “spectrum disorder” kwa sababu kuna upana katika aina na ukalifu wa dalili za tatizo ambao watu huupata. Watu wa jinsia zote, jamii zote, na wa makundi yote ya kiuchumi wanaweza kugundulika kuwa na usonji. Pamoja na kuwa usonji linaweza kuwa ni tatizo la maisha yote, tiba na huduma zinaweza kumpunguzia mtu ukali wa dalili zake na kuboresha utendaji wake wa kila siku.

Dalili Za Usonji

Watu wenye usonji wana shida katika kufanya mawasiliano na kujichanganya na jamii, kuwa na mapenzi na vitu vichache, na tabia za kujirudia.

Watoto wengine wanaonyesha dalili za usonji wakiwa bado wachanga, kama kukwepa kutazama usoni, kutoitika majina yao au kutowapenda walezi wao. Watoto wengine wanaweza kukua vizuri kwa miezi michache ya mwanzo, halafu ghafla wakabadilika na wakawa wa kujitenga au wakali au kupoteza umahiri wa lugha waliyokwishajifunza. Kwa kawaida, dalili huanza kuonekana kwenye umri wa miaka miwili.

Kila mtoto mwenye usonji atakuwa na aina yake ya tabia na kiwango cha chake cha ukubwa wa tatizo. Watoto wengine wenye usonji wana akili za kawaida au za ziada – wanajifunza haraka, lakini wana shida ya kufanya mawasiliano na kutumia walichojifunza katika maisha ya kila siku na kuendana na jamii.

Kwa sababu ya mchanganyiko wa dalili wa kila mtoto, ukubwa wa tatizo huwa wakati mwingine shida kugundulika.

Orodha ya hapa chini inaonyesha mifano ya tabia zinazoonekana mara nyingi baina ya watu wenye usonji. Haimaanishi watu wote wenye usonji watakuwa na tabia zote, lakini wengi watakuwa  na tabia kadhaa zilizoorodheshwa.

Mawasiliano Ya Kijamii Na Tabia Za Kujichanganya Katika Jamii

. Kutazama usoni mara chache au utazamaji usio wa kawaida

. Kutopenda kupakatwa na kuonyesha kupenda kucheza peke yake, akiwa kwenye ulimwengu wake wa kipekee

. Kuooneka kutotazama au kusikiliza watu wanaosema

. Mara chache sana kushiriki vitu vinavyofurahisha, hisia au kufurahia vitu au shughuli (ikiwa ni pamoja na mara chache sana kuonyesha vitu kwa watu wengine)

. Kutoitika au kuwa mzito kuitika majina yao yakiitwa au matendo mengine yakuwatahadharisha

. Hawezi kuanzisha mazungumzo au kuendeleza aliyoyakuta, akianzisha ni kuomba kitu anachokitaka

. Kupata shida katika mazungumzo yanayokwenda mbele na kurudi nyuma

. Kuendelea kuzungumza kwa muda mrefu kuhusu jambo linalomfurahisha bila kujali kama wengine wanalifurahia au la au bila kutoa nafasi kwa wengine kuchangia

. Kuoekana kutoelewa maswali au maelekezo rahisi

. Kuonyesha sura, kuwa na miondoko, na ishara za mikono au kichwa ambazo hazilingani na kile kinachosemwa

. Kuwa na toni ya sauti isiyo ya kawaida ambayo inaweza kuwa kama ya kuimba au kama ya roboti

. Kupata shida kuelewa mtu mwingine akitoa maoni yake au kupata shida kubashiri au kuelewa matendo ya mtu mwingine

. Kushindwa kurekebisha tabia kulingana na mazingira ya kijamii

. Shida kujenga urafiki au kushiriki michezo ya ubunifu.

Tabia Finyu au Tabia Za Kujirudiarudia Zinaweza Kuwa ni Pamoja na:

. Kurudiarudia tabia fulani au kuwa na tabia isiyo ya kawaida, kama kurudia maneno au misemo (echolalia)

. Kupenda aina fulani ya ulaji, kama kula chakula kidogo, au kukataa aina fulani ya mapishi

.  Hufanya vitendo ambavyo vinaweza kumwumiza, kama kujiuma au kubamiza kichwa

. Kuwa na mapenzi makali ya muda wote ya mada fulani, kama namba au hoja

. Kuonyesha mkazo wa kuzidi kwenye mapenzi ya vitu fulani, kama vitu vinavyotembea au sehemu za vitu

. Kuonyesha kuchukizwa na mabadiliko madogo ya ratiba iliyozoeleka na kuonyesha ugumu wa kubadilika

. Kuonyesha msisimko wa kuzidi au mdogo mno ukilinganisha na watu wengine kwenye vitu vya ufahamu, kama mwanga, sauti, nguo , au joto

 

Watu wenye usonji wanaweza kuwa na matatizo ya kupata usingizi na kuwa na hasira.

Watu wenye usonji wanaweza kuwa na sifa za kipekee, ikiwa na pamoja na:

. Kuweza kukisoma kitu kwa undani na kukumbuka taarifa kwa muda mrefu
. Wanaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kujifunza kwa kuona na kusikia
. Kufanya vizuri kwenye hisabati, sayansi, muziki au sanaa.

Sababu Za Usonji na Vitu Vinavyochangia Tatizo

Idadi ya watoto wanaobainika kuwa na usonji inaongezeka. Haijajulikana kwamba hii ni kwa sababu ya njia bora za kutambua tatizo au kuongezeka kwa tatizo, au pengine yote.

Watafiti hawaelewi sababu za msingi za usonji, lakini utafiti unafiri kuwa jeni za mtu zinaweza kuchanganywa na vipengele vya mazingira na kuathiri ukuaji ambao utasababisha usonji.

Usonji huwapata watoto wa jamii zote na mataifa yote, lakini vipengele fulani vinaongeza yamkini ya mtoto kupata usonji. Navyo ni:

. Jinsia ya mtoto wako: Watoto wa kiume wapo kwenye hatari mara nne ya kupata usonji ukilinganisha na wa kike

. Historia ya familia: Familia yenye mtoto mmoja mwenye usonji inaweza kupata mwingine mwenye tatizo hili. Si ajabu sana kuona wazazi wa mtoto mwenye tatizo wana matatizo madogo madogo ya mawasiliano

. Matatizo mengine: Watoto wenye maradhi mengine wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata usonji.

. Watoto wanaozaliwa kabla ya siku: Watoto wanaozaliwa kabla ya wiki ya 26 wana hatari kubwa zaidi ya kupata usonji.

. Umri wa wazazi: Kunaweza kuwa na uhusiano kati ya mtoto aliyezaliwa na wazazi wazee na usonji.

. Athari za jeni: . Kuwa na athari fulani za jeni (kama Down syndrome au Fragile X syndrome)

Tiba Ya Usonji

Hakuna dawa ya usonji na hakuna tiba inayofaa kwa wote. Lengo la tiba ni kuboresha uwezo wa mtoto wako wa kiutendaji na kumsaidia kukua na kujifunza. Kutambua tatizo mapema kabla ya miaka yake ya mwanzo ya shule kunaweza kumsaidia mtoto kujifunza mambo muhimu ya kijamii, ya mawasiliano, kiutendaji na kitabia.

Uwingi wa tiba za majumbani na mashuleni ni mkubwa mno, na mahitaji kwa mtoto wako yanaweza kubadilika baada ya muda. Mtaalamu wako wa afya atakupa ushauri wa sehemu ya kumtibu mtoto wako.

Tiba Zinaweza Kuwa:

. Tiba Ya Tabia Na Mawasiliano: Kuna programu nyingi kwa ajili ya matatizo ya tabia za kijamii na lugha kwa ajili ya wahanga wa usonji. Baadhi ya programu zinalenga kupunguza matatizo ya kitabia na kufundisha stadi mpya. Programu nyingine zinalenga kuwafundisha watoto namna ya kupambana na mazingira ya kijamii au kufanya mawasiliano mazuri na wengine.
. Tiba Za Kielimu: Watoto wenye usonjii kwa kawaida hupokea vizuri programu zilizoandaliwa kwa ustadi wa juu. Programu zinazofanikiwa ni zile zinazohusisha timu ya wataalamu na shughuli balimbali zinazolenga kuboresha ufundi wa kijamii, mawasiliano na tabia.
. Tiba Ndani Ya Familia: Wazazi na wanafamilia wengine wanaweza kujifunza namna ya kucheza na kushirikiana na watoto wao kwa jinsi ambayo itasaidia kukuza uwezo wao wa kushiriki shughuli za jamii, kudhiti matatizo yao ya kitabia, na kuwafundisha stadi za kila siku za maisha na mawasiliano.
. Tiba Nyingine: Kulingana na mahitaji ya mtoto wako, tiba ya uwezo kuzunguza ili kuboresha ufundi wa kufanya mawasiliano, tiba ya kufundisha shughuli za kila siku, na tiba za maumbile za kusaidia kutembea vizuri na kutoyumba zinaweza kuwa na msaada.
. Dawa: Hakuna dawa zinazoweza kuondoa dalili za usonji, lakini kuna dawa zinazoweza kuzidhibiti dalili hizo.

Katika mada yetu nyingine tutalizungumzia tatizo la kizunguzungu Usisite kuuliza swali ulilo nalo au kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada hii.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya saa za kazi  kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.