Kuharisha – Nini Chanzo Na Tiba Ya Kuharisha (Diarrhea)?

 

tiba ya kuharisha

 

Kuharisha ni tatizo linalowasumbua watu wengi. Kuharisha kunaweza kuwa kidogo, kwa muda mfupi au hata kuhatarisha maisha. Karibu watoto milioni 1.9 walio chini ya miaka mitano -hasa katika nchi zinazoendelea – hufa kila mwaka kwa kuharisha. Kuharisha, kwa hiyo, ni sababu ya pili ya vifo kwa watoto wa umri huo duniani.

Kuharisha (diarrhea) hutambulika kwa kupata choo kilicho laini sana au chenye majimaji. Mara nyingi kuharisha husababishwa na bakteria, virusi, au vimelea. Matatizo katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula huweza pia kusababisha kuharisha. Mtu akienda haja mara kwa mara lakini kinyesi kikawa cha kawaida, huko si kuharisha. Vile vile, watoto wanaonyonya mara nyingi huwa na kinyesi laini, kinachonata. Hii ni kawaida.

 

Kuharisha Kunatokeaje?

 

Kuharisha kukitokea, kinyesi kinakuwa laini hata kama mtu atakwenda haja kubwa mara nyingi. Ulaini wa kinyesi -ambao huwa ni wa tofauti ukianzia na ule wa laini kiasi hadi ule wa majimaji -husababishwa na kuongezeka kwa maji katika kinyesi. Umeng’enywaji wa chakula ukiwa wa kawaida, kiasi kikubwa cha maji hutemwa na tumbo, eneo la juu la utumbo mdogo, kongosho na kibofu nyongo na kukiweka chakula kwenye hali ya majimaji. Chakula ambacho hakikumeng’enywa hufika sehemu ya chini ya utumbo mdogo na utumbo mpana kikiwa cha majimaji. Sehemu ya chini ya utumbo mdogo na hasa utumbo mpana hufyonza maji na kukifanya chakula ambacho hakikumeng’enywa kuwa na ugumu wa kiasi. Uwingi wa maji katika kinyesi hutokea endapo tumbo na/au utumbo mdogo unatema majimaji mengi mno, kama eneo la chini la utumbo mdogo na utumbo mpana havifyonzi maji ya kutosha, au kama chakula cha majimaji ambacho hakikumeng’enywa kinapita kwa kasi kubwa mno katika utumbo mdogo na utumbo mpana.

Namna nyingine ya kuelezea namna kuharisha kunavyotokea ni kuigawanya hali hiyo katika aina tano tofauti:

1. Ya kwanza inaitwa secretory diarrhea kwa sababu maji mengi mno yanatolewa kuingia ndani ya utumbo.

2. Ya pili inaitwa osmotic diarrhea ambapo molekuli ndogo zinazopita na kuingia kwenye utumbo mpana bila ya kumeng’enywa na kufyonzwa zinavuta maji na electrolyte kuingia kwenye utumbo mkubwa na kinyesi.

3. Ya tatu inaitwa motility-related diarrhea ambapo misuli ya utumbo hufanya kazi kwa haraka mno na kusafirisha vitu vilivyomo kwa haraka mno bila kutoa muda wa kutosha kwa maji na electrolyte kufyonzwa.

4. Ya nne si ya kawaida. Inaweza ikaelezewa kwa kuiita collagenous colitis. Hali hii ni kushindwa kwa utumbo mpana kufyonza maji na electrolyte kwa sababu ya uwingi wa makovu kwenye ngozi laini inayofunika utumbo huo. Kuvimba kwaweza pia kuwa na mchango kwenye hali hii.

5. Aina ya tano inaitwa inflammatory diarrhea na inahusisha hali zaidi ya moja. Mathalani, baadhi ya virusi, bakteria, na vimelea husababisha kuongezeka kwa utolewaji wa majimaji, au kwa kushambulia na kuharibu utando unaofunika utumbo mwembamba (inflammation stimulates the lining to secrete fluid) au kwa kutengeneza sumu (kemikali) ambazo pia husababisha utando wa utumbo mwembamba kutoa majimaji lakini bila kuleta uharibifu. Kushambuliwa kwa utumbo mwembamba na/au utumbo mpana na bakteria au wadudu wengine kunaweza kuongeza kasi ya upitaji wa chakula katika utumbo, hivyo kupunguza muda wa ufyonzwaji wa majimaji.

Kuharisha kwa kawaida hugawanywa katika aina mbili, acute na chronic.

1. Acute diarrhea ni kuharisha kunakodumu siku chache hadi wiki.
2. Chronic diarrhea kwa kawaida ni kuharisha kunakodumu zaidi ya wiki tatu.

Ni muhimu kutofautisha kati ya acute na chronic diarrhea kwa sababu huwa na vyanzo tofauti, huhitaji vipimo na tiba tofauti.

 

Kuna baadhi ya magonjwa na hali zinazosababisha kuharisha, ikiwa ni pamoja na:

Virusi. Viral gastroenteritis ni neno la kitaalamu likimaanisha maambukizi ya virusi kwenye tumbo na utumbo mwembamba. Viral gastroenteritis ndicho chanzo kikuu cha acute diarrhea duniani.

Dalili za viral gastroenteritis mara nying hudumu kwa saa 48-72 tu na ni pamoja na:

. kichefuchefu
. kutapika
. kusokota tumbo, na
. kuharisha

Tofauti na maambukizi ya bakteria kwenye utumbo mwembamba na utumbo mkubwa (bacterial enterocolitis), wagonjwa wa viral gastroenteritis hawana damu au usaha ndani ya kinyesi na hupata homa kidogo au kutopata homa kabisa. Virusi waletao viral gastroenteritis ni pamoja na Norwalk virus, cytomegalovirus na viral hepatitis. Rotavirus ni chanzo kikuu cha acute diarrhea kwa watoto wadogo.

. Bakteria. Bakteria waletao ugonjwa wa kuharisha mara nyingi hushambulia utumbo mwembamba na utumbo mpana na hali hii huitwa bacterial enterocolitis. Bacterial enterocolitis husababisha damu na usaha ndani ya kinyesi, homa, maumivu ya tumbo na kuharisha. Campylobacter jejuni ni bakteria anayejulikana sana kuleta acute enterocolitis. Bakteria wengine waletao enterocolitis ni pamoja na Shigella, Salmonella, na EPEC. Bakteria hawa huingia mwilini kwa kunywa maji yasiyo salama au kula chakula kisicho salama kama mboga za majani, kuku ma bidhaa za maziwa.

Enterocolitis inayoletwa na bacterium aitwaye Clostridium difficile si ya kawaida kwa sababu husababishwa na tiba ya antibiotic. Huyu ni bakteria anayeambukiza sana wagonjwa wakiwa hospitalini na kusababisha kuharisha.

– Traveler’s diarrhea
Kuna koo nyingi za bakteria aitwaye E.coli.  Bakteria wa E.coli ni wa kawaida na wanaishi ndani ya utumbo mwembamba na utumbo mpana bila madhara. Bakteria hawa wasioleta magonjwa wanaweza kuleta maradhi wakienezwa nje ya utumbo, kwa mfano, kwenye mkondo wa mkojo wanakoleta madhara kwenye kibofu cha mkojo na figo na huleta madhara wakiikingia ndani ya mfumo wa damu (Sepsis).

 

kuharisha safarini

 

Baadhi ya koo za E.coli wanaweza kuleta magonjwa ndani ya utumbo mwembamba na utumbo mpana. Bakteria hawa wabaya wanaweza kusababisha kuharisha kwa kutengeneza sumu (hawa huitwa enterotoxigenic E.coli au ETEC) au kwa kushambulia utando wa juu wa utumbo mwembamba na mpana na kusababisha hali iitwayo enterocolitis (hawa huitwa enteropathogenic E.coli au EPEC). Traveler’s diarrhea kwa kawaida husababishwa na ukoo wa ETEC wa E.coli ambao hutoa sumu inayosababisha kuharisha.

Watalii kwenye nchi za hali ya uvuguvugu na huduma duni za maji wanaweza kupata ETEC kwa kula chakula ambacho si salama kama matunda, mboga za majani, samaki, nyama mbichi, maji, n.k. Sumu kutokana na ETEC huleta kuharisha kwa ghafla, kusokota tumbo, kichefuchefu, na wakati mwingine kutapika.

. Vimelea. Kimelea aitwaye Giardia lamblia husababisha kuharisha na huwasumbua sana watu wanaopanda milima na kusafiri nchi za nje. Kimelea huyu hutokana na maji yasiyo salama (yaliyochafuliwa na kinyesi cha wanyama na binadamu). Kuharisha kutokana na kimelea huyu hakuambatani na damu wala usaha na huleta homa kidogo sana. Amoeba husababisha kuharisha kunakoambatana na damu na usaha ndani ya kinyesi.

Cryptosporidium ni kimelea anayesababisha kuharisha na huenezwa na maji yasiyo salama kwa sababu huweza kuvumilia dawa za kusafishia maji (chlorinaton).

. Madawa. Kuharisha kutokana na kutumia dawa ni kitu cha kawaida sana kwa sababu dawa nyingi husababisha kuharisha. Kuharisha kunakotokana na dawa kunajitambulisha kwa kuwa hali huanza mara baada ya kuanza matumizi ya dawa. Dawa ambazo mara nyingi huleta kuharisha ni antacids na virutubishi vilivyo na magnesium.

. Chakula. Food poisoning ni kuugua kwa kipindi kifupi kunakotokana na sumu zinazozalishwa na bakteria. Sumu hizi husababisha kusokota kwa tumbo na kutapika, hali inayosababisha utumbo mwembamba kutoa kiasi kikubwa cha maji na kusababisha kuharisha. Dalili za food poisoning mara nyingi huchukua pungufu ya saa 24. Baadhi ya bakteria hutengeneza sumu kwenye chakula kabla hakijaliwa lakini bakteria wengine hutengeneza sumu ndani ya chakula ndani ya utumbo baada ya kuwa kimeliwa.

Dalili huonekana baada ya saa chache endapo sumu zilitengenezwa ndani ya chakula kabla hakijaliwa. Inachukua muda mrefu zaidi dalili kuonekana kama sumu zinatengenezwa ndani ya utumbo. Kwenye hali hii ya pili, dalili hounekana baada ya saa 5 hadi 15.

Staphylococcus aureus ni mfano wa bacterium anayetengeneza sumu ndani ya chakula kabla hakijaliwa. Chakula hatarishi ni kama saladi na nyama ambavyo havikuwekwa ndani ya jokofu usiku mzima. Bakteria wa staphylococcus huzaliana ndani ya chakula na kutengeneza sumu. Clostridium perfringens ni mfano wa bakteria anayezaliana ndani ya chakula (mara nyingi chakula cha kusindikwa), na kutengeneza sumu ndani ya utumbo baada ya chakula kuliwa.

Lactose intolerance. Lactose ni sukari inayopatikana ndani ya maziwa na bidhaa nyingine za maziwa. Watu wanaopata shida kumeng’enya lactose wanaharisha baada ya kula bidhaa za maziwa. Lactose intolerance inaweza kuongezeka na umri kwa sababu vimeng’enya vya kusaidia umeng’enyaji wa lactose hupungua baada ya utoto.

Fructose. Fructose ni sukari inayopatikana ndani ya matunda na asali. Mara nyingine huongezwa kukoleza utamu ndani ya vinywaji. Watu wenye shida ya kumeng’enya fructose wanaweza kuharisha.

. Magonjwa mengine ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Kuharisha sugu kuna baadhi ya sababu nyingine, kama, ugonjwa wa Crohn’s, ulcerative colitis, ugonjwa wa celiac, microscopic colitis na irritable bowel syndrome.

 

Madhara Yatokanayo Na Kuharisha

 

Kuharisha kunaweza kusababisha kuishiwa maji (dehydration), hali inayoweza kusababisha kifo kama hatua hazikuchukuliwa. Kupungukiwa maji ni hatari sana hasa kwa watoto, wazee na watu wenye kinga za mwili zilizo dhaifu.

Dalili Za Kupungukiwa Maji Kwa Watu Wazima

. Kiu kali
. Kukauka midomo au ngozi
. Udhaifu, kizunguzungu
. Uchovu
. Mkojo wa rangi nyeusi.

Dalili Za Kukaukiwa Maji Kwa Watoto

Ni pampja na:

. Mtoto kutokojoa kwa saa tatu au zaidi
. Kukauka midomo au ulimi
. Homa ya zaidi ya nyuzi 102 F (39C)
. Kulia bila machozi
. Kuwa goigoi
. Kunywea kwa tumbo, kusinyaa macho na mashavu.

 

Tiba Ya Kuharisha

 

Mara nyingi tatizo la kuharisha huondoka lenyewe baada ya siku chache bila tiba yo yote. Kama tatizo linaendelea kwa muda mrefu, yafaa kumuona daktari ambaye anaweza kukushauri dawa au tiba nyingine.

Antibiotics

Antibiotics zinaweza kusaidia ikiwa kuharisha kunatokana na bakteria au vimelea. Kama virusi wanahusika, antibiotics hazitakuwa na msaada.

Tiba kurudishia maji

Daktari anaweza kukushauri kurudishia maji na chumvi kwenye mwili wako. Kwa watu wazima, hii itahusu kunywa maji, juisi au vyote.

Kunywa maji ni njia nzuri ya kurudishia maji mwilini, lakini maji hayana chumvichumvi na electrolytes – madini kama sodium na potassium -ambayo ni muhimu kwa mwili wako. Unaweza kupata electrolyte kwa kunywa juisi ya matunda kwa ajili ya potassium au kwa kunywa supu kwa ajili ya sodium. Lakini baadhi ya juisi, kama juisi ya apple huongeza hali ya kuharisha.

Kwa watoto wadogo, omba ushauri kutoka kwa daktari wako kuhusu matumizi ya oral rehydration solution (ORS), kama Pedialyte.

 

Katika mada nyingine, tutauzungumzia ugonjwa wa  kufunga choo (constipation). Usisite kuuliza maswali uliyo nayo au kutoa ushauri kuhusu uandishi wa mada yetu ya leo.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.