Tatizo La Kufunga Choo – constipation – Ni Nini Chanzo Chake?

 

kufunga choo

 

Kufunga choo ni tafsiri ya neno la kiingereza “constipation”. Kitaalamu, neno constipation linatumika kuelezea hali ambapo mtu anapata choo pungufu ya mara tatu kwa wiki. Na kama mtu atakosa choo kwa wiki kadhaa au muda mrefu, neno chronic constipation hutumika. Hali hii humpata kila mmoja wetu wakati fulani katika maisha. Muda unaopita kati ya choo kimoja hadi kupata choo kingine hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Kuna watu wanaopata choo mara tatu kwa siku, wengine hupata mara chache kwa wiki. Kwenda siku tatu bila kupata choo huchukuliwa kama ni muda mrefu sana. Baada ya siku tatu, choo huwa kigumu zaidi na ni shida kukitoa. Kukosa choo -constipation- huweza kuathiri utendaji kazi wa mtu. Tiba ya constipation hutegemea chanzo chake, lakini wakati mwingIne, hakuna chanzo maalumu kinachoeleweka.

 

Dalili Za Kufunga Choo

 

. Kupata choo pungufu ya mara tatu kwa wiki
. Kutoa choo chenye mabongebonge au kigumu
. Kutumia nguvu wakati wa kupata choo
. Kuhisi kama kuna kitu kimeziba kwenye rektamu kinachozuia choo kisitoke
. Kuhisi kwamba huwezi kutoa choo chote
. Kuhitaji msaada wakati wa kutoa choo, kama kutumia mikono kuliminya tumbo au kutumia vidole kuchokonoa kinyesi kwenye rektamu.

 

Sababu Za Kufunga Choo

 

Kufunga choo mara nyingi hutokea wakati mabaki au kinyesi kinapotembea taratibu mno ndani ya mkondo wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula au kinaposhindwa kutolewa nje kupitia rektamu, hali ambayo hukifanya kinyesi kuwa kigumu na kikavu. Tatizo sugu la kukosa choo linaweza kuwa na sababu nyingi:

 

sababu za kufunga choo

 

Kuziba kwenye utumbo mpana au rektamu

Kuziba ndani ya utumbo mpana au rektamu kunaweza kupunguza kasi au kusimamisha utembeaji wa kinyesi. Sababu zaweza kuwa:

. Mipasuko midogomidogo kwenye ngozi inayozunguka mkundu (anal fissure)
. Kuziba ndani ya utumbo (bowel obstruction)
. Saratani ya utumbo mkubwa (colon cancer)
. Kupungua upana wa utumbo mpana (bowel stricture)
. Saratani nyingine za kwenye tumbo zinazouminya utumbo mpana
. Saratani ya rektamu
. Kutuna kwa rektamu kupitia ukuta wa nyuma wa uke (rectocele)

Matatizo ya neva kuzunguka utumbo mpana au rektamu

Matatizo katika mfumo wa neva unaweza kusababisha neva za kuamuru misuli ya utumbo mpana na rektamu kubana na kusukuma chakula kwenye utumbo kutofanya kazi vizuri. Sababu zinaweza kuwa:

. Uharibifu wa neva za zinazosimamia shughuli za mwili (autonomic neuropathy)
. Multiple sclerosis
. Parkinson’s disease
. Kuumia kwa uti wa mgongo
. Kiharusi

Shida kwenye misuli inayohusika na utoaji choo

Matatizo ya misuli (pelvic muscles) inayohusika na utoaji wa mabaki ya chakula yanaweza kusababisha tatizo sugu la kufunga choo. Matatizo hayo ni pamoja na:

. Misuli ya pelvic kushindwa kujilegeza ili kuruhusu kinyesi kupita (anismus)
. Misuli kushindwa kufanya mawasiliano mazuri ya kubana na kuachia (dyssynergia)
. Kudhoofu kwa misuli ya pelvic

Hali zinazoathiri homoni za mwili

Homoni husaidia kuweka uwiano wa majimaji ndani ya mwili. Magonjwa na hali zinazoathiri uwiano wa homoni zinaweza kusababisha kufunga choo, ikiwa ni pamoja na:

. Kisukari
. parathyroid kufanya kazi zaidi (hyperparathyroidism)
. Ujauzito
. Kufanya kazi kwa kiwango cha chini kwa thyroid (hypothyroidism)

 

Madhara Ya Kufunga Choo

 

Tatizo la muda mrefu la kufunga linaweza kuleta madahara yafuatayo:

 

. Kuvimba veni kwenye mkundu (hemorrhoids). Kutumia nguvu wakati wa kupata dalili za kufunga choochoo kunaweza kusababisha uvimbe kwenye veni ndani na kuzunguka mkundu na kukusababisshia ugonjwa wa bawasiri.

. Kuchanika ngozi ndani ya mkundu (anal fissure). Choo kikubwa au kigumu kinaweza kusababisha michaniko midogomidogo kwenye mkundu.

. Choo kutotoka (fecal impaction). Tatizo sugu la kufunga choo linaweza kusababisha kujikusanya kwa choo kigumu kitakachokwama ndani ya utumbo.

. Utumbo kutoka nje ya mkundu (rectal prolapse). Kutumia nguvu wakati wa kupata choo kunaweza kusababisha kiasi fulani cha utumbo kunyumbuka na kuchungulia nje ya mkundu.

 

Hatua Za Kuchukua Kuzuia Tatizo La Kufunga Choo

 

. Kula zaidi chakula chenye nyuzinyuzi kama maharage, mboga za majani, matunda, nafaka nzima

. Kunywa maji mengi

. Fanya mazoezi ya mwili

. Jaribu kudhibiti msongo wa mawazo

. Usiahirishe kwenda chooni

. Jaribu kuweka ratiba maalumu ya kujisaidia, hasa baada ya kula.

 

Katika mada yetu nyingine tutalizungumzia tatizo la mwili kutetemeka (Parkinson’s disease). Usisite kuuliza maswali uliyo nayo au kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada hii.

 

 

 

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya muda wa kazi  kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.