Ujue Ugonjwa Wa Tumbo Kujaa Maji (Ascites)

 

ascites maji kujaa ndani ya tumbo

 

Katika mada yetu ya leo tutauzungumzia ugonjwa ambao husababisha maji kujaa ndani ya tumbo na mara nyingine kusababisha mgonjwa apate matatizo katika kupumua. Ni ugonjwa ambao baadaye huweza kusababisha maambukizi ya bakteria katika tumbo – spontaneous bacterial peritonitis (SBP) na/au kushusha kinga za mwili katika eneo hilo lililojaa maji. Ugonjwa huu huitwa ascites.

Kitaalamu ascites ni ugonjwa wa kujaa maji kusiko kwa kawaida ndani ya tumbo. Maji haya hujaa ndani ya nafasi iliyopo katikati ya tabaka mbili za utando laini ambazo kwa pamoja hujenga peritoneum, mfuko laini ambao hushikilia viungo vya ndani ya tumbo. Kwa kawaida kunakuwepo na maji kiasi ndani ya nafasi hiyo (hadi mililita 20 kwa mwanamke na pungufu ya hapo kwa mwanamme). Kitaalamu maji hayo yanapozidi mililita 25, mgonjwa hutajwa kuwa ana ascites.

 

Nini Chanzo Cha Maji Kujaa Katika Tumbo?

 

Kuna sababu nyingi za kujaa maji tumboni, ikiwa ni pamoja na tuberculosis, magonjwa ya figo, matatizo ya kongosho, na kufanya kazi kwa kiwango kidogo kwa tezi ya thyroid.

Chanzo cha maji kujaa ndani ya tumbo kinachobainishwa mara nyingi zaidi ni magonjwa ya ini ya hatua mbaya (cirrhosis). Pamoja na kwamba haijajulikana kwa uhakika ni vipi ascites inatokea, nadharia nyingi zinaamini kuwa kuongezeka kwa pressure kwenye mishipa ya kupeleka damu kwenye ini (portal hypertension) kuna mchango mkubwa zaidi kuliko sababu nyinginezo.

Kanuni ya msingi inafanana na ile inayosababisha edema kwenye maeneo mengine ya mwili ambapo kunakuwa na utofauti wa msukumo kwenye sehemu mbili zinazopakana, sehemu moja ya ndani ikiwa ya msukumo mkubwa na ya nje, kwa hapa ni uwazi wa tumbo, ikiwa na msukumo mdogo. Kuongezeka kwa pressure kwenye mishipa inayolilisha ini na kupungua kwa albumin (protini iliyopo ndani ya damu) vinaweza kuwa visababishi vya tofauti hizi za msukumo na kusababisha maji kujaa ndani ya tumbo.kujaa maji tumboni

Visababishi vingine vinavyochangia tatizo la maji kujaa tumboni ni chumvi na kuzuiwa kwa maji.  Damu iliyopo ndani ya mzunguko inaweza kuchukuliwa kuwa ni ndogo ikitazamwa na figo kwa sababu ascites inapoanza, hupunguza ujazo wa damu kwenye mzunguko. Hii huzifanya figo kuhifadhi chumvi na maji zaidi kufidia upungufu huo wa damu.

Matatizo mengine yanayohusiana na utofauti wa pressure ya pande mbili ni congestive heart failure na uharibifu wa figo ulio mkubwa ambao huzuia maji ndani ya mwili.

Mara chache sana mwongezeko wa pressure kwenye mishipa ya damu ya ini hutokana na kuzibwa kwa ndani au nje kwa mishipa hiyo, hivyo kusababisha portal hypertension bila uharibifu wa ini (cirrhosis). Mifano ya hali hii ni kama uvimbe kugandamiza juu ya mishipa hiyo kutoka kwenye uwazi wa tumbo au damu iliyoganda kuziba ndani ya mishipa hiyo na kusababisha mwongezeko wa pressure (mfano, Budd-Chiari syndrome.)

Ascites huweza kujitokeza vile vile kwa sababu ya kansa, ambayo huitwa malignant ascites. Ascites ya aina hii mara nyingi ni ishara ya kansa zilizokomaa ndani ya tishu zilizomo kwenye uwazi wa tumbo, kama saratani ya utumbo mkubwa, saratani ya kongosho, saratani ya tumbo, saratani ya matiti, lymphoma, saratani ya mapafu, au saratani ya ovari.

Ascites kutokana na kongosho huonekana baina ya watu wenye tatizo sugu la pancreatitis, au uvimbe wa kongosho. Sababu kuu ya pancreatitis sugu ni matumizi ya muda mrefu ya pombe.

 

Dalili Za Maji Kujaa Tumboni

 

Kunaweza kusitokee dalili zo zote za maji kujaa tumboni hasa wakati tatizo ni dogo (maji pungufu ya mililita 100-400 kwa mtu mzima). Kadiri maji yatakavyoongezeka, kipimo cha mzunguko wa tumbo na ukubwa wa tumbo vitaongezeka na kuonekana kwa macho. Maumivu ya tumbo, kukosa raha, na kuwamba kwa tumbo kutaonekana. Kukosa pumzi kutajitokeza pale tumbo litakapojaa sana kutokana na kuongezeka kwa pressure kwenye diaphragm na majimaji kuvuka diaphragm na kusababisha maji kuingia kwenye mapafu. Dalili nyingine zaweza kuwa kichefuchefu, kutosikia njaa,
uchovu, kuziba choo na haja ndogo ya mara kwa mara.

 

 

tiba ya tumbo kujaa maji

 

 

Kuna Aina Ngapi Za Ascites?

 

Kwa desturi, ascites hugawanywa katika aina kuu 2, transudative na exudative. Mgawanyo huu hutegemea kiwango cha protini kinachoonekana ndani ya maji hayo. Namna bora zaidi iliyotumika ni kutazama kiasi cha albumin kilichopo ndani ya maji (ascitic fluid) kikilinganishwa na kiasi kilichopo ndani ya albumin iliyopatikana ndani ya damu. Hii huitwa Serum Ascites Albumin Gradient au SAAG. Acites iliyotokana na pressure kwenye mishipa mikubwa ya damu ya ini (portal hypertension) huwa juu ya 1.1, na ascites kwa sababu nyingine huwa chini ya 1.1.

 

Tiba Ya Ugonjwa Wa Maji Kujaa Tumboni

 

Tiba ya ugonjwa wa maji kujaa tumboni kwa kiasi kikubwa itategemea chanzo halisi cha ugonjwa huu. Kwa mfano, peritoneal carcinomatosis au malignant ascites  itatibiwa kwa kufanya upasuaji kuondoa eneo lililoathirika na saratani au kwa chemotherapy, wakati ascites iliyotokana na matatizo ya moyo itadhibitiwa kwa dawa za kutibu chanzo cha moyo kushindwa kufanya kazi vizuri au  masharti katika kula.

Endapo maji kujaa tumboni kumetokana na uharibifu wa ini (cirrhosis), mgonjwa atasaidiwa kwa kushauriwa kupunguza matumizi ya chumvi na kumeza vidonge vya kutoa maji yaliyozidi mwilini. Vidonge hivyo vitamfanya atoe haja ndogo mara nyingi zaidi huku vikizuia utunzwaji wa maji mwilini. Pamoja na kuwa hii ni njia bora, aina nyingine za ugonjwa huu hazisikii tiba hii.

Hali ikiwa mbaya sana, operesheni ya kubadilisha ini inaweza kuwa ndiyo uamuzi wa mwisho. Tiba nyingine ni kama zifuatazo:

Paracentesis

Kama tiba nyingine hazikutoa msaada mkubwa au kama maji ni mengi sana, paracentesis hutumika. Hii ni njia ambapo daktari huingiza sindano tumboni na kutoa maji yaliyozidi nje ya mwili.

 

 

 

 

Lengo ni kupunguza msukumo ndani ya tumbo, na kumfanya mgonjwa ajisikie vizuri. Maji yanayotolewa yanaweza kufika lita 5, ingawa kuna wagonjwa wenye hali mbaya zaidi ambao hutolewa maji zaidi ya lita 10.

 

Shunts

Endapo maji yamejaa tumboni kutokana na kansa, madaktari wanaweza kutumia mpira kuondoa maji kutoka kwenye tumbo na kuyaingiza kwenye mtiririko wa damu.

Daktari huchoma sindano kwenye neva ya shingoni na kuweka shunt kupitia
kifuani. Shunt hiyo huunganisha uwazi wa tumbo na shingo, na kuingia kwenye veni. Na hivyo maji hutiririka kupitia mrija huo hadi kwenye mzunguko wa damu.

Chemotherapy

Chemotherapy inaweza kutumika kudhibiti saratani. Inaweza kufanywa kutumia mpira unaoingizwa tumboni, ingawa hakuna ushahidi wa kuwa njia hii ina matokeo bora.

 

Katika mada yetu nyingine tutajadili tatizo la maji ndani ya mwili – edema.  Tafadhali usisite kutoa maoni yako kuhusu mada hii ya leo au kutuuliza maswali. Ni furaha kwetu kuona kuwa tumekujibu kwa wakati.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.