Ugonjwa Wa Kifafa; Ni Nini Chanzo Cha Kifafa?

 

 

Vitu vichache sana vinaweza kulinganishwa na kumwona mgonjwa wa kifafa akianguka. Mtu aliyeshikwa na kifafa haswa, anaweza kubaki ameduwaa kwa sekunde chache, anaweza kulia, kuanguka chini na kuzirai, akatupa mikono na miguu hovyo, akatoa mapovu mdomoni na mara nyingine kujikojolea. Baada ya muda mfupi, anarudiwa na fahamu, lakini akiwa mchovu. Hii ndiyo picha walio nayo wengi wakisikia neno kifafa. Lakini kifafa cha picha hii ni aina moja tu ya vifafa vilivyopo. Zipo aina nyingine nyingi na kila moja ikiwa na dalili tofauti.

Kifafa ni tatizo la kwanza kabisa la ubongo kuelezewa. Limetajwa enzi za Babiloni zaidi ya miaka 3,000 iliyopita. Mtu wa kwanza kabisa kuelezea kiusahihi kwamba kifafa ni ugonjwa wa akili alikuwa Hippocrates.

Mtu ye yote anaweza kushikwa na kifafa. Kifafa huwashika watu wa jinsia zote, wanaume na wanawake wa jamii zote, koo tofauti na wa umri wo wote.

Kifafa Ni Nini?

Kifafa ni hitilafu kwenye ubongo ambako mikusanyiko ya seli za neva, au neurons, katika ubongo wakati mwingine hutoa ishara ndivyo sivyo. Neurons kwa kawaida hufanya kazi ya kutoa mawimbi (electrochemical impulses) ambayo hutua kwenye neurons nyingine, viungo, na misuli na kuzalisha mawazo, hisia, na vitendo. Wakati wa kifafa, mtiririko huu wa shughuli za neurons hutibuka, na kuleta hisia ngeni, na tabia , au wakati mwingine maungo kutingishika, misuli kutingishika, na kupoteza fahamu. Wakati mtu ameshikwa na kifafa, neurons huweza kutema taarifa hadi mara 500 kwa sekunde, mara dufu kuliko hali ya kawaida. Kwa wengine hali hii hutokea kwa nadra, lakini wengine hutokewa zaidi ya mara 100 kwa siku.

 

Kifafa hakiambukizi na hakisababishwi na ugonjwa wa akili au mtindio wa ubongo. Kuna watu wenye mtindio wa ubongo walio na kifafa, lakini kifafa hakimaanishi kuwa utapata matatizo ya akili. Watu wengi wenye kifafa wana akili za kawaida na wengine wana akili za ziada. Watu mashuhuri waliosemekana kuwa na kifafa ni pamoja na mwandishi wa Urusi Dostoyevsky, mwana falsafa Socrates, mwanajeshi mahiri Napoleon, na mgunduzi wa baruti, Alfred Nobel, mwanzilishi wa Nobel Prize. Baadhi ya wana-olympiki mashuhuri na wanariadha walikuwa na kifafa. Mara nyingine kifafa huathiri akili, hasa pale kinapokuwa cha nguvu. Lakini kifafa cha kawaida hakijathibitishwa kuleta madhara kwenye ubongo.

Kifafa kwa sasa hakijapata tiba kamili, na kwa baadhi ya watu hutoweka chenyewe. Utafiti mmoja ulionyesha kuwa watoto waliokuwa na kifafa ambacho hakikufahamika chanzo chake, walikuwa na asilimia 68 haadi 92 ya kupona walipofika miaka 20 baada ya kugunduliwa. Watu wenye umri mkubwa au watoto wenye kifafa cha nguvu walionyesha kuwa na asilimia ndogo sana ya kupona.

Dalili za kifafa

Kwa sababu kifafa husababishwa na hitilafu katika ufanyaji kazi wa ubongo, kifafa kinaweza kuathiri shughuli yo yote inayoendeshwa na ubongo. Baadhi ya dalili zikiwa:

. Kuchanganyikiwa kwa muda
. Kipindi cha kuduwaa
. Kutupa mikono na miguu ovyo
. Kupoteza fahamu
. Athari za kiakili kama woga na wasiwasi

Dalili hutofautiana kulingana na aina ya kifafa. Kwa kawaida, mtu mwenye kifafa huona dalili zile zile kila wakati.

Madaktari hugawanya kifafa katika makundi mawili, focal na generalized, wakizingatia jinsi tatizo katika ubongo linavyoanza.

Focal Seizures

Pale kifafa kinapotokea kutokana na dosari katika eneo moja la ubongo, tatizo hili huitwa focal (partial) seizure. Aina hii hugawanyika katika aina ndogo mbili:

. Focal seizures without loss of consciousness. Kifafa hiki hakimpotezei mtu fahamu. Kinaweza kubadilisha hisia au kubadili mwonekano, harufu, ladha au sauti ya vitu. Kinaweza kusababisha kiungo cha mwili kucheza chenyewe, kama mkono au mguu, na dalili nyingine za pamoja za vitu kuchoma mwilini, kizunguzungu na vitu kuangaza.

kifafa msichana

. Focal seizures with impaired awareness. Kifafa hiki huambatana na mabadiliko katika au kupoteza ufahamu. Unaweza kuduwaa na kukosa mwitiko wa vitu vya kwenye mazingira au kufanya miondoko ya kujirudiarudia kama kusugua mikono, kutafuna, kumeza au kutembea ukilizunguka eneo moja.

Generalized seizures

Kifafa kinachotokea kikihusisha maeneo yote ya ubongo huitwa generalized seizure. Kuna aina ndogo sita za kifafa cha aina hii:

. Absence seizures. Kifafa hiki huonekana zaidi kwa watoto na kinatambulika kwa kuduwaa na miondoko ya mwili isiyo ya kawaida kama macho kukonyeza au kulamba midomo.

. Tonic seizures. Kifafa hiki husababisha kukakamaa kwa misuli. Kifafa hiki kwa kawaida huathiri misuli ya mgongoni, mikono na miguu na huweza kusababisha uanguke ardhini.

. Atonic seizures. Kifafa hiki hukusababishia ukose udhibiti wa misuli hali ambayo huweza kukufanya uzirai au uanguke.

. Clonic seizures. Hii huamabatana na kucheza kwa misuli kunakojirudiarudia kwa mpango.

. Myoclonic seizures. Hii hujitokeza kwa kucheza kwa misuli ya mikono na miguu kwa ghafla na kwa muda mfupi.

. Tonic-clonic seizures. Kifafa hiki ndicho kinachoweza kukufanya kupoteza fahamu ghafla, kukakamaa kwa mwili na kutetemeka, na wakati mwingine kujikojolea au kung’ata ulimi.

Chanzo Cha Kifafa Ni Nini?

Kifafa ni tatizo linaloweza kuwa na vyanzo vingi. Kitu cho chote kitakachovuruga mtiririko wa kawaida wa ufanyaji kazi wa neuron – kuanzia ugonjwa, uharibifu wa ubongo hadi dosari katika ukuaji wa ubongo – kinaweza kusababisha kifafa.

Kifafa kinaweza kutokea kwa sababu ya dosari za usokotwaji wa ubongo, kutokuwepo uwiano baina ya kemikali ziitwazo neurotransmitters, au mchanganyiko wa  haya mawili. Wanasayansi wanaamini kuwa baadhi ya watu wenye kifafa wana viwango vikubwa sana vya excitatory neurotransmitters ambacho huongeza shughuli za neurons, wakati wengine wana viwango vidogo mno vya inhibitory neurotransmitters ambazo hupunguza shughuli za neurons kwenye ubongo. Hali hizi zote zinaweza kusababisha kuongezeka kwa shughuli za neurons na kusababisha kifafa.

kifafa sababu

Wakati mwingine ubongo hujaribu kujikarabati baada ya maumivu ya kichwa, kiharusi au tatizo jingine linaweza kwa bahati mbaya kusababisha miunganiko isiyo sahihi ya neva ambayo itasababisha kifafa. Usokotwaji wa ubongo usio sahihi unaotokea wakati wa ukuaji wa ubongo unaweza pia kuvuruga shughuli za neuron na kusababisha kifafa.

Sababu za kiurithi. Kifafa ambacho kinajitambulisha kwa jinsi kinavyotokea, au kwa eneo la ubongo linaloathirika, huonekana kwenye familia fulani. Kwa jinsi hiyo, kinaonekana kuwa ni cha urithi.

Kuumia Kwa Kichwa. Kuumia kichwa kama kwa ajali ya gari au ajali nyingine kunaweza kusababisha kifafa.

Hali ya ubongo. Vitu vinavyoweza kuleta madhara kwenye ubongo, kama uvimbe ndani ya ubongo au kiharusi, vinaweza kisababisha kifafa. Kiharusi kinaongoza kama chanzo cha kifafa kwa watu wazima wa umri wa zaidi ya miaka 35.

Magonjwa ya kuambukiza. Magonjwa ya kuambikiza kama homa ya uti wa mgongo (meningitis), UKIMWI na viral encephalitis, yanaweza kusababisha kifafa.

Kuumia kabla ya kuzaliwa. Kabla ya kuzaliwa, watoto huweza kuumia ubongo kwa sababu kama ya maambukizi kutoka kwa mama, lishe duni au kukosa oksijeni ya kutosha. Kuumia huku kwa ubongo kunaweza kusababisha kifafa.

Pamoja na hatari nyingine nyingi zinazoweza kumpata mtu mwenye kifafa, yafuatayo yaweza pia yakatokea:

. Status epilepticus. Ni hali ambayo inamwathiri mtu ambaye anashikwa na kifafa mara kwa mara na kwa muda mrefu unaozidi dakika tano au kama anashikwa na kifafa mara nyingi bila kupata ufahamu kamili katikati. Watu wenye hali hii wana yamkini kubwa ya kupata madhara ya kudumu kwenye ubongo au kufariki.

. Sudden unexpected death in epilepsy (SUDEP). Watu wenye kifafa mara chache wanakuwa kwenye hatari ya kufa ghafla. Kiujumla, asilimia 1 ya watu wenye kifafa hufa kwa SUDEP.

Hatua Za  Kuchukua Ukimwona Mtu Ameshikwa Na Kifafa

Ukimwona mtu ameshikwa na kifafa akirusha viungo vyake ovyo na/au kupoteza ufahammu, unashauriwa kufanya yafuatayo kumsaidia:

kifafa msaada

1. Mgeuze mwathirika alale kiubavu ili asizibwe pumzi na matapishi au maji maji mengine
2. Weka kitu laini chini ya kichwa chake (kama mto)
3. Legeza nguo na vitu vingine vinavyombana mwilini au shingoni
4. Acha eneo la wazi kumzunguka ili apate hewa ya kutosha
5. Usimzuie kutembea labda tu kukiwa na hatari mbele yake
6. Usiweke cho chote kinywani mwake, hata dawa au maji. Vitu hivi vyaweza kumletea madhara ya kuziba pumzi, au kujiumiza taya, ulimi, meno.
7. Ondoa vitu vyote vyenye ncha kali ambavyo mwathirika anaweza kuviangukia akiwa ameshikwa na kifafa
8. Kaa na mwathirika hadi arudiwe na fahamu

Mada zetu nyingine zitachambua  chanzo na dalili za tatizo la hofu ya ghafla (panic attack) na tatizo la kuwa wasiwasi (anxiety disorder). Usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali kuhusu mada zetu. Ni furaha sana kwetu kuona kuwa tumekujibu vizuri.

Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini, kwa kujaza fomu, au kututumia barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu ndani ya  saa za kazi kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.