Fistula Ni Nini?

Fistula ni neno ambalo husikika mara nyingi sana na hasa kuhusiana na magonjwa  ya akina mama. Lakini hasa fistula ni tatizo gani? Mada yetu ya leo itauchambua ugonjwa huu kwa kina. Baada ya kuisoma mada hii utajua chanzo cha fistula, dalili ambazo ukiziona ujue kuwa una tatizo hili na mwisho utakuwa umepata maelezo ya jinsi ya kujitibu na tatizo hili la fistula.

Fistula huunganisha sehemu mbili za mwili ambazo kwa kawaida huwa haziungani. Fistula inaweza kutokea kwenye sehemu nyingi sana za mwili. Baadhi huondoka baada ya tiba, wakati nyingine hujirudiarudia na kuhitaji uangalizi wa juu. Fistula nyingi si za kawaida na huja wakati ambapo hukuzitegemea. Lakini fistula nyingine (kama dialysis fistulas) hutengenezwa kwa upasuaji ili kukusaidia.

Fistula Maana Yake Nini?

Fistula ni sehemu inayounganisha sehemu mbili ambazo kwa kawaida hazina mwunganiko. Huwa ni namna ya mkondo au njia, na inaweza kuruhusu vitu vya mwilini (kama usaha, kinyesi au damu) kusafiri hadi sehemu isikotakiwa.

Fistula huweza kutokea kati ya viungo viwili vya mwili au kati ya mishipa miwili ya damu. Inaweza kutokea ndani kabisa ya mwili au ikaongoza toka ndani ya mwili hadi sehemu ya nje juu ya ngozi ya mwili.

Kuna aina nyingi za fistula ambazo zinaweza kutokea maeneo mbalimbali ya mwili wako -pamoja na viungo vyako vya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula au vya uzazi. Fistula kwa kawaida ni kitu kibaya kinachohitaji tiba. Lakini watu wa afya hutengeneza aina fulani za fistula kama namna ya tiba (kwa mfano, fistula kati ya ateri na veni ili kuwezesha dialysis).

Fistula huweza kusababisha maumivu na dalili nyingine ambazo zitaleta usumbufu katika maisha yako ya kila siku. Lakini mara nyingi hutibika, mara nyingi kwa upasuaji. Yaweza ikatokea kuwa fistula ikatibiwa na isirudi tena. Lakini watu wengine watahitaji tiba kwa miezi au miaka kadhaa ambazo zitaondoka na kurudi au kuleta madhara mengineyo.

Aina Za Fistula

Fistula nyingi huvuruga utendaji kazi wa mwili. Watu wa afya wanagundua na kutibu aina zifuatazo za fistula:

Anal fistula. Huu ni mkondo kutoka ndani ya sehemu ya haja kubwa hadi nje kwenye ngozi. Hii hutokana na maambukizo ya wadudu (na jipu linalotokea sehemu ya haja kubwa) kwenye tezi zinazozunguka tundu la haja kubwa. Baadhi ya magonjwa kama Crohn’s disease yanaongeza uwezekano wa maambukizo ya wadudu na fistula.

Arteriovenous (AV) fistula. Fiastula ya AV ni muunganiko wa moja kwa moja kati ya ateri na veni -mishipa miwili ya damu ambayo huchukua njia tofauti. Ajali huwa ndiyo sababu kubwa. Lakini si fistula zote za AV zenye madhara. Watu wa afya aghalabu hutengeneza muunganiko huo kwa watu wenye matatizo ya figo wanaohitaji dialysis.

Aortoenteric fistula. Huu ni muunganiko unaotishia maisha kati ya aorta na utumbo mdogo. Unaweza kusababiabisha GI bleeding na kifo kama tiba haitatolewa kwa wakati (upasuaji wa dharura). Kuna primary na secondary aortoentric fistula. Primary fistulas kwa kawaida hutokana na aortic aneurism, uvimbe au maambukizo kama tubeculosis au syphilis. SEcondary fistula ni matokeo yasiyotegemewa ya upasuaji wa aorta.

Perilymphatic fistula. Hili ni tundu kwenye utandolaini unaotenganisha eneo la kati la sikio na eneo la ndani la sikio. Tundu hili linaruhusu majimaji kutiririka kutoka sehemu ya ndani ya sikio hadi sehemu ya kati ya sikio, na kusababisha mabadiliko ya msukumo wa hewa yanayoathiri uwezo wa kusikia na balance. Watu wengi wanahitaji upasuaji, lakini wachache wanaweza kupona kwa kupumzika kitandani.

Tracheoesophageal fistula (TEF). Huu ni muunganiko kati ya bomba la pumzi (trachea) na umio (esophagus). Hili ni tatizo ambal mara nyingi watoto wanazaliwa nalo. Watu wazima wanaweza kupata tatizo hili kutokana na saratani au magonjwa mengine.

Vaginal fistula. Fistula hii ni uwazi unaotokea kwenye kuta za uke. Uwazi huu huunganisha uke na kiungo kingine cha jirani kama nyumba ya mimba (uterus), bladder, sehemu ya haja kubwa, utumbo mpana au utumbo mdogo. Majina mengine hutumika ambayo yanaelezea zaidi kama vesicovaginal fistula (muunganiko kati ya uke na bladder) au rectovaginal fistula (muunganiko kati ya uke na sehemu ya haja kubwa). Obstetric fistula ni fistula inayotokana na uzazi.

Wakati mwingine watu wa afya hutengeneza fistula ili kuweka sawa hali ya mwili. Fistula hizi huweza kuwa za muda mfupi au za mmuda mrefu. Mfano mmoja ni mucous fistula. Hii huunganisha utumbo mdogo au utumbo mkubwa na stoma (uwazi uliotengenezwa kwa upasuaji kwenye ngozi au tumbo). Stoma huwasaidia watu wenye colostomy (uwazi kwenye utumbo mpana kupitia ngozi ya tumbo) au ileostomy (uwazi wa kwenye utumbo mdogo kupitia ngozi ya tumbo).

Dalili Na Chanzo Cha Fistula

Dalili za fistula hutofautiana kutokana na aina yake. Jedwali hapa chini limeorodhesha baadhi ya dalili zinazoweza kutokea kulingana na aina ya fistula.

Anal fistula:  Maumivu kwenye au kuzunguka sehemu ya kutolea haja kubwa, kutokwa usaha,
kinyesi au damu katoka sehemu yo yote iliyo karibu na sehemu ya haja kubwa.

Aortoenteric fistula:  Maumivu ya tumbo; matapishi yenye damu au yenye mwonekano wa kahawa iliyosagwa, kinyesi cheusi au damu ndani ya kinyesi.

Arteriovenous fistula:  Uvimbe kwenye eneo la fistula, mabadiliko ya rangi ya ngozi,kutuna kwa veni, ngozi ya joto ikiguswa

Perilymphatic fistula:  Kupoteza uwezo wa kusikia, kuhisi kama masikio yamejaa, kizunguzungu, milio kwenye masikio, matatizo ya balance

Tracheoesophageal fistula:  Maambukizo ya mara kwa mara ya kwenye mapafu, shida wakati wa kumeza, kikohozi

Vaginal fistula:  Mkojo unachuruzika ukeni, hewa, kutoka kinyesi au usaha kwenye uke; maumivu wakati wa tendo la ndoa.

 

Nini Husababisha Fistula?

 

Sababu hutofautiana kulinganan na aina ya fistula. Kwa ujumla, sababu zaweza kuwa:

. Uvimbe au maambukizo ya wadudu
. Kuumia kwenye eneo husika la mwili
. Matokeo kutokana na upasuaji
. Matokeo ya tiba, kama mionzi
. Mabadiliko wakati wa ukuaji wa kichanga tumboni

Tiba Ya Fistula Ni Nini?

Dawa au/na upasuaji ndizo tiba za kawaida za fistula.

Tatibu wako anaweza kuamua kukupa dawa za kupunguza uvimbe au kubadili utendaji wa mfumo wako wa kinga za mwili. dawa hizi zinaweza kusaidia katika kutibu chanzo cha fistula. Kama una maambukizo, unaweza ukahitaji antibiotics. Kama dawa si chaguo bora au hazisaidii, unaweza ukahitaji upasuaji.

Katika mada yetu nyingine tutauzungumzia ugonjwa wa kukojoa kitandani. Usisiste kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada yetu.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu NDANI YA MUDA WA KAZI kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.