
Tachycardia ni neno la kitaalamu linalotumika kuelezea hali ambapo mapigo ya moto yanazidi 100 kwa dakika moja. Kwa kawaida mapigo ya moyo huwa kati ya 60 na 100 mwili ukiwa umetulia. Namna nyingi ya mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida (arrhythmias) huweza kusababisha tachycardia.
Mapigo ya moyo kuwa juu si hali ambayo ni tatizo kila wakati. Kwa mfano, mapigo ya moyo kwa kawaida hupanda wakati wa mazoezi au baada ya kupata msongo wa mawazo (stress).
Kwa sababu moyo unapiga mara nyingi mno, unakosa muda wa kutosha wa kujaza damu kati ya mapigo. Hali hii huweza kuwa ni ya hatari endapo moyo utashindwa kusambaza damu na oksijeni kwenye seli zako zote.
Tachycardia inaweza isiwe na dalili zo zote au kusababisha madhara. Lakini wakati mwingine ni ishara ya kuwepo kwa tatizo la kiafya linalotakiwa kufanyiwa uchunguzi. Aina nyingine za tachycardia huweza kuleta matatizo makubwa ya kiafya endapo hatua hazitachukuliwa. Matatizo hayo ni pamoja na shinikizo la moyo, kiharusi au kufa kwa ugonjwa wa moyo.
Tiba kwa tatizo la mapigo ya moyo kwenda kasi ni pamoja na vitendo au miondoko maalumu, dawa, cardioversion, au upasuaji wa kudhibiti kasi ya mapigo ya moyo.
Aina Za Tachycardia
Kuna aina nyingi za tachycardia. Sinus tachycardia ni kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo kunakotokana na mazoezi au msongo wa mawazo.
Aina nyingine huwekwa kwenye makundi kulingana na sababu na sehemu ya moyo inayosababisha kupanda kwa mapigo. Aina zinazooneka mara nyingi ni pamoja na:
. Atrial fibrillation, au AFib. Hii ndiyo aina kuu ya tachycardia. Ishara za umeme (electrical signals) za kiholela, zisizo na mpangilio huanza kwenye vyumba vya juu vya moyo, viitwavyo atria. Ishara hizi huanzisha mapigo ya haraka -Afib. Mapigo haya ya haraka yanaweza kuwa ya muda mfupi. Lakini wakati mwingine huweza kuendelea hadi tiba itolewe.

Moyo ukiwa kwenye AFib, atria zinaweza kupiga zaidi ya mapigo 300 kwa dakika. Vyumba vya chini vitajaribu kwendana na kasi ya vyumba vya juu, na kufikia mapigo 100-200 kwa dakika. Kasi kwenye vyumba vya chini vinaweza kushuka kwa kupewa dawa, lakini vya juu hubakia na kasi ya juu.
AFib kwa yenyewe si tishio kwa maisha, lakini baina ya baadhi ya watu huweza kuleta dalili zinazosumbua, au kuongeza uwezekano wa hatari nyingine. AFib inahusishwa sana na stroke -watu wenye AFib wana yamkini ya kupata stroke mara tano zaidi ya wengine. AFib ya muda mrefu pia inaweza kuhusishwa na kufeli kwa moyo kama tiba sahihi hazitatolewa. Tiba sahahi ya AFib hurudisha mapigo ya moyo kuwa sawa au kuyadhibiti, huondoa uwezekano wa kuziba kwa damu na stroke.
. Atrial flutter. Atrial flutter hufanana na Afib, yaani hutokana na mawimbi ya umeme yasiyo na mpangilio, lakini mapigo huwa yana mpangilio zaidi. Vipindi vya atrial flutter huweza kuondoka vyenyewe au vikahitaji tiba. Watu wenye atrial flutter mara nyingi wana Afib wakati mwingine.
. Ventricular tachycardia. Mapigo haya yasiyo na mpangilio huanzia kwenye vyumba vya chini vya moyo, viitwavyo ventricles. Mapigo haya ya haraka hayaruhusu vyumba hivi kujaa na kujiminya ili kusukuma damu kwenye mwili. Vipindi vinaweza kuwa vifupi na vikadumu sekunde chache bila kuleta madhara.
. Supraventricular tachycardia (SVT). Supraventricular tachycardia ni neno pana linalojumuisha mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio yanayoanzia juu ya vyumba vya chini vya moyo. Supraventricular tachycardia husababisha vipindi vya moyo kudunda kwa nguvu vinavyoanza na kukata ghafla.
. Ventricular fibrillation. Hali hii mbaya ya mapigo ya moyo inaweza kuleta maafa ikiwa haitatulizwa katika dakika chache. Ishara za umeme za haraka na sizizo na mpango husababisha vyumba vya chini vya moyo kutetema badala ya kujiminya kwa mpango mzuri. Watu wengi wenye aina hii ya hitilafu katika mapigo ya moyo wana magonjwa ya moyo au walipata kuumia vibaya, kama kupigwa na radi.
Dalili Za Tachycardia
Watu wengine wana tachycardia na hawaoni dalili zo zote. Mapigo ya moyo ya haraka yanaweza kugundulika wakijipima afya au kuchukua vipimo vya moyo kwa sababu nyingine.

Kwa kawaida, tachycardia huwa na dalili zifuatazo:
. Moyo kukimbia, kupiga kwa nguvu kwenye kifua, hali iitwayo palpitations.
. Maumivu ya kifua
. Kuzimia
. Kusikia kichwa kuwa chepesi
. Mapigo ya haraka
. Kubanwa pumzi.
Chanzo Cha Mapigo Ya Moyo Kuwa Juu
Tachycardia ni kuogezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo kwa sababu yo yote ile. Ikiwa mapigo ya moyo yameongezeka kwa sababu ya mazoezi au msongo wa mawazo, hali hii huitwa sinus tachycardia. Sinus tachycardia ni dalili, na si ugonjwa.
Matatizo mengi ya moyo yanaweza kuleta mapigo ya juu ya aina tofauti. Mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio, yaitwayo arrhythmias, ni moja ya sababu. Mfano wa mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio ni atrial fibrillation (AFib).
Vitu vingine vinavyoweza kuleta tachycardia ni pamoja na:
. Homa
. Matumizi ya pombe ya kupita kiasi, yanayotafsiriwa kama vinywaji 14 au zaidi kwa wiki kwa mwanamme, au vinywaji 7 au zaidi kwa wiki kwa mwanamke.
. Kuacha kunywa pombe
. Caffeine nyingi mno
. Pressure ya juu au chini
. Mabadiliko ya viwango vya madini ndani ya mwili, yaitwayo electrolytes. Mifano ni potassium, sodium, calcium na magnesium.
. Baadhi ya dawa
. Tezi ya thyroid inayofanya kazi kupita kiasi (hyperthyroidism)
. Upungufu wa chembechembe nyekundu za damu (anemia)
. Kuvuta sigara au kutumia nicotine
. Kutumia vitu haramu vya kujisisimua kama cocaine au methamphetamine
. Mshituko wa moyo.
Wakati mwingine sababu kamili ya tachycardia huwa haieleweki.
Moyo Unadundaje?
Ili kujua sababu ya tachycardia, kujua namna moyo unavyofanya kazi inaweza kusaidia.
Moyo una vyumba vinne:
. Vyumba viwili vya juu huitwa atria
. Vyumba viwili vya chini huitwa ventricles.

Ndani ya chumba cha juu cha upande wa kulia kuna seli zinazoitwa sinus node. Katika kila pigo la moyo, mkusanyiko wa seli za sinus node hutoa ishara za umeme, ziitwazo impulses.
Ishara hizo husambaa kwenye vyumba vya juu vya moyo. Kisha ishara hizo hufika kwenye kikundi cha seli kiitwacho AV node, ambapo mara nyingi hupunguza kasi. Kisha ishara huteremka kwenye vyumba vya chini viitwavyo ventricles. Ishara za ventricles hufanya moyo ujikamue, na kusukuma damu sehemu zote za mwili.
Moyo ukiwa na afya njema, mfululizo huu wa ishara huendelea vizuri. Mapigo moyo ukiwa umepumzika huwa kati ya 60 hadi 100 kwa dakika. Lakini, kwenye hali ya tachycardia, kuna kitu kinachofanya moyo udunde zaidi ya mara 100 kwa dakika.
Ufanye Nini Kuzuia Tachycardia
Njia bora ya kuzuia tachycardia ni kutunza afya ya moyo. Fanya vipimo vya moyo mara kwa mara. Kama una ugonjwa wa moyo, zingatia tiba. Tumia dawa zote kama ulivyoagizwa.
Jaribu kufanya yafuatayo kuzuia magonjwa ya moyo na kuiweka sawa afya ya moyo:
. Usivute sigara
. Kula chakula chenye chumvi na mafuta (saturated fat) kidogo
. Fanya mazoezi ya angalau dakika 30 kwa siku mara nyingi katika wiki
. Tunza uzito wako wa mwili
. Punguza na dhibiti msongo wa mawazo
. Dhibiti pressure yako, cholesterol na sukari
. Hakikisha unapata usingizi wa kutosha. Watu wazima yafaa kupata saa 7-9 za usingizi kila siku.
Madhara Ya Tachycardia
Mapigo ya moyo yakienda kasi mno, moyo unaweza kushindwa kusukuma damu ya kutosha kwenda mwilini. Matokeo yake, viungo na tishu vinaweza kukosa damu ya kutosha.
Madhara ya tachycardia yanategemeana na:
. Aina ya tachycardia
. Moyo unakwenda mbio kiasi gani
. Hali ya moyo kwenda mbio inadumu kwa muda gani
. Kama kuna matatizo mengine ya moyo au la.
Matatizo yanayoweza kujitokeza ni pamoja na:
. Kuziba kwa mishipa ya damu, hali inayoweza kusababisha mshitiko wa moyo au kiharusi. Dawa za kupunguza mnato wa damu zinaweza kusaidia kupunguza hatari hii.
. Kuzirai kwa mara kwa mara au kupoteza fahamu
. Mshituko wa moyo
. Moyo kusimama ghafla. Hii mara nyingi inahusiana na ventricular tachycardia au ventricular fibrillation.
Tiba Ya Tachycardia
Lengo la kutibu tachycardia ni kupunguza kasi ya mapigo ya moyo na kuzuia hali hiyo isitokee tena baadaye.
Kama kuna tatizo jingine linalosababisha tachycardia, kutibu chanzo hicho kunaweza kupunguza au kuondoa vipindi vya tachycardia.
Kupunguza Kasi Ya Moyo Unaokwenda Mbio
Moyo unaokwenda mbio unaweza kujirekebisha wenyewe. Lakini wakati mwingine dawa au tiba za aina nyingine zitahitajika kupunguza kasi ya mapigo ya moyo.
Njia za kupunguza kasi ya mapigo ya moyo ni pamoja na:
. Vagal maneuvers. Vitendo rahisi lakini mahsusi kama kukohoa, kuchuchumaa kama unajisadia au kuweka kipande cha barafu kwenye paja la uso vinaweza kupunguza kasi ya mapigo ya moyo. Madaktari wako wanaweza kukushauri kufanya vitendo fulani pale unapobanwa na kipindi cha tachycardia. Vitendo hivi huiathiri neva ya vagus. Neva hii husaidia katika kuyadhibiti mapigo ya moyo.
. Dawa. Endapo vitendo vya vagal havisaidii katika kupunguza kasi ya mapigo ya moyo, dawa zinaweza kutolewa ili kurekebisha mapigo ya moyo.
. Cardioversion. Moyo unashituliwa kwa kutumia umeme kupitia kwenye kifua na kurudisha kasi ya mapigo ya moyo. Njia hii hutumika hasa kama kuna dharula au wakati vitendo vya vagal au dawa vikishindwa. Cardioversion inaweza pia kufanywa pamoja na dawa.
Kuzuia Vipindi Vya Moyo Kwenda Mbio Hapo Baadaye
Tiba ya tachycardia ni kuchukua hatua za kuzuia moyo usiende mbio. Tiba inaweza kuwa dawa, kuwekewa vifaa au upasuaji wa moyo.
. Dawa. Dawa mara nyingi hutumia kudhibiti kasi ya mapigo ya moyo
. Catheter ablation. Katika utaratibu huu, daktari hupenyeza vijibomba vyembamba vinavyokunjika (catheters) kupitia mshipa wa damu, mara nyingi maeneo ya kinena. Sensa kwenye ncha za catheters hutumia nishati ya joto au ubaridi kutengeneza makovu madogo kwenye moyo. Makovu haya huzuia ishara za umeme zisizo na mpangilio. Hii husaidia kuyarejesha mapigo ya moyo.
Catheter ablation haihitaji upasuaji ili kuufikia moyo, lakini inaweza kufanyika sambamba na upasuaji mwingine.
. Pacemaker. Pacemaker ni chombo kidogo kinachowekwa kwa upasuaji chini ya ngozi eneo la kifuani. Chombo hiki kikisikia mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio, kinatoa ishara za umeme za kusaidia kuyarekebisha mapigo ya moyo.
. Implantable cardioverter-defibrillator (ICD). Chombo hiki kinachoendeshwa kwa betri hupandikizwa chini ya ngozi karibu na mfupa wa juu kabisa wa shingoni (collarbone). Chombo hiki hufuatilia mapigo ya moyo wakati wote. Kukigundulika mapigo yasiyo na mpangilio, kitatuma mishituko (shocks) ya nguvu ya chini au juu ili kuweka sawa mapigo ya moyo. Daktari anaweza kushauri kuwekwa kwa chombo hiki ikiwa utakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata ventricular tachycardia au ventricular fibrillation.
. Maze procedure. Daktari anachanja njia ndogo kwenye vyumba vya juu vya moyo ili kutengeneza mpangilio fulani wa tishu zenye makovu. Mpangilio huu huitwa maze. Ishara zinazozalishwa na moyo haziwezi kuvuka tishu zenye makovu. Kwa hiyo maze inaweza kuzuia ishara zo zote za umeme zilizozagaa ndani ya moyo ambazo huweza kusababisha tachycardia.
. Upasuaji. Wakati mwingine upasuaji mkubwa unahitajika ili kuharibu njia ya ziada ya umeme inayosababisha tachycardia. Upasuaji kwa kawaida hufanywa pale ambapo njia nyingine zote hazikufanya kazi au kama upasuaji unahitajika ufanywe kwa tatizo jingine la moyo.
Katika mada yetu nyingine tutazungumzia tatizo la mshituko wa moyo.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya saa za kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.
Katika mada yetu nyingine tutalizungumzia tatizo la mshituko wa moyo. Usikose kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada yetu ya leo. Tutafurahi kukujibu.