Ugonjwa Wa Trichomoniasis: Nini Chanzo Na Tiba Yake?

 

uchafu ukeni trichomoniasisTrichomoniasis ni ugonjwa unaoonekana kwa wingi, unaotibika na unaoenezwa kwa kufanya tendo la ndoa. Watu wengi, asilimia 70,  wenye ugonjwa huu hawaoni dalili zo zote. Ugonjwa huu huenezwa na kimelea aitwaye Trichomonas vaginalis.

Trichomoniasis huwapata watu wanaoshiriki tendo la ndoa mara nyingi bila kutumia kinga wanapokutana na watu wenye vimelea hawa.

Kwa wanawake, maambukizo hupatikana kwenye eneo la mwanzo la via vya uzazi (vulva, uke, shingo ya kizazi, au njia ya mkojo.) Wanaume hupata maambukizo kwenye uume (urethra.)

Si kawaida kwa vimelea hawa kuambukiza maeneo mengine ya mwili, kama mikono, midomo au mkundu. Haijaeleweka moja kwa moja kwa nini baadhi ya watu hupata dalili za ugonjwa huu wakati wengine hawapati. Pengine hutegemeana na umri na afya ya mtu.

Dalili Za Trichomoniasis

Karibu asilimia 70 ya watu wenye maambukizo hawaoni dalili. Dalili zikitokea zinaweza kuwa ni miwasho au hata uvimbe. Baadhi ya watu huona dalili katika siku 5 hadi 28 toka siku walipoambukizwa. Wengine hawasikii kitu hadi baadaye kabisa.

Dalili kwa wanawake ni kama zifuatazo:

uchafu ukeni candidiasis

. Uchafu ukeni unaotoka kama mapovu, wenye harufu mbaya – unaoweza kuwa na rangi nyeupe, kijivu. njano au kijani wenye harufu kama ya samaki.
. Wekundu eneo la uke, kuwashwa na maumivu ukeni au nje (vulva)
. Haja ndogo mara kwa mara
. Kupata maumivu wakati wa haja ndogo au wakati wa tendo la ndoa

Ni mara chache sana wanaume kuona dalili za ugonjwa huu. Pale wanapoona, dalili huwa:

. Kuwashwa ndani ya uume
. Maumivu wakati wa haja ndogo au baada ya kumwaga shahawa
. Kutoka uchafu kwenye uume.

Bila kupata tiba ya uhakika, maambukizo haya huweza kudumu kwa miezi kadhaa au miaka.

Sababu Za Kupata Trichomoniasis

Trichomoniasis husababishwa na protozoa wa seli moja aitwaye trichomonas vaginalis, kimelea mdogo sana ambaye husafiri kutoka mtu mmoja hadi mwingine wakati wa kujamiiana. Madhara huanza kuonekana kuanzia siku ya 5 hadi 28 toka siku ya kujamiiana.

Mazingira hatarishi kwa ugonjwa huu ni:

. Kuwa na wapenzi wengi
. Kuwa umeumwa magonjwa mengine ya zinaa kabla
. Kuwa ulipata trichomoniasis kabla
. Kufanya mapenzi bila kinga

Wanawake wenye maambukizi haya huweza kuzaa watoto kabla ya muda, kuzaa watoto wenye uzito mdogo na kuwaambukiza vichanga wao wakati wa kuzaa. Pia, wanawake hawa wanakuwa kwenye hatari ya kuambukizwa UKIMWI kirahisi zaidi.

Tiba Ya Trichomoniasis

Tiba inayotumika sana kwa ugonjwa huu, hata kwa wanawake wenye ujauzito, ni megadose ya metronidazole (flagyl) au tinidazole. Wakati mwingine unaweza kuandikiwa dozi ndogo ya metronidazole ya mara mbili kwa siku, kwa siku saba.

Wapenzi wote wawili wanatakiwa kupata tiba na inatakiwa kuacha kufanya mapenzi hadi ugonjwa utakapopona, ambayo inaweza kuchukua wiki moja.

Usinywe pombe kwa saa 24 baada ya kunywa metronidazole au kwa saa 72 baada ya tinidazole, kwa sababu inaweza kukupa kichefuchefu au kukufanya utapike.

Katika mada nyingine, tataujadili ugonjwa mwingine unasababisha miwasho na kutoka uchafu ukeni, ugonjwa wa candidiasis . Usisite kutoa maoni yako kuhusu ukurasa huu wa leo au kuuliza swali ulilo nalo.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya muda wa kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.