Edema ni uvimbe unaoonekana kwa macho unaotokana na mkusanyiko wa vimiminika ndani ya tishu za mwili. Uvimbe huu hutokea mara nyingi kwenye nyayo, ankle, miguuni na mikononi ambao huitwa peripheral edema. Edema kwenye nyayo mara nyingine huitwa pedal edema. Uvimbe huu ni zao la kujikusanya kwa majimaji ya ziada chini ya ngozi kwenye nafasi zilizomo kwenye tishu za mwili.
Tishu zote za mwili huundwa kwa seli, mishipa ya damu na tishu unganishi zinazoshikilia seli kwa pamoja. Majimaji mengi ya mwili yanayopatikana nje ya seli hutunzwa ndani ya maeneo ya aina mbili; mishipa ya damu kama serum na kwenye nyufa zilizo nje ya seli. Baadhi ya magonjwa husababisha majimaji ya ziada kujikusanya ndani ya moja ya nafasi hizi au mara nyigine kwenye nafasi zote mbili.
Aina Za Edema
Edema kwa kawaida hupewa jina kutokana na eneo la mwilli husika:
Celebral edema ni mkusanyiko wa majimaji ya ziada ndani ya ubongo
Angioedema ni uvimbe chini ya ngozi. Angioedema huathiri matabaka ya chini zaidi ya ngozi na mara nyingi hutokea usoni.
Hereditary angioedema ni hali ambayo hutokana na kurithi ambapo kapilari huachia majimaji kwenye tishu za karibu na kusababisha uvimbe.
Papilledema ni uvimbe kwenye optic nerve ya jicho unaotokana na mgandamizo kwenye fuvu na kuuzunguka ubongo (intercranial pressure).
Macular edema ni uvimbe kwenye sehemu ya jicho iitwayo macula.
Dependent edema ni edema ya miguu na sehemu ya chini ya mwili, inayotokana na mvutano (gravity) na inayotegemea mtu alivyokaa. Kwa kawaida hutokea miguuni pale mtu anapokuwa amesimama, na kwenye matako pale anapokuwa amelala.
Scrotal edema ni kukua kwa mfuko wa pumbu kwa sababu ya majimaji yanayozunguka korodani.
Lipedema ni dosari kwenye tishu za mafuta (adipose tissues) ambazo husababisha uvimbe wa miguu na nyonga, na ambayo inaweza kusababisha lymphedema.
Chanzo Cha Edema Ni Nini?
Viungo vya mwili huwa na nafasi za nyufa ambamo majimaji yanaweza kujikusanya, ingawa kuna aina nyingi za edema. Kwa mfano, mkusanyiko wa majimaji kwenye nyufa zinazozunguka nafasi za hewa (alveoli) za kwenye mapafu huleta tatizo liitwalo pulmonary edema. Na, anasarca ni mkusanyiko wa majimaji ndani ya tishu na nyufa zote zilizomo kwenye mwili kwa wakati mmoja, yaani , uvimbe ulioenea mwili mzima.
Edema inayotokana na magonjwa ya moyo, ini na figo inatokana na kubakia kwa chumvi nyingi mno, ambayo inayatunza majimaji hayo ya ziada ndani ya mwili. Katika baadhi ya magonjwa ya ini na figo, viwango vidogo vya albumin ndani ya damu husababisha kubakia kwa majimaji. Moyo kushindwa kufanya kazi yake (heart failure), liver cirrhosis na ugonjwa wa figo uitwao nephrotic syndrome ni magonjwa yajulikanayo kusababisha edema.
Edema hutokea pale mishipa midogo ya damu iitwayo kapilari inapovujisha majimaji. Majimaji hayo hujikusanya kwenye tishu za karibu na kusababisha uvimbe.
Uvimbe usio na madhara sana husababishwa na:
. Kusimama au kukaa pahala pamoja kwa muda mrefu
. Kula chakula chenye chumvi nyingi
. Kuwa karibu na kupata hedhi
. ujauzito
Edema huweza kuwa ni matokeo ya kutumia baadhi ya madawa, kama:
. Madawa ya pressure
. Steroids
. Estrogens – madawa ya homoni
. Baadhi ya madawa ya kisukari (thiazolidinediones)
Mara nyingine, edema huwa ni ishara ya magonjwa mengine ya hatari. Baadhi ya magonjwa hayo ni:
.Congestive heart failure. Unapokuwa na tatizo hili, moja au chemba zote za chini za moyo wako zinapoteza uwezo wa kusukuma damu vizuri. Kwa jinsi hiyo, damu inaweza kurudi miguuni, kwenye ankle na nyayo na kusababisha edema. Congestive heart failure inaweza pia kusababisha uvimbe kwenye tumbo. Mara nyingine, hali hii inaweza kusababisha majimaji kujikusanya ndani ya mapafu (pulmonary edema), ambayo husababisha shida wakati wa kupumua.
.Cirrhosis. Majimaji yanaweza kujaa kwenye tumbo (ascites) na miguuni kutokana na kuharibika kwa ini (cirrhosis).
.Ugonjwa wa figo. Unapokuwa na ugonjwa wa figo,majimaji ya ziada na sodium ndani ya mzunguko vinaweza kusababisha edema. Edema inayohusiana na figo mara nyingi hutokea miguuni na kuzunguka macho.
.Kuharibika kwa figo. Kuharibika kwa vijishipa vidogo vya uchuchaji katika figo huweza kusababisha nephrotic syndrome. Nephrotic syndrome ni hali ya kupungua kwa protini (albumin) katika damu kunakoweza kusababisha mkusanyiko wa majimaji na edema.
.Udhaifu au uharibifu wa veni za miguuni.
.Mfumo wa limfu usiotosheleza. Mfumo wa limfu wa mwili wako una kazi ya kukusanya majimaji ya ziada kutoka kwenye tishu. Endapo mfumo una dosari – mathalani ukiharibiwa wakati wa upasuaji wa saratani – lymph nodes na mishipa ya limfu vinaweza kushindwa kufanya kazi vizuri na edema ikatokea.
.Upungufu mkubwa na wa muda mrefu wa protini. Upungufu mkubwa au ukosefu wa protini katika mlo wa muda mrefu unaweza kusababisha mkusanyiko wa majimaji na hivyo kupata edema.
Tiba Ya Edema
Edema isiyo kali sana huondoka yenyewe, na hasa kama unajitahidi kukinyanyua kiungo kilichoathirika juu zaidi ya usawa wa moyo wako.
Edema kali zaidi zinaweza kutibiwa kwa kutumia madawa ambayo yanaondoa majimaji ya ziada kupitia mkojo (diuretics). Moja ya dawa hizi inayotumika sana ni furosemide (Lasix). Lakini daktari ndiye atakayekuamulia tiba nzuri kutokana na historia yako.
Yafaa pia kupunguza matumizi ya chumvi, kukitumia kiungo na misuli iliyoathiriwa na edema, na hasa miguu, ili kusaidia kuyasukuma majimaji ya ziada kurudi kwenye moyo. Mwombe daktari akushauri kuhusu mazoezi ya mwili ambayo unaweza kuyafanya ili kupunguza uvimbe.
Uvimbe Unaobonyea – Pitting Edema
Uvimbe unaobonyea (pitting edema) hugundulika kwa kubonyeza eneo la mwili lililovimba kwa kidole. Endapo eneo hili liltaacha kijishimo kinachodumu kwa muda baada ya kidole kuondolewa, edema hii huitwa pitting edema. Mgandamizo wa aina yo yote, hata unaotokana na kuvaa socks, unaweza kusababisha kubonyea endapo mtu ana pitting edema. Karibu kila mtu anayevaa socks hupata pitting edema na mara nyingi huwa ni pitting edema isiyo na madhara
Ni Nini Kinasababisha Mwili Kuvimba Wakati Wa Ujauzito?
Wakati mwanamke ni mjamzito, mwili huzalisha damu na majimaji mengine zaidi kwa asilimia 50 kuliko kawaida ili kumsaidia kiumbe anayekua. Hii husababisha kuvimba kwa viungo vya mwili (pittig edema) ikiwa ni pamoja na mikono, uso, miguu, vifundo vya miguu na nyayo, na ni sehemu ya kawaida ya ujauzito. Uvimbe huweza kuzidi kwenye maeneo ya miguu na nyayo kwa sababu ya kutanuka kwa nyumba ya uzazi (uterus) kunachukua nafasi kwenye tumbo na kuzuia kurudi kwa majimaji kutoka kwenye maeneo ya miguu.
Pitting edema ya wakati wa ujauzito inaweza kutokea muda wo wote wakati kiumbe anakua, lakini wanawake wengi huanza kuisikia kuanzia mwezi wa tano, na huweza kuwa ya nguvu zaidi kwenye kipindi cha theluthi ya mwisho ya ukuaji wa mimba.
Uvimbe mdogo ni wa kawida, lakini kuvimba kwa ghafla kwa mikono na uso kunaweza kuashiria preeclampsia.
Edema inaweza kuendelea hata baada ya kujifungua. Uvimbe unaweza kuanza kupungua wiki moja baada ya kujifungua. Kama uvimbe hautapungua katika wiki moja au kama unajisikia maumivu ya kichwa au kwenye miguu, hii ni dalili ya pressure ya juu na preeclampsia. Yafaa kumwona daktari.
Ni Nini Kinachosababisha Kuvimba Kwa Mwili Kwa Mgonjwa Wa Homa Ya Ini?
Kwa watu wenye matatizo ya muda mrefu ya ini, ini huanza kuwa na makovu (fibrosis). Makovu haya yakizidi, tatizo hili huitwa cirrhosis. Ascites ni majimaji ya ziada yaliyomo kwenye mvungu wa tumbo. Majimaji haya ni matokeo ya cirrhosis na hujionyesha kwa tumbo kujaa. Peritoneum ni ngozi laini inayofunika mvungu wa tumbo, ngozi iliyozunguka na kufunika viungo vya ndani kama ini, mfuko wa nyongo, bandama, kongosho, na utumbo (utumbo mwembamba na utumbo mnene). Kujaa kwa majimaji (ascites) hutokea kwa sababu mbili, kuongezeka kwa msukumo (pressure) ndani ya mfumo wa veni unaosafirisha damu kutoka kwenye tumbo, utumbo, na bandama kwenda kwenye ini (portal hypertension). Kiwango kidogo cha protein albumin ndani ya damu (hypoalbuminemia). Albumin ambayo ni protini muhimu katika damu na ambayo husaidia kuweka sawa ujazo wa damu, hupungua kukiwa na cirrhosis sababu kubwa ikiwa ni ini lililoharibika kushindwa kuizalisha kwa kiwango sahihi.
Peripheral edema ambayo huonekana kama pitting edema kwenye miguu na nyayo, pia hutokea kukiwa na cirrhosis. Edema hii ni matokeo ya hypoalbuminemia na figo kutunza maji na chumvi.
Ni Nini Kinasababisha Mwili Kuvimba Kwa Mgonjwa Wa Figo?
Mtu mwenye ugonjwa unaoathiri utendaji wa figo huvimba mwili kwa sababu ya kupungua kwa uwezo wa figo wa kutoa nje pamoja na mkojo madini ya sodium. Kwa hiyo mtu mwenye hitilafu ya figo kwa sababu yo yote ile atavimba mwili iwapo atatumia madini ya sodium zaidi ya uwezo wa figo zake wa kuyatoa madini hayo nje pamoja na mkojo. Ikiwa hitilafu ya figo zake ni kubwa zaidi, na uwezo wake wa kuyatoa madini hayo utapungua zaidi. Hatua ya mwisho ya uahribifu wa figo zake ni pale anapofikia kuhitajika kufanyiwa tiba ya kidney dialysis. Kiasi chake cha chumvi sasa kitadhibitiwa na tiba hiyo tu ambayo itaitoa chumvi. Dialysis ni utaratibu wa kutoa nje ya mwili uchafu unaojikusanya figo zinaposhindwa kufanya kazi. Dialysis hufanywa kwa kuzungusha damu ya mgonjwa kupitia membrane bandia (hemodialysis) au kwa kutumia nafasi uiliyopo kwenye tumbo (peritoneal membrane) kama kifaa cha uchuchaji.
Ni Nini Kinasababisha Mwili Kuvimba Kwa Mgonjwa Wa Moyo?
Moyo kusita kuendelea kufanya kazi ni zao la utendaji mbaya ndani ya moyo na huonekana kwa kupungua kwa ujazo wa damu inayosukumwa nje na moyo (cardiac output). Moyo unaweza kusita kuendelea kufanya kazi kutokana na udhaifu wa msuli wa moyo ambao husukuma damu kuelekea sehemu zote za mwili kupitia ateri, au kutokana na valvu za moyo zinazosimamia mtiririko wa damu kwenye vyumba vya moyo kutofanya kazi vizuri. Kupungua kwa ujazo wa damu inayosukumwa nje ya moyo kunahusika na kupungua kwa damu inayozifikia figo. Kufuatia hilo, figo huhisi kuwa kuna upungufu wa damu katika mwili. Kupambana na hali hii ya upungufu wa damu, figo hutunza maji na chumvi. Kwa hiyo sasa, figo zimedanganywa kuwa mwili unahitaji kutunza zaidi ujazo wa majimaji ya mwili, wakati, kiukweli ni kwamba mwili una majimaji kuliko kiasi kinachotakiwa.
Kuongezeka huku kwa majimaji hatimaye husababisha kujazana kwa majimaji ndani ya mapafu, ambako kunasababisha pumzi ya shida (cardiogenic pulmonary edema au CPE). Kwa sababu ya kupungua kwa ujazo wa damu inayosukumwa na moyo, ujazo wa damu ndani ya ateri hupungua, pamoja na kwamba kuna mwongezeko wa ujazo wa majimaji ndani ya mwili kwa jumla. Kuongezeka huku kwa majimaji ndani ya mishipa ya damu ya mapafu kunasababisha pumzi ya shida kwa sababu majimaji ya ziada ndani ya mishipa ya damu ya mapafu huvujia ndani ya vifuko vya hewa (alveoli) na kwenye nyufa za kwenye mapafu. Hii huitwa pulmonary edema. Wakati huo huo kujazana kwa majimaji ndani ya miguu husababisha edema ya kubonyea (pitting edema) kwenye miguu. Hii hutokea kwa sababu kujazana kwa damu ndani ya veni za miguu husababisha majimaji kutoka kwenye kapilari za miguu kuvujia ndani ya nyufa.
Ufahamu wa jinsi moyo na mapafu vinavyohusiana utakusaidia kujua jinsi gani majimaji hujikusanya moyo unaposhindwa kufanya kazi. Moyo una vyumba vinne, atrium na ventricle upande wake wa kushoto na atrium na ventricle upande wa kulia. Atrium ya kushoto hupokea damu yenye oksijeni kutoka kwenye mapafu na kuisafirisha hadi kwenye ventricle ya kushoto, ambayo huisukuma damu hiyo kupitia ateri kuelekea sehemu nyingine zote za mwili. Damu kutoka mwilini hurudi kwenye moyo kupitia veni hadi kwenye atrium ya kulia ambayo huipeleka kwenye ventricle ya kulia. Ventricle ya kulia huisukuma damu hiyo kuelekea kwenye mapafu ili kurutubishwa tena na oksijeni.
Kufa kwa moyo upande wa kushoto, ambako kimsingi kunatokana na udhaifu wa ventricle ya kushoto, kunasababishwa na ugonjwa wa coronary artery, high blood pressure, au ugonjwa kwenye valvu za moyo. Mgonjwa hupata shida ya kupumua usiku wakati akiwa amelala (othopnea). Dalili hizi hutokea kwa sababu ya maji ndani ya mapafu (pulmonary edema).
Kwa upande wa pili, kufa kwa moyo upande wa kulia, ambako kunatokana na kubanwa pumzi usiku au magonjwa sugu ya mapafu kama emphysema, huanza na utunzwaji wa chumvi na peripheral edema. Utunzwaji wa chumvi wa muda mrefu husababisha mwongezeko wa damu ndani ya mishipa ya damu, na hivyo kusababisha mwongezeko wa ujazo wa majimaji ndani ya mapafu na kusababisha pumzi ya shida.
Watu wenye tatizo la moyo kushindwa kuendelea kufanya kazi kwa sababu ya udhaifu wa misuli ya moyo (cardiomyopathy), huwa na ventricle zote za kushoto na kulia zilizoathirika. Mwanzo watu hawa hupata tatizo la uvimbe ndani ya mapafu na kwenye miguu na nyayo (peripheral edema).
Katika mada nyingine tutazungumzia tatizo la chunjua (warts.) Usisite kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo au kuuliza maswali uliyo nayo.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.