Goita ni uvimbe usio wa kawaida wa tezi ya thyroid. Thyroid ni tezi yenye umbo la kipepeo iliyo sehemu ya chini ya shingo chini kidogo ya kikoromeo. Pamoja na kuwa goita hazina maumivu, goita kubwa inaweza kuleta kikohozi au kusababisha matatizo ya kumeza au kupumua.
Chanzo kikubwa cha goita katika sehemu nyingi za dunia ni ukosefu wa madini ya iodine katika chakula. Katika maeneo ambayo madini ya iodine huongezwa kwenye chumvi inayotumika, goita huwa zinatokana na uzidifu au upungufu katika uzalishwaji wa homoni ya thyroid au vivimbe vinavyojijenga kwenye tezi ya thyroid.
Tiba hutegemea ukubwa wa goita, dalili ambazo zimejitokeza na chanzo halisi cha goita hiyo. Goita ndogo ambazo hazionekani na ambazo hazileti usumbufu hazihitaji tiba.
Dalili Za Goita
Si goita zote ambazo huonyesha dalili. Pale ambapo dalili zitaonekana, zinaweza kuwa:
1. Uvimbe unaooneka eneo inapoanzia shingo
2. Kusikia kubanwa kooni
3. Kukohoa
4. Sauti kukwaruza
5. Shida kumeza
6. Shida kupumua
Chanzo Cha Goita
Tezi yako ya thyroid hutengeneza aina kuu mbili za homoni – thyroxine (T-4) na triiodothyronine (T-3). Homoni hizi mbili huzunguka katika mfumo wa damu na husaidia katika shughuli za kimetaboliki – kujenga na kuvunjavunja kemikali katika mwili. Husimamia namna mwili unavyotumia mafuta na wanga, husaidia kuweka sawa joto la mwili, kurekebisha mapigo ya moyo, na kusimamia uzalishwaji wa protini.
Tezi ya thyroid hutengeneza pia calcitonin – homoni inayosaidia kuweka sawa kiwango cha calcium ndani ya damu.
Tezo za pituitary na hypothalamus husimamia kasi ya utengenezwaji na utolewaji wa homoni hizi.
Mlolongo wa mambo huanza pale hypothalamus – eneo lililo chini ya ubongo linalofanya kazi kama thermostat ya mfumo wako mzima – inapotoa ishara kwa pituitary kutengeneza homoni iitwayo thyroid stimulating hormone (TSH). Tezi ya pitutary ambayo nayo ipo kwenye eneo la chini ya ubongo, itatoa kiasi fulani cha TSH, kulingana na kiasi gani cha thyroxine na T-3 vipo ndani ya damu. Tezi yako ya thyroid, nayo, itarekebisha uzalishaji wa homoni kulingana na kiasi cha TSH kilichotolewa na tezi ya pituitary.
Kuwa na goita hakuamaanishi kuwa tezi yako ya thyroid haifanyi kazi vizuri. Hata wakati imevimba, tezi yako inaweza kuwa inatoa kiasi cha homoni kinachotakiwa. Inaweza kuwa, pamoja na hayo, ikawa inatengeneza homoni za thyroxine ne T-3 kwa kiwango cha juu zaidi au cha chini.
Kuna vipengele vinavyoweza kusababisha tezi ya thyroid kuvimba. Sababu zinazojitokeza mara nyingi zaidi ni:
Upungufu wa iodine
Iodine ni ya lazima katika uzalishaji wa homoni za tezi ya thyroid. Kama mtu hapati kiasi cha kutosha cha iodine katika chakula chake, uzalishaji wa homoni hushuka na tezi ya pituitary hutoa ishara ya kuamuru tezi ya thyroid kuzalisha zaidi. Ishara hii ya kuongeza uzalishaji ya kila wakati husababisha tezi ya thyroid kuongezeka ukubwa wake.
Ugonjwa wa Hashimoto (Hashimoto’s disease)
Ugonjwa wa hashimoto ni matatizo ya kiutendaji ya kinga za mwili (autoimmune disorder), ugonjwa unaotokana na kinga za mwili kushambulia tishu zenye afya. Tishu za thyroid zilizoharibiwa na zilizovimba haziwezi kuzalisha homoni ya kutosha (hypothyroidism). Tezi ya pituitary ikigundua upungufu huo huiamrisha tezi ya thyroid kutengeneza homoni zaidi, na tezi hiyo huweza kuongezeka ukubwa wake.
Ugonjwa wa Grave (Grave’s disease)
Ugonjwa mwingine unaotokana na dosari katika utendaji wa kinga za mwili unaitwa Grave’s disease na hutokea pale kinga za mwili zinapotengeneza protini inayofanana kisifa na TSH. Protini hii ya kilaghai huiamrisha tezi ya thyroid kutengeneza homoni kupita kiasi (hyperthyroidism) na huweza kusababisha tezi hiyo kukua.
Thyroid nodules
Nodule ni kukua kusiko kwa kawaida kwa seli za thyroid na kutengeneza uvimbe. Mtu anaweza kuwa na nodule zaidi ya moja (multinodular goiter). Sababu ya kutokea kwa nodules hizi hazijafahamika, lakini kuna vitu vinavyochangia – urithi, chakula, staili ya maisha na mazingira. Vimbe nyingi za thyroid ni za kawaida (benign) zisizohusisha kansa.
Saratani ya thyroid
Saratani ya thyroid huonekana mara chache sana ukilinganisha na saratani nyingine na kwa kawaida hutibika. Yapata asilimia 5 ya watu wenye thyroid nodules huonekana kuwa na saratani.
Ujauzito
Homoni inayozalishwa wakati wa ujauzito, human chorionic gonadotropin (HCG), huweza kusababisha thyroid kufanya kazi kupita kiasi na kuvimba kidogo.
Uvimbe
Thyroiditis ni uvimbe wa thyroid unaotokana na matatizo ya kinga za mwili (autoimmune disorder), maambukizo ya bakteria au ya virusi, au madawa. Uvimbe huu unaweza kusababisha hyperthyroidism au hypothyroidism.
Aina Za Goita
Aina ya goita ulliyo ayo itaonyesha dalili tofauti na itahitaji tiba ya aina yake. Kuna aina kadhaa za goita:
. Multinodular goiter: Katika aina hii, vijivimbe zaidi ya kimoja vitatokea.
. Diffuse smooth goiter: Hii hutokea pale tezi yote ya thyroid inapovimba. Goita hizi zinahusishwa na utendaji wa ziada na utendaji hafifu wa tezi ya thyroid (overactive and underactive thyroid glands).
. Retrosternal goiter: Goita ya aina hii huweza kuota nyuma ya mfupa wa kidarI. Hii huweza kuziba njia ya hewa, kuminya neva za shingo, au umio, na wakati mwingine upasuaji utalazimika.
Tiba ya Goita
Tiba ya goita inategemea ukubwa wa goita, dalili zinazojionyesha, na chanzo halisi cha goita hiyo. Dakatari anaweza kupendekeza yafuatayo:
. Uangalizi. Kama goita yako ni ndogo na haileti madhara, na tezi yako ya thyroid inafanya kazi ivizuri, daktari anaweza kuchukua uamuzi wa kuiacha na kuitazamia.
. Madawa. Kama tezi yako inafanya kazi chini ya kiwango (hypothyroidism), unaweza kuongezewa homoni kwa kutumia levothyroxine (Levoxyl, Synthroid, Tirosint) ambavyo pia vitapunguza utolewaji wa TSH kutoka tezi ya pituitary, hatua ambayo mara nyingi hupunguza ukubwa wa goita.
Pale panapokuwa na vivimbe kwenye tezi ya thyroid, daktari anaweza kukuandikia aspirin au dawa ya corticosteroid kuuondoa uvimbe.
Goita zinazotokana na utendaji wa kupitiliza wa tezi (hyperthyroidism), utahitaji dawa za kupunguza viwango vya homoni.
. Upasuaji. Kuondoa sehemu au tezi yote ya thyroid (total or partial thyroidectomy) ni uamuzi endapo goita ni kubwa sana na inaleta usumbufu au kusababisha shida katika kupumua au kumeza.
Upasuaji ni tiba pia kwa saratani ya tezi ya thyroid.
Unaweza kuandikiwa kutumia levothyroxine baada ya upasuaji, kulingana na kiasi cha tezi ya thyroid kilichoondolewa.
. Radioactive iodine. Wakati mwingine, radioctive iodine hutumika kutibu tezi ya thyroid inayozidisha utoaji wa homoni. Radioactive iodine hunywewa na huifikia tezi ya thyroid kupitia mzunguko wa damu, na kuua seli za thyroid. Matokeo ni kupunguza ukubwa wa goita, lakini pia huweza kusababisha utendaji mdogo wa tezi hiyo.
Katika mada nyingine tutazungumzia umuhimu wa vitamini katika mwili. Usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali uliyo nayo.
Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au kututumia barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu ndani ya saa za kazi kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.