Chanzo Cha Ovarian Cysts Ni Nini?

 

 

Ovari ni sehemu ya viungo vya uzazi vya mwanamke. Ovari zipo sehemu ya chini ya tumbo, pande zote mbili za uterasi au mji wa mimba (uterus). Wanawake wana ovari mbili ambazo hufanya kazi ya kuzalisha mayai pamoja na homoni za estrogen na progesterone. Ovari ndicho chanzo kikuu cha homoni za mwanamke ambazo huhusika na ukuaji wa tabia za mwili wa mwanamke kama matiti, umbile la mwili, na nywele za mwilini. Ovari pia husimamia mzunguko wa hedhi na ujauzito. Katika mada yetu ya leo tutazungumzia ovarian cysts, tatizo ambalo hujitokeza katika ovari za mwanamke.

 

Ovarian Cysts Ni Nini?

 

Ovarian cyst inatokea pale majimaji yanapojikusanya kwenye utando mwembamba wa ngozi ndani ya ovari. Ukubwa wa ovarian cyst unaweza kuwa kati ya punje ya njegere na chungwa. Cyst ni neno linalotumika kuelezea kitu kilichofunikwa chenye umbo la mfuko. Cyst hutenganishwa na tishu za karibu yake na utando mwembamba wa ngozi. Ndani ya cyst kuna majimaji, hewa, au kitu kilicho kati ya maji na kitu kigumu. Eneo la nje la cyst huitwa cyst wall.

 

picha ya ovarian cysts

 

 

 

Ovarian cyst hutofautiana na jipu kwa vile haikujaa usaha.

Ovarian cysts nyingi ni ndogo na hazileti madhara kiafya. Hutokea mara nyingi wakati wa umri wa kuzaa, ingawa huweza kutokea kwenye umri wo wote. Kwa kawaida ovarian cysts hazina dalili zo zote, ingawa wakati mwingine huleta maumivu au kusababisha damu itoke. Kama ovarian cyst inazidi nusu kipenyo cha sentimenta 5, inaweza kuhitajika kuondolewa kwa upasuaji.

 

 Kuna Aina Ngapi Za Ovarian Cysts?

 

Kuna aina kuu mbili za ovarian cysts na hapa chini ni maelezo ya aina hizo mbili na sababu za kutokea kwa kila moja ya aina hizo.

. Functional ovarian cysts – hii ndiyo aina inayojitokeza mara nyingi zaidi. Aina hii ambayo haina madhara ni sehemu ya mzunguko wa kawaida wa hedhi ya mwanamke na huishi kwa muda mfupi.

. Pathological cysts – hizi ni ovarian cysts zinazojijenga ndani ya ovari; hizi huweza kuwa hazina madhara au kuleta saratani.

 

Functional ovarian cysts

Kuna aina kuu mbili za functional ovarian cysts:

1) Follicular cysts

Follicular cysts ni aina mabayo huonekana mara nyingi sana kwa wanawake. Mwanamke ana ovari mbili. Yai huvingirika kutoka kwenye ovari hadi ndani ya mji wa mimba, ambako linaweza kurutubishwa na mbegu za mwanamme. Yai huundwa ndani ya follicle, ambayo huwa na majimaji ili kulilinda yai linalokua. Yai linapoangushwa, follicle hupasuka.

 

maana ya ovarian cysts

 

Yaweza ikatokea kuwa yai linapoangushwa follicle haimwagi maji yaliyomo ndani yake na kusinyaa, au isiangushe yai kabisa. Follicle hii kwa hiyo, hutuna ikiwa na maji, na kugeuka kuwa follicular ovarian cyst.

Kwa kawaida cyst moja hutokea kwa wakati mmoja, na hupotea katika muda wa wiki chache.

2) Luteal ovarian cysts

Luteal ovarian cysts huonekana mara chache. Baada ya yai kuachiwa, huacha tishu nyuma yake iitwayo corpus luteum. Luteal cysts huweza kutokea pale corpus luteum inapojaa damu. Aina hii mara nyingi hupotea yenyewe baada ya miezi michache. Lakini wakati mwingine huweza kugawanyika, au kupasuka, na kusababisha maumivu na kuvuja kwa damu  ndani kwa ndani.

 

Pathological cysts

Kuna aina mbili za pathological cysts:

1) Dermoid cysts (cystic teratomas)

Dermoid cyst kwa kawaida haina madhara. Hizi ni tishu zinazotokana na seli zinazotengeneza yai. Tishu hizi za ovari huweza kukua na kutengeneza tishu nyingine za mwili kama nywele, ngozi au meno. Cysts za aina hii hutakiwa kutolewa kwa upasuaji.

 

ovarian cysts dermoid

 

Dermoid cyts ni aina ya pathological cysts ambazo huonekana sana kwa wanawake walio chini ya umri wa miaka 30.

2) Cystadenomas

Cystadenomas ni ovarian cysts zinazojengwa kutokana na seli zinazofunika ovari kwa nje. Baadhi huwa zimejaa kitu kizito, kama kamasi, wakati mwingine hujaa majimaji mepesi.

Badala ya kuota ndani ya ovari, cystadenomas hunata kwenye ovari kupitia kikonyo. Kwa vile huishi nje ya ovari, cystadenomas huweza kukua na kuwa kubwa sana. Ni mara chache sana kuwa na saratani, lakini hutakiwa kuondolewa kwa upasuaji.

Cystadenomas huonekana zaidi kwa wanawake wenye umri unaozidi miaka 40.

Aina nyingine ni:

“Chocolate cysts:” Endometriosis ni hali ambapo seli ambazo kwa kawaida hukua ndani kama ukingo wa mji wa mimba (uterus), zinakua nje kwenye sehemu ambazo si za uterus. Ovari ni sehemu rafiki sana ya endometriosis. Wakati endometriosis imetokea kwenye ovari, eneo lenye tishu za endometriosis linaweza kukua na baadaye kutoa damu, na kusababisha cyst iliyojaa damu yenye vitu vyekundu au vya kahawia viitwavyo endometrioma au “chocolate cyst.”

Polycystic ovarian syndrome. Hali iitwayo polycystic ovarian syndrome (PCOS) hujitambulisha kwa uwepo wa cysts ndogo nyingi ndani ya ovari za pande zote mbili. PCOS inahusiana na baadhi ya matatizo ya homoni na ni moja ya sababu kuu ya ugumba kwa wanawake.

 

Dalili Za Ovarian Cysts

 

Ovarian cysts nyingi hazitambuliwi na hupotea zenyewe bila hata mwanamke mwenyewe kujua kuwa alikuwa nazo. Wakati cysts zinaonyesha dalili, maumivu maeneo ya tumbo au kwenye nyonga hujitokeza. Maumivu haya husababishwa na:

. kupasuka kwa cyst,
. ukuaji wa haraka na kunyumbuka,
. damu kutoka kwenye cyst,
. kujinyonga kwa cyst kwenye mishipa ya damu (torsion).

Kama cyst imekuwa kubwa, dalili nyingine huweza kujitokeza kutokana na msukumo au kujinyonga kwa viungo vingine vya mwili vilivyo karibu (torsion). Endapo ovari itajinyonga au kuhama kutoka sehemu yake ya awali, mtiririko wa damu kuelekea kwenye ovari hukatwa, na kama hakuna tiba itakayotolewa, tishu za ovari zinaweza kuharibika au kufa. Ovarian torsion inachangia asilimia 3 ya upasuaji wa dharura wa viungo vya uzazi vya akina mama. Katika mazingira hayo dalili hizi zinaweza kujitokeza:

. kujaa kwa tumbo, kutanuka tumbo,
. maumivu eneo la chini ya mgongo,
. chakula kutomeng’enywa tumboni,
. kusikia umeshiba baada ya kula chakula kidogo tu
. kusikia haja ndogo kwa ghafla
. kushindwa kumaliza kabisa haja ndogo
. Kujisikia haja kubwa kila wakati
. kupata haja kubwa kwa shida
. maumivu wakati wa tendo la ndoa

 

Dalili Za Ovarian Cysts Iliyopasuka

Ovarian cyst iliyopasuka haitoi dalili zo zote, na hasa kama ni ndogo. Lakini wakati mwingine kupasuka kwa ovarian cyst kunaweza kusababisha maumivu makali na kuvuja damu ndani kwa ndani. Maumivu ya kupasuka kwa ovarian cyst huja ghafla na hutokea upande mmoja tu. Maumivu haya huanza wakati wa shughuli fulani kama mazoezi mazito au yaweza kuanza wakati wa tendo la ndoa. Ovarian cyst iliyopasuka haileti homa.

 

Tiba Ya Ovarian Cysts

 

Ovarian cysts nyingi zinazotokea kwa wanawake wa umri wa kuzaa ni za aina ya follicular au corpus luteum (functional cysts) ambazo hupotea zenyewe katika kipindi cha mwezi mmoja hadi miezi mitatu, ingawa zinaweza kupasuka na kusababisha maumivu. Huwa hazina madhara na hazileti matatizo ya muda mrefu ya kiafya. Zinaweza zikaonekana wakati wa kuchukua vipimo vingine vya sehemu za nyonga. Wanawake wote hupata ovarian cysts wakati fulani katika maisha yao na mara nyingi hupotea bila kutambuliwa.

Kipimo cha ultrasound hutumika kutambua kama cyst ni simple cyst (majimaji bila vitu vigumu, ikimaanisha kuwa si ya hatari) au compound cyst (yenye vitu vigumu, hivyo kuhitaji upasuaji).

Kwa kifupi, tiba sahihi itategemea sababu ya kutokea kwa ovarian cyst na kama inatoa dalili au la. Umri wa mwanamke, ukubwa wa cyst (na mabadiliko katika ukubwa wa cyst), na mwonekano wa cyst kwenye vipimo vinaweza kusaidia kuamua aina ya tiba itakayotolewa. Functional cysts huchunguzwa kwa utaratibu na kuchukuliwa vipimo mara kwa mara, labda kama zitapasuka na kusababisha kuvuja damu, ambapo upasuaji utahitajika.

 

Katika mada ya leo tumejadili kwa kina kuhusu tatizo la ovarian cysts tukiwa tumeelezea aina zake, dalili zake kwa mwanamke na tiba zinazoweza kutolewa. Katika mada nyingine tutazungumzia tatizo la uvimbe katika tumbo la mwanamke (fibroids).

Tunakuomba usisite kutoa ushauri wako kuhusu mada hii au kuuliza maswali uliyo nayo. Ni furaha kwetu kuona tumekujibu kwa ufasaha.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya muda wa kazi  kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.