Mada hii ni muendelezo wa mada iliyopita ambamo tulijadili sababu zinazopelekea mtu kuupata ugonjwa huu wa saratani na baadaye tuliona aina mbalimbali za saratani. Leo tutaona dalili za ugonjwa wa kansa na tiba mbalimbali ambazo zinatumika kuuponya ugonjwa huu wa kansa. Moja kwa moja tuanze kwa kuona dalili za kansa.
Dalili Za Kansa
Ugonjwa wa kansa una ishara nyingi ambazo hutegemea zaidi kansa hiyo ipo kwenye sehemu gani ya mwili, imekwisha enea kwa kiwango gani na ukubwa wa uvimbe wa kansa hiyo. Kansa nyingine huonekana kwa macho au kwa kupapasa juu ya ngozi – uvimbe juu ya ziwa au kwenye korodani huweza kuwa ishara ya kansa. Kansa aina ya melanoma mara nyingi hutambuliwa kutokana na mabadiliko ya vijipele juu ya ngozi. Kansa nyingine hutoa mabaka meupe ndani ya midomo au madoa meupe kwenye ulimi.
Kansa nyingine hutoa dalili ambazo hazionekani dhahiri. Uvimbe wa kwenye ubongo, mathalani, huathiri jinsi mtu anavyoweza kutambua vitu na kansa za kwenye kongosho hazitoi ishara mapema hadi maumivu yatakapoanza pale neva za maeneo ya karibu zitakapoanza kuminywa au shughuli za ini zitakapoathiriwa na kusababisha ngozi na macho kuwa ya rangi ya njano (jaundice).
Ishara nyingine zitaonekana uvimbe utakapoanza kusukuma viungo vya karibu au mishipa ya damu. Kwa mfano, kansa za kwenye utumbo huweza kusababisha kukosa choo kikawaida, kuharisha au kiasi cha kinyesi kinachotolewa. Kansa za tezi dume huathiri ufanyakazi wa kibofu cha mkojo na kusababisha kupata haja ndogo mara kwa mara au kutopata haja ndogo.
Kwa vile seli za kansa hunyonya nguvu za mwili na kuvuruga mfumo wa kinga za mwili, ishara nyingine za homa, uchovu, kutokwa jasho, kukosa damu, kupungua uzito kusiko na sababu huweza kutokea.
Kansa iliyoenea hadi kwenye maeneo ya ubongo husababisha kizunguzungu na maumivu ya kichwa. Kansa ya mapafu inawezaa kusababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ini linaweza kuwa kubwa na kusababisha ugonjwa wa homa ya manjano, mifupa huweza kuuma na kuvunjika kirahisi.
Tiba Ya Kansa
Tiba ya ugonjwa huu wa saratani inatolewa kwa kutegemea aina ya kansa aliyo nayo mgonjwa, kansa hiyo imeenea kiasi gani katika mwili wa mgonjwa huyo, umri wa mgonjwa, afya aliyo nayo na mambo mengine yanayoendana na mgonjwa huyo. Hakuna tiba ya wote na mara nyingine mgonjwa atapewa mchanganyiko wa tiba na uangalizi. Tiba zilizopo zinaangukia katika makundi yafuatayo: upasuaji, mionzi, chemotherapy, immunotherapy, hormone therapy au gene therapy. Tutapitia kwa kifupi aina hizi za tiba za kansa hapa chini.
Tiba Ya Kansa Kwa Upasuaji: Tiba ya kansa kwa upasuaji ndiyo tiba ambayo imetumika kwa muda mrefu zaidi kuliko tiba nyingine zote. Endapo kansa ya eneo moja haijaenea kwenye sehemu nyingine ya mwili, mgonjwa anaweza kupona kabisa kwa tiba hii ya upasuaji. Mafanikio makubwa kabisa ya tiba hii yameonekana katika tiba za kansa za maziwa na kansa za tezi dume. Kansa ikiishaenea toka sehemu moja ya mwili hadi nyingine, tiba hii haiwezi kuondoa seli zote za kansa.
Tiba hii inapotumika kwa sasa hivi kuondoa uvimbe, madaktari huondoa kipande cha seli za kawaida kuzunguka eneo la seli za kansa kuhakikisha kuwa seli zote za kansa zimeondolewa. Mgonjwa hulazilka kubaki kwenye nusu-kaputi wakati vipimo vinachukuliwa kuhakikisha kuwa eneo la kiada lililoondolewa halina seli za kansa na kwa bahati mbaya wakigundua uwepo wa seli hizo za kansa, humrudia mgonjwa na kukata kipande zaidi.
Maendeleo ya teknolojia sasa hivi yamekuja na kifaa kipya kitwacho IKnife ambacho chenyewe hugundua seli za kansa hivyo kuwawezesha madaktari kujua upeo wa eneo la kulikata na kuondoa seli zote za kansa bila ya kusubiri vipimo vya kwenye maabara.
Tiba Ya Kansa Kwa Mionzi: Tiba hii ambayo pia huitwa radiotherapy huondoa kansa kwa kuelekeza mionzi yenye nguvu kwenye seli za kansa. Mionzi hii huziharibu seli hizo na kuzifanya zijiue zenyewe. Tiba hii ya mionzi hutumia mionzi yenye nguvu inayoitwa gamma-rays inayotolewa na machine maalumu.
Tiba za mwanzo kwa kutumia mionzi zilikuwa na madhara makubwa ya kuharibu seli za kawaida lakini maendeleo katika teknolojia yameiboresha tiba hii na sasa mionzi hiyo ina uwezo wa kulenga seli za kansa kwa uhakika zaidi na hivyo kutoleta madhara kwa seli za kawaida. Radiotherapy hutumika kufanya uvimbe unywee au kuharibu seli za kansa (pamoja na kansa za aina ya leukemia na lyphoma). Tiba hii hutumika pia pamoja na tiba nyingine za kansa.
Tiba Ya Kansa Ya Chemotherapy: Chemotherapy ni tiba inayotumia kemikali ambazo zinavuruga tendo la seli za mwili kujigawa na kusababisha seli hizo kujiua zenyewe. Tiba hii hulenga zile seli ambazo zinajigawa kwa haraka na kwa kawaida hutumika kutibu kansa zilizoenea kutoka eneo moja ya mwili hadi eneo jingine
(metastatic cancers) kwa sababu kemikali hizi zina uwezo wa kusambaa katika mwili wote wa mgonjwa. Hii ni tiba ya lazima kwa aina fulani ya kansa za aina ya leukemia na lymphoma.
Chemotherapy hutolewa kwa vipindi ili mwili uweze kupona katikati ya dozi moja na nyingine. Madhara ya tiba hii ni pamoja na kunyonyoka nywele, kichefuchefu, uchovu wa mwili na kutapika. Ni tiba ambayo mara nyingine hutolewa kwenda sambamba na tiba nyingine za saratani.
Tiba Ya Kansa Ya Immunotherapy: Immunotherapy ni tiba inayokusudia kuziongeza kinga za mwili ili mwili uweze kupambana na uvimbe. Sindano inaweza kudungwa kwenye eneo lililoathirika ili uvimbe unywee (Local immunotherapy). Namna nyingine ni kuuwezesha mwili wote kuongeza kinga ili kupambana na uvimbe katika sehemu zote za mwili (Systemic immunotherapy). Tiba hii bado ni changa lakini zimeonyesha mafanikio katika kutibu kansa za maziwa.
Utafiti unaendelea na kila siku wanasayansi wanakuja na tiba nyigine na kuzijaribu. Tiba ambazo zipo kwenye majaribio ni pamoja na Gene therapy yenye lengo la kukarabati genes zilizoharibika.
Mada yetu ya leo imezungumzia dalili za kansa na tiba zinazotumika kutibu kansa. Mada iliyotanguli ilizungumzia chanzo na aina za kansa. Katika mada nyingine tutauzungumzia ugonjwa wa UKIMWI na kuona ulitoka wapi, aina za virusi wa UKIMWI na namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Ndugu msomaji wetu kuwa huru kuuliza maswali uliyo nayo na kutoa maoni yako. Tunaahidi kukujibu katika wakati mwafaka.
Jee, Unasumbuliwa Na kansa?
Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au kututumia barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu ndani ya saa za kazi kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.