Figo ni viungo viwili vilivyo sehemu ya chini ya mgongo. Figo moja ipo kila upande wa uti wa mgongo. Figo hufanya kazi ya kuchuja damu na kutoa sumu nje ya mwili wako. Sumu hizi husafirishwa hadi kwenye kibofu cha mkojo na hutolewa nje pamoja na mkojo. Figo hufeli wakati zinapopoteza kwa kiwango kikubwa uwezo wa kuchuja mabaki ndani ya damu.
Umbo La Figo
Figo hutoa mabaki na maji ya ziada nje ya damu kwa kupitia vitengo vidogo vya uchujaji vinavyoitwa nephrons. Kila nephron ina kichuchaji (glomerulus) kilicho na mfumo wa nyavunyavu wa mishipa ya damu midogo iitwayo capillaries. Damu ikipita ndani ya glomerulus, molekuli ndogo -maji, madini muhimu na virutubishi, na mabaki -hupita kwenye kuta za kapilari. Molekuli kubwa kama za protini na chembechembe nyekundu za damu, huzuiwa. Mchaganyiko uliochujwa kisha hupita sehemu nyingine ya nephron iitwayo tubule. Maji, virutubishi na madini yanayohitajika na mwili hurudishwa ndani ya mfumo wa damu. Maji ya ziada na mabaki mengine huwa ndiyo mkojo na hutiririka kuelekea kwenye kibofu cha mkojo.
Kuna vipengele vingi vinavyoathiri afya na utendaji wa figo, navyo ni kama:
. baadhi ya magonjwa ya ghafla na magonjwa sugu
. mazingira yenye uchafuzi na baadhi ya madawa
. kukaukiwa maji mwilini kwa kiasi kikubwa
. mtiririko mdogo wa damu kuelekea kwenye figo
. kuumia kwa figo
Figo zako zisipofanya kazi sawasawa, mwili hujaa sumu. Hali hii inaweza kusababisha figo kufeli,na baadaye inaweza kusababisha kupotea kwa maisha endapo tiba haitatolewa.
Aina Za Kufeli kwa Figo
Kuna aina tano za kufeli kwa figo. Acute kidney failure ni pale figo zinapoacha kufanya kazi vizuri ghafla. Chronic kidney failure ni kufeli kwa figo kunakotokea baada ya muda mrefu.
Aina hizo tano ni:
. Acute prerenal kidney failure. Mzunguko mdogo wa damu kwenye figo ni sababu ya acute prerenal kidney failure. Figo haziwezi kuchuja sumu kutoka kenye damu kama hakuna mzunguko mkubwa wa damu. Aina hii ya kufeli kwa figo mara nyingi hutibika pale chanzo cha upungufu wa mzunguko wa damu kinapobainishwa.
. Acute intrinsic kidney failure. Kufeli huku kwa figo kunatokana na kuumia kwa moja kwa moja kwa figo, kwa mfano kwa ajali. Sababu nyingine ni kuzidi kwa sumu na kupungua kwa damu (ischemia), ambapo ni upungufu wa oksijeni kwenye figo. Ischemia inaweza kusababishwa na kuvuja damu kwa wingi, mshituko, zuio katika renal blood vessel, na glomerulonephritis, hali ambapo vijishipa vidogo vya damu ndani ya figo hujeruhiwa.
. Chronic prerenal kidney failure. Ikitokea kwamba damu haifiki kwenye figo kwa kipindi kirefu, figo huanza kusinyaa na kupoteza uwezo wake wa kufanya kazi.
. Chronic intrinsic kidney failure. Hii hutokea kutokana na uharibifu wa figo wa muda mrefu kutokana na ugonjwa sugu. Intrinsic kidney disease hutokana na kuumia kwa moja kwa moja kwa figo, kama kuvuja damu kwa wingi au ukosefu wa oksijeni.
. Chronic post-renal kidney failure. Kuziba kwa muda mrefu kwa mkondo wa mkojo husababisha kukosa mkojo. Hii husababisha msukumo mkubwa na mwisho kufeli kwa figo.
Dalili Za Kufeli Kwa Figo
Hatua za mwanzo za kufeli kwa figo huwa hazina dalili za wazi. Karibu asilimia 90 ya watu wenye magonjwa sugu ya figo hawajui kama wana tatizo.
Kadiri ugonjwa unavyozidi, dalili zinazoweza kujionyesha ni:
. kupungua kwa kiasi cha mkojo unaotolewa
. kuvimba kwa miguu, vifundo vya miguu, na nyayo kutokana na kubakia kwa majimaji mwilini kwa sababu figo zimeshindwa kuyatoa maji hayo ya ziada
. kubanwa pumzi kusiko na sababu
. uchovu na usingizi mzito
. kichefuchefu kisichoisha
. kuchanganyikiwa
. maumivu kwenye kifua
. kifafa
. kupoteza fahamu.
Sababu Za Kufeli Kwa Figo
Kufeli kwa figo kunaweza kutokana na sababu nyingi. Lakini, sababu kuu mbili zinazojulikana zaidi ni high blood pressure na kisukari.
Watu walio kwenye hatari kubwa wana moja au zaidi kati ya haya.
Ukosefu Wa Mtiririko Wa Damu Kwenye Figo
Kukatika kwa ghafla kwa mtiririko wa damu kuelekea kwenye figo kunaweza kusababisha kufeli kwa figo. Hali zinazoweza kusababisha damu isitiririke kuelekea kwenye figo ni pamoja na:
. heart attack
. magonjwa ya moyo
. makovu kwenye ini au kufeli kwa ini
. ukosefu wa maji ndani ya mwili
. vidonda vikubwa vya moto
. mzio
. maambukizo makubwa, kama sepsis (uwepo wa bakteria wanaotunga usaha au kuleta sumu ndani ya damu au tishu za mwili).
High blood pressure na matumizi ya dawa za anti-inflammatory vinaweza kupunguza mtiririko wa damu.
Shida Katika Kutoa Mkojo
Mwili ukishindwa kutoa mkojo nje, sumu hujazana na figo huzidiwa. Baadhi ya saratani huziba njia ya mkojo, kama:
. kansa ya tezi dume
. kansa ya utumbo
. kansa ya shingo ya kizazi
. kansa ya kibofu cha mkojo
Hali nyingine zinazoweza kuvuruga utolewaji wa mkojo na kusababisha kufeli kwa figo, ni pamoja na:
. kokoto ndani ya figo
. kupanuka kwa tezi dume
. kuganda kwa damu katika njia ya mkojo
. kuharibiwa kwa neva zinazodhibiti utendaji kazi wa kibofu cha mkojo.
Sababu Nyingine
Sababu nyingine zinazoweza kusababisha kufeli kwa figo ni pamoja na:
. Kuganda kwa damu karibu au ndani ya figo
. maambukizo
. sumu za metali nzito
. madawa na pombe
. magonjwa ya mishipa ya damu
. ugonjwa wa lupus
. magonjwa ya mishipa midogo ya damu ndani ya figo (glomerulonephritis).
. kuvunjikavunjika kwa chembechembe nyekundu za damu baada ya maambukizo ya bakteria (hemolytic uremic syndrome), hasa ndani ya utumbo
. saratani ya seli za plasma ndani ya uboho (multiple myeloma)
. ugonjwa wa ngozi (scleroderma)
. ugonjwa unaosababisha damu kuganda ndani ya mishipa midogo ya damu (thrombotic thrombocytopenic purpura)
. dawa za chemotherapy za saratani
. rangi zitumikazo kwenye imaging tests
. baadhi ya antibiotics
. kisukari ambacho hakikudhibitiwa
Hatua Za Ugonjwa Sugu Wa Figo
Magonjwa ya figo hupangwa katika hatua tano. Yanatofautiana kuanzia yale ya mwanzo hadi kufeli kabisa kwa figo. Dalili na madhara huongezeka katika kila hatua.
Stage 1
Hii ni hatua isiyo na shida. Unaweza usione dalili yo yote wala kupata madhara. Uharibu wa figo upo. Bado unaweza kupunguza kuongezeka kwa ugonjwa kwa kuchukua hatua katika namna yako ya kuishi. Hii ni pamoja na kula milo kamili, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kutotumia bidhaa za tumbaku. Kuuweka mwili katika uzito unaofaa kutasaidia. Kama una kisukari, yafaa kuhakikisha unakidhibiti.
Stage 2
Hatua hii bado huchukuliwa kuwa siyo mbaya, lakini kuna vitu vitaanza kujionyesha kama protini ndani ya mkojo au madhara kwenye umbo la figo yataanza kuonekana. Hatua zile zile za kimaisha za stage 1 zitasaidia. Yafaa pia kuzungumza na daktari ili upate ushauri zaidi.
Stage 3
Kwenye hatua hii, figo hazifanyi tena vizuri kama inavyotakiwa. Mara nyingine hatua hii hugawanywa kati ya stage 3a na stage 3b. Kipimo cha mabaki kutoka ndani ya mwili wako kitasaidia kutofautisha kati ya hatua hizo mbili. Dalili huweza kuwa zimeanza kuwa wazi kwenye hatua hii. Uvimbe kwenye mikono na miguu, maumivu ya mgongo na mabadiliko ya ukojoaji vyaweza kujitokeza.
Kubadili namna ya kuishi kunaweza kusaidia. Daktari anaweza kukuanzishia dawa kuzuia ugonjwa kukua.
Stage 4
Hatua hii huchukuliwa kama ya kati hadi mbaya. Figo hazifanyi kazi vizuri, lakini hazijafikia kufeli. Dalili zaweza kuwa ukosefu wa damu, high blood pressure, na magonjwa ya mifupa.
Kubadili mtindo wa kuishi ni lazima. Daktari atakuweka kwenye mpango maalumu wa tiba kuzuia uharibifu zaidi wa figo.
Stage 5
Hatua hii huittwa end-stage kidney disease (ESKD) au end-stage renal disease (ESRD) na ni hatua ya mwisho ya chronic kidney disease (CKD). Katika hatua hii figo zinakaribia au zimefeli kabisa. Dalili za figo kutofanya kazi zitaonekana, kama kutapika na kichefuchefu, shida katika upumuaji, miwasho kwenye ngozi, na mengineyo.
Hatua hii inataka ufanyiwe dialysis mara kwa mara au kubadilishiwa figo.
Vipimo Vya Figo
Dakatari anaweza kutumia vipimo kadhaa kutambua kufeli kwa figo. Vipimo vinavyotumika zaidi ni:
. Urinalysis. Dakatari wako anaweza kuamua kuchukua sampuli ya mkojo na kuoima kama kuna vitu visivyo vya kawaida, kama protini au sukari vinavyoingia kwenye mkojo. Daktari anaweza pia kupima uwepo wa seli za chembechembe nyekundu na nyeupe za damu, uwingi wa bakteria na idadi ya chembechembe za cellular casts.
Daktari anaweza kuita sampuli za mkojo za saa 24. Sampuli hizi zitamsaidia kuona ni kwa kasi gani creatinine inatolewa nje ya mwili. Creatinine ni mabaki ya tishu za misuli zilizovunjwavunjwa.
. Urine volume measurements. Kupima ujazo wa mkojo unaotolewa ni njia rahisi ya kujua utendaji kazi wa figo. kwa mfano, ujazo mdogo unaashiria ugonjwa wa figo unaotokana na kuziba kwa mkojo.
. Blood samples. Daktari anaweza kuitisha vipimo vya damu ili kuona vitu vitu vinavyochujwa na figo, kana vile blood urea nitrogen na creatinine. kuongezeka kwa vitu hivi kunaashiria kufeli kwa figo kwa ghafla. Kwa kawaida figo huchuja kabisa creatinine kwenye damu, kwa hiyo uwepo wa kiasi kikubwa cha cratinine ndani ya damu (1.2 mg/dL kwa wanawake na 1.4mg/dL kwa wanaume) ni dalili ya tatizo kwenye figo. BUN hupima kiasi cha nitogen ndani ya damu. Urea nitrogen ni mabaki ya kuvunjwa kwa protini. Kiasi cha BUN kati ya 7 na 20mg/dL ni cha kawaida. Kipimo cha juu ni ishara ya matatizo ya kiafya.
. Imaging. Vipimo vya ultrasounds, MRI na CT scans hutoa picha ya figo na njia ya mkojo ili kubaini kuziba na matatizo mengine.
. Kidney tissue sample. Sampuli za tishu huchunguzwa ili kuona kutuama kwa vitu visivyo vya kawaida, makovu au vijidudu wabaya. Daktari atachukua sampuli kutumia kidney biopsy.
Tiba ya Figo
Hakuna tiba kamili kwa kufeli sugu kwa figo. Kuna hatua zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza kasi ya kuongezeka kwa tatizo.
Dawa
Kufeli kwa figo kunahusiana na high blood pressure, kwa hiyo daktari anaweza kukupa dawa za high blood pressure. Unaweza pia kupewa dawa ziitwazo statins ili kupunguza cholesterol mwilini.
Mara nyingi kufeli kwa sugu huambataba na upungufu wa damu. Unaweza kuhitaji dawa za kuongeza utengenezwaji wa seli nyekundu za damu. Aghalabu, unaweza kuongezewa damu. Iwapo tatizo lako la figo linasababisha maji kubaki mwilini, diuretics zinaweza kusaidia kupunguza uvimbe. Dawa hizi hukufanya ukojoe mara nyingi zaidi.
Matumizi ya calcium na vitamini D ya ziada yatasaidia kuilinda mifupa yako. Kama una ugonjwa sugu wa kufeli figo, utakuwa na kiwango kidogo sana cha vitamini D, ambayo ni muhimu katika ufyonzwaji wa calcium. Kutumia vitamini D kutapunguza hatari ya kuvunjika kwa mifupa yako. Kiwango cha phosphates kitapanda pale figo zinapofeli, hali ambayo itapunguza ufyonzwaji wa calcium. Daktari anaweza kukuandikia phosphate binders, dawa za kudhibiti kiwango cha phosphates ndani ya mwili.
Antihistamines zinaweza kupunguza tatizo la miwasho kwenye ngozi.
Antiemetics zinaweza kupunguza kichefuchefu.
Chakula
Mabadiliko katika ulaji yanaweza kuwa ya lazima. Watu wenye tatizo sugu la kufeli figo kwa kawaida wanatakiwa kupunguza ulaji wa protini. Mwili unaposaga protini, hutoa mabaki. Figo hufanya kazi ya kuyachuja mabaki hayo. Chakula chenye protini ndogo husaidia ufanyaji kazi wa figo.
Utatakiwa kuwa makini na viwango vya chumvi, potassium, na phosphate. Figo zako huafanya kazi ya kuondoa potassium iliyozidi ndani ya mwili. Zisipofanya kazi vizuri, viwango vya potassimu mwili vitazidi (hyperkalemia), hali ambayo hutishia maisha. Hyperkalemia huathiri utendaji kazi wa moyo na kusababisha kupooza.
Figo zenye dosari haziwezi kuondoa phosphate. Uwingi wa phosphate husababisha mwili ushindwe kufyonza calcium. Chakula chenye phosphate kwa wingi ni pamoja na samaki, mayai, bidhaa zinazotokana na maziwa na nyama.
Unaweza kushauriwa kupunguza vinywaji ili figo zififanye kazi sana.
Mtindo Wa Maisha
Unashauriwa kuacha kuvuta sigara na kuzingatia sindano zako, pamoja na zile za mafua.
End-Stage Treatment
Kuna tiba kadhaa zinazoweza kutolewa kwa figo zilizofeli. Aina ipi itatumika, itategemea sababu ya kufeli kwa figo na hatua iliyofikiwa.
Dialysis
Dialysis huchuja na kusafisha damu kwa kutumia mashine. Mashine hufanya kazi ya figo. Kulingana na aina ya dialysis, mgonjwa unaweza kuunganishwa kwenye mashine kubwa (hemodialysis) utaujaza uwazi wa tumbo lako na mchanganyiko maalumu kupitia catheter (peritoneal dialysis). Machanganyiko huu utafyonza maji ya ziada na mabaki kabla haujatolewa nje ya mwili. Kwa sababu dialysis hufanya mara kadhaa kila wiki, ni mtindo mpya wa maisha na kuna hatari ya kupata maambukizo ya wadudu.
Pamoja na dialysis, utahitajika kuwa mlo maalumu wenye viwango vidogo vya potassium na chumvi.
Dialysis haifanyi uponyaji wa figo, bali inaweza kuongeza urefu wa maisha kama utakwenda mara kwa mara na kufuata masharti.
Kidney transplant
Uchaguzi mwingine kwa tiba ya figo zilizofeli ni kidney transplant. Figo iliyopandikizwa inaweza kufanya kazi vizuri na hutahitaji dialysis.
Kwa kawaida inachukua muda mrefu kabla ya kumpata mtoaji wa figo ambaye mwili wake unaendana na wa kwako. Kama una mtoaji aliye hai, muda utakuwa mfupi.
Mtoaji lazima awe wa kundi la damu sawa na la kwako. Figo kutoka kwa mtoto wako au ndugu wa karibu huwa bora zaidi.
Upasuaji wa kidney transplant si tiba sahahi kwa kila mtu. Upasuaji unaweza usifanikiwe.
Utatakiwa kutumia immunosuppressant drugs baada ya upasuaji kuzuia mwili wako usiikatae figo uliyowekewa. Dawa hizi zina madhara , mengine yakiwa ya kuhatarisha.
Katika mada nyingine tatalizungumzia tatizo la kufeli kwa figo kutokana na kisukari. Usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali uliyo nayo kuhusu mada hii.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wetu wa Facebook wa LINDA AFYA YAKO kupata mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya mwanadamu na tiba mbalimbali. Usikose kuweka LIKE endapo utafurahishwa na mada hizo.
Kwa mawasiliano na maelezo zaidi tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: +255 655 858027 au +255 756 181651.