Watu wengi wanasumbuliwa na tatizo la mgandamizo wa damu kuwa mkubwa na kwa lugha nyepesi ya mtaani watu huliita tatizo hili – blood pressure. Katika ukurasa wetu wa leo tumedhamiria kueleza nini maana ya mgandamizo wa damu kuwa mkubwa (high blood pressure), dalili ambazo ukiziona ujue kuwa unanyemelewa na tatizo hili, namna ya kupima mgandamizo wa damu na tiba ambazo unaweza kutumia pale itakapobainika pasi shaka kuwa una tatizo hili la high blood pressure.
Kwanza tuwekane sawa kuwa msukumoo wa damu ni muhimu kwa maisha yetu, bila kuwepo na msukumo wa damu wa kuifanya damu izunguke ndani ya miili yetu, hewa ya oksijeni na virutubishi havitaweza kupita kwenye ateri na kuvifikia viungo vya miili yetu. Sasa msukumo huu wa damu unaweza kuwa mkubwa mno (hypertension), au mdogo mno kuliko inavyostahili na hapo ndipo tunasema kuna tatizo. Kuna kipimo kinachotakiwa ili kuziwezesha chembechembe za damu, zikiwemo chembechembe nyeupe za damu kwa ajili ya kinga, kuzunguka katika miili yetu.
Mgandamizo Wa Damu (Blood Pressure) Ni Nini?
Mgandamizo wa damu ni nguvu ya damu ya kusukuma kuta za mishipa ya damu. Nguvu hiyo inategemeana na uwingi wa damu inayosukumwa na moyo na uwezo wa mishipa ya damu ya arteri wa kuhimili nguvu hiyo. Kiwango cha damu inayosukumwa na moyo kikiwa kikubwa na kipenyo cha arteri kikiwa kidogo, mgandamizo wa damu kwenye kuta za arteri hizo utakuwa mkubwa. Kadri uwingi wa damu utakavyoongezeka kutoka kwenye moyo au kipenyo cha arteri kitakavyopungua, ndivyo mgandamizo wa damu kwenye kuta za arteri utakavyoongezeka.
High blood pressure ni hali ya kuwepo kwa muda mrefu kwa mgandamizo wa damu kwenye kuta za arteri ambao ni mkubwa kiasi cha kuweza kuleta matatizo ya kiafya.
Unaweza kuwa na tatizo hili la kuwa na mgandamizo mkubwa wa damu – high blood pressure au hypertension – kwa miaka mingi bila kuanza kuona dalili zo zote au kutopata matatizo yo yote. Pamoja na kuwa hujaanza kuona dalili zo zote, uharibifu wa mishipa ya damu na moyo huendelea na baadaye unaweza kupata matatizo makubwa ya kiafya kama shinikizo la damu (heart attack) na kiharusi (stroke). Yafaa basi kujipima na kujua mapema kuwa una tatizo la high blood pressure ili uanze kuidhibiti hali hiyo.
Tatizo la kuwa na mgandamizo mkubwa wa damu huongezeka taratibu kwa miaka mingi na karibu kila mmoja wetu huathiriwa na tatizo hili. Inakladiriwa kuwa ifikapo 2025, watu bilioni 1.56 katika dunia watakuwa wanaishi na tatizo hili. Bahati nzuri ni kuwa linaweza kugundulika kirahisi sana na kudhibitiwa.
High Blood Pressure Ni Nini?
Mgandamizo wa damu (Blood Pressure) hupimwa kwa kulinganisha mgandamizo wa damu kwenye kuta za arteri wakati moyo unasukuma damu ( systolic reading) na mgandamizo huo wakati moyo unajilegeza na kuruhusu damu kujaa ndani yake (diastolic reading).
High blood pressure ni kuwa na mgandamizo wa damu unaozidi 140 juu ya 90 mmHg, kama inavyochukuliwa na vyombo vya mwongozo wa tiba.
Maana yake ni kuwa, mtu atahesabika ana tatizo pale mgandamizo wake wa damu utakapozidi 140 mmHg wakati moyo unasukuma damu na unapozidi 90 mmHg moyo wake unapojilegeza na kujaza damu. Kiwango hiki kimewekwa kwa ajili ya ufanisi katika tiba. Viwango vya chini ya hivi ni vizuri zaidi kwa afya, na nchi nyingine zinaelezea kwa undani zaidi viwango hivi kama ifuatavyo:
. Normal blood pressure ni kuwa kipimo chini ya 120 systolic na chini ya 80 diastolic
. Prehypertension ni 120-139 systolic au 80-89 diastolic
. Stage 1 high blood pressure (hypertension) ni 140-159 systolic au 90-99 diastolic
. Stage 2 high blood pressure (hypertension) ni 160 au juu zaidi systolic au 100 au juu zaidi diastolic
. Hypertensive crisis (Hali mbaya) ni wakati mgandamizo ni juu zaidi ya 180 systolic au juu ya 110 diastolic.
Mgandamizo mkubwa wa damu unaweza kuleta matatizo kwenye viungo vitakavyoathiriwa na mgandamizo huo. Mgandamizo huo mkubwa wa damu ukienda kwa muda mrefu unaweza kusababisha yafuatayo kutokana na mishipa ya damu kusinyaa (arteriosclerosis).
. Kupanuka au kudhoofika kwa moyo hadi kufikia kushindwa kusukuma damu ya kutosha (heart failure)
. Aneurysm – uvimbe mkubwa kwenye kuta za arteri
. Kusinyaa kwa mishipa ya damu – kwenye figo, na kusababisha figo kushindwa kufanya kazi; na kwenye moyo, ubongo na miguu na kuweza kusababisha moyo kushindwa kuendelea kufanya kazi, kiharusi au kukatwa miguu.
. Mishipa ya damu kwenye macho inaweza kupasuka na kusababisha macho kutoona vizuri au upofu ( (hypertensive retinopathies).
Dalili Za High Blood Pressure
Watu wengi wenye pressure ya juu hawapati dalili zo zote, hii ndiyo sababu watu huuita ugonjwa huu “the silent killer”. Pressure ikifika kiwango cha 180/120 mmHg, ni hali inayoitwa hypertensive crisis, na tiba ya haraka inahitajika.
Kwenye kiwango hiki mtu anaweza kusikia:
. kichwa kuuma
. kichefuchefu
. kutapika
. kizunguzungu
. damu kutoka puani
. mapigo ya moyo kwena mbio
. shida kupumua.
Ukisikia dalili hizi yafaa kuomba ushauri wa tiba mara moja.
Dalili kwa wanawake
Tofauti za homoni huleta tofauti ya athari za pressure baina ya wanaume na wanawake. Hatari ya kupata tatizo la pressure kwa wanawake huongezeka kutokana na:
. ujauzito
. kukoma hedhi
. kutumia vidonge vya uzazi wa mpango
Wakati wa ujauzito, pressure ya juu huweza kuashiria preeclampsia, hali hatarishi inayoweza kuleta mattizo kwa mama na kichanga cha tummboni.
Dalili za preeclampsia ni pamoja na:
. maumivu ya kichwa
. mabadiliko ua uonaji
. maumivu ya tumbo
. kuvimba kutokana na edema
Dalili kwa vijana wa miaka ya mwanzo ya 20
Vijana wadogo wanaweza kuapata tatizo la pressure kutokana na unene au tatizo jingine la kiafya. Baadhi ya sababu za kiafya ni:
. sababu za kimetaboliki, kama type 2 diabetes
. magonjwa ya figo
. magonjwa ya mfumo wa homoni, yanayoathiri homoni
. magonjwa ya mishipa ya damu
. magonjwa neva
Dalili kwa watoto wadogo
Tatizo la pressure huweza kuwapata watoto wadogo. Kuwa na unene wa kupindukia na kisukari huongeza uwezekano wa pressure, lakini sababu nyingine zaweza kuwa:
. uvimbe
. matatizo ya moyo
. matatizo ya figo
. obstructive sleep apnea
. matatizo ya thyroid
. magonjwa ya urithi, kama Cushing’s syndrome
. matumizi ya baadhi ya madawa
. Chakula chenye chumvi nyingi au mafuta
Sababu Za High Blood Pressure
Mgandamizo wa damu katika mwili huwa na kawaida ya kubadilika, hushuka wakati mtu amelala na kupanda anapoamka. Hupanda vilevile mtu anaposhikwa na butwaa, anapokuwa na wasiwasi na wakati anafanya shughuli za nguvu zinazotumia viungo vya mwili. Kwa hiyo ni jambo la kawaid kuwa na mgandamizo mkubwa wa damu kwa vipindi vifupi, mtu atahitaji kuwa makini pale vipimo vinapobakia kuwa juu muda wote.
Sababu za kuwa na high blood pressure (Hypertension) ni pamoja na:
Staili ya maisha: Baadhi ya sababu za high blood pressure zinazotokana na mtindo wa maisha ni:
. Kutojishughulisha
. Chumvi kwenye chakula cha kusindikwa na chenye mafuta
. Pombe na uvutaji wa tumbaku
. Chakula kisicho na madini ya potassium ya kutosha.
Mambo mengine ni pamoja na:
Umri: Kila mtu anakuwa hatarini kupatwa na high blood pressure umri wake unapokuwa mkubwa. Tatizo huonekana zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi.
Urithi: Wamarekani weusi wanapatwa zaidi na tatizo hili kuliko watu weupe
Uzito: Watu wenye uzito mkubwa au wanene wapo kwenye hatari kubwa zaidi
Jinsia: Pamoja na kuwa jinsia zote zipo hatarini, wanaume huwa kwenye hatari wakiwa kwenye umri mdogo wakati wanawake hupatwa zaidi na tatizo hili wanapokuwa na umri mkubwa
Msongo wa mawazo: Msongo wa mawazo huongeza hatari ya kupata tatizo la high blood pressure.
Sababu hizi zote tulizoziorodhesha hapo juu husababisha aina ya high blood pressure inayoitwa Primary Hypertension. Primary hypertension huwa haitokani na chanzo kimoja bali ni mchanganyiko wa sababu kama tulizoziorodhesha hapo juu – haina chanzo kimoja kinachoeleweka moja kwa moja. Kwa nyongeza; ujazo wa plasma katika damu na homoni ya kudhibiti ujazo wa damu na mgandamizo wa damu, pia huchangia kwenye aina hii ya high blood pressure.
Aina ya high blood pressure ambayo chanzo chake kinaeleweka -ambayo inatokana na chanzo kingine – huitwa Secondary hypertension. Mifano ya vyanzo vya aina hii ya high blood pressure ni:
. Ugonjwa wa figo
. Saratani aina ya Pheochromocytoma
. Cushing syndrome inayotokana na matumizi ya madawa (corticosteroid drugs)
. Congenital adrenal hyperplasia – matatizo ya tezi ya adrenal
. Hyperthyroidism – tezi ya thyroid kufanya kazi zaidi
Tiba Ya High Pressure
Kubadili namna ya mtu anavyoishi ndicho kitu muhimu zaidi katika kuzuia na kutibu tatizo la high blood pressure, na hili linaweza kuwa na matokeo mazuri kama yale ya kutumia dawa. Wataalamu wanashauri yafuatayo katika kupunguza blood pressure:
. Kupunguza matumizi ya chumvi
. Kupunguza unywaji wa pombe
. Kuongeza ulaji wa mboga za majani na matunda
. Kupuguza uzito wa mwili
. Kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara – mtu mwenye high blood pressure anashauriwa afanye mazoezi kama ya kutembea, jogging, kuendesha baiskeli, kuogelea kwa angalu dakika 30 kwa siku, mara 5 hadi 7 kwa wiki.
Dawa za kutibu high blood pressure
Dawa za kutibu high blood pressure zinatolewa kulingana na vipengele kadhaa, ikiwa ni pamoja na kiwango cha pressure na hatari iliyopo ya magonjwa ya moyo na stroke. Daktari atatoa dawa tofauti kulingana na kuongezeka kwa pressure. Ikiwa kiwango ni cha juu kidogo ya kawaida, mgonjwa nanweza kushauriwa kuhusu kubadili mtindo wa maisha na kufuatilia pressure yake.
Pressure ikifikia viwango vya juu, mgonjwa atashauriwa kutumia dawa. Dawa zinaweza kubadilishwa baada ya muda kulingana na ukali wa pressure yake au kama kuna magonjwa ya ziada yatakayojitokeza, kama magonjwa ya figo. Watu wengine watahitaji mchanganyiko wa madawa.
Madawa
Madawa yanayotumika kutibu pressure ni pamoja na:
Angiotensin Converting enzyme inhibitors
Angiotensin converting enzyme (ACE) inhibitors huzuia utendaji kazi wa baadhi ya homoni zinazosimamia pressure ya damu, kama angiotensin II. Angiotensin II husababisha mishipa ya damu kubana na kuongeza uwingi wa damu, na hivyo kuongeza pressure.
ACE inhibitors huweza kupunguza upelekwaji wa damu kwenye figo, na kupunguza utendaji wa figo. Kwa hiyo, watu wanaotumia dawa hizi wanatakiwa kuchukua vipimo vya damu mara kwa mara.
Yashauriwa kuacha kutumia ACE wakati wa ujauzito au kama kuna mazingira yanayoathiri mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.
ACE inhibitors zinaweza kusababisha hali zifuatazo, ambazo hupotea zenyewe baada ya siku chache:
. kizunguzungu
. uchovu
. udhaifu wa mwili
. maumivu ya kichwa
. kikohozo kikavu kisichoisha
Calcium channel blockers
Calcium channel blockers (CCBs) zinalenga kupunguza kiwango cha calcium katika mishipa ya damu. Hii itanalegeza msuli wa mshipa, na kupunguza nguvu ya kukaza ya msuli kukaza, ateri kupanuka, na pressure ya damu kupungua.
Lakini, CCBs si nzuri sana kwa watu wenye historia ya magonjwa ya moyo, maini au matatizo ya mzunguko wa damu.
Hali zifuatazo zinaweza kujitokeza baada ya kutumia CCBs, lakini mara nyingi hupotea baada ya siku cahche:
. wekundu kwenye ngozi, hasa shingoni na kwenye nyayo
. maumivu ya kichwa
. uvimbe kwenye vifundo vya miguu na nyayo
. kizunguzungu
. uchovu.
. ukurutu
. kuvimba tumbo, mara chache.
Thiazide diuretics
Thiazide diuretics huzisaidia figo kutoa maji na sodium, na hivyo kupunguza ujazo wa damu na pressure.
Hali zifuatazo zaweza kujitokeza na nyingine zikadumu kwa muda:
. upungufu wa potassium katika damu, hali inayoweza kuathiri utendaji wa moyo na figo
. kupungua kwa ustahimilivu wa glucose
. jogoo kushindwa kuwika (erectile dysfunction)
Watu wanaotumia thiazide diuretics wanatakiwa kuchukua vipimo vya damu na mkojo mara kwa mara ili kujua viwango vyao vya sukari na potassium,
Beta-blockers
Beta-blockers zilitumika sana katika kutibu pressure hapo zamani, lakini sasa madaktri watatumia tiba hii endapo tiba nyingine hazileti mafanikio.
Beta-blockres hupunguza kasi ya mapigo ya moyo na hivyo kupunguza nguvu ya msukumo wa moyo na kusababisha kupuguza msukumo wa damu.
Beta-blockers zikitumika zinaweza kusababisha yafuatayo:
. uchovu
. ubaridi kwenye mikono na nyayo
. mapigo ya moyo kuwa chini
. kichefuchefu
. kuharisha
Mara chache yafuatayo hutokea:
. kukosa usingizi mnono
. kuota ndoto mbaya
. jogoo kushindwa kuwika (erectile dysfunction)
Beta-blockers zimebakia kwa matumizi ya watu wenye pressure ya juu sana, hali iitwayo hypertensive crisis.
Renin inhibitors
Aliskiren (Tekturna, Rasilez) hupunguza uzalishwaji wa renin, kimeng’enya kinachozalishwa na figo.
Renin husaidia utengenezwaji wa homoni inayopunguza kipenyo cha mishipa ya damu na kupandisha pressure. Kupunguza uzalishwaji wa homoni hii kunasababisha mishipa ya damu kupanuka na kushusha pressure.
Hali tokanazo zaweza kuwa:
. kuharisha
. kizunguzungu
. mafua
. uchovu
. kikohozi
Ushauri wa Chakula
Kula chakula kinachoshauriwa kutasaidia kuzuia au kutibu high blood pressure.
Chakula kinachotokana na mimea
Mlo kamili wenye virutubishi ni ule ulio na matunda na mboga za kutosha, mafuta ya mboga na omega, nafaka bora isiyokobolewa, kama nafaka nzima. Watu wanaotumia bidhaa za mimfugo katika chakula chao wanapaswa kuondoa mafuta na kukwepa nyama za kusindikwa.
Kupunguza matumizi ya chumvi
Wataalamu wanashauri kupunguza chumvi na kuongeza ulajiwa potassium ili kuzuia kupanda na kudhibiti pressure. Kutmia chumvi kiasi kisichozidi gramu 6 kwa siku kunaweza kuboresha afya ya moyo na kupunguza systolic blood pressure kwa kiwango cha 5.6 mmHg baina ya watu wenye pressure.
Mafuta yenye lishe bora
Ulaji wa kawaida wa mafuta yanayotokana na mimea, kama avocado, njugu, mafuta ya mzeituni na mafuata ya omega, unaweza kuwa na manufaa. Watu wanashauriwa kupunguza ulaji wa saturated fats na trans fats, aina za mafuta yanayopatikana kutokana na bidhaa za wanyama na chakula kilichosindikwa.
DASH diet
Wataalamu wa afya wanapendekeza mlo uitwao DASH diet kwa ajili ya watu wenye pressure. Mlo huo unaweka msisitizo kwenye nafaka nzima, matunda, mboga za majani, mbegu, maharage na bidhaa za wanyama zenye mafuta kidogo.
Mazoezi ya mwili
Watu wenye afya wanashauriwa kufanya mazoezi ya mwili ya kawaida hadi mazito ya angalau dakika 150 kwa wiki. Hii inaweza kuwa kipindi kimoja cha dakika 30 – au vipindi vitatu vya dakika kumi kumi kwa siku – siku 5 kwa wiki.
Kiwango hiki hiki kinafaa kwa mtu mwenye high blood pressure.
Lakini mtu ambaye hakufanya mazoezi kwa kipindi kirefu kidogo au aliyegundulika sasa hivi kuwa ana tatizo la pressure anatakiwa apate ushuri wa daktari kabla ya kuanza mazoezi ya mwili wake.
Kupunguza uzito
Tafiti zimeonyesha kuwa kupunguza uzito kwa kiasi kidogo tu kama cha kilo 4.5 kinaweza kusaidia kupunguza pressure. Kupunguza uzito kutasaida pia utendaji wa dawa za kupunguza pressure.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wetu wa Facebook wa LINDA AFYA YAKO kupata mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya mwanadamu na tiba mbalimbali. Usikose kuweka LIKE endapo utafurahishwa na mada hizo.
Usisite kuulizwa swali ulilo nalo au kutoa maoni yako binafsi kuhusu mada hii yetu ya leo. Tutafurahi sana kusikia kutoka kwako.
Kwa mawasiliano na maelezo zaidi tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya saa za kazi kwenye nambari zifuatazo: +255 655 858027 au +255 756 181651.