fumo wa kinga za mwili ni ulinzi wa mwili dhidi ya viumbehai na vivamizi wa aina nyingine. Kupitia hatua kadhaa ziitwazo immune response, mfumo wa kinga za mwili hushambulia viumbehai na vitu vinavyouvamia mwili na kusababisha maradhi. Mfumo wa kinga za mwili unaundwa na mtandao wa seli, tishu na viungo vinavyofanya kazi kwa pamoja ili kuulinda mwili. Mfumo huu wa kinga za mwili hufanya kazi ya kutulinda dhidi ya viini vya maradhi na vijiumbe wadogo kila siku wakimemo bakteria, virusi, vimelea n.k. Kiujumla, mfumo huu hufanya kazi nzuri ya kuwaweka binadamu kwenye afya bora na kuzuia maradhi. Lakini wakati mwingine matatizo katika mfumo huu wa kinga za mwili huweza kuleta maradhi na maambukizi ya wadudu.
Mtandao huu wa seli na tishu kila wakati upo macho kubaini vivamizi, na mara adui akionekana, shambulio kubwa hufanywa dhidi yao.
Mfumo huu wa kinga za mwili umesambaa mwili mzima na unahusisha aina nyingi za seli, viungo, protini, na tishu. Tabia ya maana sana ni kuweza kutofautisha tishu za miili yetu na tishu za vivamizi. Seli zenye hitilafu na zilizokufa hutambuliwa na kutolewa nje na kinga hizi.
Kinga za mwili zikigundua kiambukizi cha magonjwa kama vile bakteria, kirusi, au kimelea, huanzisha shambulio (immune response).
Sasa tuone vitu muhimu vinavyounda mfumo wa kinga za mwili wa binadamu.
Chembechembe Nyeupe Za Damu (White Blood Cells)
Chembechembe nyeupe za damu huitwa pia leukocytes. Chembechembe hizi huzunguka katika mfumo wa damu ndani ya mishipa ya damu na ndani ya mishipa ya mfumo wa limfu (lymphatic vessels) ambayo imetanda mwilini sambamba na veni na ateri. Chembechembe nyeupe za damu muda wote huwa kwenye doria kuchunguza uwepo wa viambukizi vya magonjwa. Chembechembe hizi zikigundua adui hujikusanya na kutoa ishara kwa seli za namna nyingine.
Chembechembe nyeupe za damu huhifadhiwa sehemu tofauti za mwili, sehemu ambazo huitwa lymphoid organs. Sehemu hizi ni kama:
. Thymus – tezi iliyopo kati ya mapafu na chini kidogo ya shingo
. Bandama (spleen) – ogani inayofanya kazi ya kuchuja damu. Ogani hii ipo juu ya tumbo upande wa kushoto.
. Uboho (bone marrow) – Huu unapatikana ndani ya mifupa, pia hutengeneza chembechembe nyekundu za damu.
. Lymph nodes – tezi ndogo zilizopo sehemu mbalimbali mwilini, zinazounganishwa na mishipa ya limfu.
Kuna aina kuu mbili ya chembechembe nyeupe za damu:
1. Phagocytes
Seli hizi huvizunguka na kuvifyonza viini vya magonjwa na kuvivunjavunja, na kuvimeza. Mlolongo wa hatua za kuangamiza na kumeza vitu vinavyovamia seli za mwili huitwa phagocytosis. Kuna aina kadhaa ya seli hizi zikiwemo:
. Neutrophils — Hii ndiyo aina ya phagocytes inayoonekana kwa wingi zaidi na hufanya kazi ya kuvamia bakteria.
. Monocytes — Hizi ndizo seli zenye umbo kubwa zaidi na hufanya kazi kadhaa.
. Macrophages — Macrophages huanzia maisha ndani ya uboho. Seli hizi hufanya doria dhidi ya viini vya magonjwa na kuondoa seli za mwili zilizokufa au zinazokufa.
. Mast cells — Seli hizi hufanya kazi nyingi ikiwa ni pamoja na kuponya vidonda na kujilinda dhidi ya viini vya maradhi.
2. Lymphocytes
Lymphocytes hufanya kazi ya kukumbuka vivamizi na kuvitambua wakati vikija kufanya uvamizi tena kwenye mwili.
Maisha ya lymphoctes yanaanzia ndani ya uboho. Seli nyingine hubaki ndani ya uboho na kugeuka kuwa B lymphocytes (B cells), wakati nyingine huelekea hadi kwenye thymus na kugeuka kuwa T lymphocytes (T cells). Seli za aina hizi mbili hufanya kazi tofauti:
. B lymphocytes — hutoa kingamwili (antibodies) na kusaidia kutoa tahadhari kwa T lymphocytes.
. T lymphocytes — Huvunja na kutoa nje seli za mwili zilizochoka na kusaidia kutoa tahadhali kwa chembechembe nyeupe za damu zingine.
Jinsi Kinga Za Mwili Zinavyofanya Kazi
Kinga za mwili zinatakiwa kuwa na uwezo wa kupambanua kati ya seli na tishu za mwili na vitu kutoka nje. Kinga huweza kufanya upambanuzi kwa kuchunguza protini zilizo juu ya seli. Hujifunza kuziacha (kutozidhuru) protini binafsi katika hatua za awali kabisa.
Kitu cho chote kinachosababisha kinga za mwili kuanzisha shambulio huitwa antigen.
Mara nyingi antigen huwa ni bacteria, fangasi, sumu, chembechembe za vumbi, au kiumbe kingine kutoka nje. Lakini inaweza kuwa ni seli ya mwili yenye dosari au iliyokufa. Seli za aina nyingi kwa pamoja hutambua uwepo wa antigen kama adui.
Kazi Ya B Lymphocytes
Mara baada ya kumwona adui yaani antigen (antigen ni kifupi cha “antibody generators”), B lymphocytes hutoa kingamwili . Kingamwili (antibody) ni protini za kipekee ambazo humzunguka adui.
Kila seli ya B lymphocyte hutoa kingamwili ya aina yake. Kwa mfano seli moja itatoa kingamwili dhidi ya bakteria aletae pneumonia, na nyingine inaweza kutambua kirusi aletae mafua.
Kingamwili (antibodies) ni sehemu ya familia ya kemikali ziitwazo immunoglobulins, ambazo zina kazi nyingi katika ulinzi dhidi ya adui. Kazi ya kingamwili ni kumnasa na kumzungua adui, lakini si kuua. Kuua ni kazi ya seli nyingine, kama phagocytes.
Kazi za T Lymphocytes
Kuna aina tofauti mbili za T lymphocytes:
Helper T cells (Th cells) — Zinafanya kazi ya kuratibu mashambulizi dhidi ya adui. Baadhi huwasiliana na seli nyingine, nyingine huzichochea B cells ili zitoe kingamwili zaidi. Nyingine huziita T cells au seli zinazotafuna seli za adui-phagocytes.
Killer T cells (cytotoxic T lymphocytes) — Seli hizi huua seli nyingine. Seli hizi ni muhimu sana katika kupambana na virusi.
Kinga Za Mwili
Kila mtu ana kinga za mwili zilizo tofauti na kinga za mtu mwingine, lakini kwa kawaida kinga za mwili huwa imara zaidi mtu anapofikia utu uzima, kwa sababu muda huu, ameshapambana na aina nyingi sana za viini vya magonjwa na kujijengea kinga zaidi.
Hii ndiyo sababu vijana hupata maradhi mara chache zaidi kuliko watoto wachanga.
Kingamwili ikishatengenezwa mara moja, kivuli chake huwekwa ndani ya mwili hivi kwamba antigen yule yule akija tena, atashughulikiwa haraka zaidi.
Hii ndiyo sababu baadhi ya magonjwa, kama tetekuwanga, huja mara moja tu katika maisha ya mtu kwa vile kingamwili za tetekuwanga zilikwisha andaliwa na kuhifadhiwa tayari kutumika pale ugonjwa unaporudi. Hii huitwa kinga ya mwili.
Chanjo Dhidi Ya Magonjwa
Mtu anapopewa chanjo dhidi ya ugonjwa, antigen au viini vya ugonjwa vilivyodhoofishwa huingizwa ndani ya mwili wake kwa jinsi ambavyo havitaweza kumletea ugonjwa bali atengeneze kingamwili. Kwa vile mwili hutunza kivuli cha kingamwili zilizotengenezwa, utalindwa ikiwa ugonjwa huo utamvamia tena katika maisha yake.
Dosari Katika Mfumo Wa Kinga Za Mwili
Kwa vile mfumo wa kinga za mwili una vipengele vingi sana, kuna namna nyingi ambavyo unaweza kujikuta haufanyi kazi ipaswavyo. Dosari za kinga za mwili huangukia katika makundi matatu yafuatayo:
Immunodeficiencies. Haya ni matatizo ya ukosefu wa kinga mwilini yatokanayo na sehemu ya mfumo wa kinga mwilini kukosekana au kutofanya kazi vizuri. Watu wengine huzaliwa wakiwa na ukosefu wa kinga – hii huitwa primary immunodeficiency, ingawa dalili zake hujitokeza baadaye sana katika maisha yao. Ukosefu wa kinga mwilini huweza kutokea kwa sababu ya maambukizi ya wadudu au matumizi ya madawa – secondary immunodeficiency.
Immunodeficiencies huweza kuathiri B lymphocytes, T lymphocytes, au phagocytes. Mfano wa primary immunodeficiency inayowaathiri watoto na vijana ni IgA deficiency. Immunoglobulin A (Iga) ni immunoglobulin ambayo hupatikana katika mate na majimaji mengine ya mwili. IgA deficiency ni hali ambapo mwili hauzalishi kiasi cha kutosha cha kingamwili IgA. Watu wenye IgA deficiency huwa wana matatizo ya mzio au kupata mafua mara kwa mara na maambukizi kwenye mfumo wa upumuaji.
Mfano wa Acquired (secondary) immunodeficiency ni UKIMWI ambao ni ugonjwa ambao taratibu huharibu mfumo wa kinga za mwili. Husababishwa na kirusi – VVU ambaye hubomoa aina fulani za lymphocytes – T-helper cells. Bila T -helper cells, mwili unashindwa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya hata vijidudu ambavyo kwa kawaida huwa si wabaya.
Autoimmunity. Mfumo wa kinga za mwili kwa makosa hushambulia seli zenye afya badala ya viini vya maradhi au seli zenye dosari. Katika hali hii, kinga za mwili zimeshindwa kutofautisha seli binafsi na seli za vitu kutoka nje.
Magonjwa yatokanayo na tatizo hili (autoimmune diseases) ni pamoja na celiac disease, type 1 diabetes, rheumatoid arthritis, na Grave’s disease.
Hypersensitivity
Allergic Disorders. Matatizo ya mzio (allergic disorders) yanatokea wakati mfumo wa kinga za mwili unatoa shambulio kubwa kuliko inavyotakiwa pale panapotokea antigen. Vitu vinavyochokoza mashambulio hayo huitwa allergens.
Mzio (allergy) hutokea pale mwili wako unaposhambulia kitu kutoka nje – kama poleni, sumu ya nyuki au manyoya ya mnyama – au hata chakula, ambavyo havileti madhara kwa watu wengi.
Mwili hutoa kingamwili (antibodies) ziitwazo Immunoglobulin E (IgE) ambazo hutambua allergen hiyo kama kitu kibaya, wakati si kweli, na kuanza mashambulizi. Unapokutana na allergen, shambulio la kinga zako za mwili husababisha uvimbe juu ya ngozi, njia za hewa au kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Mfumo wa kinga za mwili huweza pia kusababisha majimaji machoni na kupiga chafya. Dawa ziitwazo antihistamines huweza kuondoa dalili hizi.
Matatizo ya mzio ni kama:
. Pumu (asthma). Dosari katika mfumo wa upumuaji ambayo inaweza kuleta matatizo katika upumuaji, ambayo mara huletwa na matatizo katika mapafu. Kama mapafu yana usikivu mkubwa zaidi kwa allergens (poleni, manyoya au vumbi), njia za upumuaji hubana na kuvimba, hivyo kusababisha shida ya upumuaji.
. Eczema. Ni uvipele vidogo vinavyowasha. Eczema hutokea ziadi kwa watoto wadogo na vijana wenye mzio, pumu au waliotoka kwenye familia zenye historia ya tatizo hili.
Katika mada nyingine tatazungumzia historia ya UKIMWI na kujadili kwa kina kuona UKIMWI ni ugonjwa gani. Tunakuomba msomaji wetu kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo na kuuliza maswali yo yote uliyo nayo. Kwetu sisi ni faraja kubwa kuona tumekujibu kiufasaha.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.