Kifua Kikuu (Tuberculosis-TB) Ni Ugonjwa Gani

 

mgonjwa wa TB

 

Kifua Kikuu (Tuberculosis) ni ugonjwa wa kuambukiza ambao mara nyingi hushambulia mapafu. Ugonjwa huu unachukua nafasi ya pili duniani ya vifo vinavyotokana na maambukizi yanayotokana na kitu kimoja. Ugonjwa wa kifua kikuu huenezwa na bakteria na  kifua kikuu (TB) huenea kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia matone madogo yanayotolewa na mtu akikohoa au kupiga chafya. Awali, ugonjwa huu ulikuwa nadra katika nchi zilizoendelea, lakini maambukizi yalianza kuongezeka mwaka 1985, kwa namna fulani yakichangiwa na kuibuka kwa HIV, virusi waletao UKIMWI.

Vizazi vingi vya bakteria wa tuberculosis vimekuwa sugu kwa dawa ambazo zilikuwa zikitumika kuuponya ugonjwa huo. Watu wenye ugonjwa huo wanawajibika kutumia dawa za aina nyingi kwa muda mrefu ili waweze kupona.

Katika miaka ya katikati ya karne za 18 na 19, kulitokea milipuko ya ugonjwa huu huko Ulaya na Marekani Ya Kaskazini, kabla ya mwanasayansi kutoka Ujerumani, Robert Koch, kumgundua bakteria anayesababisha kifua kikuu mwaka 1882.

Kufuatia ugunduzi wa Robert Koch, ugunduzi na utumiaji wa chanjo na dawa za kuponya kifua kikuu ulileta imani kuwa ugonjwa huu ungetokomezwa. Mara moja Shirika la Umoja Wa Mataifa lilibashiri kuwa ugonjwa huu utakuwa umetokomezwa kufikia 2025.

Lakini katika miaka ya kati ya 1980 na 1990, TB iliongezeka kwa kasi duniani, hivi kwamba mwaka 1993 Shirika La Afya Duniani (WHO) lilitangaza hali ya hatari, kwa mara ya kwanza kabisa ugonjwa kutangazwa kwa namna hiyo.

Kwa bahati nzuri, kwa kufuata tiba kikamilifu, watu wengi waliopata TB hupona. Bila kupewa tiba nzuri, katika idadi ya wagonjwa wote wa TB, wagonjwa wafikiao hadi theluthi mbili watafariki dunia.

 

Tuberculosis Ni Nini?

 

Madakatari hutofautisha kati ya aina mbili za maambukizi ya kifua kikuu: latent na active.

 

TB aina za TB

 

Latent TB – bakteria hubaki ndani ya mwili bila kuleta madhara. Hawatoi dalili zo zote, na hawaambukizi, lakini wanaweza kuja kuanza kuleta madhara.

Active TB – bakteria wanaleta madhara na wanaweza kuambukiza kwa wengine.

Inaaminika kuwa karibu theluthi moja ya watu duniani wana latent TB. Kuna asilimia 10 ya uwezekano wa watu hawa kupata active TB, uwezekano huo ukichagizwa na upungufu wa kinga za mwili au kukosa mlo wa kutosha au kuvuta sigara.

TB ni ugonjwa unaoshambulia watu wa rika zote na watu wa pande zote za dunia. Lakini ugonjwa huu hushambulia zaidi vijana na watu wanaoishi kwenye nchi zinazoendelea. Takwimu za 2012 zilionyesha kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wa TB walitoka katika nchi 22 tu.

 

Kifua Kikuu Husambazwa Na Nini?

 

TB husambazwa na bakteria aitwaye Mycobacterium tuberculosis. Bakteria huyu husambaa kwenye hewa wakati mtu mwenye TB (ambaye mapafu yake yameshambuliwa) akikohoa, akipiga chafya, akitema mate, akicheka , au akizungumza.

TB huambukiza lakini siyo rahisi kuipata. Uwezekano wa kupata TB kutoka kwa mtu unayeishi au kufanya naye kazi ni mkubwa kuliko kutoka kwa mgeni. Watu wengi ambao tayari wamaeanza tiba sahihi angalau kwa wiki 2 hawaambukizi.

Toka antibiotics zilipoanza kutumika kutibu TB, baadhi ya aina ya bakteria hao wamegeuka sugu kwa dawa. Multidrug-resistant TB (MDR-TB) ni hali ambapo dawa haziwezi tena kuwaua bakteria wote, bakteria wanaosalia wakijijengea usugu wa dawa hiyo na dawa nyingine pia kwa wakati mmoja.

Multidrug-resistant TB (MDR-TB) inatibika kwa kutumia dawa za kipekee (very specific anti-TB drugs) ambazo ni chache na hazipatikani kirahisi. Katika mwaka 2012, karibu watu 450,000 walipata MDR-TB.

Watu wenye upungufu wa kinga za mwili huwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata active TB. HIV hudhoofisha kinga za mwili, na kuufanya mwili kupata shida ya kudhibiti bakteria wa TB. Watu wenye mchanganyiko wa HIV na TB wana uwezekano wa kupata active TB kwa kiwango cha asilimia 20-30 ukilinganisha na wale ambao hawana HIV.

Matumizi ya tumbaku yamedhihirika kuongeza uwezekano wa kupata active TB. Asilimia 20 ya TB duniani huhusishwa na matumizi ya tumbaku.

 

Dalili Za Kifua Kikuu

 

Wakati latent TB haina dalili zo zote, active TB huwa na dalili zifuatazo:

. Kukohoa, wakati mwingine kukiwa na makohozi au damu
. Kusikia baridi
. Uchovu
. Homa
. Kukonda kwa mwili
. Kukosa hamu ya kula
. Kutoa jasho usiku

 

dalili za kifua kikuu

 

Kifua kikuu huathiri hasa mapafu, lakini kinaweza kuathiri vile vile sehemu nyingine za mwili. Wakati TB imeathiri sehemu tofauti ya mwili, dalili zinaweza kubadilika. Bila kupata tiba, TB huweza kusambaa kwenye sehemu nyingine za mwili kupitia mfumo wa damu.

. Tb ikishambulia mifupa inaweza kuleta maumivu ya uti wa mgongo na kuharibu maungio ya mifupa
. TB ikishambulia ubongo husababisha meningitis
. TB ikishambulia maini na figo huweza kusababisha damu ndani ya mkojo
. TB ikishambulia moyo inaweza kuathiri uwezo wa moyo wa kusukuma damu na kusababisha cardiac tamponade ambayo inaweza kuua.

 

Tiba Ya Kifua Kikuu

 

Wagonjwa wengi wa TB wanaweza kupona kama dawa stahiki itakuwepo na kutolewa inavyopaswa. Aina ya dawa na urefu wa muda wa matumizi vitategemea umri wa mgonjwa, hali yake ya afya kwa ujumla, usugu wa mwili wake kwa dawa, kama TB in latent au active, sehemu yake ya mwili iliyoathirika (i.e mapafu, ubongo, figo)
Watu wenye latent TB wanaweza kuhitaji aina moja tu ya dawa, wakati watu wenye active TB (na hasa MDR-TB) watahitaji mchanganyiko wa dawa.

 

TB tiba ya TB

 

Antibiotics za TB hutakiwa kutumiwa kwa muda mrefu kidogo, muda wa wastani ukiwa ni miezi 6.

Matumizi ya dawa za kifua kikuu huweza kusababisha sumu kwa ini, ingawa ni mara chache hili kutokea, linapotokea, linaweza kuleta matatizo makubwa. Madhara ya dawa hizi yanapojitokeza, ni lazima taarifa itolewe kwa daktari. Madhara hayo ni pamoja na:
.  Mkojo mweusi
.  Homa
.  Homa ya manjano
.  Kukosa hamu ya kula
.  Kichefuchefu na kutapika

Ni muhimu kwa mgonjwa kuhakikisha kuwa anamaliza dawa, hata kama dalili za TB zitakuwa zimeondoka. Bakteria waliosalia na kuvumilia tiba iliyotolewa wanaweza kugeuka sugu kwa tiba hiyo na kupelekea kupata MDR-TB hapo baadaye.

Kataka mada nyingine tatajadili kuhusu ugonjwa wa homa ya ini (hepatitis) .

Ndugu msomaji, usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali kuhusu mada hii. Tutafurahi kuwa nawe na kukujibu.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.