Kukojoa kitandani (nocturnal enuresis or bedwetting) ni hali inayotokea ambapo mkojo hutoka wenyewe usiku wakati wa kulala. Kukojoa kitandara ni ishara ya matatizo ya udhibiti wa kibofu cha mkojo kama ya kushindwa kujizuia kukojoa (incontinence) au kibofu cha mkojo kufanya kazi kuliko kawaida au pengine ni matatizo makubwa zaidi ya kimaumbile kama ya kukua kwa tezi dume au saratani ya kibofu cha mkojo. Utafiti unaonyesha kwamba asilimia 1 hadi 2 ya watu wazima hukojoa kitandani, ingawa watafiti wamaamini kwamba takwimu hizi ni za chini kutokana na kwamba watu hawajitokezi kwa sababu ya kuona aibu. Kuliko kulificha tatizo, yafaa kufanya utafiti kuhusu tiba ambazo zinaweza kusaidia kulipunguza tatizo na kukusaidia uondokane na wasiswasi kila unapokwenda kulala usiku.
Yafaa kutambua kuwa tatizo la kukojoa kitandani kwa watu wazima lina tofauti na lile linalowasumbua watoto wadogo. Yafaa vile vile kutambua kuwa kukojoa kitandani ni jambo ambalo halikusudiwi na siyo kosa la mtu.
Ili kulitambua vizuri tatizo hili, yafaa kujikumbusha kidogo kuhusu maumbile ya njia ya mkojo.
Mkojo hutengenezwa na figo na husafiri kupitia mirija miwili (ureters) kuelekea kwenye kibofu cha mkojo ambako hutunzwa. Kibofu cha mkojo ni kifuko cha musuli kinachotunza mkojo hadi utakapotakiwa kutolewa kupitia mrija wa mkojo (urethra) unaounganisha kibofu na eneo la nje ya mwili. Kibofu cha mkojo kikijikamua, urinary sphincter huachia. Urinary sphincter iliyojilegeza hufanya kazi ya mlango unaofunguka na kuacha mkojo upite kwenda nje ya mwili. Kukitokea kizuizi kutoka kiungo cha mwili au kukosa mawasiliano ya mishipa ya fahamu, kutoka kwa mkojo kutakuwa na matatizo au kutofuata utaratibu.
Ni Nini Sababu Ya Kukojoa Kitandani?
Urithi
Kama ilivyo kwa magonjwa mengi, kitu cha kwanza kukitazama ni historia ya familia. Utafiti umeonyesha kuwa tatizo la kukojoa kitandani huweza kurithiwa. Utafiti mmoja ulionyesha kuwa mtu ambaye wazazi wake wote wawili wana tatizo hili ana asilimia 77 ya kulirithi tatizo. Kama mzazi mmoja alikuwa akikojoa kitandani wakati mdogo, mwanawe wa kiume au binti yake ana asilimia 40 za kuwa anakojoa kitandani.
Sababu Ya Homoni
Mwili hutengeneza homoni iitwayo antidiuretic hormone (ADH) wakati wa usiku, homoni ambayo hupunguza uzalishwaji wa mkojo wa figo wakati ukilala. Miili ya watu wanaokojoa usiku kitandani inatengeneza homoni hii kwa kiwango kidogo na kusababisha kukojoa kitandani. Hii inaweza kuwa ni dalili ya kisukari Type I na Type II.
Wakati mwingine mwili unatengeneza kiasi cha kutosha cha ADH, lakini figo hazitambui na kuendelea kutengeneza kiasi kile kile cha mkojo. Utengenezwaji huu wa kiasi kikubwa cha mkojo wakati wa usiku huitwa nocturnal polyuria. Dosari hii huweza kusababisha nocturnal enuresis kwa watu wazima.
Sababu Za Kimaumbile
Kukojoa kitandani kunaweza kuwa ni ishara ya matatizo ndani ya mrija wa mkojo (urethra), tezi dume, nyonga (pelvis), pamoja na maambukizi kwenye njia ya mkojo, kokoto ndani ya njia ya mkojo, kuvimba kwa tezi dume, saratani ya tezi dume na saratani ya kibofu cha mkojo.
Kibofu Cha Mkojo Kidogo
Wagonjwa wenye vibofu vya mkojo vidogo wana tatizo la primary noctural enuresis. Kiukweli si kwamba kinakuwa kidogo bali ni uwezo wa kiutendajo wa kibofu cha mkojo (functional bladder capacity – FBC) kuwa mdogo na kusababisha kibofu kutunza kiasi kidogo cha mkojo.
Misuli Ya kibofu Cha Mkojo Kufanya Kazi Zaidi (Overactive bladder muscles)
Ikiwa misuli ya kibofu cha mkojo iitwayo detrusor muscles, inafanya kazi kupita kiwango, nocturnal enuresis inaweza kutokea. Kitakwimu, utendaji kazi wa misuli ya kibofu cha mkojo wa kupitiliza umeonyesha kuhusika kwa asilimia 70 hadi 80 baina ya watu wazima wanaokojoa kitandani.
Msongo Wa mawazo
Msongo wa mawazo au mfadhaiko vinaweza kusababisha wakati mwingine watu wakakojoa kitandani.
Madawa
Madawa yameonyesha kusababisha mtu mzima akojoe kitandani. Madawa ya magonjwa ya akili, ya kuondoa tatizo la kukosa usingizi kama thioridazine, clozapine na risperidone yanaongeza uwezekano wa kupata tatizo hili.
Tiba Ya tatizo la Kukojoa Kitandani
Tiba Kwa kubadili Tabia
. Kuwa makini na kiasi cha maji unayokunywa. Kupunguza kiasi cha maji ya kunywa inapofika jioni na usiku kabla ya kulala kutapunguza kiasi cha mkojo utakaotengenezwa usiku.
. Kutumia bedwetting alarm. Kuna aina nyingi za alarm hizi, kuanzia za mtingishiko (vibration) hadi za kutoa sauti na vifaa vingine ambacho vitashikizwa kwenye chupi au kwenye kitu ambacho juu yake mtu analala.
. Kuamka. Kila mara unategesha alarm ili ikuamshe uende ukakojoe.
Tiba Kwa Upasuaji Kwa Tatizo La Kukojoa Kitandani
Utolewaji wa tiba kwa njia ya upasuaji kwa ajili ya tatizo la kukojoa kitandani ili kutibu misuli ya detrusor inayofanya kazi kupita kiasi unatakiwa ufikiriwe tu pale tiba za aina nyingine zikishindwa. Njia zote zilizotajwa hapa chini zinaweza kuleta madhara ya aina yake ambayo yanatakiwa yafikiriwe na kujadiliwa na mtaalamu wako wa tiba.
. Sacral Nerve Stimulation. Neva za sacral zinasisimuliwa na kusababisha nyuroni za misuli ya detrusor kusimama kufanya kazi. Nyuroni za misuli ya detrusor ikipunguza utendaji kazi, misuli hiyo haitajikamua mara kwa mara, na kupunguza haja ya kukojoa. SNS inashauriwa kwa watu wenye hali mbaya ya mkojo kutoka bila hiari au kwa wale ambao tiba nyingine hazikufanikiwa au haziwezi kutolewa..
. Clam Cystoplasty. Katika upasuaji huu kibofu cha mkojo hufunuliwa na kiraka cha utumbo kuwekwa katikati ya nusu mbili za kibofu hicho. Lengo ni kuimarisha kibofu cha mkojo na kuuongeza uwezo wake.
. Detrusor Myectomy. Upasuaji huu huitwa autoaugmentation na hufanyika kwa kuondoa sehemu au misuli yote inayozunguka kibofu cha mkojo. Lengo ni kuimarisha ukamuaji wa kibofu cha mkojo kwa kupunguza idadi ya misuli hiyo.
Tiba Kwa Kutumia Dawa
Ingawa hakuna dawa iliyoonyesha kuondoa kabisa tatizo la kukojoa kitandani kwa watu wazima, baadhi zimeoyesha kupunguza tatizo. Dawa hizi zikitumiwa pamoja na njia za kubadili tabia zinaleta matokeo mazuri zaidi.
. Desmopressin. Kwa kufanya kazi ya ADH au vasopressin, figo zitatengeneza mkojo kidogo.
. Imipramine. Ina mafanikio kwa asilimi 40 lakini ina muda wa kuwa na mafanikio kabla ya kugeuka kuwa sumu.
. Anticholinergic Medications. Dawa hii inasaidia kutuliza utendaji wa kupitiliza wa detrusor, na kutoa mafanikio kwa silimia 5 hadi 40. Madhara tokanayo na dawa hii ni kukauka midomo, kizunguzungu, na kutoona vizuri.
. Darifenacin. Dawa hii hupunguza kujikamua kwa kibofu cha mkojo na kuondoa tatizo la kibofu cha mkojo kufanya kazi zaidi (overactive bladder).
. Oxybutynin. Hulegeza misuli ya detrusor ya kibofu cha mkojo.
. Tolterodine. Dawa hii hufanya kazi sawa na oxybutynin.
. Trospium Chloride. Dawa hii hufanya kazi kwa kukilegeza kibofu cha mkojo ili kisifanye kazi ya ziada.
. Solifenacin. Hii ni aina mpya ya dawa ya kulegeza misuli ya detrusor.
Katika ukurasa wetu mwingine tutalizungumzia tatizo la kukojoa kitandani kwa watoto wadogo. Usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali uliyo nayo.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.