Mtoto akiwa anakojoa kitandani bila kukusudia akiwa usingizini, tunasema ana tatizo la kukojoa kitandani au kitaalamu nocturnal enuresis au bedwetting kwa lugha ya kawaida. Watoto wengi hufikia uwezo wa kudhibiti kibofu cha mkojo wanapoofikia umri wa miaka 4 na asilimia 10 ya wa watoto wa umri wa kati miaka 6 hadi 7 bado wanakuwa na tatizo la kukojoa usiku kitandani. Kama mtoto bado hajaufikia uwezo wa kudhibiti kibofu cha mkojo akiwa usingizini akiwa na umri wa miaka zaidi ya 7, yafaa kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya. Tatizo la kukojoa kitandani linajitokeza zaidi kwa watoto wa kiume kuliko wa kike. Kukiwa na uvumilivu na kwa kutumia nyenzo bora za tiba, watoto wengi wataacha kukojoa kitandani.
Kuna aina mbili za nocturna enuresis, aina zote zikiwa na tiba zinazofanana.
. Primary nocturnal enuresis inawaelezea watoto ambao hawakuweza kupata uwezo wa kuacha kukojoa kitandani tangu walipoanza kufundishwa kujisaidia wenyewe (mara nyingi hawa ni watoto ambao huwa hawajikojolei mchana).
. Secondary nocturnal enuresis ni wale watoto walipata kuacha kukojoa kitandani angalau kwa miezi sita lakini baadaye wakarudia kukojoa tena. Mara nyingi hawa huathirika baada ya tukio fulani lililowapa msongo wa mawazo ( kwa mfano, kuzaa kichanga, wazazi kutengana, n.k.). Tabia mbaya za kula au matumizi ya madawa yanaweza kusababisha kukojoa usiku.
Jinsi Mfumo Wa Mkojo Unavyofanya Kazi
Mkojo ni mabaki ya maji kutoka ndani ya mwili. Mkojo hutengenezwa figo zinaposafisha damu yako. Mfumo wa mkojo inahusisha viungo vyote vya mwili wako vinavyotengeneza, vinavyotunza na vinavyotoa mkojo nje ya mwili.
Kwa kawaida, figo za mtu mzima huzalisha lita moja na nusu hadi lita mbili za mkojo kila siku, pungufu kwa watoto. Mkojo hutiririka kutoka kwenye figo hadi kwenye kibofu cha mkojo kupitia mirija miwili iitwayo ureters. Kibofu cha mkojo kina kazi ya kutunza na kuutoa mkojo. Msuli wa kwenye shingo ya kibofu cha mkojo hufunga ili kuutunza mkojo. Urethra ni mrija unaosafirisha mkojo kutoka kwenye kibofu cha cha mkojo na kuutoa nje ya mwili. Eneo hili hubaki limefungwa na misuli ya sphincter.
Ubongo hufanya kazi na kibofu cha mkojo ili kuamuru mkojo utolewe au la. Ukiwa tayari kuutoa mkojo, ubongo hutoa ishara kwa kibofu cha mkojo na misuli ya kibofu hicho hukaza. Tendo hilo husukuma nje mkojo kupitia urethra. Misuli ya sphincter hufunguka, na mkojo hutoka nje ya mwili.
Mwanzoni, mtoto mdogo hutoa mkojo bila mpangilio, mkojo ukijitokea wenyewe. Kadiri mtoto anavyokua, kuna vitu vinavyokua ili kumfanya mtoto aanze kudhibiti namna ya kuutoa mkojo:
. Kibofu cha mkojo hukua ili kiweze kutunza mkojo mwingi zaidi.
. Kwenye umri wa miaka 2 hadi 3, mtoto anaweza kudhibiti misuli ya sphincter na misuli ya pelvic floor (misuli ya kwenye uvungu kati ya kinene na sehemu ya haja kubwa). Mtoto akiibana misuli hii anaweza kuuzuia mkojo usitoke hadi akifika chooni.
. Ubongo hukomaa na umri na kumfanya mtoto aweze kuibana au kulegeza misuli hii muda wo wote. Hapa ndipo wanapokuwa wamehitimu “kutumia choo”.
Wanapofikia miaka 7, asilimia 90 ya watoto wanaweza kudhibiti vibofu vyao mchana na usiku. Endapo watahitaji kwenda chooni usiku, wataamka na kwenda.
Sababu Za Kukojoa Usiku
Uvivu au kuwa mkaidi si sababu ya mtoto kushindwa kudhibiti mkojo. Baina ya watoto wachache, tabia huweza kuwa sababu. Kwa hali yo yote, wazazi wanatakiwa kutoa ushirikiana na msaada. Kukojoa kitnadani kunachangiwa na sababu nyingi.
Historia ya familia (genetics)
Kukojoa kitandani kunaweza kuwa ni urithi. Jeni ya kukojoa usiku inaweza na nguvu sana kwenye familia fulani. Nusu ya watoto wenye tatizo hili wana mzazi mmoja ambaye alisumbuka na tatizo hili. Asilimia hii hupanda hadi 75 endapo wazazi wote wawili walikuwa na tatizo hili. Ndugu wa karibu (mashangazi, wajomba na babu na bibi) wanaweza pia kuambukiza tatizo hili, ingawa hutajua. Mtoto ambaye hana ndugu wenye wenye tatizo ana asilimia 15 tu ya kuweza kuathirika.
Ukuaji wa taratibu wa udhibiti wa ubongo wa kibofu cha mkojo
Watoto wanaokojoa kitandani huitwa “deep sleepers” yaani wanalala fofofo. Usingizi mzito unaathiri namna kibofu cha mkojo kinavyowasiliana na ubongo. Baada ya kuamka na kwenda kukojoa chooni, misuli ya pelvic ya mtoto inajilegeza na kuachia mkojo wakati mtoto amelala. Udhibiti wa ubongo wa kibofu cha mkoja utakua wenyewe taratibu, unaweza kuchochewa kwa tiba.
Kibofu cha mkojo kidogo
Watoto wwengine wenye tatizo la kukojoa kitandani wana vibofu vya mkojo vidogo ambavyo haviweza kutunza mkojo wote. Hali hiyi husababisha watoto kushindwa kumaliza usiku bila kukojoa kitandani.
Kutengeneza mkojo mwingi wakati wa usiku
Figo za mwanao zinaweza kuwa zinatengeneza mkojo mwingi mno wakati wa usiku, na kibofu cha mkojo hakiweza kuhimili kuutunza wote. Kwa kawaida, ubongo hutengeneza homoni iitwayo “antidiuretic hormone (ADH)” ambayo hupunguza kasi ya utengenezwaji wa mkojo. Homoni hii husaidia kutengeneza mkojo kidogo usiku. Endapo ubongo unatengeneza ADH kwa kiwango kidogo au figo zikipoteza usikivu wa homoni hii, mkojo hutengenezwa kwa wingi. Itabidi sasa mtoto au aamke mara kadhaa usiku au akojoe kitandani. Vinywaji vyenye caffeine na vyenye gesi ya kaboni huweza kusababisha figo zizalishe mkojo mwingi zaidi.
Kisukari (Type 1 diabetes) husababishwa na ukosefu wa homoni ya insulin. Homoni hii husaidia kuweka sawa kiwango cha sukari mwilini. Mgonjwa wa kisukari asipotibiwa, sukari hupotea ndani ya mkojo. Hii husababisha upotevu mkubwa wa maji. Baadhi ya watoto hukojoa kitandani ikiwa ni ishara ya kuanza kwa ugonjwa huu.
Matatizo ya usingizi
Baadhi ya watoto wana matatizo ya usngizi kama kutembea wakiwa usingizini (sleep walking) au kupata vipindi vya kusimama upumuaji (obstructive sleep apnea – OSA). Mtoto mwenye OSA, hukosa oksijeni ya kutosha na kusababisha moyo kutengeneza “atrial natriuretic peptide (ANP) ambayo husababisha figo kutengeneza mkojo wa ziada usiku.
Kukosa Choo – constipation
Rektamu ipo nyuma ya kibofu cha mkojo. Kufunga choo kunasababisha kujaa ndani ya rektamu na kukisukuma kibofu cha mkojo. Hali hii hupunguza uweza wa kibofu kuhifadhi mkojo, na kusababisha kuvuja.
Msongo wa mawazo
Namna yo yote ya msongo wa mawazo inaweza kusababisha kukojoa kitandani. Kama kukojoa kiatndani kwenyewe kunaleta msongo wa mawazo kwa mtoto wako au familia yako, hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Watoto wanaokojoa kiatndani mara nyingi wanaogopa kujulikana na kuchekwa na marafiki zao. Kihisia, mtoto anaweza kujisikia vibaya na kuwa na wasiwasi. Watoto wenye matatizo ya kusoma au wasio na utulivu mara nyingi huwa na msongo wa mawazo. Kwa kawaida watoto hawa hukojoa usiku kitandani. Kuwa makini na vitu vinavyoweza kusababisha msongo wa mawazo na kusababisha kukojoa kitandani, kama:
. Kaka au dada mwingine
. Kulala peke yake
. Kuanza shule mpya
. Ugomvi ndani ya familia
. Ajali au maumivu.
Tiba Kwa Tatizo La Kukojoa Kitandani
Kuna tiba nyingi kwa tatizo la kukojoa kitandani, baadhi ni nzuri kuliko nyingine. Kwa kawaida, tiba huanza na mabadiliko madogo kama:
. Kupunguza kiasi cha maji anachokunywa mtoto saa moja hadi mbili kabla ya kulala
. Kutengeneza ratiba ya kwenda chooni
. Kutumia wetting alarms
. kutumia dawa
Mikakati inaweza kutumiwa mmoja baada ya mwingine au yote kwa pamoja.
Kupunguza kiasi cha maji anachokunywa mtoto saa moja hadi mbili kabla ya kulala
Anza kwa kumfundisha mtoto kunywa maji glasi moja au zaidi asubuhi au wakati wa chakula cha mchana. Halafu jioni, mtoto anywe amji kidogo tu ya kutuliza kiu. Jaribu kumzuia kunywa maji saa moja au mbili kabla ya kulala. Vile vile, mzuie mtoto kunywa vinywaji vyenye caffeine au vyenye kaboni kama soda.
Kutengeneza ratiba ya kwenda chooni (kubadili tabia ya kwenda chooni)
Kukizoesha kibofu cha mkojo ni kuandaa ratiba ya kwenda chooni na mtoto wako. Kwa mfano, hakikisha mtoto wako anakwenda na kukaa chooni mara 5 kwa siku na kabla ya kulala, hata kama hana haja ndogo.
Kutumia wetting alarms (enuresis alarms)
Bedwetting alarms zina sensa maalumu inayotambua umyevu kwenye pajama ya mtoto. Zitafanya kengele ilie kama kuna unyevu. Mtoto ataamka kwa kuisikia kelele za alarm na kuamka kwenda chooni kabla hajajikojolea. Mtu mzima atalazimika kutoa msaada kwani watoto wanaokojoa vitandani hulala usingizi mzito sana na hawataweza mwanzoni kuamka wenyewe. Alarm hii inafanya kazi ya kumzoesha mtoto kuamka ukifika muda wake wa kukojoa. Aina hii ya tiba kwa kujenga tabia imeonyesha kuleta mafanikio makubwa.
Mafanikio ya tiba hii ya alarm yanategemea sana uelewa wa mzazi kwamba ni wakati wa kujifunza tabia. Kuna hatia za mtoto na mzazi za kuzipitia ili kupata matokeo bora. Bila ustahimilivu, kuchoshwa kwa mzazi na mtoto kunaweza kuwafanya waache. Tafadhali jaribu kutokata tamaa.
Katika hatua ya kwanza na ya pili ya tiba, wazazi lazima waamke baada ya alarm na kwenda kumwamsha mtoto. Mtoto anaamka, anaenda chooni, anajaribu kukojoa kwa dakika kadhaa. Wanajasafisha, na wanabadilisha mashuka au nguo. Wazazi wanatakiwa kutoa msaada. Kisha mtoto anategesha upya alarm na kuingia kitandani. Kwenye hatua ya tatu ya tiba, mtoto anatakiwa aweze kuamka mwenyewe kibofu cha mkojo kikijaa. Mtoto akiweza kuifikia hatuia hii, wazazi wanatakiwa wamhimize mtoto kuendelea kutumia alarm kwa wiki mbili au tatu zaidi ili kuikazia tabia.
Dondoo kufikia mafanikio:
. Chagua nmiezi 3 hadi 4 mwafaka kwa kulifanya zoezi hili mtoto akiwa nyumbani.
. Mkubaliane na mtoto tarehe ya kulianza zoezi.
. Fanya mazoezi machache mchana mkiitumia alarm wakati wa mchana ili mtoto atambue ni nini akitegemee na nini atakifanya.
. Weka kalenda ndani ya chumba cha mtoto ili ufuatilie maendeleo yake
. Usimwadhibu mtoto akikosea. Adhabu hupunguza maendeleao. Badala yake, toa zawadi kwa ushirikiano wake katika tiba na kukamilisha zoezi.
Tiba ya Tatizo La Kukojoa Kitandani Kwa Kutumia Dawa
Desmopressin acetate (DDAVP)
Desmopressin inatengenezwa kwa kutumia homoni iitwayo “vasopressin”.
Katika hali ya kawaida, vasopressin hutengenezwa na figo wakati mwili ukijaribu kutunza maji. Kwa mfano, wanariadha hutoa homoni hii zaidi wakati wakiwa kwenye mbio na wanatoka jasho jingi. Watu wengi wana viwango vikubwa vya vasopressin ndani ya miili yao wakati wa usiku. Hii ni sehemu ya sababu inayotufanya tuweze kwenda muda mrefu usiku bila kwenda chooni. Ndani ya miili ya watoto wengi wanaokojoa usiku, mwongezeko huu wa homoni usiku hautokei. DDAVP hupatikana kama kidonge. Kinaweza kutolewa saa moja kabla ya kulala kwa kipindi cha miezi 3 hadi 6, kukiwa na kupumzika kwa wiki moja katikati. Kwa sababu hufanya kazi kwa kupunguza kiwango cha mkojo kinachotengenezwa, kinatumika pamoja na ratiba ya kupunguza unywaji wa maji.
Pamoja na kuwa kina utendaji mzuri na kina bei nzuri, kidonge hiki kimeonyesha kufanya kazi vizuri kwa nusu ya idadi ya watoto wanaokitumia na miili ya watoto inaweza kukizoea baada ya muda na kisifanye kazi tena.
Oxybutynin na Tolterodine
Dawa hizi zinamsaidia mtoto ambaye ana kibofu cha mkojo chenye ujazo mdogo, kwa kuongeza ujazo wa kibofu hicho. Ni dawa ambazo zinaweza kutumika pamoja na desmopressin ili kufanya kazi vizuri zaidi. Ni dawa salama zinazoweza kuvumiliwa na watoto. Lakini hazifanyi vizuri kwa watoto wote na zinaweza kusababisha kukauka midomo, kufunga choo na vipele usoni. Na kama kukitokea kufunga choo, tatizo la kukojoa kitandani linaweza kuwa kubwa zaidi.
Imipramine
Imipramine ni anti-depressant ambayo imetumika kwa miak mingi kutibu watoto wanaokojoa kitandani. Haimaanishi kuwa mfadhaiko ni chanzo cha kukojoa kitandani. Haijafahamika kwa nini dawa hii imesaidia tatizo hili, lakini inaaminika kuwa pengine ni kwa sababu dawa hii inaboresha tabia ya ulalaji wa mtoto na ujazo wa kibofu cha mkojo. Dawa hii inaweza kumfanya mtoto kuwa na hasira, kukosa usingizi, mwenye kusinziasinzia, kukosa hamu ya kula, na mabadiliko ya kitabia. Kuzidisha dozi kunaweza kulata maafa. Dawa hii inatakiwa kutumiwa na kutunzwa kwa uangalifu.
Katika mada nyinge tutalitazama tatizo la kukojoa kitandani kwa watu wazimana hatua za kuweza kuchukua. Usisite kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada hii au kuuliza maswali uliyo nayo.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651. (Usitume SMS).
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.