Leo tutazungumzia tatizo linalowapata watu wengi sana pale umri wao unapokuwa umezidi miaka 50 na hasa wale wenye miili mikubwa. Nina uhakika kuwa umewaona akina mama wenye umri mkubwa na miili mikubwa wanavyopata shida kutembea huku wakiinama toka upande mmoja hadi mwingine kila wakipiga hatua au shida wanayopata pale inapowabidi kupanda ngazi au kukuchuchumaa. Maneno kama “ugonjwa wa kuumwa joints, nina tatizo la joints, maumivu ya joints” na maumivu ya mifupa umeyasikia mara nyingi. Tatizo hasa hapa ni nini? Ungana nami katika mada hii uujue ugonjwa huu wa arthritis.
Ugonjwa Wa Arthritis Ni Nini?
Arthritis ni ugonjwa unaotokana na namna yo yote ya hitilafu katika maungio ya mifupa ya binadamu ambao husababisha maumivu na pengine kuvimba katika sehemu moja au zaidi ya maungio hayo. Neno arthritis halilengi ugonjwa mmoja bali jamii ya magonjwa ambayo kwa ujumla yapo zaidi ya 100. Tabia kuu ya magonjwa haya ni maumivu kwenye maungio ya mifupa (joints) ambayo ni endelevu na ambayo hutokea eneo hilo moja.
Chanzo Cha Arthritis Ni Nini?
Kusudi kuelewa chanzo cha ugonjwa huu, hebu kwanza tutazame muundo wa joint au sehemu mifupa miwili inapokutana. Fikiria goti ambapo mifupa miwili mmoja wa paja na mwingine wa mguu vinapokutana:
Ligaments: Ndicho kitu kinachoshikilia mifupa hii miwili pamoja. Hii ni kama utepe wa plastiki au mpira unaonyumbuka uliozunguka eneo hilo kwa nje, ukikunja goti inanyumbuka na ukinyoosha mguu inarudi.
Cartilage: Huu ni utando unafunika eneo ambalo mifupa hugusana ili kuzuia mifupa hii isisuguane moja kwa moja. Utando huu ambao kwa kiswahili tunauita gegedu huyawezesha maungio hayo kufanya kazi kiulaini pasipo kusababisha maumivu.
Capsule: Hiki ni kitu kinachofunika maungio haya kikizunguka pande zote. Ndani ya mfuko huu wa capsule kuna ukano (synovial fluid) ambao huzalishwa na synovial membrane. Ukano ni ute wa kulainisha sehemu hiyo ya maungio na synovial membrane ni utando ulio kwenye kuta za ndani za capsule.
Ugonjwa wa arthritis unasababishwa na hitilafu yo yote katika sehemu hizo za maungio ya mifupa. Inaweza kuwa gegedu inalika, upungufu wa ukano (synovial fluid), maambukizi ya vijidudu katika moja ya maeneo hayo au mchanganyiko wa matatizo.
Aina Za Ugonjwa Wa Joints-Arthritis
Kama nilivyoeleza hapo juu, kuna aina zaidi ya 100 za ugonjwa huu wa joints au arthritis. Katika mada yetu ya leo tutatazama aina kama nne hivi za ugonjwa huu, tukielezea chanzo cha kila aina.
Osteoarthritis: Hii ni aina ya arthritis inayosumbua watu wengi zaidi kuliko aina nyingine zote. Ugonjwa huu huwapata zaidi watu wenye umri mkubwa. Osteoarthritis hutokea pale cartilage inapopoteza uwezo wake wa kubonyea na kuwa ngumu hivyo kuharibika haraka. Cartilage ni kiungo cha kuhimili migandamizo ya ghafla (shock absorber). Cartilage hii inapopoteza ubora wake, tendons na ligaments huvutika na kusababisha maumivu. Hali ya uharibifu huu wa cartilage ikiendelea, mwishowe mifupa huanza kusuguana moja kwa moja na ndipo mgonjwa atakapoanza kupata maumivu makali sana.
Athari za ugonjwa huanza taratibu na kuongezeka na muda. Kutaanza kutokea maumivu kwenye joint baada ya kufanya shuguli fulani au baada ya mapumziko ya muda mrefu. Joints zitakaza, hasa mapema asubuhi unapotaka kuanza shughuli zako za kawaida. Siku zinavyosogea ndivyo utakavyoona ni vigumu zaidi kukitumia kiungo chako. Mara nyingine utaona uvimbe kwenye joint. Osteoarthritis hushambulia zaidi nyonga, mikono, magoti na uti wa mgongo.
Rheumatoid arthritis: Ugonjwa huu hutokea pale mfumo wa kinga ya mwili kwa bahati mbaya kuanza kushambulia viungo vya mwili ikiwa ni pamoja na synovial membrane (synovium) na kusababisha uvimbe na maumivu. Hali hii isipodhibitiwa, huweza kusababisha ulemavu. Ugonjwa huu unaweza pia kushambulia macho, ngozi, mapafu, midomo, damu na mishipa ya damu. Huu ni ugonjwa ambao zaidi ni wa wanawake na huwatokea zaidi wawapo kati ya umri wa miaka 40 hadi 60. Mgonjwa atasikia maumivu na kuona uvimbe kwenye joints za pande zote za mwili, yaani kama ni magoti, yote mawili la kulia na la kushoto, yote yatashambuliwa. Viungo vinavyoshambuliwa zaidi ni vidole, viwiko vya mikono na miguu.
Athari zake huonekana zaidi asubuhi unapoamka na maumivu yanaweza kudumu kwa muda wa hadi nusu saa. Muathirika wa ugonjwa huu hujisikia mchovu muda wote, hukosa hamu ya kula na hupungua uzito.
Ugonjwa katika hatua zake za baadaye huleta matatizo katika viungo vyote vya mwili. Matatizo yanayoweza kujitokeza ugonjwa ukikua ni kama yafuatayo:
– Macho. Ukavu, maumivu, wekundu, kutopenda mwanga na kutoona vizuri
– Midomo. Ukavu, maumivu na maambukizi ya fizi
– Ngozi. Vijinundu chini ya ngozi kwenye maeneo yenye mifupa
– Mapafu. Kushindwa kupumua vizuri
– Mishipa Ya Damu. Uharibifu wa mishipa ya damu
– Damu. Upungufu wa chembechembe nyekundu za damu
Infectious arthritis (septic arthritic): Aina hii ya arthritis inatokana na maambukizi ya bacteria kwenye synovial fluid. Maambukizi haya yanaweza kuwa pia ni ya fungus au virusi. Wadudu kutoka sehemu nyingine ya mwili iliyo karibu na maungio ya mifupa huweza kusambaa kupitia mfumo wa damu hadi kwenye joint na kuleta maambukizi. Mara nyingi mtu mwenye aina nyingine ya arthritis ndiye anayepata maambukizi ya namna hii. Mgonjwa ataanza kwanza kupata homa, maumivu na uvimbe kwenye joint. Maeneo ambayo hushambuliwa zaidi na aina hii ya arthritis ni goti, mabega, kiwiko cha mkono, kiganja (wrist) na vidole na mara nyingi ni eneo moja tu ndilo litakaloshambuliwa.
Juvenile rheumatoid arthritis (JRA): Juvenile rheumatoid arthritis (JRA) ni ugonjwa ambao huwapata zaidi vijana walio na umri ulio chini ya miaka 16 na unakuja kwa namna nyingi. Kuna aina kuu tatu za ugonjwa huu:
1. Pauciarticular JRA, huu ndiyo unaoonekana zaidi na hauna madhara makubwa ukilinganisha na aina nyingine. Mtoto atasikia maumivu kwenye joints zinazofikia nne.
2. Polyarticular JRA, huu hushambulia joints nyingi zaidi, zaidi ya nne na maumivu yake ni makali zaidi. Kadri siku zinavyoongezeka, ndivyo maumivu yatakavyozidi.
3. Systemic JRA, huu huonekana kwa nadra ambapo maumivu hujitokeza kwenye maeneo mengi na madhara yake kuwa makubwa zaidi.
Mtoto ataanza kusikia homa za vipindi ambapo huzidi zaidi nyakati za jioni. Hali hii inaweza kumtokea mtoto kwa muda mfupi au kwa wengine kwa muda mrefu sana . Mtoto atapata mauvimu kwenye maungio ya mifupa (joints), uvimbe kwenye maungio hayo na kukakamaa kwa viungo. Mtoto huyu atakosa hamu ya kula hivyo kumfanya akonde. Ugonjwa ukizidi, mtoto anaweza kudumaa (kushindwa kukua), ukuaji wa mifupa yake kuathirika na kupata matatizo ya macho (uveitis).
Kwa sababu ya urefu wa mada hii, leo tutaishia hapa na katika muendelezo wake katika ukurasa nyingine tutaujadili ugonjwa wa gout na Tiba Za Magonjwa Ya Joints. Tunaomba maoni yako kuhusu mada hii na usisite vilevile kuuliza maswali uliyo nayo. Tutafurahi sana kupata mchango wako au kuona tumekujibu vizuri maswali yako.
Katika mada nyingine, tutaelezea kifurushi cha kampuni ya Green World ambacho kinafanya vizuri katika kutibu matatizo haya ya maungio ya mifupa.
Unasumbuliwa na ugonjwa huu wa Arthritis?
Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au tutumie barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.