Matatizo Ya Macho Yatokanayo Na Kisukari: Diabetic Retinopathy

Watu wenye tatizo la kuwa na sukari nyingi ndani ya damu zao wanaweza kuwa na ugonjwa uitwao diabetic retinopathy. Huu ni ugonjwa unaotokea wakati viwango vya juu vya sukari katika damu
vinapoleta uharibifu kwenye mishipa ya damu iliyo kwenye eneo la retina. Mishipa ya damu ya  eneo hili inaweza kuvimba au kuvuja. Au inaweza kuziba, na kuzuia damu isipite. Wakati mwingine, mishipa mipya isiyo ya kawaida inaweza kuota kwenye retina. Haya yote yanapotokea, yanaweza kuharibu uonaji wako.

Hatua Mbili Za Ugonjwa Wa Macho Wa Kisukari

Kuna hatua kuu mbili za ugonjwa huu wa macho unaotokana na kisukari.

NPDR (non-proliferative diabetic retinopathy)

Hii ni hatua ya awali ya ugonjwa wa macho unaotokana na kisukari. Watu wengi wenye kisukari wapo
kwenye hatua hii.

Kwenye hatua hii, vijishipa vidogo vya damu huvujisha damu, na kuifanya retina kuvimba. Macula
ikivimba, hali hii huitwa macula edema. Hii ndiyo sababu kuu ya watu wenye kisukari kupoteza
uonaji.

Vile vile, kwenye hatua ya NPDR, mishipa midogo ya damu ya kwenye retina inaweza kuziba. Hii huitwa
macula ischemia. Hii ikitokea, damu haifiki kwenye macula. Wakati mwingine, chembechembe ndogo ziitwazo exudates hutokea kwenye retina. Hizi zinaweza vile vile kuathiri uonaji wako.

Ukiwa na NPDR uonaji wako unakuwa ni wa ukungu.

PDR (proliferative diabetic retinopathy)

Hii ni hatua ya mbele zaidi ya ugonjwa wa macho wa kisukari. Hii inatokea wakati retina inapoanza kuotesha mishipa mipya ya damu. Hali hii huitwa neovascularization. Vijishipa hivi dhaifu huvujisha damu ndani ya vitreous. Vikivujisha kiasi kidogo, unaweza kuona vitu vichache vyeusi vinavyoelea (floaters).

Vikivujisha kwa kiwango kikubwa, unaweza usione kabisa.

Mishipa hii mipya inaweza kutengeneza makovu. Makovu huweza kuleta matatizo kwenye macula au kusababisha kubanduka kwa retina (detached retina).

PDR ni mbaya, na inaweza kuharibu uonaji wa mbele na pembeni (central and peripheral vision).

Nini Hutokea Ukiwa Na Diabetic Retinopathy?

Unaweza ukawa na diabetic retinopathy na usijue. Hii ni kwa sababu ugonjwa huu hauna dalili katika hatua
zake za awali. Hali ikizidi kuwa mbaya, dalili zifuatazo unaweza kuziona:

. Kuongezeka kwa idadi ya floaters
. Kuona kwa ukungu
. Mabadiliko katika kuona, mara ukungu mara wazi kabisa.
. Kuona uwazi au maeneo meusi katika eneo unaloliona
. Kuona kwa shida gizani
. Kuona rangi zimepauka
. Kupoteza nguvu ya kuona

Dalili hizi za diabetic retinopathy mara nyingi huathiri macho yote mawili.

Diabetic Retinopathy Hutibiwaje?

Tiba ya diabetic retinopathy hutegemea daktari wako wa macho alivyoliona tatizo lako. Baadhi ya
tiba ni kama:

Uangalizi

Kuidhibiti sukari na pressure yako vinaweza kunusuru uonaji wako. Zingatia kwa makini mpango wa
chakula ulioshauriwa. Tumia dawa za sukari ulizopewa. Wakati mwingine, udhibiti wa sukari unaweza
kukurudishia kiasi fulani cha uonaji wako. Udhibiti wa pressure ya mwili wako utalinda afya ya mishipa ya
damu ya macho yako.

Dawa

Aina moja ya dawa inaitwa anti-VEGF medication. Hii inajumuisha Avastin, Eylea, na Lucentis.  Anti-VEGF
medication husaidia kupunguza uvimbe kwenye macula, kupunguza kasi ya uharibifu wa uonaji na

pengine kuboresha uonaji. Dawa hii hutolewa kama sindano kwenye jicho. Dawa ya steroid ni aina nyingine inayoweza kupunguza uvimbe kwenye macula. Hii vile vile hutolewa kama sindano kwenye jicho

Laser Surgery

Upasuaji wa laser unaweza kutumika ili kuziba mishipa ya damu inayovuja. Hii inaweza kupunguza kuvimba kwa retina. Laser surgery inaweza vile vile kusaidia kunywea kwa mishipa ya damu na kuzuia isikue tena. Mara nyingine tiba hii hufanyika zaidi ya mara moja.

Vitrectomy

Kama una PDR ya juu, daktari wako wa macho anaweza kukushauri upasuaji wa vitrectomy. Daktari ataondoa vitreous gel na damu kutoka kwenye mishipa inayovuja nyuma ya jicho lako. Hii itasaidia mionzi

kutua sehemu sahihi juu ya retina. Makovu yanaweza pia kuondolewa kwenye retina.

Katika mada yetu nyingine, tutalizungumzia tatizo la kutoona vizuri usiku. Usisite kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo. Tutafurahi kukujibu maswali uliyo nayo.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu NDANI YA MUDA WA KAZI kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.