Mawe Katika Figo (Kidney Stones). Nini Chanzo Cha Mawe Ndani Ya Figo?

 

mawe kwenye figo

Mawe katika figo (kidney stones) au kwa lugha ya kitaalamu, renal lithiasis au nephrolithiasis ni vitu vigumu kama mawe vinavyojengwa na madini na chumvi ndani ya figo zako. Mawe haya yanaweza kusababishwa na vyanzo tofauti na yanaweza kuathiri sehemu yo yote ya mkondo wako wa mkojo – kuanzia ndani ya figo hadi kwenye kibofu cha mkojo. Mara nyingi mawe hujijenga pale mkojo unapokuwa mzito na kuruhusu madini kuganda na kushikamana.

kidney stones sehemu athirika

Utokaji wa mawe haya nje ya njia ya mkojo unaweza kuleta maumivu makali, lakini mawe haya yanaweza yasilete madhara endapo yatagundulika mapema. Mara nyingi utatakiwa kutumia dawa za maumivu na kunywa maji mengi ili kuruhusu mawe haya kuondoka. Endapo mawe haya yatakwama na kusababisha maambukizo kwenye njia ya mkojo, upasuaji unaweza kuhitajika.

Dalili Za Kuwa Na Mawe Ndani Ya Figo

Mawe ndani ya figo yanaweza yasitoe dalili zo zote hadi pale yatakapoanza kutembea ndani ya figo au kuteremka kwenye mirija inayounganisha figo na kibofu cha mkojo (ureters). Jiwe likikwama ndani ya ureter, linaweza kuziba mtiririko wa mkojo na kusababisha figo kuvimba, na kuleta maumivu makali. Ndipo utakapoanza kuona baadhi ya dalili kama zifuatazo:

. Maumivu makali mgongoni chini ya mbavu
. Maumivu yanayoenea eneo la chini ya tumbo na kinena
. Maumivu yanayokuja kwa muda na machungu yanayobadilikabadilika
. Maumivu wakati wa haja ndogo
. Mkojo wa pinki, mwekundu au wa kahawia
. Mkojo wenye harufu mbaya
. Kichefuchefu na kutapika
. Kukojoa mara kwa mara
. Homa (kama kuna maambukizo)
. Mkojo kutoka kidogo

Maumivu yanayoletwa na mawe kwenye figo hubadilikabadilika – huhama kutoka sehemu moja hadi nyingine na kupungua na kuongezeka kadiri mawe yanavyotembea ndani ya mkondo wako wa mkojo.

Chanzo Cha Mawe Katika Figo

kidney stones njia ya mkojo

Mawe katika figo hayana sababu moja maalumu, ingawa kuna vipengele vinavyoweza kuongeza hatari ya kupatwa na tatizo hili.

Mawe katika figo hujitengeneza pale mkojo unapokuwa na vitu vingi zaidi vinavyosababisha kujijenga kwa chembechembe – vitu kama calcium, oxalate na uric acid – kuliko mkojo unavyoweza kuviyeyusha. Vile vile, inaweza kuwa mkojo wako unakosa vitu vya kuzuia chembechembe zisinatane, na hivyo kuweka mazingira mazuri ya mawe kutokea.

Aina Za Mawe Ya Kwenye Figo

Kujua aina ya mawe uliyo nayo husaidia kujua chanzo chake, na husaidia kubainisha hatua za kuchukua ili yasiongezeke. Kama umepata bahati ya kuona jiwe moja lililotoka, lihifadhi na mwonyeshe daktari ili likafanyiwe uchunguzi.

Mawe ya ndani ya figo ni ya aina nyingi, ambazo ni:

kidney stones mwonekano wake

. Calcium stones. Mawe mengi ya ndani ya figo ni ya aina hii, nayo zaidi ni ya muundo wa calcium oxalate. Oxalate ni kitu kinachopatikana ndani ya chakula, na kinachotengenezwa kila siku na maini. Baadhi ya matunda na mboga, mbegu na chocolate, vina oxalate kwa wingi.

Ulaji wa chakula, matumizi makubwa ya vitamini D na baadhi ya dosari katika shughuli za kimetaboliki vinaweza kuongeza kiwango cha calcium au oxalate katika mkojo.

Mawe ya calcium yanaweza kuwa na muundo wa calcium phosphate. Aina hii ya mawe hutokana zaidi na shughuli za kimetaboliki, kama renal tubular acidosis. Inaweza ikatokana na maumivu ya kichwa – kipandauso au kwa kutumia baadhi ya dawa kama topiramate (Topamax).

. Struvite stones. Mawe ya aina hii huwapata watu wenye maambukizo, kama maambukizo kwenye mkondo wa mkojo. Mawe haya huweza kukua kwa haraka na kuwa makubwa sana, mara nyingine bila dalili zo zote.

. Uric acid stones. Mawe ya uric acid yanaweza kuwatokea watu wasiokunywa maji kwa kiwango cha kutosha au wanaopoteza maji kwa wingi, wale wanaokula chakula chenye protini nyingi na wenye gout.

. Cystine stones. Mawe haya huwatokea watu wenye tatizo la kurithi ambapo figo zao hutoa aina fulani ya amino acid (cystinuria) kwa kiwango kilicho zaidi ya kawaida.

Mazingira Hatarishi Kwa Mawe Ya Kwenye Figo

Vipengele kadhaa huongeza hatari ya kupata mawe katika figo, navyo ni:

. Historia binafsi au ya familia. Kama kama mtu katika familia yenu ana mawe katika figo, uwezekano wa wewe kuyapata upo. Na kama ulishawahi kuwa na jiwe moja aua zaidi ndani ya figo zako, uko kwenye hatari ya kupata mawe mengine.

. Dehydration. Kutokunywa maji ya kutosha kila siku kunaongeza hatari ya kupata mawe kwenye figo. Watu wanaoshi kwenye mazingira ya joto na wale wanaotoa jasho jingi wapo kwenye hatari ya kupata mawe kwenye figo.

. Baadhi ya chakula. Kula chakula chenye uwingi wa protini, chumvi na sukari kunaongeza uwezekano wa kupata baadhi ya aina za mawe kwenye figo. Chumvi nyingi ndani ya chakula kunaongeza kiwango cha calcium kinachotakiwa kuchujwa na figo na kuongeza uwezekano wa kupata mawe katika figo.

. Unene. Kuwa na BMI (body mass index) kubwa, kiuno kipana na uzito mkubwa vimehusishwa na hatari ya mawe kwenye figo.

. Magonjwa ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na upasuaji. Gastric bypass surgery, magonjwa ya tumbo na kuharisha sugu vinaweza kubadili mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kuathiri ufyonzwaji wa calcium na maji, na kuongeza kiwango cha vitu vinavyojenga mawe katika mkojo.

. Magonjwa mengine. Magonjwa mengine yanayoweza kukuweka katika hatari ya kupata mawe kwenye figo ni renal tubula acidosis, cystinuria, hyperparathyroidism na maambukizi kwenye njia ya mkojo.

DAWA YA MAWE KATIKA FIGO

Katika mada nyingine tutauzungumzia ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo (meningitis). Usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali uliyo nayo kuhusu uandishi wa mada hii yetu ya leo.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.