Mara nyingi sana umesikia mtu akisema “nina stress”, mwingine akasema ana msongo wa mawazo na mara chache katika mazungumzo ukasikia mtu akitumia neno mfadhaiko. Haya ni maneno yanayoingiliana kimazungumzo mitaani na mara nyingi mtu hutumia neno moja katika hayo bila kujua tofauti zake. Katika mada yetu tutayachambua na kujua tofauti za matatizo yanayowasumbua watu hadi kupelekea kuyatumia maneno haya. Na mwisho tutatoa ushauri wa namna ya kuondokana na matatizo hayo.
Maana Ya Stress Au Msongo Wa Mawazo
Maisha ya dunia ya leo yamejaa pilikapilika za kila aina, una vitu vingi vya kuvifanya katika muda uliopangiwa (deadlines), vitu vingi vya kukukatisha tamaa na matakwa mengi ya binafsi na watu walio karibu na wewe. Mtindo huu wa kuishi umekuwa karibu ni wa kila mtu. Kila wakati unakuwa na msongo wa mawazo (Stress). Msongo wa mawazo kwa kiasi fulani siyo mbaya, unakusaidia kutekeleza majukumu yako ukiwa umebanwa na kukupa nguvu ya ziada ya kuyafanya vizuri kadiri ya uwezo wako. Lakini kama utaendelea kufanya shughuli zako kwa mtindo huu, wakati utafika ambapo ubongo wako utachoka na kupata tatizo la kiafya linaloitwa mfadhaiko (Depression).
Kwa hiyo msongo wa mawazo (Stress) ni namna ya kawaida ya mwili wako kukabiliana na mambo ya kukutisha au kukufanya uwaze.
Unapohisi hatari, ya kweli au siyo ya kweli, mwili hukupa nguvu haraka kukabilina na suala lililopo mbele yako, hii ni ni namna ya mwili wako kukulinda. Katika mazingira hayo, mwili hukufanya uwe mwangalifu zaidi na kukupa nguvu ya ghafla. Katika mazingira ya hatari, unaweza kuokoa maisha yako kwa kupata hiyo nguvu na ujasiri wa ghafla. Mfano mzuri ni pale unapoendesha gari na ghafla ukakanyaga breki za gari kuzuia ajali mbele yako.
Msongo wa mawazo hukusaidia kukabiliana na vikwazo mbalimbali. Utakuwa makini sana wakati unawasilisha mada mbele ya kadamnasi, utakuwa na umakini zaidi wakati unashiriki kwenye mechi na timu pinzani na utasukumwa kwenda kusoma ili ujiandae kwa mitihani yako badala ya kuangalia kipindi kizuri cha kwenye luninga unachokipenda.
Lakini kama tulivyodokeza hapo awali, kiwango cha msongo wa mawazo kikizidi, badala ya kukusaidia kitakuletea matatizo ya afya, kitaathiri utendaji wako wa kazi, kitavuruga mahusiano yako na wengine na kudunisha maendeleo yako ya maisha.
Visababishi Vya Msongo Wa mawazo
Kuna vitu vingi vya kimazingira au kimsukumo vinavyoweza kusababisha uwe na msongo wa mawazo, vitu hivi hutwa “stressors”. Nafikiri msomaji wangu unafikiri kuwa kila kitu kinachokuletea msongo wa mawazo (Stressor) ni kibaya, kama kubanwa sana na kazi au mahusiano mabaya ya kimapenzi. Stressor ni kitu cho chote kinachodai matumizi ya juu ya uwezo na nguvu zako za mwili. Inawezekana kuwa kikawa kitu kizuri tu, kama kuoa/kuolewa, kununua nyumba, kujiandaa kwenda chuoni au hata kupandishwa cheo kazini.
Msongo wa mawazo unaweza kutokana na fikra zako binafsi mbali na sababu hizo ambazo ni za nje ye mwili wako. Unaweza kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kukifikiria na kukiogopa kitu ambacho kinaweza kutokea au ambacho hakiwezi kutokea au tu ukawa na mawazo chanya kuhusu maisha.
Ni kitu gani kitakupa msongo wa mawazo na kipi hakitakusumbua inategemea sana na namna wewe mwenyewe binafsi utakavyokichukulia kitu kilicho mbele yako, kitu hicho hicho ambacho wewe kinakusumbua, kinaweza kuwa ni burudani kwa mtu mwingine. Kuendesha gari katika foleni toka Mbezi kuingia kazini kwako Posta kunaweza kuwa kero kubwa kwako, wakati kwa mwingine ni fursa yake ya kupata muziki mwororo asubuhi.
Vitu ambavyo vinasababisha msongo wa mawazo ni pamoj na:
- Mabadiliko ya maisha
- Kazi au shule
- Matatizo katika mahusiano
- Matatizo ya kifedha
- Kubanwa na shughuli nyingi
- Watoto na familia
- Wasiwasi wa muda mrefu
- Tabia ya kuona kila kitu ni kibaya
- Kupenda yasiyowezekana
- Kutaka kila kitu kiwe sahihi (kikae juu ya mstari) kila wakati
- Kutopenda kushauriwa au kubadilika kutokana na hali halisi
- Kujidharau mwenyewe kwenye mazungumzo
Msongo wa mawazo unaotokana na majibizano na rafiki yako, au ule unaotokana na msongamano wa magari au wa kuwa na ratiba ndefu na ngumu ya shughuli ni tofauti na msongo wa mawazo wa kuwa na majukumu mengi katika familia. Msongo wa mawazo unaokwenda kwa muda mrefu ni hatari kwa afya na huweza kuvuruga vitu vingi katika mwili wako ukaishia na magonjwa kama ya high blood pressure, upungufu wa kinga za mwili, kiharusi, ukosefu wa uwezo wa kuzaa au kuzalisha na kuzeeka haraka. Msongo wa mawazo wa muda mrefu huweza kusababisha mfadhaiko (Depression).
Dalili Za Kuwa Na Msongo Wa Mawazo
Dalili za kawaida za kuwa na msongo wa mawazo ni:
- Kupata usingizi kwa shida
- Kuona kuwa kila wakati umezidiwa na shughuli
- Kukosa kumbukumbu
- Kukosa uwezo wa kutuliza akili kwenye jambo moja
- Mabadiliko katika tabia yako ya kula
- Kuwa na wasiwasi
- Kusikia uchungu, hasira au kukata tamaa haraka
- Kuona kuwa huwezi kufanikisha mambo yako katika maisha
Wasiwasi (Anxiety)
Matatizo yanayowapelekea watu kwa wingi kuwaona wataalamu wa tiba ya akili ni msongo wa mawazo (Stress), mfadhaiko (Depression)na wasiwasi (Anxiety).
Wasiwasi (Anxiety) ni hali ya kuwa na hofu kuwa kuna jambo kubwa na baya litatokea juu yako. Wasiwasi unaweza kuwa wa kawaida tu au ukalenga sehemu fulani, kikundi fulani cha watu au kitu fulani.
Katika kurasa zinazofuata utapata maelezo ya namna ya kuondoa msongo wa mawazo na utasoma kuhusu tatizo la kuwa na mfadhaiko (Depression) na jinsi ya kuondoa mfadhaiko.
Tafadhali ndugu msomaji wetu, usisite kutoa maoni au kuuliza swali kuhusu hili somo letu la leo. Itakuwa furaha kubwa kwetu kukujibu.