Jee, ulishawahi kufikiria kutafuta dawa ya mikunyanzi ya ngozi ya juu ya mwili wako au kwa maneno mengine wrinkles ? Kwa walio wengi jibu ni ndiyo na sababu kubwa ikiwa ni kujaribu kupata mwonekano wa ujana zaidi. Katika mada nyingine, tuliona kuwa mtu huonekana mzee kutokana na vitu viwili. Kwanza ni namna anavyotenda vitendo vyake vya mwili, kwa mfano kutembea.
Tuliona kuwa mwili wa mtu unaongeza mahitaji ya madini ya calciumu kadiri umri unavyoongezeka na ukikosa madini hayo kutokana na chakula anachokula, mtu huyu hushindwa kukidhi mahitaji ya mwili na mwili hulazimika kupata mahitaji yake kutoka kwenye mifupa na hivyo kuifanya mifupa kuwa dhaifu. Sababu ya pili ya kuwa na mwonekano wa uzee ni kutokana na mikunyanzi ya juu ya ngozi ya mwili (wrinkles) na tulisema kuwa ukosefu wa collagen mwilini husababisha mikunyanzi hiyo. Katika mada ya leo, tutaijadili collagen na jinsi inavyofanya kazi ya kuondoa mikunyanzi au wrinkles kwenye ngozi.
Kuna njia nyingi zinazotumika kuondoa mikunyanzi ya ngozi ikiwa ni pamoja na creams na lotions. Njia nyingine ambayo hutumika ni kuondoa tabaka la juu la ngozi lililoathirika kwa kuikwangua au kwa kuiyeyeyusha kwa kutumia kemikali. Mara nyigine mionzi hutumika kuondoa mikunyanzi ya juu ya ngozi.
Kudungwa sindano za botox huondoa mikunyanzi inayotokana na kujikunja kwa ngozi kwa kuonyesha hisia kwenye maeneo ya macho na midomo. Katika mada yetu ya leo tutajadili jinsi ya kuondokana na mikunyanzi ya juu ya ngozi (wrinkles) kwa kutumia njia rahisi – collagen.
Kwanza tuone ni sababu zipi zinafanya ngozi ya mwili wako kuwa na mikunyanzi. Imebainika kuwa kuna sababu nyingi sana ambazo kwa pamoja huchangia hali hiyo, baadhi ya sababu hizo zinaweza kuzuilika na baadhi haziwezi kuzuilika kabisa.
Umri: Umri unapokuwa mkubwa ngozi yako hupunguza uwezo wake wa kunyumbuka na kuwa ngumu. Utengenezaji wa seli mpya hupungua na kufanya tabaka la chini ya ngozi (dermis) kupungua unene wake. Kupungua kwa utengenezaji wa mafuta hufanya ngozi yako ikauke. Mafuta yaliyo chini ya ngozi yako hupungua na kuifanya ngozi yako kulegea, kutengeneza vijibonde na kufanya mistari ionekane juu ya ngozi hiyo.
Mionzi ya jua ( ultraviolet (UV) light): Mionzi ya ultraviolet inayoongeza kasi ya kuzeeka ndicho chanzo kikubwa cha kuwa na mikunyanzi juu ya ngozi ya binadamu. Mionzi hiyo huvunjavunja vitu vya kuunganisha ngozi – collagen na elastin ambavyo huwa chini ya ngozi kwenye tabaka la dermis. Bila vitu hivi vya kuiunganisha na kuifanya kuwa imara, ngozi huanza kulegea na mikunyanzi kuanza kujitokeza. Uvaaji wa kofia kubwa na uvaaji wa nguo zinazofunika sehemu za mwili husaidia kutopata wrinkles haraka.
Uvutaji wa tumbaku: Kuvuta tumbaku kunapunguza kiwango cha damu kinachoifikia ngozi kwa kupunguza kipenyo cha mishipa ya damu inayoelekea kwenye matabaka ya juu ya ngozi . Kemikali zilizomo ndani ya tumbaku pia huharibu collagen na elastin.
Kujikunjakunja kwa mara kwa mara kwa ngozi wakati wa kuonyesha hisia: Mistari ya juu ya kope za macho na ile inayoanzia kwenye kona za macho inaaminika kujenga mistari kutokana na matendo ya kuonyesha hisia.
Matendo kama ya kutabasamu, kukunja sura kuonyesha hasira na kukonyeza yanachangia katika kuleta mikunyanzi ya ngozi.
Collagen Ni Nini?
Collagen ni protini ngumu, isiyoyeyuka na iliyoumbwa kama nyuzinyuzi. Protini hii inayotengenezwa na amino acids hufanya theluthi moja ya protini yote iliyomo ndani ya mwili. Kuna aina nyingi za collagen, kama aina 16 hivi. Collagen hizi za ndani ya mwili ni ngumu sana na aina nyingine za collagen ni ngumu kuliko hata chuma.
Collagen hupatikana zaidi kwenye ngozi na mifupa na hufanya kazi ya kuupa mwili uimara na nguvu ikiambatana na elastin. Kwenye tabaka la dermis, collagen hasaidia kujenga mtandao wa nyuzinyuzi unaosaidia seli mpya kukua juu yake. Kwa vile uzalishaji wa collagen mwilini hupungua na umri, ngozi hupoteza hali yake ya kunyumbuka na kuifanya ngozi kubonyea chini. Hivyo, mistari na mikunyanzi hujitokeza. Kupungua kwa collagen husababisha pia udhaifu wa cartilage kwenye maungio ya mifupa (joints). Collagen huzalishwa na seli mbalimbali lakini haswa na seli za kuunganisha viungo (connective tissue cells). Mwili wa binadamu huendelea kuzalisha collagen vizuri hadi umri wa mtu unapofikia miaka 40 hivi, baada ya hapo uzalishaji hupungua na kuwa kidogo sana umri unapofika miaka 60.
Collagen hutumika kuondoa mistari na mikunyanzi ya juu ya ngozi (kuondoa wrinkles) na pia husaidia kuondoa makovu juu ya ngozi, yale ambayo hayana ncha kali. Collagen inayotumika inatokana na binadamu na wanyama wa jamii ya ng’ombe.
Collagen ni protini ambayo, kama protini nyingine inatengenezwa na amino acids. Kuna amino acids 9 ambazo ni muhimu katika utengenezaji wa collagen na ambazo hupatikana kutokana na chakula tunachokula .
Chakula Gani Ni Chanzo Kizuri ha Collagen?
Chakula ambacho ni chanzo kzuri cha collagen ni pamoja na:
. Samaki
. Nyama ya kuku
. Sehemu nyeupe ya yai
. Matunda ya jamii ya sitriki (machungwa, malimau, ndimu, mabalungi n.k.)
. Berries (kama forosadi, fuu, kunazi)
. Mboga za majani nyekundu na za njano
. Vitunguu saumu
. Korosho
. Nyanya
. Pilipili
Katika mada nyingine inayofanana na hii, namna ya kuondoa uzee, tumejadili njia mbalimbali unazoweza kufanya ili kuondoa mwonekano wa uzee. Na kuna ukurasa pekee ambamo tumejadili Chakula cha Kuzuia Kuzeeka Haraka.
Tafadhali tunaomba mchango wako kuhusu mada hii. Unaweza kuuliza swali au kutoa maoni yako kwa kutumia njia yo yote katika hizi ambazo tumeziorodhesha hapa chini. Tutafurahi sana kukujibu.
Kwa maelezo zaidi na ya kina, tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au tutumie barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu ndani ya saa za kazi kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.