Nini Maana Ya Presha Ya Kushuka (Low Blood Pressure)?

 

Blood pressure ni nguvu ya mgandamizo juu ya kuta za mishipa ya damu inayotokana na damu inayozunguka mwilini. Blood pressure huchangia kwenye moja ya ishara kuu za uhai ambazo ni mapigo ya moyo, upumuaji na joto la mwili. Blood pressure (mgandamizo wa damu juu ya mishipa ya damu) hutokana na moyo kusukuma damu ndani ya ateri, ikirekebishwa na upokeaji wa ateri wa msukumo huo wa damu. Mada yetu ya leo itazungumzia presha ya kushuka (low blood pressure).

Presha ya kushuka (low blood pressure) au kwa kitaalamu, hypotension, ni neno linalotumika kuelezea hali ambapo mgandamizo wa damu kwenye ateri ni chini ya kiwango cha kawaida (chini ya 90/60).

Kipimo cha pressure ya damu huwa na namba mbili. Namba ya kwanza na ambayo huwa ya juu huwa ni kipimo cha systolic pressure, yaani mgandamizo wa damu kwenye kuta za ateri wakati moyo unadunda na kuzijaza ateri na damu.  Kipimo cha pili ni cha diastolic pressure, yaani mgandamizo wa damu wakati moyo unapumzika kati ya misukumo miwili.

blood pressure chart

Kipimo kizuri cha pressure ni chini ya 120/80 (systolic/diastolic). Kipimo cha chini kikiwa kati ya 60 na 80mmHg na cha juu kati ya 90 na 120mmHg. Blood pressure juu ya 130/80 huhesabiwa kuwa ni juu. Blood pressure ya juu huongeza uwezekano wa:

. Kupata magonjwa ya moyo

. Kupata magonjwa ya figo

. Kukakamaa kwa ateri (atherosclerosis au arteriosclerosis)

. Kuharibika kwa macho

. Kiharusi (stroke)

Low blood pressure (hypotension) ni pressure ya chini mno hadi kusababisha dalili za low blood pressure kutokana na upungufu wa mtiririko wa damu kwenye ateri na veni. Inapotokea kuwa mtiririko wa damu ni mdogo sana na kushindwa kusambaza kiasi cha kutosha cha oksijeni na virutubishi kwenye viungo muhimu kama ubongo, moyo, na figo, viungo hivi havifanyi kazi yao ipasavyo na vinaweza kuharibika kwa muda au moja kwa moja.

low blood pressure function

Tofauti na high blood pressure, low blood pressure inatambulika kwa dalili zinazotokea na si kwa kipimo kinavyosoma. Watu wengine wanaweza kuwa na vipimo vya 90/50 kwa kipindi kirefu na wasiwe na dalili, kwa hiyo hawana tatizo la low blood pressure. Wakati huo huo, wengine wenye blood pressure ambayo huwa ya juu wanaweza kuonyesha dalili za low blood pressure endapo pressure yao itashuka hadi 100/60.

Ujauzito husababisha blood pressure kushuka. Blood pressure wakati wa ujauzito inaweza kuwa chini ya 100/60

Kwa mtu mwenye afya nzuri, pressure ya chini bila dalili zo zote huwa si tatizo na hakuna haja ya tiba. Lakini pressure ya chini inaweza kuwa ni ishara ya tatizo – na hasa kwa mtu wa umri mkubwa – hali ambayo inaweza kusababisha upungufu wa damu inayosukumwa kuelekea kwenye moyo, ubongo, na viungo vingine muhimu.

Hali sugu ya kuwa na pressure ya chini si tatizo. Lakini tatizo linaweza kujitokeza pale pressure inaposhuka ghafla na ubongo ukakosa damu kwa kiwango kinachotakiwa. Hii inaweza kuleta kizunguzungu au kuzimia. Kushuka ghafla kwa pressure kunaweza kutokea pale mtu anaponyanyuka ghafla kutoka hali ya kulala au kuketi. Aina hii ya pressure ya chini huitwa postural hypotension au orthostatic hypotension. Aina nyingine ya low blood pressure ni ile inayotokea pale mtu anaposimama kwa muda mrefu. Hii huitwa neurally mediated hypotension. Ikileta umauti huitwa vasovagal syncope.

Uwezekano wa kupata pressure ya chini na pressure ya juu huambatana na umri kwa sababu ya mabadiliko ya kawaida yanayoendana na umri. Kwa nyongeza, mtiririko wa damu kuelekea kwenye misuli ya moyo na ubongo hupungua umri unapokuwa mkubwa, hasa kwa sababu ya kujijenga kwa tabaka (plaque) za mafuta juu ya mishipa ya damu. Kwa wastani, asilimia 10 hadi 20 ya watu wa umri wa miaka zaidi ya 65 wana postural hypotension.

Blood Pressure Inafanya Kazi Namna Gani?

Wakati moyo unajilegeza (diastole), ventricle ya kushoto inajazwa na damu inayorudi kutoka kwenye mapafu. Ventricle ya kushoto kisha hujikamua na kusukuma damu ndani ya ateri (systole). Pressure ya damu ndani ya ateri wakati huu (systolic pressure) huwa juu kwa sababu damu inasukumwa kwenye ateri. Pressure huwa chini wakati ventricle hii ikijilegeza (diastolic pressure), kwani hakuna damu inayosukumwa ndani ya ateri. Mapigo ya moyo tunayoyasikia tukiweka vidole juu ya ateri husababishwa na kujikamua kwa ventricle ya kushoto na kusukumwa kwa damu.

Blood pressure huchangiwa na vitu viwili: 1) Uwingi wa damu iliyosukumwa na ventricle ya kushoto ya moyo ndani ya ateri 2) Ukinzani kwa mtiririko wa damu unaotolewa na ateri ndogo za damu (arterioles).

Kiujumla, pressure ya damu huwa juu kama damu nyingi zaidi inasukumwa ndani ya ateri au kama ateri ndogo za damu ni nyembamba na/au ngumu. Ateri ndogo nyembamba au ngumu  huzuia mtiririko wa damu, huongeza blood pressure. Ateri ndogo huwa nyembamba kama misuli inayozizunguka ikijikaza. Ateri ndogo huweza kuwa nyembamba na ngumu kwa watu wa umri mkubwa wakipata tatizo la atherosclerosis.

Blood pressure huwa chini kama kiasi cha damu kinachosukumwa ndani ya ateri ni kidogo au kama ateri ndogo ni kubwa zaidi na zilizolegea, na hivyo kutoa ukinzani mdogo kwa mtiririko wa damu.

Mwili una mfumo wa kurekebisha au kuacha blood pressure na mtiririko wa damu. Kuna vitambuzi vinavyochunguza blood pressure kwenye kuta za ateri na kupeleka ishara kwenye moyo, mishipa midogo ya damu (arterioles), veni, na figo ambavyo vitafanya mabadiliko ili kuipandisha au kuiteremsha blood presure. Blood pressure inarekebishwa kwa kurekebisha kiwango cha damu kinachosukumwa na moyo (cardic output) ndani ya ateri, kiwango cha damu ndani ya veni, ukinzani wa mishipa midogo ya damu, na ujazo wa damu.

Figo huweza kurekebisha pressure ya damu kwa kuongeza au kupunguza kiasi cha mkojo unaozalishwa. Kimsingi mkojo ni maji yanayotolewa nje ya damu. Figo zikizalisha mkojo kwa wingi, ujazo wa damu katika mishipa hupungua, na pressure ya damu hushuka. Na figo zikizalisha mkojo kidogo, kiwango cha damu kinachojaza ateri na veni huwa juu, na pressure ya damu huwa juu. Figo huleta mabadiliko ya pressure ya damu taratibu sana, baada ya saa au siku kadhaa.

Upungufu wa kiwango cha damu unaotokana na kutokwa na damu (kama kidonda cha tumbo au kidonda kikubwa kutokana na kujikata) kwa mfano, hushusha pressure ya damu. Mwili huchukua hatua zifuatazo kwa haraka ili kuongeza pressure ya damu:

. Moyo huongeza kasi ya mapigo yake na kusukuma damu nyingi zaidi.

. Veni hubana ili damu irudi kwa wingi kwenye moyo na kusukumwa tena.
. Mtiririko wa damu kuelekea kwenye figo hupungua ili kupunguza utengenezwaji wa mkojo.

. Mishipa midogo ya damu hubana ili kuongeza ukinzani kwenye mtiririko wa damu.

Mabadiliko haya hurudisha pressure ya damu kuwa kawaida isipokuwa kama damu inayopotea ni nyingi mno kiasi kwamba mabadiliko yanazidiwa.

Jee, Blood Pressure Ya Chini Ni Tatizo?

Watu wenye blood pressure ya chini wanakuwa hawana hatari ya kupatwa na kiharusi, magonjwa ya figo na moyo.

Wanariadha, watu wanaofanya mazoezi kila wakati, wenye uzito mdogo, na watu wasiovuta sigara huwa na pressure ya chini. Pressure ya chini ni nzuri ilimradi haiwi chini mno na kuleta matatizo katika mwili.

Dalili Za Pressure Ya Chini

Dalili za kawaida za low blood pressure ni:

. Kizunguzungu
. Kizimia
. Kutoona vizuri
. Kichefuchefu
. Uchovu
. Kushindwa kutuliza mawazo

 

dalili za low pressure

 

Dalili za low blood pressure kutokana na mazingira au magonjwa:

. Orthostatic hypotension: Kuinuka baada ya kuketi au kulala huleta low blood pressure kwa kusababisha damu kutuama kwenye veni za sehemu ya chini ya mwili.

. Magonjwa ya moyo: Maumivu ya kifua (dalili ya angina) au moyo kushindwa kuendelea kufanya kazi yanaweza kutokea kama hakutakuwa na damu ya kutosha kwenda kwenye ateri za coronary (ateri zinazopeleka damu kwenye moyo).

. Magonjwa ya figo: Kama damu inayopelekwa kwenye figo ni ndogo, figo zitashindwa kutoa uchafu nje ya mwili, kwa mfano, urea (BUN na creatinine).

. Shock ni hali inayoweza kuua na hutokea pressure ya chini ya kudumu inaposababisha viungo kama figo, maini, moyo, mapafu, na ubongo kushindwa kufanya kazi ghafla.

Ni Nini Chanzo Cha Presha Ya Kushuka?

Kukosa Maji Na Kutoka Damu

. Ukosefu wa maji (dehydration) ni hali inayowatokea wagonjwa wenye kichefuchefu, waliotapika, walioharisha kwa muda mrefu au watu wa mazoezi mazito, ambapo damu kutoka kwenye viungo vya mwili huelekezwa kwenda kwenye misuli. Kiasi kikubwa cha maji kinapotea wakati mtu anatapika au kuharisha.
Sababu nyingine za kupoteza maji ni mazoezi, kutoka jasho, na homa. Ukosefu wa maji kwa kiasi kidogo huleta kiu na kukauka kwa midomo. Ukosefu wa zaidi huleta orthostatic hypotension na kukosa maji kwa kiwango kikukbwa sana na kwa muda mrefu kunaweza kuleta shock, kufeli kwa figo, kuchanganyikiwa, uwingi wa asidi mwilini, coma na hata kifo.

. Kutoka damu kwa wingi kunapunguza damu ya mtu kwa kiasi kikubwa na kusababisha orthostatic hypotension.

Magonjwa ya moyo

. Msuli wa moyo kudhoofika kunaweza kusababisha moyo kufeli na kusukuma damu kwa kiwango kidogo. Sababu ya kawaida ya kudhoofu kwa msuli wa moyo na kufa kwa sehemu kubwa ya msuli wa moyo kunakotokana na heart attack moja kubwa au heart attacks ndogo ndogo nyingi. Hali nyingine zinazodhoofisha uwezo wa moyo wa kusukuma damu ni sumu za madawa kwenye moyo, moyo kushambuliwa na virusi (myocarditis), na ugonjwa wa valvu za moyo kama aortic stenosis ambao hupunguza uwezo wa moyo wa kusukuma damu kwenye ateri.

. Pericarditis ni uvimbe kwenye pericardium (mfuko unaouzunguka moyo). Pericarditis unaweza kusababisha majimaji kujaa kwenye pericardium na kuufinya moyo, hivyo kupunguza uwezo wa moyo wa kutanuka, kujaza na kusukuma damu.

. Pulmonary embolism ni hali ambapo donge la damu iliyoganda katika veni (deep vein thrombosis au DVT) linaondoka na kusafiri kuelekea kwenye moyo na hatimaye kwenye mapafu. Donge kubwa linaweza kuziba damu inayoelekea kwenye ventricle ya kushoto kutoka kwenye mapafu na kwa kiasi kikubwa kupunguza damu inayorudi kwenye moyo kwa ajili ya kusukumwa tena. Pulmonary embolism ni tatizo linaloweza kukatisha maisha ya mtu.

. Kasi ndogo ya mapigo ya moyo (bradycardia) inaweza kupunguza kiasi cha damu kinachosukumwa na moyo. Kasi ya mapigo ya moyo ya mtu mwenye afya wakati amepumzika ni kati ya mapigo 60 hadi 100 kwa dakika. Bradycardia (mapigo ya damu pungufu ya 60 kwa dakika) haileti pressure ya chini kila wakati. Kwa mfano, wanariadha waliofundishwa wanaweza kuwa na mapigo kati ya 40 hadi 50 kwa dakika bila ya kuwa na dalili zo zote. Kasi ndogo ya mapigo hurekebishwa na kujikamua kwa nguvu zaidi kwa moyo kunakosukuma damu zaidi. Lakini kwa wagonjwa wengi bradycardia huweza kushusha presha ya damu na kusababisha kizunguzungu, na hata kuzimia.

Baadhi ya sababu za bradycardia ni pamoja na:

1) Sick sinus syndrome: mfumo wa umeme wa moyo hautoi ishara za umeme kwa spidi inayotakiwa kuweka sawa kasi ya mapigo ya moyo

2) Heart block: tishu maalumu zinazosafirisha ishara za umeme katika moyo kuharibiwa na heart attacks, kudhoofishwa na atherosclerosis, na madawa. Heart block huzizuia baadhi au ishara zote za umeme kufikia baadhi ya maeneo ya moyo, hivyo kuufanya moyo kushindwa kujikamua ipaswavyo.

3) Drug toxity: madaya ya tiba ya presha ya juu huweza kupunguza kasi ya kusambaa kwa umeme katika moyo na kusababisha bradycardia na hypotension.

Aina Za Low Blood Pressure

Madaktari hugawa pressure ya chini ya damu katika makundi kulingana na vyanzo na vipengele vingine. Baadhi ya aina za low blood pressure ni pamoja na:

. Pressure Ya Chini Wakati Wa Kusimama (Postural au Orthostatic Hypotension). Hii ni kushuka ghafla kwa blood pressure wakati ukisimama au baada ya kuwa ulilala.

Usimamapo damu huvutwa chini kuelekea kwenye miguu.  Kwa kawaida, mwili hurekebisha kwa kuongeza mapigo ya damu na kubana vishipa vya damu na kuhakikisha damu ya kutosha inarudi kwenye ubongo.

Watu wenye orthostatic hypotension, urekebishaji huu haufanikiwi na pressure ya damu hushuka na kusababisha kizunguzungu, kutoona vizuri na hata kuzimia.

pressure ya chini wakati wa kusimama

Orthostatic hypotension huweza kutokea kwa sababu nyingine, ikiwa ni pamoja na upungufu wa maji, ujauzito, kisukari, matatizo ya moyo, kuungua sehemu za mwili, joto kali, veni kuwa kubwa (large varicose veins), na matatizo mengine ya neva.

Baadhi ya madawa husababisha orthostatic hypotension kama dawa za kutibu high blood pressure, na zile za kutibu parkison’s disease na jogoo kushindwa kuwika.

Tatizo huonekana zaidi kwa watu wa umri mkubwa ingawa huweza kutokea kwa vijana wadogo, watu wenye afya nzuri wanaweza kutokewa na hali hii pale ambapo wanasimama ghafla baada ya kuketi wakiwa wamepishanisha miguu au kuruka kichurachura kwa muda mrefu.

. Pressure Ya Chini Baada Ya Kula (Postprandial Hypotension). Kushuka huku kwa pressure baada ya kula mara nyingi huwashika wazee.

Damu hutiririka kuelekea kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula baada ya kupata lishe. Kwa kawaida, moyo huongeza kasi ya mapigo na vishipa vya damu hubana ili kuweka sawa pressure. Kwa baadhi ya watu, urekebishaji huu haufanyi vizuri na husababisha mtu kupata kizunguzungu, kuzimia au kuanguka.

Postprandial hypotension huwaathiri zaidi watu wenye high blood pressure au wenye ugonjwa wa Parkinson’s.

. Pressure Ya Chini Kutokana Na Dosari Za Ishara Za Ubongo (Neurally Mediated Hypotension). Tatizo hili linatokea baada ya mtu kusimama kwa muda mrefu, na kwa kawaida huwaathiri zaidi vijana na watoto wadogo. Inafikiriwa kuwa linatokana na mawasiliano mabaya kati ya moyo na ubongo.

. Bood Pressure Ya Chini Kutokana Na Dosari Za Mfumo Wa Neva (Multiple System Atrophy With Orthostatic Hypotension). Ugonjwa huu huitwa pia Shy-Drager syndrome. Tatizo hili linalowatokea watu wachache sana huendelea kuharibu mfumo wa neva (autonomic nervous system), ambao husimamia masuala ya blood pressure, mapigo ya moyo, upumuaji na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Huambatana na kuwa na pressure ya juu mtu akiwa amelala.

Tiba Ya Low Blood Pressure

Pressure isiyoleta dalili mbaya au yenye dalili ndogo ni mara chache sana itahitaji tiba.

Endapo umepata dalili, tiba itaendana na chanzo cha tatizo lako. Kwa mfano, kama pressure yako ya chini inatokana na matumizi ya madawa, tiba itakuwa kubadilishiwa au kuacha kuzitumia dawa hizo.

Kama chanzo cha pressure yako kuwa chini hakijawa bayana au kama tiba yake haipo, basi tiba italenga kupandisha pressure na kuondoa dalili zilizokwisha jitokeza. Kulingana na umri wako, afya yako na aina ya low blood pressure yako, unaweza kuyafanya yafuatayo:

. Ongeza matumizi ya chumvi. Wataalamu hushauri kutumia chumvi kidogo kwa sababu sodium huweza kupandisha pressure, mara nyingine ghafla. Kwako mtu mwenye low blood pressure, chumvi yaweza kuwa kitu kizuri kwako.

 

tiba ya low blood pressure

 

. Kunywa maji mengi zaidi. Majimaji huongeza ujazo wa damu na kusaidia upungufu wa maji, vyote vikisaidia kutibu hypotension.

. Vaa stockings zinazobana. Stockings za kunyumbuka zinazotumika kupunguza maumivu na uvimbe unaotokana na varicose veins zinaweza kusaidia kuzuia kutiririka kwa damu kuelekea maeneo ya miguu.

 

low blood pressure stockings

 

. Baadhi ya dawa zinatumika kupunguza hypotension inayotokea wakati unasimama (orthostatic hypotension). Kwa mfano, fludrocortisone.

Madaktari wanatumia midodrine (Orvaten) kupandisha pressure wakati wa kusimama kwa watu wenye orthostatic hypotension. Dawa hii hufanya kazi kwa kupunguza uwezo wa mishipa ya damu kupanuka, na hivyo kuongeza pressure.

. Kuwa makini na mikao ya mwili wako. Inuka taratibu kutoka hali ya kuketi hadi kusimama. Usiketi huku miguu yako ikipishana (legs crossed).

Unapoamka asubuhi, vuta pumzi chache za nguvu kwa dakika kadhaa, kisha keti taratibu kabla ya hujasimama. Kulala huku sehemu ya kichwa ikiwa imenyanyuka kidogo itakusaidia.

Endapo ukiwa umesimama utaanza kusikia dalili, weka mguu mmoja juu ya kiti au sehemu iliyonyanuka kisha inamisha sehemu ya juu ya mwili kadiri utakavyoweza.

Katika mada ijayo tutalijadili tatizo la pressure ya juu (high blood pressure) na katika mada nyingine tutayajadili matatizo ya ovarian cyst  na ugumba kwa mwanamke.

Usisite kutoa maoni uliyo nayo kuhusu mada yetu ya leo na tunaahidi kujibu maswali yako yote na kwa wakati.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya mida wa kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.