Saratani Ya Shingo Ya Kizazi – Cervical Cancer

 

 mgonjwa wa saratani

 

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayoanzia kwenye sehemu ya mwisho ya nyumba ya uzazi (cervix), pale sehemu hiyo inapoungana na sehemu ya juu ya uke ( vagina) Saratani ya shingo ya kizazi husumbua wanawake dunia nzima na ni kansa inayoonekana na kuua wanawake wengi zaidi katika nchi zinazoendelea, wasiopata fursa ya kuchukua vipimo (Pap testing) vya afya ya shingo za kizazi au kupewa chanjo dhidi ya human papillomaviruses( HPVs)

Sataratani ya shingo ya kizazi hutofautiana sana na saratani nyingine za kwenye mfuko wa uzazi kama kansa ya uterus au endemetrial cancer. Kansa hii ikigundulika mapema ina uwezekano mkubwa sana wa kupona. Chanjo dhidi ya HPVs, virusi wanaosadikika kuleta saratani ya shingo ya kizazi ni hatua madhubuti ya kuzuia ugonjwa huu.

 

Ni Nini Chanzo Cha Saratani Ya Shingo Ya Kizazi?

 

Karibu saratani zote za shingo ya kizazi husababishwa na maambukizi ya muda mrefu ya moja ya virusi wa aina ya HPVs. Maabukizi ya HPV ni ya kawaida na watu wengi walioambukizwa HPV hawapati saratani ya shingo ya kizazi. Kuna aina tofauti za HPV zaidi ya 100, na baadhi ya aina chache ndiyo wanaohusishwa na saratani ya shingo ya kizazi. HPVs wengine husababisha chunjua (benign warts) juu ya ngozi au sehemu za siri. HPVs wale wanaoitwa “high-risk” ndio waletao saratani ya shingo ya kizazi au saratani ya uume kwa wanaume. HPVs wanaweza kuleta saratani za midomo, koromeo, na mkundu kwa jinsia zote.

 

saratani ya kizazi

 

Virusi hawa HPV huambukizwa kupitia ngono au kwa kugusana ngozi. Utafiti unaonyesha kuwa watu wengi huambukizwa virusi hawa katika kipindi fulani cha maisha yao. Mambukizi hawa kwa kawaida hupona yenyewe. Kwa baadhi ya wanawake, maambukizi haya huendelea kudumu na kuanza kuleta mabadiliko kwenye seli za cervix. Mabadiliko haya huweza kugndulika kwa kuchukua vipimo vy amara kwa mara – Pap testing.

 

Dalili Za Kansa Ya Shingo Ya Kizazi Ni Zipi?

 

Saratani ya shingo ya kizazi inaweza isitoe dalili zo zote zile.Na hasa, katika hatua za mwanzo kabisa, saratani ya shingo ya kizazi haitoi dalili. Dalili huanza kujitokeza wakati seli za saratani ya shingo ya kizazi zinapoanza kushambulia maeneo ya karibu.

Dalili za saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na:

. Kutokwa damu ukeni kusiko kwa kawaida
. Kutokwa damu ukeni baada ya kukoma hedhi
. Kutokwa damu ukeni baada ya tendo la ndoa
. Kutokwa damu ukeni katikati ya mzunguko wa hedhi
. Hedhi ndefu kuliko kawaida
. Kutokwa uchafu ukeni kusiko kwa kawaida
. Maumivu wakati wa tendo la ndoa

Yafaa kuzingatia kuwa dalili hizi si za kipekee kwa saratani ya shingo ya kizazi na kwamba matatizo mengine ya kiafya yanaweza kutoa dalili kama hizi.

 

Vitu Gani Vingine Vinaweza Kusababisha Saratani Ya Shingo Ya Kizazi?

 

Kama ilivyoelezwa hapo juu, saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na virusi waitwao high-risk HPV. Kwa sababu si kila mtu aliyeambukizwa HPV atapata saratani ya shingo ya kizazi, kuna vitu vingine vinavyochangia ukuaji wa saratani ya aina hii. Vitu kadhaa vimebainishwa kuchangia katika ukuaji wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake:

. Uvutaji wa tumbaku
. Virusi wa HIV
. Kuwa na upungufu wa kinga za mwili
. Unene
. Utumiaji wa muda mrefu wa vidonge vya uzazi wa mpango
. Kuwa na mimba 3 au zaidi mfululizo za miezi 37 hadi 41
. Msichana wa chini ya miaka 17 kuwa na mimba ya kwanza ya miezi 37 hadi 41
. Umaskini
. Kuzaliwa kwenye familia yenye historia ya saratani ya shingo ya kizazi.

 

Hatua Za Saratani Ya Shingo Ya Kizazi

 

Hatua za saratani ya shingo ya kizazi ni kielelezo cha namna saratani hiyo ilivyosambaa ndami ya mwili wa mgonjwa siku alipofasnyiwa uchunguzi. Kujiua hatua ya ugonjwa huu ni muhimu katika kuamua aina bora ya tiba ya kumpa mgonjwa huyu. Hatua ya saratani ya shingo ya kizazi huamuliwa kwa kutazama kiwango cha uvimbe, usaambaaji kwenye lymph nodes, na usambaaji kwenye sehemu nyingine za mabali. Saratani ya shingo ya kizazi imepangwa katika hatua kuanzia 0 hadi IV, kukiwa na vipengele vidogo kwenye hatua hizo kuu.

 

hatua za saratani ya shingo ya kizazi

 

Kiujumla, saratani ya shingo ya kizazi hupangwa katika hatua zifuatazo:

. Stage 0: Hatua hii si ya kansa inayoshambulia. Seli ambazo si za kawaida bado zipo kwenye ngozi ya juu ya cervix.

. Stage I: Kuna kiwango kidogo cha uvimbe ambao bado haujaanza kusambaa kwenye lymph nodes au seheme za mbali.

. Stage II: Saratani imesambaa ha nje ya cervix na uterus, lakini bado haijashambulia kuta za pelvis au sehemu za chini za uke.

. Stage III: Saratani imesambaa hadi kufikia maeneo ya chini ya uke au kuta za pelvis. Uvimbe unaweza kuwa unaziba ureters (mirija ya kutiririsha mkojo kutoka kwenye figo hadi kibofu cha mkojo). Kansa bado haijasambaa kwenye sehemu nyingine za mwili.

. Stage IV: Hii ni hatua juu kabisa ya ugonjwa huu, hatua ambapo saratani imesambaa hadi kwenye kibofu cha mkojo au mkundu, au kwenye maeneo mengine ya mwili.

 

Tiba Ya Saratani Ya Shingo Ya Kizazi

 

Tiba ya saratani y shingo ya kizazi hutegemea vitu vingi, pamoja na hatua ya saratani iliyofikiwa wakati wa uchunguzi. Njia za kawaida ni upasuaji, tiba ya mionzi, chemotherapy, na targeted therapy. Madaktari wengi wanaweza kuhusishwa kwa wakati mmoja.

 

tiba ya saratani ya shingo ya kizazi

 

Upasuaji hufanywa kuondoa seheme iliyoathiriwa na saratani, hasa saratani ikiwa kwenye hatua za mwanzo. Hysterectomy (upasuaji wa kuondoa nyumba ya uzazi – uterus) huweza kufanyika, lakini kwa wanawake wa umri mdogo na ili kulinda uwezo wa kuweza kutunga mimba, upasuaji wa aina nyingine unaweza kufanywa. Cone biopsy (kuondoa seheme za ndani za cervix ambako uvimbe mwingi huanzia) na trachelectomy (kuondoa sehemu ya juu ya uke na cervix) ni upasuaji unaoweza kufanywa kwa uvimbe mdogo na kwa lengo la kulinda kizazi. Kwa hatua za juu zaidi za saratani ya shingo ya kizazi, tumbo la uzazi, lymph nodes za karibu na viungo vingine vinavyozunguka eneo la saratani huondolewa (pelvic exenteration).

Tiba ya mionzi ni tiba nyingine inayotumika sana kwa saratani ya shingo ya kizazi. Mionzi yaweza kulengwa kwa kutumia kifaa cha nje (external beam radiation therapy) au kwa kutumia kifaa kinachoingizwa ukeni hadi eneo la uvimbe kwa muda fulani (brachytherapy ). Wakati mwingine njia zote mbili hutumika kwa pamoja. Kama tiba ya mionzi imechaguliwa kuwa ndiyo tiba kuu, tiba ya chemotherapy hutumika sambasamba na tiba hiyo ya mionzi.

 

tiba ya mionzi

 

Madhara ya tiba hii ya mionzi ni pamoja na uchovu, kuharisha, mabadiliko ya ngozi, kichefuchefu, kutapika, miwasho ukeni au kwenye kibofu cha mkojo, na wakati mwingine mabadiliko ya mzunguko wa hedhi au kukoma hedhi mapema, kama ovari zitapata mionzi.

Tiba ya chemotherapy yaweza kushauriwa kutumika pamoja na tiba ya mionzi katika hatua fulani za saratani ya shingo ya kizazi. Inaweza pia kutumika kabla au baada ya tiba ya mionzi. Chemotherapy ni tiba inayofaa kwa saratani ya shingo ya kizazi iliyojirudia baada ya tiba. Madhara ya tiba ya chemotherapy ni pamoja na kichefuchefu, uchovu, kutapika, kunyonyoka nywele na maumivu ya mdomo.

 

tiba ya chemotherapy

 

Targeted therapy ni tiba inayohusisha matumizi ya madawa ambayo yametengenezwa mahsusi kwa ajili ya kusimamisha shughuli za seli zinazochangia ukuaji wa seli za kansa. Tiba hii mara nyingine hutumika kwa kansa za zilizofikia hatua za juu.

Katika mada nyingine tutazungumzia aina nyingine za saratani, magonjwa ya homa ya ini – hepatitis B na kukosekana kwa kinga za mwili – UKIMWI. Usisite kutoa maoni yako kuhusu somo la leo au kuuliza maswali uliyo nayo, tutafurahi sana kukujibu.

Unasumbuliwa na saratani ya shingo ya kizazi?  Wasiliana nasi.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.