Katika mfulululizo wa mada hii yetu ya leo, tulianza kwa kuona mzunguko wa hedhi ni nini na matatizo yanayojitokeza wakati wa mzunguko wa hedhi. Tukazungumzia awamu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi – Kutoa Damu – inayoanza siku ya kwanza mwanamke anapoanza kutokwa na damu. Tutaendelea kwa kuzungumzia awamu nyingine tatu za mzunguko huo na mwisho kubainisha siku ambazo mwanamke anaweza kubeba mimba katika mzunguko huo. Karibu tuanze na awamu ya pili:
The Follicular Phase
Hii ndiyo awamu inayofuatia mara baada ya awamu ya kwanza ya Kutoa Damu (The bleeding Phase). Awamu hii imepewa jina hilo kwa sababu tezi ya pituitary (Pituitary Gland) inatoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone (FSH) ambayo inatoa ishara ambayo itavifanya vifuko vinavyotunza mayai (follicles) kukomaa. Shughuli katika awamu hii ya mzunguko wa hedhi huanzia kwenye tezi ya hypothalamus inayopatikana katika ubongo. Tezi hii inashughulika na usimamiaji wa kiu, njaa, usingizi, hamu ya mapenzi n.k. Hypothalamus hutoa kemikali iitwayo Follicle Stimulating Hormone Releasing Factor (FSH-RF) ambayo itaiamuru tezi ya pituitary kutoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone (FSH) na kiasi kidogo cha homoni ya Leutenizing Hormone (LH). Utolewaji wa homoni hizi katika damu husababisha vifuko vya mayai (follicles) kukomaa.
Vifuko vya mayai vikianza kukomaa vitatoa homoni nyingine iitwayo estrogen. Kadiri vifuko hivi vinavyozidi kukomaa katika siku saba, homoni ya estrogen hutolewa zaidi na zaidi. Pamoja na estrogen, testosterone homoni ya aina nyingine huongezeka katika damu. Kuongezeka kwa homoni hizi mbili huufanya mwili kupata nguvu na ufanyaji kazi wa ubongo huboreshwa. Mwanamke atasikia hali ya kujiamini na mwenye kupenda kuthubutu. Kuongezeka kwa testosterone kutamfanya ajisikie kupenda kufanya mapenzi wakati oestrogen itamfanya apende kuwa mtu wa kutoka na kuonekana wakati huo hamu ya kula ikipungua. Ni kipindi cha kusikia ukamilifu na bora kwa kufanya maamuzi na kuthubutu mipango mikubwa na migumu.
Homoni ya estrogen huifanya ngozi nyororo inayotanda juu ya nyumba ya uzazi (uterus) kuwa nene na kuleta mabadiliko kwenye ute wa mwanamke (cervical mucous). Kiwango cha estrogen kikifikia kiasi fulani, hypothalamus hutoa Leutenizing Hormone Releasing Factor (LH-RF) ambayo itaifanya tezi ya pitutary kutoa kiasi kikubwa cha Leutenizing Hormone (LH). Tendo hili hukifanya kifuko cha yai kilichokomaa kupita vyote kupasuka na kuachia yai.
The Ovulatory Phase
Kutolewa kwa yai (ovulation) ni kilele cha shughuli zote zilizokuwa zikiendelea katika mwili wa mwanamke katika wiki chache sasa toka alipoanza kutoka damu. Yai lililotolewa na kifuko katika ovari lina uhai wa wastani wa saa 12 hadi 24 kabla ya kunywea.
Yai linapokaribia kuachiwa, kiwango cha damu kinachopelekwa kwenye ovari huongezeka na misuli inayoshikilia ovari hujikunja ili kusogeza ovari karibu na mrija wa uzazi (fallopian tube), kulifanya yai litakaloachiwa kuingia kirahisi ndani ya mrija wa uzazi. Muda mfupi kabla ya yai hili kuachiwa, mlango wa uke (cervix) hutoa ute kwa wingi. Ute huu unaonata husaidia mbegu za kiume kusafiri kuelekea kwenye yai. Baadhi ya wanawake hutumia ute huu kama ishara ya siku ambazo wanaweza kupata ujauzito.
Yai likiwa ndani ya mirija ya uzazi husafirishwa kwa kutumia namna ya vijinywele viitwavyo “cilia” kuelekea kwenye nyumba ya uzazi (uterus). Yai hili litarutubishwa endapo kutakuwa na mbegu za kiume.
Tofauti na mwanamme ambaye hutengeneza mbegu za kiume kila siku na kwa karibu muda wote wa maisha yake, mwanamke anazaliwa na mayai yake ndani ya vikapu vyake miwili – ovari. Mwanamke huzaliwa na mayai yake haya machanga yapatayo milioni moja hadi mbili ndani ya ovari. Katika maisha yake mayai mengi hufa, kuanzia anapokuwa mchanga, na hubakia na mayai yapatayo 400,000 anapofikia kuvunja ungo. Kila anapoingia mwezini, mayai yapatayo 1,000 hupotea na ni moja tu linalofikia kukomaa (ovum) na kuachiwa liingie ndani ya mrija wa uzazi. Katika mayai yake yote milioni moja au ambili aliyozaliwa nayo, ni mayai kama 450 tu yatakayofikia kukomaa.
Ni kiasi kidogo sana cha follicles kitakuwa kimebakia mwanamke huyu anapofikia kukoma hedhi hali ambayo kwa wanawake wengi hutokea kwenye miaka kati ya 48 na 55. Hata hivyo follicles hizi si rahisi kukomaa tena na kutoa mayai kutokana na mabadiliko ya homoni yanayoendana na kukoma kwa hedhi.
The Luteal Phase
Luteal phase ni kipindi cha kuiandaa endometrium na mwili kwa ajili ya ujauzito. Mwili hutegemea kabisa kuwa yai lililodondoshwa lilirutubishwa. Baada ya yai kuangushwa, follicle iliyoangusha yai hilo hugeuka kuwa corpus luteum. Corpus luteum hutoa homoni za estrogen na progesterone.
Wakati homoni ya estrogen ni muhimu, progesterone ni ya muhimu zaidi katika kipindi hiki. Progesterone ina shughuli nyingi, ikiwa ni pamoja na:
. Kuzuia utendaji kazi wa GnRH, FSH, na LH: homoni ambazo huamsha ovari na kusababisha yai kutolewa, vinginevyo mwanamke anaweza kupata ujauzito tena wakati tayari ni mjamzito.
. Kuiandaa endometrium: progesterone huiamuru endometrium kutoa aina fulani ya protini, ambazo hulisha embryo.
. Kuzuia hedhi: progesterone huzuia ngozi laini inayotanda juu ya endometrium isibanduke, tendo ambalo lingeweza kusababisha kutoka kwa mimba (miscarriage) kama mwanamke ana ujauzito.
Progesterone husababisha joto la mwili kupanda. Joto la mwili wa mwanamke hupanda mara baada ya ovulation. Mwanamke akipata ujauzito, joto la mwili litabaki juu kipindi chote cha luteal na kuendelea baada ya hapo. Kama hakuna ujauzito, joto la mwili litaanza kushuka kabla ya kuanza hedhi. Kushuka kwa progesterone kutashusha joto na kuruhusu hedhi.
Luteal Phase Huwa Ina Urefu Gani ?
Kwa wastani, luteal phase hudumu siku 12 hadi 14. Lakini yaweza kuwa fupi ya siku 8 au ndefu ya kufikia siku 16. Urefu wo wote ulio wa kawaida kwa mwili wako, huwa ni wa kujirudiarudia katika mzunguko wako wa hedhi.
Mathalani, mwanamke mwenye urefu wa kawaida wa siku 12, huchukua siku 11 hadi 13. Endapo urefu utazidi siku 13, basi mojamoja huwa ni dalili ya ujauzito.
Urefu wa siku pungufu ya 8 (au 10), huashiria matatizo ya uzazi, ingawa si lazima. Wakati wanawake wengi wanaohangaika kupata ujauzito au wenye matatizo ya mimba kuharibika huwa na luteal fupi, si ajabu kwa mwanamke mwenye kizazi kizuri kuwa na luteal fupi.
Siku 2 hadi 3 baada ya yai kutolewa, viwango vya estrogen na testosterone vitaanza kushuka katika damu na homoni ya progesterone kuanza kutengenezwa. Progesterone ni homoni inayopunguza wasiwasi katika mwili hivyo kuufanya mwili kuwa tulivu. Katika siku zinazofuata, wanawake wengi hujisikia vibaya kutokana na Premenstrual Syndrome (PMS), tatizo ambalo limejulikana kwa miaka mingi.
Premenstrual Syndrome ni jumla ya matatizo yanayowapata wanawake na kuwafanya wajisikie vibaya kutokana na viwango vya homoni kuwa juu kabla, na wakati mwingine, wakati wakiwa katika hedhi.
Aina moja ya PMS hujionyesha kwa mwanamke kuwa na wasiwasi, kuwa na hasira na asiyetabirika. Mara nyingi hali hiyo hupotea mara baada ya kuingia kwenye siku zake. Hii inaweza kutokana na uwiano wa estrogen na progesterone. Estrogen ikizidi, wasiwasi hutanda na progesterone ikizidi, hali ya kuwa na mfadhaiko hujionyesha.
Aina nyingine ya PMS ni kupenda sana sukari (chocolate, mikate , wali mweupe n.k.), uchovu wa mwili na maumivu ya kichwa. Hii inaweza kuwa inatokana na mwili kuongeza usikivu wa insulin unaotokana na kuongezeka kwa viwango vya homoni kabla ya hedhi.
Wakati huu kuna mabadiliko yanayotokea kwenye uterus na ovari. Kile kifuko kilichotoa yai hubadilika rangi na kuwa cha njano “corpus luteum.” Kifuko hiki kinavyoendelea kupona, kinatoa homoni ya estrogen na kiwango kikubwa cha progesterone, homoni muhimu katika utunzaji wa mimba. Hapo baadaye endapo mimba haikutungwa, kifuko hiki hubadilika rangi na kuwa cheupe ” corpus albicans”.
Homoni ya progesterone huifanya ngozi laini inayotanda juu ya uterus (endometrium) kufunikwa na ute, unaozalishwa na tezi zilizopo katika ngozi hiyo. Kama yai halikurutubishwa na mimba kutungwa, arteri za kwenye ngozi nyororo ya juu ya uterus hujifunga na damu kusitishwa kuelekea kwenye ngozi hiyo. Vijibwawa vya damu katika veni hupasuka, pamoja na utando wa endometrium, hutoka nje ya mwili na kuwa ndiyo mwanzo wa hedhi. Urefu wa hedhi hutofautiana baina ya wanawake na hubadilika katika maisha yao.
Siku Za Kupata Mimba Katika Mzunguko Wa Hedhi
Baada ya kuuelewa vizuri mzunguko wa hedhi wa mwanamke, sasa tunaweza kuzungumzia siku za kupata mimba mwanamke. Kimsingi kuna siku 6 ambazo mwanamke anaweza kubeba mimba – siku 5 kabla ya kutoa yai na saa 24 baadaya yai kutolewa. Hii ni kwa sababu mbegu za mwanamme zina uwezo wa kukaa kwa siku 5 ndani ya mwili wa mwanamke kabla hazijafa na yai (ovum) la mwanamke lina uwezo wa kuishi kwa saa 12 hadi 24.
Kitu cha msingi ni kujua siku ambayo mwanamke anatoa yai, kazi ambayo kidogo inataka ujanja kwa sababu mwanamke hatoi yai siku ile ile katika mzunguko wake. Vitu vinavyoweza kutumika ni kufuatilia utokwaji wa ute unaonata na joto la mwili wa mwanamke mapema asubuhi kabla hajaamka na kula kitu cho chote.
Kwa mwanamke wa kawaida mwenye mzunguko unaojirudia wa siku 26-32, unaweza kuchukulia kuwa siku za kupata mimba ni siku zote kuanzia siku ya 8 toka alipoanza hedhi hadi siku ya 19. Katika kipindi hiki, mwanamke akifanya mapenzi mara kwa mara, yamkini ni kubwa kuwa atapata ujauzito.
Katika ukurasa unaoutangulia huu tulizungumzia maana ya mzunguko wa hedhi na sababu zinazoweza kuvuruga mzunguko wa hedhi wa mwanamke na kujadili kuhusu awamu ya kwanza ya mzungumko wa hedhi – Kutoa damu. Katika mada nyingine tutaona sababu za ugumba kwa mwanamke na tiba za ugumba kwa mwanamke. Lakini kabla ya kuzisoma mada hizo, hebu tuvione kwa kina vipindi katika mzunguko wa hedhi.
Usisite kuuliza swali au kuomba ushauri kuhusu mada yetu, ni furaha kwetu kuwasiliana nawe na kukujibu.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya muda wa kazi kwenda nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.i
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu