Uke wa mwanamke hufanya kazi ya kutoa njia kati ya sehemu ya nje ya mwili na viungo vya uzazi vya ndani vya mwanamke. Hali ya kawaida ya majimaji yaliyomo katika uke wa mwanamke huwa ni ya tindikali ili kuzuia maambukizi ya vijidudu wa kuleta maradhi. Hali hii ya utindikali huletwa na bacteria waishio katika uke wa mwanamke. Bacteria hawa ni wa kawaida na hawana madhara kwa mwili. Uke ulio katika hali nzuri hutoa majimaji haya ili kujisafisha. Majimaji haya yanayotengenezwa katika uke na kwenye eno la cervix hufanya kazi ya kuondoa seli zilizokufa na bacteria waharibifu nje ya mwili na huu ndio uchafu wa kawaida ambao mwanamke hutoa ukeni. Kutoa uchafu huu sehemu za siri ni njia ya kuusafisha uke na kuzuia maambukizi ya magonjwa. Kitu cho chote ambacho kitaharibu uwiano wa utengenezwaji wa majimaji haya ndani ya uke kinaweza kujenga mazingira ya maambukizi katika uke.
Uchafu Wa Sehemu Za Siri Ulio Wa Kawaida
Wanawake wote hutoa uchafu sehemu za siri. Kiwango cha uchafu unaotoka, rangi yake na harufu yake vitabalikabadilika kutoka kipindi kimoja hadi kingine kulingana na muda mwanamke aliopo katika mzunguko wake wa mwezi. Uchafu huu utabadilika vilevile kama ananyonyesha, atakuwa na hisia za kufanya mapenzi, atakuwa na mabadiliko ya lishe, anatumia madawa hasa ya mpango wa uzazi au atakuwa na ujauzito. Kwa kawaida uchafu huu huwa usio na rangi, wenye rangi yenye weupe wa mawingu au njanonjano pale unapokaukia kwenye nguo. Unaweza kuwa na vijipande vidogovidogo na mara nyingine ukawa wa kunatanata.
Dalili Za Uchafu Wa Ukeni Usio Wa Kawaida
Madiliko ya uwingi wa uchafu unaotoka au katika rangi ya uchafu unaotoka ni dalili ya maambukizi ya magonjwa katika uke. Maambukizi katika uke ni tatizo la kawaida kwa wanawake na wanawake wengi wameshapata tatizo la maambukizi angalau mara moja katika maisha yao. Ukiona yafuatayo, ujue unaweza kuwa na tatizo la maambukizi ya vijijidudu vya maradhi katika uke wako:
- Kutokwa na uchafu ukeni kunakoambatana na kuwashwa au vijipele
- Kutokwa na uchafu ukeni ambako ni endelevu na kwa kiwango kinachozidi kila siku
- Kusikia maumivu wakati wa kutoa haja ndogo
- Kutokwa na uchafu mweupe, mzito kama jibini
- Uchafu wa kijivu/mweupe au njano/kijani unaotoa harufu mbaya
Aina Za Uchafu Wa Ukeni Usio Wa Kawaida
Kitu cho chote kitakachoharibu uwiano wa bakteria wa kawaida waishio katika uke kinaweza kuleta mabadiliko katika rangi, harufu au muundo wa uchafu utakaotoka katika uke. Hapa chini naonyesha aina ya uchafu unaotoka, maana yake au chazo chake na dalili ambazo zitatokea kwenye mwili wa mwanamke husika:
Uchafu Wenye Damu Au Wa Rangi Ya Kahawia
Hii ni dalili ya mzungumko wa mwezi wa mwanamke uliovurugika na mara chache ni dalili ya kansa ya Cervix au aina nyingine ya kansa iitwayo endometrial cancer. Mwanamke mwenye tatizo hili atatoa damu nyingi ukeni na kuumwa nyonga.
Uchafu Wenye Rangi Ya Mawingu Au Njano
Hii ni dalili ya ugonjwa wa kisonono (Gonorrhea). Mwanamke atatokwa na damu katikati ya siku zake, atatokwa na mkojo bila kukusudia na kupata maumivu ya nyonga.
Uchafu Wa Njano Au Kijani Wenye Harufu Mbaya
Endapo uchafu utatoka kama mapovu, wenye rangi ya kijani au njano ukiambatana na harufu mbaya , hii ni dalili ya Trichomoniasis, maambukizi (parasitic) yanayotokana na ngono zembe. Dalili nyigine ni maumivu na kuwashwa wakati wa kutoa haja ndogo.
Uchafu Mweupe Mzito Kama Jibini
Hii ni dalili ya maambukizi ya aina ya fungus (Yeast infection) na dalili nyingine atakazozisikia mwanamke huyu ni kuvimba na maumivu kwenye sehemu za nje za siri (vulva), kuwashwa na maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Uchafu Mweupe, Wa Njano Au Wa Kijivu Wenye Harufu Ya Samaki
Uchafu wa aina hii ni dalili za maabukizi ya Bacterial Vaginosis. Mwanamke mwenye tatizo hili atasikia miwasho au maumivu, kuvimba kwa uke au sehemu ya nje ya uke (vulva).
Aina Ya Maambukizo Ya Ukeni
Kuifanya mada yetu iwe na maana na msaada zaidi, tutazungumzia kwa undani zaidi aina chache za maambukizi ya ukeni ambazo zinawasumbua wanawake wengi zaidi, ambapo tutatazama dalili zake na kuelezea tiba ambazo zinawea kutolewa kuondoa matatizo hayo. Hapa tutazungumzia Bacterial Vaginosis, Trichomoniasis na Monilia (Yeast) Infection.
Bacterial Vaginosis: Chanzo halisi cha ugonjwa huu hakifahamiki. Kinachotokea ni kuongezeka kwa ghafla kwa idadi ya bacteria hawa ambao ni kawaida kupatikana kwenye uke na kubadilisha uwiano wao kwenye mazingira ya uke. Wanawake wenye wapenzi wengi au wanaofanya mapenzi kupitia midomo wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya Bacterial Vaginosis.
Dalili za Bacterial Vaginosis:
– Kuongezeka kwa uchafu unaotoka ukeni
– Kutokwa na uchafu wa kijivu/mweupe, mwepesi au wa majimaji
– Harufu kama ya samaki ikiambatana na uchafu
– Harufu inayozidi au uchafu unaozidi mara baada ya kufanya tendo la ndoa.
Tiba kwa tatizo la bacterial vaginosis zipo za aina mbili. Tiba ya aina ya kwanza ni kutumia metronidazole (Flagyl) na tiba ya pili ni kutumia antibiotic ya vidonge au ya cream.
Trichomoniasis: Maambukizi haya hutokana na aina ya protozoa wa seli moja. Trichomoniasis maranyingi huambukizwa kwa kufanya ngono. Protozoa huyu huweza kukaa kwenye mazingira ya unyevunyevu kwa muda wa saa 24 bila kufa hivyo kufanya taulo na nguo nyingine za kuogea kuwa chanzo kingine kikuu cha maambukizi.
Dalili Za Trichomoniasis
– Kutokwa na uchafu wa rangi ya njano/kijani ulio kama mapovu
– Harufu mbaya inayoambatana na kutokwa na uchafu
– Kuongezeka kwa uwingi wa uchafu wa ukeni
– Maumivu ya ukeni au sehemu za nje ya uke (vulva)
– Kujisaidia haja ndogo mara nyingi zaidi
– Kuwashwa sehemu za siri
Tiba ya Trichomoniasis ni kunywa vidonge vya antibiotic, metronidazole.
Monilia (Yeast) Infection: Kwa kawaida kuna kiwango kidogo cha yeast (Candida albicans) katik uke. Tunasema kuna maambukizi ya yeast pale kiwango chao kinapozidi hali ambayo inatokana na kubadilika kwa hali ya ukeni (change in the pH balance of the vagina). Maambukizi ya yeast hayatokani na tendo la ngono. Kuna mambo ambayo yanaweza kusababisha kuongezeka kwa yeast katika uke, nayo ni; msongo wa mawazo, matumizi ya dawa za kuzuia mimba, kisukari, ujauzito na matumizi ya antibotics.
Dalili Za Monilia (Yeast) Infection
– Mwongezeko wa uchafu unaotoka ukeni
– Uchafu mweupe unaotoka katika vifungu vidogo kama vya jibini
– Kuwashwa na mauvivu ya ukeni au sehemu za nje (vulva)
Tiba ya Monilia (Yeast) Infection inalenga kuzuia mwongezeko wa yeast katika uke na kuwarudisha kwenye kiwango kinachofaa na si kuwaondoa. Tiba ni kutumia vidonge vya antifungal na cream za kupaka ukeni. Kuna dawa nyingi za kuweza kuondoa tatizo hili.
Cytolytic Vaginosis: Hii ni hali inayojitokeza pale kunapotokea kuongezeka kwa bakteria aitwaye Lactobacillus acidophilus kwenye uke. Lactobacilli ni bakteria wazuri wanaoishi ukeni bila kuleta matatizo ya aina yo yote. Kwa kawaida uwepo wa bakteria hawa unasaidia sana katika kupambana na wadudu aina nyingine wenye madhara kwa mwili – huongeza kinga ya mwili .
Lakini endapo mazingira dhalili ya uke yatabadilika, bakteria hawa wazuri wanaweza kuzaliana kupita kiwango kinachotakiwa. Hii inaweza kutokea, kwa mfano, kunapotokea matumizi ya mara kwa mara ya antibiotics au dawa za kuzuia na kuua fungus.
Ni tatizo ambalo linawapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa – miaka 25 – 40 – kwa sababu ya uwepo wa homoni ya estrogen.
Dalili za cytolytic vaginosis ni:
– Kutoka uchafu kwa wingi wenye rangi nyeupe, wa maji maji au mzito kama maziwa ya mgando
– Miwasho ya sehemu za ndani au nje ya uke
– Maumivu wakati wa kutoa haja ndogo
– Maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa
Dalili za tatizo hili ni rahisi sana kuzichanganya na zile za matatizo mengine ya hapo juu na hasa vaginal candidiasis (monilia).
Tatizo hili halina tiba bali kufanya yafuatayo:
– Kuacha kutumia antibiotics au dawa za fungus
– Kuacha kutumia sabuni ukeni na kutumia maji ya uvuguvugu tu
– Kutovaa nguo za ndani usiku
– Kutofanya tendo la ndoa
– Kupunguza kiwango cha sukari katika mlo
– Kujiosha mara kwa mara ukeni kwa kutumia baking soda. Unaweza vile vile kuchanganya baking soda na maji ukatengeneza namna ya uji na kuuweka kwenye pedi.
Soma zaidi kuhusu tatizo la cytolytic vaginosis kwenye ukurasa mwingine wa tatizo la kutoa uchafu mweupe ukeni (cytolytic vaginosis).
Katika mada yetu ya leo tumeona kwa nini uchafu hutoka katika uchi wa mwanamke, kutofautisha baina ya uchafu wa kawaida na uchafu usio wa kawaida. Tumeona vilevile aina za maambukizi ya ukeni mbayo huwasumbua wanawake wengi na tiba inayoweza kutolewa.
Katika mada nyingine tatajadili tatizo la uchi kulegea au hali ya maumbile ya mwanamke kuwa mapana kuliko kawaida.
Tunaomba mchango wako wa mawazo kuhusu mada yetu ya leo na kama una maswali yo yote usisite kutuuliza. Ni faraja kwetu kuona tumekujibu vizuri.
Kwa mawasiliano tumia anuani promota927@gmail.com, au jaza fomu iliyopo chini kwenye ukurasa huu. Unawaewza kuzungumza nasi moja kwa moja kwa simu kwa namba 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.