Tuanze kwa kukitazama kisa hiki. Miezi michache baada ya paka mgeni kuletwa katika nyumba, baba anaanza kuwashwa na macho na mara kadhaa anapiga chafya. Mmoja wa watoto watatu wa familia anaanza kukohoa na kupumua kwa shida. Mama na watoto wengine wawili hawana shida yo yote iliyotokana na ujio wa huyu paka. Huu ni mfano wa kuelezea uwepo wa tatizo la mwili linaloitwa mzio au kwa kitaalamu allergy.
Allergy au mzio ni majibu ya kuzidi kiwango yanayotolewa na mfumo wa kinga za mwili baada ya mwili kukiona kitu ambacho unahisi si salama. Tunasema ni majibu ya kuzidi kiwango kwa sababu kitu hicho hicho huonekana si cha hatari ndani ya mwili wa mtu ambaye hana mzio na hakuna shambulio la kutoa majibu linalofanywa.
Vitu vinavyosababisha allergy huitwa allergens. Mifano ya allergens ni poleni za mimea, wadudu wadogo ndani ya vumbi, udongo wa mboji, protini ya wanyama, chakula, na madawa. Mtu mwenye mzio akikutana na allergen, kinga zake za mwili huandaa majibu kupitia kingamwili (antibody) ya IgE.
Nini Husababisha Allergy?
Mfumo wa kinga za mwili ni mpangilio maalumu wa mwili wa kujilinda dhidi ya vitu kutoka nje vinavyouvamia mwili, na hasa maabukizo ya wadudu. Kazi yake ni kutambua na kujilinda dhidi ya wadudu hawa wa nje, ambao huitwa antigens. Antigens mara nyingi husababisha mwili kujibu kupitia utengenezaji wa antibodies, ambazo ni protini za kujilinda, ambazo kila moja hutengenezwa mahsusi kwa aina fulani ya antigen. Antibodies hizi, immunoglobulins (IgG,IgM, na IgA), ni kwa ajili ya ulinzi na husaidia kufanya ulinzi kwa kunasa kwenye antigen, na kuruhusu seli za kinga ya mwili kufanya maangamizi. Mtu mwenye mzio hutengeneza aina fulani ya kingamwili iitwayo immunoglobulin E, au IgE, kutoa kinga dhidi ya vitu ambavyo kwa kawaida si vya hatari, kama manyoya ya paka, poleni ya mimea, au chakula. Antigens nyingine, kama bakteria, hazisababishi utengenezwaji wa IgE, kwa hiyo hazisababishi mwili kujaribu kujilinda (allergic reaction). Mara IgE ikitengenezwa, itatambua antigen na kuanzisha allergic response. IgE iligunduliwa mwaka 1967 na Kimishige na Teriko.
Katika mfano wa hapo juu wa paka, baba na binti mdogo wa mwisho walitengeneza antibodies za IgE kwa wingi ndani ya miili yao zilizolenga allergen ya paka. Baba na binti wakawa wamejengewa usikivu, au wakawa wahanga wa allergic reactions, pale watakapokutana na allergen ya huyu paka. Kwa kawaida, kuna kipindi cha kujenga usikivu huu, ambao waweza kuwa kati ya siku chache hadi miaka, kabla ya kuwa tayari kuanza kutoa allergic response. Ni muhimu kujua kuwa mtu hawezi kuwa allergic wa kitu ambacho hakuwahi kukutana nacho kabla. Mtu anaweza kuwa amekutana na allergen kwa mara ya kwanza akiwa tumboni mwa mama yake, kupitia maziwa aliyonyonya au kupitia kwenye ngozi.
IgE ni kingamwili ambayo kila mmoja wetu anayo kwa kiwango kidogo. Watu wenye allergy, kwa kawaida, hutengeneza IgE kwa wingi.
Ukali wa allergy hutofautiana kutoka mtu hadi mtu na unaweza kuwa ni usumbufu mdogo hadi mtu kupata anaphylaxis – hali hatarishi inayotaka msaada wa haraka. Wakati ambapo allergy nyingi hazina tiba, baadhi ya dawa zinaweza kupunguza makali ya allergy.
Dalili Za Allergy
Dalili za allergy, ambazo hutofautiana kulingana na sehemu husika, zaweza kuathiri njia za hewa, sehemu za wazi kati ya mifupa (sinuses) na njia za pua, ngozi, na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Allergic reactions zaweza kuwa ndogo au kali. Baadhi ya dalili kali, zinaweza kuhatarisha maisha, hali iitwayo anaphylaxis.
Mafua yaletwayo na vumbi (hay fever), ambayo pia huitwa allergic rhinitis, yaweza kusababisha:
. Kupiga chafya
. Kuwashwa pua, macho, au sehemu ya juu ya mdomo
. Kuvuja kamasi
. Majimaji machoni, macho mekundu au yaliyovimba (conjunctivitis)
Allergy ya chakula yaweza kusababisha:
. Msisimko mdomoni
. Kuvimba mdomo, ulimi, uso au koo
. Hives, ugonjwa wa mabaka ngozini
. Anaphylaxis
Kung’atwa na mdudu kwaweza kusabababisha:
. Eneo kubwa lililovimba (edema) kuzunguka sehemu iliyong’atwa
. Kuwasha au Hives mwili mzima
. Kukohoa, kubanwa mbavu, kukorota au kupumua kwa shida
. Anaphylaxis
Allergy ya dawa yaweza kusababisha:
. Hives
. Kuwashwa ngozi
. Vipele vidogo (rash)
. Kuvimba uso
. Kupumua kwa shida
. Anaphylaxis
Atopic dermatitis, mzio wa ngozi uitwao eczema, waweza kusababisha:
. Mwasho
. Wekundu
. Ngozi kubanduka
Madhara ya allergy
Kuwa na allergy kunaongeza uwezekano wa kupata magonjwa mengine, ambayo ni pamoja na:
. Anaphylaxis. Kama una allergy kali, unakuwa kwenye hatari ya kupata hali hii. Chakula, dawa na kung’atwa na wadudu ni vitu vinavyoweza kulata anaphylaxis.
. Asthma. Kama una allergy unaweza kupata asthma – athari inayotokana na kinga za mwili inayoathiri njia za hewa na upumuaji. Mara nyingi asthma huamshwa na kuwa mkabala na allergen katika mazingira (allergy-induced asthma).
. Sinusitis na maambukizo kwenye masikio na mapafu. Uwezekano wa kupatwa na hali hizi ni mkubwa kama una hay fever au asthma.
Tiba ya allergy
Tiba za allergy ni pamoja na:
. Kuepuka allergen. Daktari atakusaidia kuchukua hatua za kugundua na kukwepa vitu vinavyokusababishia allergy. Kwa ujumla hii ndiyo ya muhimu sana katika kuzuia mjibizo wa mwili kwa allergy na kupunguza dalili zake.
. Dawa. Kulingana na allergy yako, dawa zinaweza kusaidia kupunguza mjibizo wa kinga zako za mwili na kupunguza dalili. Daktari anaweza kukuandikia vidonge au dawa ya maji, Spray ya puani, au matone ya macho.
. Immunotherapy. Kwa allergy ambazo ni kali au zile ambazo hazikubali tiba za kawaida, daktari anaweza akashauri immunotherapy. Tiba hii inahusisha sindano kadhaa zenye mchujo halisi wa allergen, ambazo atapewa kwa kipindi kirefu kidogo.
Namna nyingine ya immunotherapy ni kidonge kinachowekwa chini ya ulimi (sublingual) hadi kiyeyuke. Vidonge hivi hutumika kutiba baadhi ya allergy za poleni.
. Emergency epinephrine. Kama una allerguy kali, unaweza kuhitaji kupewa sindano ya epinephrine.
Katika mada nyingine, tutauzungumzia ugonjwa wa kizunguzungu (vertigo). Usisite kuuliza maswali uliyo nayo au kutoa ushauri kuhusu uandishi wa mada yetu ya leo.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya saa za kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.