Pumu ni ugonjwa ambao unashambulia watu wa pande zote za dunia, na inakadiriwa kuwa karibu watu milioni 300 wana ugonjwa huu duniani. Ni ugonjwa ambao hushambulia watu wa jinsia zote na rika zote lakini mara nyingi zaidi watu hupata ugonjwa huu utotoni. Watoto wengi huanza kupata dalili za ugonjwa huu wanapofikia umri wa miaka mitano. Watoto walio kwenye hatari kubwa zaidi ya kupatwa na maradhi haya ni wale wanaozaliwa wakiwa na uzito mdogo, wale wanaolelewa kwenye mazingira yenye moshi wa sigara na wale wanaozaliwa kwenye familia zenye kipato kidogo. Watoto wenye ngozi nyeusi wanakuwa hatarini zaidi kuliko weupe.
Mambo mengine yanayochangia ni mtoto kuwa na mzio (allergy) wa kitu fulani na/au kuzaliwa na wazazi wenye asili ya kuwa na maradhi haya. Watoto wa kiume hupata ugonjwa huu zaidi ya watoto wa kike, lakini hali hubadilika wanapokuwa wakubwa.
Katika ukurasa huu tutaona ni nini tiba ya pumu na jinsi ya kufanya ukiwa na ugonjwa huu ili uweze kuishi na kufanya shughuli zako za maisha bila kusumbuliwa na maradhi haya.
Pumu inatoka Wapi?
Katika ukurasa uliotangulia wa “ujue ugonjwa wa pumu” tuliona nini maana ya pumu na ni nini kinatokea tunaposema mtu amebanwa na pumu. Nina uhakika umekuwa unajiuliza huu ugonjwa unatoka wapi au unasababishwa na nini. Kwa kifupi sana hapa chini tutatoa majibu kwa swali lako. Vyanzo vya pumu vimeeleweka kuwa ni kama ifuatavyo:
Mzio (Allergy): Karibu watu wote wenye pumu wana mzio (allergy) ambayo ni hali ya miili yao kutopenda vitu fulani pale vinapovutwa na hewa mtu anapopumua, vikiliwa, vikiingizwa mwilini kwa kudungwa sindano au vikigusa ngozi zao. Lo lote likitokea katika hayo mtu mwenye mzio anaweza akawashwa macho, akatokwa na kamasi, akapumua akitoa sauti ya vifilimbi, akatokwa na vijipele juu ya ngozi au akapata tumbo la kuharisha. Baadhi ya vitu vinavyosababisha hali hiyo (allergens) ni protini za wanyama, poleni ya mimea, nyasi, vumbi, mende na baadhi ya madawa.
Katika kujilinda, kinga za miili yetu zilizopo ndani ya damu mara nyingi husababisha njia za kupitisha hewa kutoka na kwenda mapafuni kuvimba ambako kunahusishwa na pumu.
Moshi Wa Tumbaku
Uchafuzi Wa Mazingira: Dalili nyingi za pumu zinatokana na uchafuzi wa mazingira na hasa wa majumbani kutokana na mvuke unaotokana na vifaa vya kusafishia nyumba na rangi za kutani. Majiko ya kupikia yanayotumia gesi yanayotoa hewa aina ya nitrogen oxide ambayo pia huhusishwa na tatizo la pumu. Watu wanaopika kwa kutumia gesi hupatwa na matatizo yanayoambatana na pumu kama kupumua kwa shida na kubanwa na pumu.
Vitu vingine kwenye mazingira vinavyoaminika kusababisha pumu ni sulfur dioxide, nitrogen oxide, ozone, hali ya hewa ya baridi na hali ya kuwa na unyevunyevu mwingi katika hewa (high humidity).
Kula Kupita Kiasi: Watu wazima wenye uzito mkubwa sana wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata pumu ukilinganisha na wale wenye uzito wa kawaida. Utafiti unaonyesha kuwa hatari ya kupata pumu isiyotokana na mzio (nonallergic asthma ) ni kubwa zaidi kuliko ile inayotokana na mzio (allergic asthma).
Ujauzito Na Uzazi: Jinsi uliovyoingia katika dunia hii ina uhusiano na uwezekano wa kupata pumu baadaye. Watoto waliozaliwa kwa operesheni wana asilimia 20 zaidi ya uwezekano wa kupata pumu baadaye – inawezekana kuwa maambukizo yanayoathiri kinga za mwili kutokana na uwepo wa bacteria wakati wa operesheni yanahusika na tofauti hii.
Akinamama wanaovuta sigara wakati wa ujauzito husababisha watoto wao matumboni kuwa na uwezo mdogo wa kupumua na kuongeza hatari ya watoto wao watakaozaliwa kupata pumu. Utafiti umeonyesha kuwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti) wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuja kupata pumu baadaye.
Msongo Wa Mawazo: Kupatwa na msongo wa mawazo mara kwa mara kunaongeza uwezekano wa kupata pumu, moja ya sababu ni tabia za mtu anapokuwa na msongo wa mawazo kama vile kuvuta sigara kunakochochewa na msongo wa mawazo. Maelezo ya hapa karibuni yanaonyesha kuwa mfumo wa kinga za mwili hubadilika mtu anapokuwa na msongo wa mawazo.
Urithi: Wazazi wanahusika katika kumfanya mtoto awe na pumu, inakadiriwa kuwa katika watoto watano wenye pumu, watatu huwa ni pumu za kurithi kutoka kwa wazazi wao.
Namna Ya Kutibu Pumu
Pumu ni ugonjwa wa kudumu ambao haujapatiwa dawa ya kuuondoa moja kwa moja. Tunapozungumzia tiba ya pumu tunamaanisha ushirikiano wa pamoja wa daktari na mgonjwa au na mzazi wa mtoto mgonjwa katika kuudhibiti ugonjwa huu ili:
1. Kuzuia mgonjwa asirudiwe na matatizo ya mara kwa mara ya kukohoa, kubanwa pumzi na mengineyo yanayoambatana na ugonjwa huu
2. Kupunguza uwezekano wa kuzidiwa na kuhitaji huduma ya dharura
3. Kuyaweka mapafu katika hali nzuri wakati wote
4. Kumwezesha mgonjwa kushiriki katika shughuli za kawaida za kimaisha na kupata usingizi mzuri
5. Kuzuia mgonjwa asibanwe na pumu na kusabibisha tiba za dharura
Mgonjwa anahitaji kuwa na mpango mzuri unaoelekeza namna ya kutumia dawa ipasavyo, namna ya kuzuia mgonjwa asikumbane na vitu vinavyochochea pumu (asthma triggers), namna ya kufuatilia jinsi mgonjwa alivyoweza kuudhibiti ugonjwa huu na namna ambavyo mgonjwa atakavyoweza kupata huduma ya dharura endapo atazidiwa.
Tiba ya pumu huwa inagawanywa kwenye makundi mawili; tiba ya kutoa msaada wa haraka na tiba ya muda mrefu ya kudhibiti pumu. Tiba ya kutoa msaada wa haraka ni ile inayotolewa pale mgonjwa anapoona dalili za kubanwa pumu na tiba ya muda mrefu ya kudhibiti pumu inalenga kupunguza athari zinazotokea kwenye njia za hewa na hivyo kuzuia kutokea kwa kubanwa na pumu.
Dawa za pumu huweza kutolewa kama vidonge, lakini nyingi huwa kama unga au mvuke ambavyo mgonjwa atavitumia kupitia kinywani mwake kwa kutumia kifaa kinachoitwa Inhaler. Inhaler ni kifaa kinachosaidia dawa kupita kirahisi katika njia za hewa kuelekea kwenye mapafu.
Tiba Ya Pumu Ya Kutoa Msaada Wa Haraka
Mgonjwa ye yote wa pumu lazima awe na njia ya kupata msaada wa haraka ili kuzuia tatizo lisiwe kubwa pale anapohisi dalili za kubanwa na pumu. Chaguo la kwanza kwa mgonjwa wa pumu la kupata msaada pale anapoanza kujihisi vibaya ni Inhaled short-acting beta2-agonists. Hizi ni dawa ambazo mtumiaji atazipata kupitia kifaa kinachoitwa Inhaler. Dawa hizi hufanya kazi haraka sana na kulegeza misuli ya njia ya hewa iliyokaza pale mgonjwa anapobanwa na pumu na hivyo kufungua njia ya hewa. Vifaa hiivi vipo vya aina tofauti, yafaa kumwuliza daktari wako kuhusu njia nzuri ya kukitumia kifaa ulicho nacho.
Mgonjwa anatakiwa kutumia inhaler mara tu anapoanza kusikia dalili za kubanwa na pumu, hivyo basi mgonjwa anashauriwa kuwa na kifaa chake po pote alipo. Kifaa hiki kinashauriwa kisitumike zaidi ya mara mbili kwa wiki, endapo matumizi yanaanza kuzidi idadi hiyo ni vizuri mgonjwa amwambie daktari wake kuhusu hali yake ili aweze kubadilishiwa mpango wake wa kuudhibiti ugonjwa wa pumu. Kifaa hiki hata hivyo hakipunguzi tatizo la kuathirika kwa njia za hewa kama tutakavyoona katika tiba ya muda mrefu ya kudhibiti pumu.
Tiba Ya Muda Mrefu Ya Kudhibiti Pumu
Watu wengi wenye pumu hutumia njia za muda mrefu za kudhibiti pumu kila siku ili kuzuia uwezekano wa kutokea matatizo yanayoambatana na ugonjwa huo. Njia hizi za muda mrefu hupunguza kuathirika kwa njia za hewa (kuvimba kwa ndani na kuwa sikivu kuzidi kiwango) na hivyo kuondoa uwezekano wa kutokea kwa kubanwa na pumu. Njia hizi hazisaidii kutoa msaada wa haraka kwa mgonjwa.
Watu wengi wenye pumu hutumia corticosteroids ( inhaled corticosteroids ) kila siku ili kudhibiti ugonjwa wa pumu walio nao. Corticosteroids ni kundi la kemikali ambazo hutengenezwa na figo au kwenye maabara ambazo hufanya kazi nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na kupunguza vimbe katika mwili. Matumizi ya dawa hii yameonyesha kuwa bora katika kuzuia kutokea kwa uvimbe na athari nyingine kwenye njia za hewa zinazotokana na mtu kuvuta hewa yenye vitu visivyopendwa na mwili wa muathirika. Dawa hii hutumiwa kwa kuvutwa kwa mdomo kutoka kwenye kifaa maalumu.
Matumizi ya inhaled corticosteroids yana athari zake zikiwa ni pamoja na maambukizi ya mdomoni (thrush) yanayosabababishwa na matone ya dawa hiyo kuangukia kwenye mdomo au kooni. Dawa hiyo pia huweza kuathiri mboni za macho na kupunguza uimara wa mifupa endapo itatumika kwa muda mrefu.
Dawa nyingine zinazotumika katika udhibiti wa pumu wa muda mrefu ni:
-Cromolyn
-Omalizumab
-Inhaled long-acting beta2-agonists
-Leukotriene modifiers
-Theophylline
Peak Flow Meter
Hiki ni kifaa kidogo cha kushikwa mkononi ambacho kinaonyesha jinsi hewa inavyotoka kutoka katika mapafu ya mtumiaji. Mtumiaji anapuliza kwa mdomo kwenye kifaa hicho na ataonyeshwa alama alizopata ( peak flow number) ambazo ni ishara ya ubora wa kiafya wa mapafu yake kwa wakati huo alipopuliza kwenye kifaa hicho. Mtumiaji anakitumia kifaa hicho kwa namna na muda alioshauriwa na daktari wake, kwa mfano, daktari anaweza kumshauri mgonjwa kukitumia kifaa hichio kila siku asubuhi na kunukuu alama anazopata kisha kumpelekea baada ya kipindi fulani ili aweze kushauriwa dawa za kuendelea kuzitumia.
Matumizi ya kifaa hiki yanaweza kukupa taarifa mapema ya hali ya kubanwa na pumu inayotegemea kukupata, ukajihami kwa kutumia dawa za kutoa msaada wa haraka na baadaye kujipima tena baadaye ili kuona msaada uliopewa na dawa ulizozitumia.
Katika mada ya leo tumeona ni nini chanzo cha ugonjwa huu wa pumu, njia zinazotumika kutoa msaada wa haraka mtu anapobanwa na pumu na njia za muda mrefu za kudhibiti ugonjwa huu wa pumu. Kama hujasoma jinsi pumu inavyotokea na aina mbalimbali za pumu, rejea ukurasa wetu wa “Ujue Ugonjwa Wa Pumu.”
Katika mada nyingine tutaujadili ugonjwa wa kifua kikuu. Tunaomba maoni yako kuhusu ukurasa wetu huu wa leo, na kama una maswali, usisite kuuliza.
Kwa maswali na msaada wa ziada wa kukabiliana na ugonjwa huu wa pumu, wasiliana nasi kwa kupitia anuani yetu promota927@gmail.com au unaweza kutupigia simu moja kwa moja ndani ya muda wa kazi kwa kutumia nambari 0655 858027 au 0756 181651 au jaza fomu chini ya ukurasa huu.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.