Ugonjwa Wa Kisonono (Gonorrhoea): Chanzo Na Tiba

maambukizi ya kisonono

Ugonjwa wa Kisonono (Gonorrhoea) ni ugonjwa unaoshambulia watu wengi, wanaume kwa wanawake. Ni ugonjwa unaotibika ingawa kwa miaka ya karibuni, wadudu wa ugonjwa huu wameonyesha kuanza kutosikia tiba zinazotolewa. Kisonono kisipotibiwa kikamilifu, huweza kuleta madhara ya kudumu kwenye mwili wa mgonjwa na kumfanya aweze kuambukizwa au kuambukiza UKIMWI kwa urahisi. Katika ukurasa huu tutaona chanzo cha ugonjwa huu, dalili zake na mwisho kinga na tiba inayoweza kutolewa kwa ugonjwa huu.

Chanzo Cha Kisonono (Gonorrhoea)

Kisonono ni ugonjwa unaoambukiza kwa ngono – sexually transmitted infection (STI) – na unasababishwa na bakteria aitwaye Neisseria gonorrhoeae au gonococcus. Bakteria huyu hupenda kuzaliana kwenye maeneo ya joto, yenye unyevunyevu yakiwemo maeneo ya shingo ya uzazi (cervix), nyumba ya uzazi (uterus), mirija ya uzazi (fallopian tubes) na mrija wa kutolea mkojo nje (urethra). Bakteria hawa pia huweza kuzaliana kwenye mdomo, mkundu na mara chache kwenye koo na macho.

Kimsingi bakteria hawa hupatikana kwa wingi katika shahawa na usaha unaotoka katika uume wa mwanamme mgonjwa na katika majimaji ya ukeni. Bakteria hawa huambukiza kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa njia zifuatazo:

. Ngono zembe kupitia uke, mdomo au mkundu. Mwanamme anaweza kumwambukiza gono mwanamke hata kama hakutoa shahawa (manii) wakati wa kufanya tendo la ndoa
. Kuchangia vifaa vya kujistarehesha ambavyo havikuoshwa au kufunikwa na kondomu, kama vibrators na vimwanasesere vya aina nyingine.

Mama mjamzito mwenye maambukizo anaweza kumwambukiza mtoto anayezaliwa na endapo mtoto huyo hatapewa tiba, anaweza kupata upofu wa kudumu. Hivyo, mama mjamzito mwenye maambukizo anatakiwa apewe tiba kabla ya kujifungua.

Bakteria wa kisonono hawaambukizi kwa kubusiana, kushikana mikono, kuchangia bafu au taulo, mabwawa ya kuogelea, vyoo, kuchangia vikombe na vyombo ya kulia kwa sababu wadudu hawa wa kisonono hawana uwezo wa kuishi kwa muda mrefu nje ya mwili wa binadamu.

Dalili Za Kisonono

Sio watu wote wenye kisonono wataona dalili za ugonjwa huu. Pale ambapo mgonjwa ataona dalili, zitaonekana katika siku kama 10 baada ya kupata maambukizo ingawa inaweza ikachukua hadi siku 30. Dalili atakazoziona mwanamme zinaweza kuwa tofauti kidogo na zile atakazoziona mwanamke.

Dalili Za Kisonono Kwa Mwanamme

kisonono

. Kutokwa na uchafu uumeni wenye rangi nyeupe, njano au kijani unaofanana na usaha
. Maumivu kwenye mapumbu
. Maumivu wakati wa haja ndogo
. Kutokwa na uchafu kwenye mkundu, kuwashwa, kutokwa damu wakati wa haja kubwa
. Koo kukauka, kuwashwa, kumeza kwa shida au uvimbe shingoni
. Maumivu kwenye macho, macho kutopenda mwanga mwingi na kutokwa uchafu machoni unafanana na usaha
. Maumivu na kuvimba kwenye sehemu za maungio ya mifupa

Dalili Za Kisonono Kwa Mwanamke

kisonono kwenye uke

. Maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa
. Homa
. Kutokwa uchafu ukeni wenye rangi ya njano au kijani
. Kuvimba eneo la uke
. Kutokwa damu katikati ya siku za mwezi
. Kutokwa damu baada ya kufanya tendo la ndoa
. Kutapika, maumivu ya tumbo na maumivu ya nyonga
. Maumivu wakati wa haja ndogo na kupata haja ndogo mara nyingi
. Kutoa uchafu kwenye mkundu, kuwashwa, maumivu au kutoa damu wakati wa haja kubwa
. Kukauka koo, kuwashwa, kumeza kwa shida au uvimbe kooni
. Maumivu kwenye macho, kutopenda mwanga mkali na/au kutoa uchafu kwenye macho unaofanana na usaha
. Kuvimba na joto kwenye maungio ya mifupa

Madhara Ya Kisonono

Kisonono ambayo haikutibiwa inaweza kuleta madhara makubwa na ya kudumu kwa jinsia zote.

Kwa wanawake, kisonono ambayo haikutibiwa inaweza kusababisha – pelvic inflammatory disease (PID) – ambayo inaweza kuharibu mirija ya uzazi na mara nyingine kusababisha ugumba. Kisonono ambayo haikutibiwa inaweza pia kusababisha mimba kutungwa nje ya nyumba ya uzazi (ectopic pregnancy), hali ambayo inaweza kumhatarishia mwanamke maisha yake.

ugonjwa wa kisonono

Kisonono kinaweza kumsababishia mwanamke kuzaa njiti (mtoto kuzaliwa kabla ya siku) au mimba kuharibika. Mwanamke mwenye kisonono anaweza kumwambukiza kichanga wakati wa uzazi na kukisababishia kichanga upofu wa kudumu, maambukizo kwenye maungio ya mifupa au maambukizo kwenye damu.

Mwanamme ambaye ana kisonono isiyotibiwa anaweza kupata maumivu makali kwenye mapumbu kutokana na ugonjwa uitwao epididymo- orchitis na kumsababishia ugumba. Kisonono ambayo haikupewa tiba ya kutosha inaweza kumletea madhara kwenye tezi dume (prostate) na anaweza kupata makovu ndani ya mrija wa kutolea mkojo nje (urethra) na kufanya mkojo utoke kwa shida.

Kisonono huweza kusambaa hadi kwenye mifupa na damu hali ambayo ni hatari kwa maisha. Mtu mwenye gono anaweza kuambukizwa UKIMWI kwa urahisi zaidi.

Tiba Ya Kisonono

Endapo vipimo vimeonyesha kuwa una kisonono, wewe na mwenzi wako wote mnatakiwa kutibiwa kwa kutumia antibiotics na kuacha kujihusisha na masula ya mapenzi hadi hapo tiba itakapokwisha. Baada ya kumaiza tiba, inashauriwa kujipa mapumziko ya angalau miezi 3 kuhakikisha kuwa maabukizo yote yamekwisha.

Ndugu msomaji, jisikie huru kuuliza maswali au kutoa maoni uliyo nayo kuhusu mada yetu ya leo, tutafurahi kuona tumekujibu vizuri.

Katika mada zetu nyingine tutauzungumzia ugonjwa mwingine unaoambukizwa kwa kufanya ngono – UKIMWI – ambamo tutaona chanzo chake, aina za virusi wa UKIMWI, na  jinsi gani ugonjwa huo unaweza kuambukizwa.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu NDANI YA SAA ZA KAZI kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.

Laurian