Pumu ni ugonjwa sugu wa mapafu unasababishwa na kuvimba na kukaza kwa misuli inayozunguka njia za hewa, na kusababisha upumuaji kuwa wa shida. Mgonjwa akibanwa hupata dalili za kukohoa, kutoa sauti za filimbi, kupumua kwa shida, kubanwa kifua na nyinginezo. Pumu (asthma) ni ugonjwa unaowapata watu wa rika zote lakini mara nyingi ni ugonjwa unaoanza utotoni. Ni ugonjwa wa kudumu ambao hadi sasa haujapata tiba, lakini kuna njia nyingi na rahisi za kuweza kumsaidia mtu mwenye ugonjwa huu kuzuia asibanwe na pumu. Mtu mwenye tatizo hili anahitaji kuchukua hatua za kuulinda mwili wake na kuwa na mpango mzuri wa kuufuata katika kuhakikisha kuwa hapati dalili za ugonjwa huu mara kwa mara.
Kuna watu wengi mashuhuri duniani walioishi na wanaoendelea kuishi na ugonjwa huu. Baadhi ya Wanasiasa ni: Bill Clinton, rais wa 42 wa Marekani; Che Guevara, mwanaharakati wa Marekani Ya Kusini; na John F. Kennedy, rais wa 35 wa Marekani.
Jerome Bettis ni mchezaji wa mpira wa miguu wa kimataifa aliyeishi na kushiriki michezo akiwa na pumu; Tom Malchow, mwogeleaji aliyepata medali ya Olympiki na wengineo wengi katika fani mbalimbali.
Pumu ni ugonjwa usio na tiba, lakini kukiwa na mpango mzuri wa kuulinda mwili, hakuna sababu ya mtu mwenye pumu kutoishi maisha ya kawaida na kutoshiriki katika shughuli za kawaida za maisha.
Pumu Ni Nini?
Pumu ni ugonjwa wa muda mrefu (wa kudumu) wa mapafu ambao husababisha njia za kupitisha hewa kuvimba na kupunguza kipenyo cha njia za kupitisha hewa. Hali hii humfanya mwenye pumu kurudiwa na vipindi vya kubanwa na kifua, kushindwa kupumua vizuri, kutoa sauti kama ya filimbi wakati akipumua na kukohoa. Hali hii ya kubanwa na pumu hutokea zaidi usiku au mapema asubuhi.
Ili kulielewa vizuri tatizo hili la pumu tutatazama namna njia hizi za kupitishia hewa zilivyoumbwa na jinsi zinavyofanya kazi. Njia za kupitishia hewa zimeumbwa kwa mfano wa tyubu (tubes) na zinafanya kazi ya kupeleka na kurudisha hewa kutoka kwenye mapafu. Njia za hewa za mtu mwenye pumu huwa zimevimba na zenye usikivu wa hali ya juu sana ambapo huhisi kwa haraka sana pale ambapo baadhi ya vitu vitakuwa vimevutwa ndani pamoja na hewa mtu huyu anapopumua. Kuvimba kwa njia hizi tayari huwa kumepunguza uwezo wa kuingiza hewa kwa wingi ndani ya mapafu kwa sababu ya kupunguzwa kwa kipenyo cha tyubu hizi. Mtu huyu akivuta hewa yenye baadhi ya vitu, njia hizi hukaza na kupunguza zaidi kipenyo cha njia hizo. Seli za njia hizo zinaweza pia kutengeneza ute (mucus) kuliko kawaida na kufanya njia ya hewa kuwa ndogo zaidi. Ute huu ni majimaji mazito yanayonata.
Hali hii ya kuvuta kitu kisichotakiwa na mwili wa mgonjwa huyu na kusababisha kukaza kwa misuli ya njia za hewa kukiambatana na utengenezaji wa ute kwa wingi na hivyo kumsababishia mtu huyu apumue kwa shida, ndiko tunakokuita kushikwa na pumu au kubanwa na pumu. Mara nyingine hali hii hutokea na isiwe mbaya sana na inaweza ikaondoka yenyewe au baada ya tiba ndogo. Wakati mwingine inaweza ikatokea na hali ikawa mbaya zaidi na kuhitaji tiba na uangalizi wa juu zaidi. Ni muhimu kuchukua hatua zinazofaa mara baada ya dalili hizi kujitokeza kuzuia hali isiwe mbaya zaidi.
Bahati nzuri ni kwamba ugonjwa huu sasa umeeleweka vizuri sana na una njia nyingi sana za kupunguza makali yake. Watu wengi wameweza kuishi maisha ya kawaida baada ya kuelewa namna ya kudhiti tatizo lao. Wamekuwa wakisumbuliwa mara chache sana na wameweza kupata usingizi mzuri bila ya kusumbuliwa na ugonjwa huu. Kinachotakiwa ni mtu mwenye tatizo hili kushiriki kikamilifu katika kuulinda mwili wake na kudhibiti ugonjwa huu na kujenga mahusiano ya karibu sana na madaktari na wahudumu wa vituo vya afya.
Aina Za Pumu
Child-Onset Asthma: Pumu ya aina hii huanza utotoni ambapo mtoto huwekwa kwenye mazingira ya vitu ambavyo mwili wake huviona kama ni vitu visivyofaa kwa mwili wake (allergens) kwa sababu za kiurithi. Mwili wa mtoto huyu huwa umerithi tabia ya kubagua vitu fulani na kinga zake za hujikinga na vitu hivyo.
Kila mtu ana vitu vyake ambavyo mwili wake hutambua kama ni vitu visivyofaa kwake, ambavyo mara nyingi huwa ni protini ya wanyama, fungus, poleni ya mimea, vumbi la nyumbani na vumbi za aina nyingine. Seli za njia za hewa huwa sikivu kwa vitu vya aina fulani na endapo mtoto atawekwa kwenye mazingira hayo kwa muda mrefu sana, anaweza kuanza kujijengea hali ya pumu kupambana na vitu hivyo.
Adult-Onset Asthma: Aina hii ya pumu huanza kutokea mtu anapokuwa na umri wa miaka 20 au zaidi. Hii ni aina ya pumu inayowapata wanawake zaidi kuliko wanaume na wagonjwa wa aina hii ya pumu ni wachache kuliko wale wa aina ya kwanza hapo juu. Chanzo cha aina hii ya pumu kinaweza kuwa ni kuwa ni mzio (allergy) wa kitu fulani pia, ambapo inakadiriwa kuwa kama asilimia 50 ya watu wanaopata pumu wakiwa wakubwa sababu kubwa ni allergy. Asilimia iliyobakia ambayo chanzo chake cha pumu hakihusiani na allergens, tunasema wana pumu iitwayo non-allergic adult-onset asthma au intrinsic asthma. Kuwepo kwenye mazingira ya kitu au kemikali fulani ya plastiki, chuma, dawa au vumbi la mbao kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha Adult-Onset Asthma.
Exercise-Induced Asthma: Hii ni aina ya pumu ambayo humpata mtu kwa sababu ya kufanya mazoezi au mwili wake kuchoka. Kuna watu wengi ambao hupatwa na pumu pale tu wanapoanza kufanya mazoezi, hili huwatokea hata wanamichezo wakubwa kwenye mashindano kama ya Olympiki. Njia zake za hewa husinyaa kati ya dakika tano hadi ishirini baaada ya kuanza mazoezi hivyo kumfanya apumue kwa shida kunakoweza kuambatana na sauti za filimbi au kukohoa. Daktari anaweza kumshauri mwanamichezo huyu kutumia asthma inhaler kabla ya mazoezi. Asilimia 80 ya watu wenye pumu husikia dalili za exercise-induced asthma wanapofanya mazoezi lakini watu wenye exercise-induced asthma huwa hawasikii dalili za pumu pale wasipofanya mazoezi.
Cough-Induced Asthma: Dalili za pumu ya aina hii ni kukohoa sana, ni ngumu sana kuigundua na kuitofautisha na matatizo mengine ambayo yanasababisha kukohoa kama postnasal drip, sinusitis, chronic bronchitis n.k. Mtu ataanza kukohoa bila kuonyesha dalili nyingine za pumu na kukohoa huku kunaweza kutokea muda wo wote wa mchana au usiku.
Occupational Asthma: Ugonjwa huu hutokana na vitu vilivyopo kwenye eneo la kazi au vitendea kazi. Ni ugonjwa unaompata mtu pale tu anapokuwa kazini ambapo atashindwa kupumua vizuri na kuonyesha dalili nyingine za pumu.
Watu wengi wanaoathirika na aina hii ya pumu hutoa kamasi mfululizo, kuwashwa macho au kukohoa. Kazi ambazo husababisha sana aina hii ya pumu ni ufugaji, ukulima, kunyoa nywele, unesi, kupaka rangi na useremala.
Nocturnal Asthma: Pumu ya aina hii huitwa pia Nighttime asthma. Pumu ya aina hii humshika mtu kati ya saa 6 usiku na saa 2 asubuhi na husababishwa na vitu kama vumbi, manyoya ya wanyama au mazingira ambayo hayaruhusu upatikanaji wa hewa ya kutosha. Pumu ya aina hii mara nyingine haiambatani na kuwa na dalili za pumu wakati wa mchana. Mtu anaweza kupumua kwa shida kukiambatana na sauti fulani bila yeye mwenyewe kujielewa hadi atakapojisikia vibaya usiku wa manane – kati ya saa 8 hadi saa 10 za usiku. Hali hii inaweza kuwa ni ya mara moja moja au mara kadhaa kwa wiki. Mtu mwenye pumu ya kawaida mchana anaweza pia kupatwa na aina hii ya pumu.
Katika kurasa zinazofuta tutaona ni nini tiba ya pumu, dawa kwa ajili ya kupunguza makali ya ugonjwa huu wa pumu na hatua za kuchukua ili kuweza kuishi maisha ya kawaida pale unapokuwa na tatizo hili la pumu.
Tunakuomba ndugu msomaji kutoa maoni yako kuhusu mada yetu na kuuliza swali lo lote pale unapoona hapaeleweki. Ni faraja kwetu kupokea maoni yako na kuhakikisha kuwa tumekujibu.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu ndani ya muda wa kazi kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.
Ukurasa 1 2