Tumeshashuhudia watu wengi wamekufa na tukaambiwa wamekufa kwa tetanus. Maneno kama tetanus haina tiba au ukiumwa tetanus unaganda shingo ni ya kawaida. Kwamba ukijichoma na kitu chenye ncha kali chenye kutu, uwahi ukachomwe sindano ya tetanus. Lakini, tetanus ni ugonjwa gani hasa?
Mada yetu ya leo itauchambua ugonjwa huu wa tetanus ili uweze kujua chanzo cha tetanus, dalili zake, tiba au kinga ya tetanus. Bila kupoteza muda, tuanze mara moja.
Tetanus Ni Nini?
Tetanus ni ugonjwa mkali, ambao mara nyingi unaua, ni wa mfumo wa neva unaosababishwa na sumu zinazotengenezwa na bakteria aitwaye Clostridium tetani. Bakteria huyu hupatikana kwenye udongo na kwenye utumbo wa binadamu na wanyama (kinyesi). Bakteria huyu huweza kuwa kimya kwa miaka mingi kama spore kabla ya kuzinduka na kugeuka bakteria anayezaliana.
Bakteria huyu huzaliana kwenye kidonda. Vidonda vyenye kina au vile vyenye tishu zilizokufa ndiyo maeneo ambayo bakteria huyu anaweza kuingilia kirahisi mwilini.
Vidonda vinavyotokana na kujitoboa kama vile vya misumari, vibanzi au vipande vya vioo vyenye ncha kali, vidonda vya upasuaji, vidonda vya kupigwa risasi au vya kuumwa na wadudu ndizo sehemu ambazo bakteria huyu hupata nafasi ya kuingia katika mwili. Bakteria huyu anaweza pia kupitia vidonda vya kuungua na moto na matundu ya sindano. Tetanus inaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto mchanga (kupitia uterus baada ya uzazi na kupitia kwenye kitovu).
Sumu kali (tetanospasmin) inayozalishwa wakati bakteria hawa wanazaliana ndicho chanzo cha madhara makubwa ya tetanus.
Sumu za tetanus huharibu mawasiliano baina ya neva na misuli inayoamshwa na neva hizo, na hasa sehemu vinapokutana (neuromuscular junction). Sumu za tetanus hukuza ishara za kikemikali kutoka kwenye neva kwenda kwenye misuli, hali inayosababisha misuli kukaza moja kwa moja.
Dalili Za Tetanus
Tetanus huchukua muda wa wastani wa kati ya siku 2 hadi miezi miezi 2 kuanza kuonyesha dalili zake, lakini kwa kawaida ni katika siku 14 toka siku ya kupata jeraha.
Dalili za kawaida ni:
. Kukaza kwa misuli kwenye taya (trimus)
. Ugumu wa misuli ya shingo
. Shida wakati wa kumeza
. Ugumu wa misuli ya tumbo
. Mikazo ya misuli inayodumu kwa dakika kadhaa, mikazo ambayo inasababishwa na vitu vidogovidogo kama sauti kubwa, kuguswa au mwanga.
Dalili nyingine zinaweza kuwa:
. Homa
. Jasho kali
. Kupanda kwa pressure
. Mapigo ya moyo kwenda mbio
Katika siku saba za mwanzo baada ya maambukizo ya bakteria, kukaza kwa misuli kunakosababishwa na sumu za tetanus kwenye eneo la kidonda kutasambaa hadi sehemu nyingine zote za mwili. Kukosa utulivu na maumivu ya kichwa vitaonekana. Hii itahusisha misuli yote ya mwili ikiwa ni pamoja na misuli muhimu inayohusika na upumuaji. Misuli hii ya upumuaji inapokosa nguvu, kupumua inakuwa ni shida au haiwezekani na kifo kinatokea endapo msaada wa kuokoa maisha utakosekana. Pamoja na vifaa vya kusaidia upumuaji, maambukizi kwenye njia za hewa ndani ya mapafu yanaweza kusababisha kifo.
Kinga Ya Tetanus
Njia bora kabisa ya kupambana na tetanus ni kuizuia. Sumu za tetanus zikishanata kwenye maeneo zinapoishia neva, hakuna njia za kuziondoa. Ili kupona kutokana na sumu ya tetanus inabidi neva mpya ziote, tendo ambalo linalochukua hadi miezi kadhaa.
Unaweza kujikinga na tetanus kirahisi sana kwa kutumia chanjo.
Watoto wote wanatakiwa wapewe chanjo ya tetanus, kuanzia wanapokuwa na miezi 2 na kuimaliza wanapofikia miaka 5. Sindano za ziada (Booster vaccination) zinapendekezwa wanapofikia miaka 11.
Baadaye wanatakiwa kupata chanjo (follow-up booster vaccination) kila baada ya miaka 10.
Tiba Ya Tetanus
Ugonjwa wa tetanus hauna dawa.
Tiba hutolewa ili kuwaua bakteria kwa kutumia antibiotics wakati mgonjwa akichunguzwa juu ya dalili zo zote za kushindwa kupumua. Tiba inalenga kuzuia utengenezwaji wa sumu, kupunguza makali yake, na kudhibiti mikazo ya misuli.
Hali ikiwa mbaya zaidi, mgonjwa atapewa vifaa vya kumsaidia kupumua.
Sumu inayozunguka ndani ya mwili itaondolewa kwa kutumia antitoxin drugs. Sumu ya tetanus haisababishi madhara ya kudumu kwenye mfumo wa neva. Baada ya kupona, mgonjwa bado atatakiwa kupata chanjo dhidi ya tetanus.
Katika mada nyingine tofauti kabisa na hii, tutazungumzia homa ya matumbo (typhoid) na tatizo la vidonda vya tumbo.
Tafadhali unakaribishwa kutoa maoni yako kuhusu mada yetu au kuuliza maswali uliyo nayo. Kwa mawasiliano tumia namba 0655 858027 au 0756 181651.
N. B. Piga simu ndani ya saa za kazi tuwasiliane tafadhali, usitume SMS.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa MAFUNZO YA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.