Upasuaji wa mtoto wa jicho ni hatua inayochukuliwa ya kuondoa lensi ya jicho ya asili yenye ukungu (iliyo kwenye eneo la mbele la jicho) na kuweka lensi bandia iliyo angavu. Upasuaji mwingi huleta mafanikio ya kurudishia uonaji na kupunguza dalili nyingi zinazoendana na mtoto wa jicho kama kupungua kwa nguvu ya kuona na kushindwa kutofautisha rangi ambazo zilihitaji mwanga mkali zaidi ili kuona. Pamoja na kwamba upasuaji huu ni wa muda mfupi, hauambatani na maumivu, kuna kipindi cha maandalizi na kipindi cha kusubiri uponaji. Kama ilivyo kwa tiba nyingine, kunaweza kutokea vitu ambavyo havikutarajiwa ambavyo itabidi kuvifanyia kazi. Mada yetu ya leo ni maelezo ya aina mbali mbali za upasuaji na hali ambazo zinaweza kutokea baada ya upasuaji huo.
Upasuaji wa mtoto wa jicho hufanywa bila mgonjwa kutakiwa kulazwa. Mgonjwa anaweza kuruhusiwa muda mfupi tu baada ya upasuaji.
Wakati upasuaji ukiendelea, daktari huivunjavunja lensi ya awali katika vipande vidogo na kuvitoa nje. Kisha daktari huweka lensi ya kutengenezwa (intraocular lens -IOL).
Kwa sababu upasuaji unafanyika kwa kutumia njia ya ganzi ya matone, mgonjwa huruhusiwa baada ya
upasuaji. Upasuaji halisi huchukua chini ya dakika 30 lakini mgonjwa anaweza kuwepo hospitalini
kwa saa kadhaa kwa ajili ya uchunguzi wa kabla na baada ya upasuaji.
Kama mgonjwa ana mtoto wa jicho katika macho yake yote mawili, upasuaji utafanyika kwa awamu, jicho
la pili likifanyiwa upasuaji baada ya wiki chache ili kuruhusu jicho la kwanza kupona vizuri.
Lensi Bandia -Intraocular lenses (IOLs)
Lensi bandia zinazowekwa badala ya lensi asili hutengenezwa kwa kutumia mali ghafi za aina nyingi.
Lensi nyingi hata hivyo hutengenezwa kwa kutumia acrylic na silicone. Lensi hizi hupakwa vitu mahsusi ambavyo husaidia kuyalinda macho kutokana na mionzi ya jua isiyo salama iitwayo ultra violet rays.
Acrylic ni aina ya plastiki iliyo ngumu na angavu. Lensi za acrylic zinaweza kuwa za kupindika au ngumu
zisizopindika kutegemea kiwango cha maji yaliyomo ndani yake. Lensi zisizopindika za acrylic hutengenezwa kutokana na polymethyl methacrylate (PMMA), wakati zile zinazopindika hutengenezwa kutokana na hydrophobic au hydrophilic acrylic.
Silicone ni polymer ya kibayolojia isiyo na sumu. Lensi ya kukunjika ambayo ilikuwa ya kwanza kupasishwa na FDA ilitengenezwa na silicone na ilipasishwa mwaka 1990.
Mali ghafi nyingine za kutenegenezea lensi ni pamoja na collamer, Styrene copolymer, hydroxyethyl
methacrylate (HEMA) n.k.
Kila mali ghafi iliyotumika kutengeneza lensi ina tabia tofauti na nyingne na kila moja ina sifa nzuri na
mapungufu yake. Kwa mfano mali ghafi za hydrophobic zinaweza kwa kiasi fulani kupoteza sifa ya kupitisha mwanga baada ya kuwa zimewekwa kwenye jicho.
Mbinu Za Upasuaji Wa Mtoto Wa Jicho
Kuna mbinu kadhaa zinazotumika katika upasuaji wa mtoto wa jicho. Daktari wako atachagua aina ya
upasuaji kulingana na ukubwa na sehemu mtoto wa jicho alipo.
Phacoemulsification
Hii ndiyo njia inayotumika zaidi katika kuondoa mtoto wa jicho. Daktari atatumia kijiwembe cha upasuaji
kukata eneo dogo (kati ya milimita 2 hadi 3) kwenye cornea. Kisha atakata tena kwenye capsule (namna ya
kijifuko kinachohifadhi lensi).
Kifaa cha ultrasound kitapenyezwa kwenye sehemu iliyokatwa na mawimbi ya sauti yaliyolengwa
yatakayotolewa na kifaa hicho yataivujavunja ile lensi yenye ukungu na kuwa vijipande vidogo.
Vijipande hivyo vitavutwa nje ya jicho kwa kutumia vacuum iliyounganishwa na mashine ya mawimbi. Kisha lensi bandia inapenyezwa ndani ya capsule.
Sehemu iliyokatwa hufungwa kwa kutumia namna ya majimaji maalumu, aghalabu ushonaji huhitajika.
Extracapsular Cataract Extraction ((ECCE))
Upasuaji wa aina hii hutumika mara chache na daktari huchana eneo kubwa zaidi (yapata milimita 10)
juu ya jicho ili kuiondoa lensi ikiwa nzima. Ufyonzaji unaweza kutumika kama vipande vitabaki.
Kama ilivyo kwa phacoemulsification, lensi bandia (IOL) hutumbukizwa baada ya kuondoa lensi ya asili
yenye ukungu. Eneo lililokatwa hushonwa kwa nyuzi kadhaa.
Intracapsular Cataract Surgery (ICCE)
Daktari atakata eneo kubwa zaidi juu ya cornea -sehemu ya mbele ya jicho (iliyo ngumu) inayowezesha miali ya mwanga kupenya- kisha atatumia vifaa mbalimbali kuiondoa lensi asili kutoka ndani ya jicho. Lensi kwanza huvunjwavunjwa na kuwa vipande vidogo ambavyo hufyonzwa nje ya jicho. Capsule pia huondolewa.
Lensi ikishaondolewa, daktari hupenyeza lensi bandia (IOL). Lensi hii bandia ni plastiki angavu inayochukua nafasi ya lensi ya awali. Lensi bandia huwa imekujwa na hupenyezwa kupitia tundu dogo la kwenye cornea. Lensi hii ikisha kuwa kwenye nafasi yake hukunjuka na kuchukua umbo la lensi asilia.
Watu walio wengi hupona katika wiki chache.
Njia hii ya upasuaji haitumiki mar anyingi kama njia nyingine katika uapasuaji wa mtoto wa jicho kwa sababu inahitaji kupasua eneo kubwa zaidi na hivyo mgonjwa kuchukua muda mrefu zaidi wa kupona.
Laser-Assisted Cataract Surgery (FLACS)
Femtosecond laser assisted cataract surgery (FLACS) ni upasuaji unaohusisha teknolojia ya optical coherence tomography imaging ili kumsaidia daktari kukata eneo kiusahihi juu ya cornea na kisha kwenye capsule kwa kutumia mawimbi ya laser. Laser hiyo kisha hulaisha cataract na kuivunjavunja kuwa vipande vidogo. Hii ni njia ya kisasa kabisa na yenye uhakika zaidi.
Kamera au kifaa cha ultrasound huchukua piacha ya jicho na lensi na kupeleka taarifa kwenye kompyuta ambayo itaandaa laser ya kutumika (to a computer that programs a laser). Lase itachana eneo juu ya cornea na lensi, na inaweza kuilanisha cataract. Kifaaa cha ultrasound (probe) kitaivunjavunja lensi na kisha vipande kuondolewa. Lensi bandia itaingizwa ndani ya capsule kuchukua nafasi ya lensi ya zamani ya asili yenye ukungu.
Lensi hii mpya inaweza mara nyingine kusaidia kuondoa tatizo liitwalo astigmatism.
Uangalizi Baada Ya Upasuaji
Baada ya upasuaji wa mtoto wa jicho, jicho lako litachukua wastani wa wiki nane ili kupona kabisa. Watu walio wengi (yapata asilimia 90) hupata matokeo mazuri baada ya upasuaji, ingawa, uonaji wao hauwezi kuwa kamilifu kabisa.
Watu wengi huhitaji miwani au contact glasses baada ya upasuaji, hasa hasa kwa kazi maalumu, kama kusomea.
Mwisho, yafaa kueleza vile vile kuwa baada ya upasuaji utahitaji kurejea kwenye kituo chako cha afya kwa ajili ya uchunguzi na kuona kama kuna mambo yaliyojitokeza baada ya upasuaji na afya ya jicho kwa jumla.
Mambo Ambayo Yanaweza Kujitokeza
Upasuaji wa aina yo yote una mambo yasiyotegemewa ambayo yanaweza kutokea, na upasuaji wa mtoto wa jicho hauna tofauti. Lakini mambo mengi yasiyotarajiwa yanaweza kuzuilika au kufanyiwa marekebisho ya haraka.
Mambo ambayo yanaweza kujitokeza ni pamoja na:
. Kuvimba kwa Cornea: Hali hii ikitokea inaweza kusababisha kuona kwa ukungu siku ya pili baada ya
upasuaji. Hali ikizidi, matone ya steroids yanaweza kutumika kupunguza uvimbe huo.
. Kuongezeka Kwa Pressure Ndani Ya Jicho: . Tatizo hili mara nyingi ni la muda muda mfupi, saa chache mara baada ya upasuaji. Kwa baadhi ya watu, hali hii inaweza kuendelea kwa muda mrefu na hata kuhitaji tiba ya kupunguza pressure.
. Posterior Capsular Rupture: Hii ni hali ambapo sehemu ya nyuma ya capsule inatatuka. Hii inatokea wakati upasuaji ukiendelea na inaweza kurekebebishwa kwa aina nyingine za upasuaji.
. Posterior Capsular Opacification: Hali hii inatokea wakati sehemu ya nyuma ya capsule yenye lensi mpya
inapokuwa nene na kuzuia mwanga usipite. Uonaji unakuwa wa ukungu, hali inayolingana na ya kabla ya
upasuaji. Hali hii huondolewa kwa tiba iitwayo YAG capsulotomy.
Na mara chache haya yanaweza kujitokeza:.
. Jicho Kuvuja damu (suprachoroidal hemorrhage): Hii hutokea kwa sababu ya kutatuka kwa mishipa ya damu ndani ya eneo la suprachoroid lililo kati ya sclera na choroid. Hii hutokea wakati wa upasuaji na hurekebishwa wakati upasuaji ukiendelea.
. Maambukizo ndani ya jicho (endophthalmitis): Ingawa mara chache, hili ni moja kati ya matatizo makubwa na yenye kuleta madhara makubwa yanayoweza kutoke baada ya upasuaji wa mtoto wa jicho. Huleta maumivu makali, jicho kuwa jekundu, na kupoteza uonaji.
. Kubanduka Kwa Retina: Hii huambatana na ghafla kuongezeka kwa vitu vyeusi vinavyoelea (floaters)
au miale ya mwanga mweupe bila kusikia maumivu yo yote. Hii hutokea zaidi kwa watu wenye tatizo la
kuona karibu’
. Kuhama Kwa Lensi Iliyowekwa: Hii ni hali inayotokea pale lensi inapohama kutoka sehemu yake ya kawaida. Inaweza kutoka siku au miaka kadhaa baada ya upasuaji na kutoa dalili kama za kuona kwa ukungu, kuona vitu viwili viwili, na kuona ukingo wa lensi mpya uliyowekewa.
Katika mada nyingine, tutayaona matatizo ya macho yanayoletwa na kisukari. Usisite kutoa maoni yako au kuuliza maswali uliyo nayo kuhusu mada yetu ya leo. Itakuwa furaha kwetu kuwa nawe.
Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au kututumia barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu ndani ya saa za kazi kwenye namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.